Jinsi Ninajua
Mwaliko Wangu kwa Wokovu
Kama kijana, nilitembelea makanisa mengi na nilichanganyikiwa kwa sababu kila moja lilifundisha ufafanuzi tofauti wa maandiko. Sikuhisi vizuri kuhusu utovu wa heshima niliopata katika baadhi yao, hivyo basi nikaacha kujaribu kutafuta kanisa la kuhudhuria.
Miaka kadhaa baadaye rafiki yangu, Cleiton Lima, alibatizwa katika Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Sikuza Mwisho. Hakunielezea haya hata vile tulivyokuwa marafiki wazuri, lakini muda ulivyoendelea, nilianza kuona mabadiliko ndani yake. Siku za Jumapili kwa kawaida nilienda nyumbani kwake asubuhi ili tuweze kucheza kandanda, lakini kamwe singempata nyumbani. Hii ilitokea Jumapili mbili au tatu mfululizo. Mwishowe Cleiton aliniambia kuwa hangeweza kucheza Kandanda tena Jumapili kwa sababu alikuwa akiheshimu siku ya Bwana. Nilimwambia, “Kanisa hili linakufanya uwe zuzu.”
Kisha Cleiton akanialika kuhudhuria kanisa. Nilimpa udhuru kwa sababu nilikuwa bado sijihusishi na dini. Kwa miezi 10, Cleiton aliwaleta wamisioari kunifundisha, lakini daima nilitoa sababu au kuwaambia kuwa nilikuwa na shughuli sana. Lakini kamwe hakufa moyo.
Siku moja Juni, alinialika nihudhurie ngoma Kanisani. Nilimkejeli, “Je, kutakuwa na chakula ya bure na wasichana wengi?” Akicheka, alisema ndiyo!
Lazima nikubali kuwa nilishindwa na tumbo langu. Nilitembelea kanisa na kulipenda. Nilikaribishwa na kila mtu, nilikula sana, na nikawa na nia ya kuhudhuria mkutano. Nilipofika kanisani Jumapili, nilikutana na watu wengi na kusikia ushuhuda wao. Sikuwa na ufahamu wa Kitabu cha Mormoni, lakini nilihisi Roho wa Bwana wakati washiriki mbalimbali wa Kanisa walishuhudia, “Najua kwamba Kitabu cha Mormoni ni kweli, kwamba hili ni Kanisa la Yesu Kristo, na kwamba Joseph Smith alikuwa nabii aliyeitwa na Mungu.” Nikuwa kamwe sijahisi vizuri kama hivi. Bado sikutaka kukutana na wamisionari, lakini mkutano huo wa ushuhuda ulinigusa.
Wiki iliofuata, Cleiton alinialika tena kwenda kanisani. Sikuweza kwa sababu nilikuwa na wajibu mwingine. Ningeona huzuni usoni mwake nilipomwambia sikujua kama ningeweza kwenda.
Hata hivyo, siku ya Jumapili asubuhi niliamka na hamu ya kwenda kanisani Niliamka saa 12:50 asubuhi, ambayo ilikuwa ni vigumu kwangu, na nilijitayarisha na kusubiri Cleiton aje. Alishangaa aliponiona nimevaa na nikisubiri. Jumapili hiyo Askofu alifundisha kuhusu ukuhani. Nilihisi Roho sana na nikawa na hisia kwamba nilipaswa kuchukua masomo ya wamisionari. Mwishoni mwa mkutano ya Wavulana, nilijua kwamba nitabatizwa.
Kanisa lilipomalizika, nilimuambia Cleiton, “Nataka kubatizwa!”
Alidhani nilikuwa na utani. Lakini, kisha akasema, “Nikiwaita wamissionari, je, utakutana nao?” Nilimjibu ndiyo.
Nilifundishwa na wamissionari wazuri. Niliposikia ujumbe wa Urejesho, nilipata uthibitisho hata zaidi kwamba nilifaa kubatizwa. Lakini nilitaka kujijulia mwenyewe ukweli wa Kitabu cha Mormoni. Wamisionari waliweka alama Moroni 10:3–5 katika Kitabu cha Mormoni changu na wakaniaalika kuomba na kuuliza Mungu kama ni kweli.
Jioni iliyofuata nilikumbuka kuwa bado sikuwa nimesoma Kitabu cha Mormoni. Nilipoanza kusoma, nilihisi roho kwa nguvu sana. Niliomba, na kabla nimalize, nilijua kwamba Kitabu cha Mormoni ni kweli. Namshukuru Mungu kwa kujibu maombi yangu. Nilibatizwa mnamo Julai 2006.
Baadaye nilihudumu kama mmisionari katika Misheni ya Brazil Cuiaba, na rafiki yangu Cleiton akahudumu katika Misheni ya Brazil Santa Maria. Tulifanya kile ambacho Cleiton alinifanyia: kuwaalika watu kumjia Kristo na kuwasaidia kupokea injili ya urejesho kwa kufanya imani katika Yesu Kristo, kutubu, kubatizwa, na kupokea kipawa cha Roho Mtakatifu. Hii kwa kweli ndio njia ya wokovu.
Daima tuwaalike marafiki zetu na jamaa kujifunza Injili hii, kwa kuwa Mwokozi alimwalika kila mtu aliposema, “Njoni kwangu” (Matthew 11:28). Najua kuwa hili ni Kanisa la Yesu Kristo na kwamba sasa ndio wakati wa kumkaribisha kila mtu kuja Kwake.