2023
Amani ya Kukabiliana na Dhoruba za Maisha
Machi 2023


“Amani ya Kukabiliana na Dhoruba za Maisha,” Kwa Ajili ya Nguvu Kwa Vijana, Machi 2023.

Amani ya Kukabiliana na Dhoruba za Maisha

Bwana Yesu Kristo husema kwako wakati wa dhoruba katika maisha yako: “Nyamaza, utulie.”

Picha
Dieter F. Uchtdorf

Mzee Uchdorf pamoja na vijana kwenye matangazo ya BYU–Pathway Worldwide mnamo Februari 7, 2017.

Baada ya siku nzima ya kufundisha ufukweni mwa bahari, Bwana Yesu Kristo alipendekeza kwa wafuasi kwamba wavuke ng’ambo nyingine ya Bahari ya Galilaya. Baada ya kuondoka, Yesu alipata sehemu ya kupumzika ndani ya mashua na akalala.

Punde mawingu yakatanda “palitokea dhoruba kuu na upepo, na mawimbi yakapiga chombo, hata kujaa maji” (ona Marko 4:37).

Wanafunzi kadhaa wa Yesu walikuwa wavuvi wazoefu na walijua namna ya kushughulikia mashua nyakati za dhoruba. Lakini dhoruba ikawa kali sana, na walianza kushikwa na hofu. Mashua ilionekana kuanza kuzama.

Katika haya yote, Yesu alikuwa bado amelala.

Hatujui ni kwa muda gani wanafunzi walihangaika katika dhoruba, lakini mwishowe hawakuweza kusubiri zaidi. Walimwamsha Yesu na kulia, “Mwalimu, si kitu kwako kuwa tunaangamia?” (Marko 4:38).

Picha
merikebu baharini

Vielelezo na Adam Howling

Dhoruba za Maisha

Sisi sote ghafla tunakabiliana na dhoruba katika maisha. Unaweza kuangalia shida za ulimwenguni kote au mazingira yako mwenyewe na kuhisi kuhuzunika, kuvunjika moyo na kusikitishwa. Moyo wako unaweza kuvunjika kwa ajili yako wewe mwenyewe au mtu unayempenda. Unaweza kuwa na wasiwasi au kuhofia na kuhisi kwamba tumaini limekuacha milele.

Katika nyakati hizi, unaweza kulia kama wanafunzi wa Yesu, “Mwalimu, si kitu kwako kuwa mimi ninaangamia?”

Nilipokuwa umri wenu, mojawapo ya nyimbo zangu nilizopenda ulikuwa “Bwana, Dhoruba Yavuma.”1 Ningeweza kujiona mwenye kwenye mashua wakati “Mawimbi [yalikuwa] makali!” Sehemu muhimu na iliyo nzuri ya wimbo inafuata: “Upepo, mawimbi yaitika: Nyamaza, tulia.” Kisha unakuja ujumbe muhimu: “Hakuna maji ya kumdhuru Bwana wa bahari, nchi, mbingu.”

Baada ya wanafunzi Wake kulia kwa ajili ya msaada, Yesu “alisimama na kuukemea upepo na kuiambia bahari, Nyamaza, utulie. Na upepo ukakoma, kukawa shwari kuu” (Marko 4:39).

Kama utamkaribisha Yesu Kristo, “Mfalme wa Amani” (Isaya 9:6), katika mashua yako, unaweza kupata amani kati ya dhoruba na ghasia za kutisha ambazo huzunguka ndani yako na karibu nawe.

Maneno yale yale Yesu aliyosema kwa Bahari ya Galilaya usiku ule wenye dhoruba hapo zamani, Yeye anasema kwako wakati wa dhoruba katika maisha yako: “Nyamaza, utulie.”

Picha
mashua katika dhoruba na amani

Tegemea Nguvu Zake za Kutuliza

Je, unaweza kufikiria jinsi ambavyo wanafunzi walihisi mara walipoona upepo, mvua na bahari zikitii amri ya Bwana? Yote waliyoweza kusema ilikuwa, “Ni nani huyu, basi, hata upepo na bahari humtii?” (Marko 4:41).

Yesu Kristo si kama mtu yeyote ambaye ameshawahi kutembea katika dunia hii. Yeye alikuja kutuokoa. Katika Bustani ya Gethesmane, Yeye alilipia fidia ya dhambi zetu zote. Pia aliteseka maumivu na huzuni yetu yote. Mateso haya makubwa yasiyopimika yalisababisha Yeye kuvujwa na damu kutoka kwenye kila kinyweleo (ona Luka 22:44; Mafundisho na Maagano 19:18).

Kile Bwana alichokifanya kutokana na upendo kamili kunapita uwezo wangu wa kuelewa. Lakini ninajua Yeye alifanya hivyo kwa ajili yangu, kwa ajili yako na kwa ajili ya kila nafsi ambayo imewahi kuishi au itaishi duniani. Yeye alitoa vyote ili tuweze kupokea vyote.

Kamwe hakuna mtu yeyote atakayepata kupitia mateso ambayo Yesu aliteseka, bali wewe na mimi tutakuwa na dhoruba zetu wenyewe za giza na chungu za kukabiliana nazo. Kama utauinua moyo wako kwa Bwana, Yeye atatuliza dhoruba zako, kwani Yeye amezipitia hizo zote. Yeye aliteseka kwa ajili yako na anao uwezo wa kukuimarisha, kukutia moyo na kukubariki.

Yeye anaahidi “Amani nawaachieni, amani yangu nawapa: niwapavyo mimi, sivyo kama ulimwengu utoavyo. Msifadhaike mioyoni mwenu, wala msiwe na woga” (Yohana 14:27).

Njia za Kupata Amani

Bwana Yesu Kristo amekupa wewe njia za kuhisi amani Yake. Yeye alisema, “Jifunze kwangu, na sikiliza maneno yangu; enenda katika unyenyekevu wa Roho wangu, na utapata amani kwangu” (Mafundisho na Maagano 19:23).

Jifunze juu Yake kupitia maisha na mafundisho Yake katika maandiko. Inua moyo wako katika sala. “Simama … mahali patakatifu,” ikijumuisha hekaluni (Mafundisho na Maagano 87:8; ona pia 45:32).

Sikiliza maneno Yake kutoka kwa manabii wanaoishi. Fuata mwongozo wa Roho Mtakatifu. Tumia zawadi ya kiungu ya toba. Njoo katika Kanisa Lake ili kushirikishwa, kufundishwa na kulishwa neno jema la Mungu.

Enenda katika unyenyekevu wa Roho Wake kwa kuifanya nyumba yako kuwa mahali ambapo Roho Wake anaweza kuhisiwa. Wasaidie wengine na kwa shangwe mtumikie Yeye. Kumbuka, “Kuna amani katika kutenda haki.”2 Jitahidi kubakia mwaminifu na kuwa “[mfuasi] wa amani wa Kristo” (Moroni 7:3).

Kama utajifunza, utasikiliza, na kutembea pamoja na Bwana, kisha huja ahadi Yake kuu: Utakuwa na amani Yake.

Imani Kukaa Tuli

Kwa imani katika Bwana Yesu Kristo, unaweza “kutulia” wakati dhoruba za maisha zitakapokuja juu yako. Amani yawezekana isiwe upesi kama ilivyokuwa kwa wanafunzi katika Bahari ya Galilaya, lakini Bwana atakuimarisha kupitia dhoruba unazokabiliana nazo.

Rafiki yangu mpendwa, ninashuhudia kwamba Yesu Kristo yu hai.

Yeye anakupenda.

Yeye anakujua.

Yeye anakuelewa.

Yeye hatakuacha bila faraja katika wakati wako wa uhitaji.

Amani ya kweli huja tu katika na kupitia Kwake. Amani Yake ni kwa ajili ya wote ambao watamgeukia Yeye.

Mihtasari

  1. “Bwana, Mawimbi Yavuma,” Nyimbo za Kanisa, na. 53.

  2. “Chagua Jema,” Nyimbo za Kanisa, na. 135.

Chapisha