“Yesu Kristo: Amani kati ya Dhoruba,” Kwa Ajili ya Nguvu Kwa Vijana, Machi 2023.
Njoo, Unifuate
Yesu Kristo: Amani kati ya Dhoruba
Siku moja, yawezekana ukahisi kusukwasukwa na dhoruba za maisha. Lakini Yesu Kristo ana uwezo wa kukuletea amani ambayo wewe hauwezi kuipata mahali pengine popote.
Katikati ya mwaka wangu wa mwisho wa shule ya upili, nilipata mshangao mkubwa. Wazazi wangu walikuwa wameitwa kuongoza Misheni ya Uruguay Montevideo, ambayo ilimaanisha walikuwa wangehamia upande mwingine wa dunia pamoja na wadogo zangu wanne. Tayari nilikuwa na hofu kuhusu kuhitimu shule ya upili, lakini sasa ningekuwa ninahudhuria chuo nikiwa peke yangu, wazazi wangu wakiwa katika bara tofauti. Nilijawa na hofu.
Mabadiliko yangu kutoka shule ya upili hadi chuoni yalikuwa magumu sana kwangu. Nikiwa nimezungukwa na wanadarasa wapole na maelfu ya wanafunzi, kamwe sikuwahi kujihisi mpweke sana. Shinikizo la shule lilikuwa la kuogofya. Sikujua kile nilichokuwa nataka kujifunza na niliona masomo kuwa magumu. Nilikuwa pia ninasumbuliwa na uhusiano wa kihisia wa kilaghai, ambao uliumiza sana afya yangu ya kiakili. Hofu yangu ya siku za baadaye ilinizidia.
Punde hisia zangu za mfadhaiko, hofu na upweke zilifanya iwe vigumu kufanya lolote. Hata mambo ya kawaida yakaonekana kutowezekana. Asubuhi moja, nilikuwa ninamwomba Baba wa Mbinguni anipe nguvu za kuimaliza siku hiyo. “Siwezi kuendelea kufanya hivi peke yangu,” niliomba. Katika wakati finyu wa uimara wa akili na hisia, maneno yalinijia akilini mwangu “Haupaswi kufanya hivyo.” Amani ilifurika akilini mwangu. Dhoruba ndani ya akili yangu ilitulia.
Miezi michache iliyofuata (na miaka) haikuwa rahisi. Hisia zangu za mfadhaiko na upweke haikuondoka mara moja. Lakini kwa mara ya kwanza, nilielewa katika kiwango changu binafsi kile ilichomaanisha kuwa na Mwokozi. Nilijua Yeye alielewa changamoto zangu na uchungu wangu. Nilijua Yeye alikuwa mtu wa pekee ambaye angenisaidia, na Yeye alifanya hivyo.
Miaka mingi baadaye, mimi sasa ni mmisionari aliyerejea, nimehitimu chuo na nina ndoa yenye furaha. Na ninajua nisingeweza kufanikiwa kwenye lengo lolote kati ya hayo kama nisingekuwa nimemtumaini Bwana.
Nyamaza, Utulie
Yesu alikuwa amelala ndani ya mashua akiwa na Mitume Wake wakati dhoruba ilipoanza. Mitume walimwamsha Yesu, wakisema, “Mwalimu, si kitu kwako kuwa tunaangamia?” (Marko 4:38). Wakati tu walipokuwa wanadhani watakufa katika dhoruba iliyokuwa inanguruma, Bwana alisimama na “kuukemea upepo na kuiambia bahari, Nyamaza, utulie. Na upepo ukakoma, kukawa shwari kuu” (Marko 4:39).
Ni mara ngapi katika maisha yako umejiuliza, “Mwalimu, si kitu kwako kuwa mimi ninaangamia?” Wakati mwingine, unapokuwa unaishi katika changamoto ngumu, inaweza kuwa rahisi kujihisi mpweke na kutelekezwa. Unaweza kujiuliza kwa nini Bwana hatulizi dhoruba zako. Inaweza kuonekana maisha yako kamwe hayatafikia ile “shwari kuu” ambayo mstari wa 39 unazungumzia.
Hata hivyo, sehemu muhimu ya hadithi hii ni ile kanuni ambayo Mwokozi aliifundisha baadaye. Yeye alisema: “Mbona mmekuwa waoga? Hamna imani bado?” (Marko 4:40). Katika ule wakati wao wa woga na mahangaiko, Mitume walikuwa wamemsahau yule waliyekuwa pamoja naye. Mwana wa Mungu, ambaye aliumba hiyo dunia, alikuwa amelala ndani ya mashua yao. Kwa nini walihofu?
Vivyo hivyo, Mwokozi anao uwezo wa kutuliza dhoruba yoyote katika maisha yako. Yeye anaweza kuponya maumivu yako, kupunguza mizigo yako na kutoa nuru wakati ukiwa gizani. Sehemu yako katika mchakato huu ni kuonyesha imani kubwa kabisa katika Yesu Kristo.
Kupata Nguvu kutoka kwa Bwana
Kuishi kwa ongezeko la imani kunaweza kuleta wingi wa nguvu za Kristo katika maisha yako. Wakati Razafimalaza kutoka Madagaska alikuwa anamaliza mwaka mgumu wa shule, shangazi yake alifariki. Yeye alifadhaika sana. Ilikuwa vigumu sana kuzingatia masomo wakati wa shule. Alikuwa anajiandaa kufanya mtihani wa mwisho wa mwaka. Alisali, “Tafadhali niondolee majonzi yangu na unipe nguvu za kufanya mtihani kesho.” Baada ya sala, Razafimalaza alihisi kuimarishwa. “Nilihisi kama nimesahau majonzi yangu,” alisema. “Mungu ananipa nguvu za kufanya jambo lolote.”
Ni muhimu kukumbuka kwamba wakati mwingine Bwana hutuliza dhoruba katika maisha yako, na wakati mwingine Yeye hukutuliza na kukufariji wewe wakati dhoruba imechafuka. Unapokuwa na imani katika Yeye, wewe pia unatumainia katika mapenzi Yake na wakati Wake. Unaamini kwamba Yeye atakusaidia, bila kujali ni lini amani na utulivu kwako hasa vitafika.
Kutumaini katika Wakati Wake
Msichana anayeitwa Ann alikuwa mzoefu wa hisia za hofu. “Mimi nina wasiwasi mwingi na tatizo kidogo la kufokasi kwenye mambo (ADHD),” alisema. “Wakati mwingine hii huniacha na hisia za kutoeleweka kwa wengine, na ni vigumu kuwa na mtazamo wa milele. Hivi karibuni nilisoma kitabu cha Mwanzo kuhusu Sara, ambaye alingojea miongo mingi kabla ya kupata mtoto. Nilitambua kwamba ningeweza kungojea muda mrefu ili kupona vizuri. Ninajua kwamba Kristo hataniacha wakati ninapopitia wasiwasi. Yeye yuko hapo kunisaidia nivuke.”
Kuchagua kumtumaini Bwana hakumaanishi utapuuza changamoto kali katika maisha yako. Hata hivyo, inamaanisha unapaswa “kufokasi kwenye ukuu usio na mwisho, uzuri na nguvu kamili za Mungu [wako], kumtumaini Yeye … kwa moyo wa furaha.”1 Unapokuwa mpweke, mwenye huzuni, mwenye wasiwasi au unasubiria baraka zilizoahidiwa, kumbuka swali hili: Je, unasubiria “shwari kuu” kwa moyo wa woga au kwa moyo wa imani?