“Kisanduku cha Ustawi wa Afya ya Hisia,” Kwa Ajili ya Nguvu kwa Vijana, Julai 2024.
Msaada wa Kimaisha
Kisanduku cha Ustawi wa Afya ya Hisia
Hapa kuna vidokezo vya kujiweka mwenye hisia zenye afya.
Pengine unaweza kufikiria njia nyingi za kuweka mwili wako kuwa na afya kadiri unavyoendelea kukua. Unajua kwamba Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo wanakupenda na wanataka uutunze mwili wako. Na “kutunza mwili wako kunajumuisha kutunza afya yako ya akili na afya ya hisia” (Kwa Ajili ya Nguvu kwa Vijana: Mwongozo wa Kufanya Chaguzi [2022], 29). Hapa kuna mambo unayoweza kufanya ili kukusaidia kuwa na hisia zenye afya pia!
-
Jiunganishe na wengine. Hasa unapohisi huzuni, unaweza kutaka kuwa peke yako. Hiyo ni sawa kwa muda fulani, lakini ni muhimu pia kutumia muda na watu wenye kuinua. Kujitenga karibu kila mara hufanya changamoto kuwa ngumu zaidi.
-
Eleza hisia zako. Jizoeze kuwa mwaminifu kuhusu jinsi unavyohisi. Zungumza kuhusu hisia zako kwa njia maalumu. Na kwa kweli, ni SAWA kulia! Fikiria kuhusu wakati Yesu alipolia (ona Yohana 11:32–35).
-
Tambua kuwa hisia ni taarifa. Ingawa zinaweza kuwa si za faraja, hisia zenyewe haziwezi kukuumiza. Jaribu kuzitambua hisia zako na kufahamu kile zinachokuambia.
-
Jizoeze ujuzi wa kukabiliana. Unapokuwa na huzuni au uchungu, jifunze kudhibiti hisia hizo kwa njia yenye afya. Kwa mfano, watu wengi wanaona kuwa inasaidia kwenda kutembea, kusikiliza muziki, kuchora, kusali au kuandika katika shajara.
-
Acha hisia zisizo za faraja zije na kuondoka. Vuta pumzi ndefu na uwazie mawingu yakipeperushwa angani, au maji yakitiririka chini ya mto. Tambua mawazo na hisia zako na jaribu kuziacha ziondoke.
-
Endelea kuilisha roho yako. Maandiko, nyimbo, sala, kanisa—mambo haya yote yanasaidia kuimarisha roho yako, ambayo itasaidia sehemu yako iliyosalia iwe yenye afya njema.
-
Jaribu kubaki na mwili wenye afya. Afya ya hisia zetu na afya ya mwili vimeunganishwa. Kula chakula chenye lishe, kupata usingizi wa kutosha na kujijengea mazoea ya kufanya mazoezi kutakusaidia kuwa na afya njema ya hisia kadiri unavyokua.
-
Omba msaada pale unapouhitaji. Miili yetu wakati mwingine inahitaji usaidizi wa kitaalamu ili kuwa na afya na kuwa vyema. Nyenzo hizi ni baraka kutoka kwa Baba wa Mbinguni, ambaye anataka kutusaidia. Katika njia iliyo sawa na hiyo, yawezekana tukahitaji msaada kutoka kwa madaktari na washauri ili tuwe na hali nzuri ya kihisia nyakati fulani. Kama unahisi kuwa una huzuni katika vipindi vya muda mrefu, au kama una mawazo ya kujiumiza mwenyewe, tafadhali muombe mtu mzima akusaidie. Huhitaji kupitia hili peke yako! Fikia baraka zote ambazo Baba wa Mbinguni ameziweka kwa ajili yako.