“Kuwa Bingwa wa Kweli,” Kwa Ajili ya Nguvu Kwa Vijana, Machi 2023.
Kuwa Bingwawa Kweli
Felipe ni mmoja wa wasanii bora wa michezo ya sanaa za vita duniani kama vile karate, judo na Michezo Mseto ya Sanaa za Kijeshi (MMA). Lakini kutumikia misheni ilikuwa kipaumbele chake nambari moja.
Felipe F. Kutoka Pará, Brazil, hafananii kama kijana wa umri wa miaka 18. Yeye ameshindana katika mashindano mseto ya sanaa za vita (MMA) za kulipwa, judo na karate. Na yeye ni mzuri sana katika kile anachofanya. Ameshinda mashindano ya kimataifa ya Iron Man MMA. Yeye ni bingwa wa jimbo la Pará mara 2, bingwa mdogo wa Brazil, na bigwa mdogo wa kimataifa wa judo. Na yeye ni bingwa wa jimbo la Pará mara kumi, bingwa wa Brazil mara 10, bingwa wa Amerika Kusini, bingwa wa Amerika Nzima na bigwa wa dunia wa karate mara tatu. Waohh!
Sababu za Mafaniko Yake
Felipe amekuwa akifanya mafunzo tangu akiwa umri wa miaka saba. Lakini yeye anaamini sababu kubwa ya mafanikio yake ni Mungu. “Daima mimi nasali kwa ajili ya msaada wa Bwana,” yeye anasema.
Wakati wa mashindano yake ya mwisho ya karate ya Amerika Nzima, Felipe hakuhisi kujiamani sana. Lakini baadaye baba yake alimpa baraka ya ukuhani. “Baada ya hivyo akili yangu ikawa vyema zaidi, na hiyo ilinisaidia kushinda mashindano ya siku hiyo. Mechi mbili za mwisho nilizoshinda, nilikuwa na sekunde tu iliyobakia. Kila mtu alidhani haitowezekana! Nilifanya kitendo kisichotarajiwa ambacho kilinisaidia kushinda, kwangu mimi, yote ilikuwa kwa sababu ya baraka za baba yangu.
Baba yake alikuwa amempatia baraka nyingi kwa miaka mingi iliyopita. Felipe anajua kwamba kupokea baraka daima hakumaanishi yeye daima atashinda, lakini anaamini kwamba Bwana anaweza kumsaidia kubaki amefokasi na kuboresha vipaji vyake. “Hii hunisaidia kujiamini zaidi,” Felipe anasema. “Najua kwamba bila kujali matokeo, mkono wa Bwana ulikuwa pale.”
Watu wengine wa familia yake wamekuwa msaada mkubwa pia. Katika mchuano mmoja wa MMA, Felipe aliona familia yake kwenye mabenchi. “Wote walikuwa pale wakishangilia jina langu. Sikuwa na cha kusema.” Anaongezea, “ninawashukuru sana baba yangu na mama yangu, ambao wamenionyesha njia sahihi.”
Felipe anahisi kwamba kufuata njia hiyo kumemsaidia katika mchezo wake. Marafiki zake walikuwa wakimcheka mara nyingi alipokuwa hafanyi mambo ambayo wao walikuwa wanafanya. Lakini Felipe hajuti. “Kama vile tu injili huleta baraka, katika michezo pia huleta mafanikio! Kutokwenda kwenye starehe na marafiki zangu na kula chakula sahihi yote yamechangia katika matokeo.
Kuamua Kutumikia Misheni
Sasa kwamba yeye ana umri wa miaka 18, Felipe anazo fursa nyingi sana. Hivi karibuni alialikwa kujifunza katika chuo chenye hadhi kubwa cha MMA na ana maombi kutoka kwa mameneja kote ulimwenguni. Lakini yeye anataka kutumikia misheni kwanza.
“Kwangu mimi, hili ni chaguo rahisi,” alisema. “Bwana yu katika nafasi ya kwanza. Mengine yanaweza kusubiri, kwa sababu Yeye daima hukubariki kwa kuwa mtiifu.”
Kaka mkubwa wa Felipe, Júnior, ambaye karibuni alirejea kutoka misheni, alikuwa sehemu ya motisha. Alimwambia Felipe kwamba hakuna kilicho bora kuliko kutumikia misheni na kwamba yeye anapaswa kwenda hata kama watu wanajaribu kumshawishi asifanye hivyo.
Na Felipe amekuwa na watu wanaomwambia akae tu. Watu wengi katika familia yake kubwa sio waumini wa Kanisa. “Wao hawaelewi kwamba kutumikia misheni kuna thamani zaidi kuliko utajiri na umaarufu. Ninajaribu kufundisha injili tu nyakati hizo zinapotokea,” Felipe anasema. Na mojawapo ya nyakati hizo ziliongoza hadi kwenye tukio lenye nguvu la kimisionari.
Binamu wa Felipe alikuwa amefariki hivi karibuni na mjomba wa Felipe alikuwa anaomboleza kifo cha mwanawe. Felipe alimwambia mjomba wake kuhusu mpango wa wokovu. Baadaye mjomba wake alimkumbatia na kuomba msamaha kwa kumwambia asiende misheni. “Aliniambia kwamba nilikuwa na kipawa cha kugusa mioyo ya watu na kwamba nilihitaji kutumikia,” Felipe anakumbuka. “Ulikuwa wakati maalumu kwangu wakati mtu mmoja ambaye hakuelewa misheni ni nini alielewa madhumuni yake halisi.”
Felipe alikuwa na nyakati ambapo hakuwa na uhakika kuhusu hiyo misheni yeye mwenyewe. “Nilisoma maandiko yangu kila siku, na usiku mmoja nilikuwa na mashaka mengi kuhusu uchaguzi wangu. Nilianza kufikiria, ‘Je, napaswa kubaki na kushindana kwa muda zaidi?’ Basi kisha nikasoma katika Kitabu cha Mormoni kuhusu Wanefi waliokuwa hawana shukrani na kiburi. Yakobo aliwafundisha kwamba walihitaji kumweka Bwana kuwa wa kwanza. [Ona Yakobo 2:12–21.] Wakati huo sikuwa na shaka kuhusu chaguo langu.”
“Leo mimi najua kile ninachotaka, na ninajua kwamba nitarejea kutoka misheni na nitabarikiwa katika njia fulani. Inaweza kuwa ni kucheza MMA au kitu fulani kingine, lakini najua Mungu hutupa kile tunachohitaji.”
Nguvu ya Uongofu wa Kila Siku
Felipe hakuwa daima akihisi msisimko sana na kujiamini kuhusu misheni—au Kanisa. “Nilikuwa na wakati katika maisha yangu ambapo sikuwa imara katika injili, na daima nilihisi kama kulikuwa na kitu fulani kilichokosekana,” alisema. “Unajua mtu ambaye anaenda tu kanisani na hafanyi kitu kingine chochote? Huyo alikuwa mimi.” Baada ya kuzungumza na kaka yake na askofu kuhusu kutumikia misheni, aliamua kuanza kusali na kusoma maandiko kila siku.
“Ninafikiria kile kilichonisaidia ilikuwa ni uongofu wa kila siku. Nilikulia katika Kanisa, na kwa muda kidogo sikutafuta uongofu kwa sababu nilikulia katika nyumba iliyo na imani na nilidhani kwamba hiyo ilikuwa inatosha. Lakini sasa ninatafuta ushuhuda kila siku.”
Bingwa kwa Sababu ya Bwana
Felipe anajua kwa kuchagua kilicho sahihi haimaanishi daima atashinda au kupata mambo yaende vile anavyotaka. “Nakumbuka kwenda kwenye mashindano nikifikiria nilikuwa nimejiandaa, na nilishindwa hatua ya kwanza tu. Wakati mwingine nilipata jeraha nyumbani. Nakumbuka kuamka mapema, nikitazama darini, nikishangaa kama haya yote yalikuwa na maana kweli. Wakati mwingine nilitaka tu kugeuka na kuendelea kulala, lakini nilisimama na nikaenda kufanya mazoezi. Ili kuwa bingwa ni zaidi ya wakati wa ushindi. Ni mtu ambaye hushinda kila siku, hushinda mapungufu, hushinda majaribu.”
Mwokozi ni motisha kwa Felipe ya kushinda katika hali zote za maisha. “Kama tunataka kuwa kama Yeye alivyo, tunahitaji kufanya kile Yeye hufanya, daima kujaribu kusimama kwa uthabiti, kujiimarisha wenyewe, na kufikiria kile ambacho Yeye angefanya. Hiyo inanipa mwongozo katika matendo yangu kila siku, ili kuwa kama Yeye. Ninapoona kitu fulani ambacho ninaweza kubadili, ninasali na kuomba msamaha, nikijaribu kuwa bora daima. Bingwa wa kweli ni mtu ambaye huanguka mara nyingi na hata katikati ya kuvunjika moyo huamka na kuendelea mbele.
“Mimi ni bingwa kwa Sababu ya Bwana,” Felipe anasema. “Kama haikuwa kwa sababu Yake, sijui ningekuwa wapi. Lakini nina hakika nisingelikuwa na haya yote niliyonayo leo. Kuishi injili kumenifanya mimi kuwa bingwa katika maisha na katika michezo.”