“Marafiki zangu hucheza kamari. Najua ni makosa. Ninawezaje kuwaelezea?” Kwa Ajili ya Nguvu Kwa Vijana, Machi 2023.
Kwenye Hoja
Marafiki zangu hucheza kamari. Najua ni makosa. Ninawezaje kuwaelezea?
Kamari humaanisha kuhatarisha fedha kwenye michezo ya bahati nasibu au kuweka dau juu ya matokeo ya mambo. “Kanisa linapinga na kushauri dhidi ya kamari ya aina yoyote. Hii inajumuisha kuweka dau katika michezo na bahati nasibu zinazodhaminiwa na serikali” (Kitabu cha Maelezo ya Jumla: Kuhudumu katika Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho, 38.8.17, ChurchofJesusChrist.org).
Tunaepuka kucheza kamari kwa sababu nyingi. Sio tu ni kupoteza wakati na fedha, lakini pia huharibu maisha ya watu. Inaweza kuwa tamaa, hata uraibu.
Pia kamari hufundisha kwamba unaweza kupata kitu bila kutoa kitu. Hiyo ni dhana hatari na ya uongo. Kushinda katika kamari hakuna uhakika na hakuwezi kutegemewa. Mafanikio uliyoyafanyia kazi ni ya kuridhisha sana, ni ya uhakika na yanadumu muda mrefu.
Kama unao marafiki wanaocheza kamari, unaweza kujaribu kuwasaidia. Unaweza kuwaambia—na, cha muhimu sana, waonyeshe—kwamba kuna njia bora zaidi za kutumia wakati wako na fedha zako. Unaweza kuwaonyesha wao kwamba maisha ni bora wakati unapokuwa hauhatarishi fedha zako na ustawi wa afya yako kwa tabia ambayo huleta kukosa uimara na dhiki kwa watu wengi sana.