Maandiko Matakatifu
Moroni 6


Mlango wa 6

Watu waliotubu wanabatizwa na kushirikishwa—Washiriki wa Kanisa wanaotubu wanasamehewa—Mikutano inaendeshwa kwa uwezo wa Roho Mtakatifu. Karibia mwaka 401–421 B.K.

1 Na sasa ninazungumza kuhusu ubatizo. Tazama, wazee, makuhani, na walimu walibatizwa; na hawangebatizwa kama hawangezaa matunda yapasayo toba.

2 Wala hawakumpokea yeyote kwenye ubatizo kama hangekuja na moyo uliopondeka na roho iliyovunjika, na kushuhudia kwa kanisa kwamba wametubu kwa kweli kutoka kwenye dhambi zao.

3 Na hakuna waliopokelewa kwenye ubatizo isipokuwa wajivike juu yao jina la Kristo na kukata kauli kumtumikia hadi mwisho.

4 Na baada ya hao kupokewa kwenye ubatizo, na kupokelewa na kusafishwa kwa uwezo wa Roho Mtakatifu, walihesabiwa miongoni mwa watu wa kanisa la Kristo; na majina yao yalichukuliwa ili wakumbukwe na kulishwa na neno nzuri la Mungu, kuwaweka kwenye njia nzuri, kuwaweka waangalifu siku zote kwenye sala, wakitegemea tu katika nguvu ya wokovu wa Kristo, ambaye alikuwa mwanzilishi na mtimizaji wa imani yao.

5 Na washiriki wa kanisa walikutana pamoja mara kwa mara, kufunga na kuomba, na kuzungumza mmoja na mwingine kuhusu ustawi wa nafsi zao.

6 Na walikutana pamoja mara kwa mara kushiriki kwa mkate na divai, katika kumkumbuka Bwana Yesu.

7 Na walikuwa waangalifu kwamba kusiwe na uovu miongoni mwao; na yeyote aliyepatikana akitenda uovu, na mashahidi watatu wa kanisa waliwahukumu mbele ya wazee, na kama hawakutubu, na hawakukiri, majina yao yalitolewa nje, na hawakuhesabiwa miongoni mwa watu wa Kristo.

8 Lakini kila mara walipotubu na kutafuta msamaha, na kusudi halisi, walisamehewa.

9 Na mikutano yao iliendeshwa na kanisa kulingana na njia ambayo Roho aliwaongoza, na kwa uwezo wa Roho Mtakatifu; kwani vile uwezo wa Roho Mtakatifu ulivyowaongoza kuhubiri, au kuhimiza, au kuomba, hata hivyo ndivyo ilivyofanywa.