Kanisa kwa ajili ya Zulma
Pengine kulikuwa na zaidi ambayo Mungu alitaka Zulma aelewe.
“Tafuteni, na mtapata” (3 Nefi 14:7).
Zulma aliketi kwenye mojawapo ya benchi za Kanisa na kunyoosha sketi ya sare zake za shule. Mwangaza wenye rangi tofauti uling’aa kupitia madirisha yenye vioo vya rangi, na msalaba ulisimama mbele ya kanisa. Zulma alisomea katika shule ya kanisa, kwa hivyo alihudhuria ibada mara mbili kwa siku pamoja na wanafunzi wengine. Zulma alipenda Kanisa. Alimpenda Yesu na alipenda kujifunza juu Yake.
Aliketi kwa utulivu wakati kasisi alipoanza kuzungumza. Lakini leo alihisi kitu tofauti. Ghafla wazo jipya lilimjia akilini na moyoni mwake: Kuna ukweli zaidi huko nje.
Zulma alijikuna nyusi. Ukweli Zaidi? Hilo lilimaanisha nini?
Wazo likaja tena. Kuna ukweli zaidi.
Zulma alifumba macho na kufokasi kwenye kile alichokuwa akihisi. Alikuwa amejifunza vitu vingi vizuri kanisani. Lakini sasa alijiuliza kama kuna kitu kilichokuwa kinakosa. Pengine kulikuwa na zaidi ambayo Mungu alimtaka afahamu. Lakini angewezaje kuyapata?
Baadaye alizungumza na kaka yake mkubwa, Alberto, kuhusu mawazo yake.
“Unafikiri kuna ukweli zaidi huko nje?” Alberto aliuliza.
Zulma aliitikia kwa kichwa. “Ninataka kujifunza kuhusu makanisa mengine,” alisema.
“Sawa,” Alberto alijibu. “Niteanda pamoja nawe!”
Kwa miaka kadhaa, Zulma na Alberto walitembelea makanisa tofauti. Baada ya ibada katika kanisa moja, Alberto alisema, “Lile Kanisa lilifundisha mambo mazuri.”
Zulma alikubaliana naye, lakini bado walihisi kuna kitu kilikosekana, kwa hivyo waliendelea kutafuta.
Siku moja Alberto alikimbia juu ya ngazi kuelekea nyumbani kwao. “Nimelipata kanisa tulilokuwa tunalitafuta!” Alberto alisema. Alimkumbatia Zulma.
Macho ya Zulma yalifunguka wazi kabisa. “Wapi? Kivipi?
“Rafiki yangu alikutana na wamisionari kutoka Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho,” Alberto alisema. “Niliwasikiliza, na ninaamini kile walichofundisha!”
Zulma na Alberto walikuwa na furaha kubwa kwamba walidensi kuzunguka nyumba. Lakini Zulma akapata habari mbaya. Mamá hakutaka akutane na wamisionari. “Una miaka 12 tu,” Mamá alisema. “Wewe ungali mdogo sana.”
Kwa sababu Alberto alikuwa mkubwa, alikubaliwa kuendelea kukutana na wamisionari. Wiki chache baadaye, alibatizwa.
Zulma aliendelea kumuuliza Mamá tena na tena kama angeweza kujifunza kutoka kwa wamisionari. Hatimaye, Mamá alisema sawa.
Wakati wamisionari walipomfundisha Zulma, alihisi joto moyoni mwake. Mmoja wa wamisionari alikuwa na wakati mgumu kuzungumza Kihispania, lakini hilo halikuwa hoja. Cha muhimu ilikuwa ni jinsi alivyohisi Zulma. Wakati alipojifunza kuhusu Joseph Smith na Kitabu cha Mormoni, alijua alikuwa amepata ukweli aliokuwa akiutafuta!
Zulma alitaka kubatizwa. Lakini Mamá angesema nini? Zulma alifurahia sana wakati Mamá aliposema sawa! Siku ya kubatizwa kwake, Zulma alivalia mavazi meupe. Alijua Mungu Alimpenda. Alijua Alimfahamu. Na alijua kwamba alikuwa amemsaidia kupata Kanisa Lake lililorejeshwa! ●