2022
Funguo Nne za Nefi kwa ajili ya Kumwelewa Isaya
Septemba 2022


“Funguo Nne za Nefi kwa ajili ya Kumwelewa Isaya,” Kwa Ajili ya Nguvu kwa Vijana, Sept. 2022.

Njoo, Unifuate

Isaya

Funguo Nne za Nefi kwa ajili ya Kumwelewa Isaya

Je, unapata matatizo kusoma Isaya? Msaada wa Nefi uko hapa ili kukusaidia.

Picha
Nefi akiandika kwenye mabamba ya dhahabu

Vielelezo na Kevin Keele

Ni wazi kwamba maandishi ya Isaya katika Agano la Kale ni ya muhimu kwa sababu yamenukuliwa mara nyingi katika Agano Jipya na katika Kitabu cha Mormoni. Mwokozi Mwenyewe alisema, “Maneno ya Isaya ni makuu” (3 Nefi 23:1).

Bado, ni kwa nini yawe magumu sana kueleweka?

Usife moyo! Nefi alijua kuhangaika kwetu. Alikubali kwamba “Isaya aliongea mambo mengi sana ambayo yalikuwa magumu … kueleweka” (2 Nefi 25:1). Kwa shukrani, Nefi ametupatia funguo nne ambazo zinaweza kusaidia kufungua maana ya maneno ya Isaya.

Ufunguo wa Kwanza: Ishi katika Siku za Mwisho

Nefi aliandika kwamba wale wanaoishi katika “siku za mwisho” wangeweza “kuelewa” maneno ya Isaya (2 Nefi 25:8). Pengine hiyo ni kwa sababu watu katika siku za mwisho wangekuwa na mtazamo ambao watu wa wakati wa Isaya hawakuwa nao. Zamani za kale, watu yawezekana wasingeelewa jinsi ambavyo watu wangeweza “kuita uovu wema, na wema uovu” (Isaya 5:20) na bado sisi tunaona hili likitokea kote kutuzunguka sisi.

Pia, watu siku zilizopita yawezekana wasingeelewa kile Bwana alichomaanisha wakati Yeye aliposema, “nitafanya kazi ya ajabu kati ya watu hawa, kazi ya ajabu na muujiza” (Isaya 29:14).

Manabii wa sasa wametuambia sisi hii “kazi ya ajabu na muujiza” inatajwa kuwa ni kuja kwa Kitabu cha Mormoni na Ufunuo unaoendelea wa injili ya Yesu Kristo. Una heri wewe kuishi katika wakati ambapo unaweza kushuhudia kutimizwa kwa unabii mwingi wa Isaya.

Ufunguo wa Pili: Uwe na Roho ya Unabii

Nefi alisema kwamba maneno ya Isaya yanaweza kuwa “wazi kwa wale wote ambao wamejazwa na roho wa unabii” (2 Nefi 25:4). Hiyo inaweza kusikika kama inakwaza mwanzoni, lakini hii haimaanishi kwamba ni manabii pekee yao wanaweza kumwelewa Isaya. Maandiko yanafundisha kwamba “ushuhuda wa Yesu ndio roho ya unabii” (Ufunuo 19:10). Kwa maneno mengine, kama unamwamini Yesu Kristo, tayari unao mwanzo wa kile kinachohitajika kumwelewa Isaya.

Maandishi ya Isaya yanamshuhudia Yesu Kristo na Upatanisho Wake. Hata jina lake linashuhudia juu ya Mwokozi! Jina la Isaya maana yake “Bwana ni Wokovu,” au “Yesu anaokoa.”

Ufunguo wa Tatu: Elewa Ushairi na Ishara

Nefi alielezea kwamba maneno ya Isaya ni magumu kwa wale ambao hawana mazoea na “mtindo wa kutoa unabii miongoni mwa Wayahudi” (2Nefi 25:1). Maneno ya Isaya ni rahisi kueleweka tunapojifunza zaidi kuhusu desturi za kuandika za Mashariki za wakati wa Isaya, kama vile ushairi na ishara. Isaya mara nyingi alitumia ishara zilizo ngumu kufahamika katika maandishi yake.

Kwa mfano, Isaya aliandika kuhusu watu wale walio `“juu na kuinuliwa” kama kuwa “mierezi ya Lebanoni” na “mialoni ya Bashani [Syria]” (2 Nefi 12:13). Mierezi na miaroni ni miti migumu. Isaya alitumia njia ya kishairi kusema kwamba watu wenye kiburi na maringo ni kama miti mirefu kwa sababu wamefanya mioyo yao kuwa migumu na wanafikiri kwamba wao ni bora kuliko wengine Kuisoma Isaya kama shairi inaweza kutusaidia kuelewa vyema kile alichofundisha.

Ufunguo wa Nne: Elewa Jiografia

Isaya anataja maeneo 108 tofauti katika maandishi yake. Hii inaweza kukuchanganya sana kukumbuka, hususani kama hujawahi kuishi huko! Ufunguo wa nne wa Nefi ni kujua “maeneo kuzunguka” Yerusalemu (2 Nefi 25:6).

Yerusalemu iko katika eneo hilo hilo ambapo imekuweko daima, lakini hapo kale ilikuwa katikati ya mataifa makuu matatu yenye nguvu ulimwenguni Mashariki ilikuwepo Babeli, kituo cha sanaa na mitindo. Kaskazini ilikuweko Assyria, nguvu ya kijeshi katika siku za Isaya. Kusinimagharibi ilikuwa Misri, kituo cha kibiashara. Kujua kiasi hiki tu inaweza kutusaidia kufuatilia ni nani aliyekuwa akiitishia kuivamia Israeli na kuwachukua mateka. Kiishara, Babeli iliwakilisha malimwengu, Assyria kiburi, na Misri utajiri.

Maneno ya Isaya ni kwa ajili Yako Wewe

Isaya alifundisha mambo mengine mengi ambayo ni muhimu kwetu kuyaelewa. Alishuhudia juu ya kutawanywa na kukusanywa kwa Israeli, ambako Rais Russell M. Nelson amesema “ndicho kitu muhimu zaidi kinachofanyika duniani hivi leo. … Na kama utachagua, kama unataka, wewe unaweza kuwa sehemu kubwa ya hilo” (“Tumaini la Israeli” [worldwide youth devotional, Juni 3, 2018], 8, HopeofIsrael.ChurchofJesusChrist.org; ona Isaya 49:13–23).

Picha
Ujio wa Pili wa Yesu Kristo

Isaya pia alishuhudia juu ya ujenzi wa Sayuni katika maandalizi ya Ujio wa Pili wa Mwokozi na utawala wa milenia (ona, kwa mfano, Isaya 5152). Pamoja na ushuhuda juu ya Yesu Kristo, Roho anaweza kukushuhudia wewe juu ya umuhimu wa maneno ya Isaya na jinsi yanavyoweza kutusaidia na kubariki maisha yetu leo.

Chapisha