2020
”Tazama Kile Imani Ndogo Inachoweza Kufanya?”
Aprili 2020


”Tazama Kile Imani Ndogo Inachoweza Kufanya?”

Godfrey J. Ellis

Washington, Marekani

family caught in rainstorm

Kielelezo © Gary Alphonso, i2iart.com

Kitambo kidogo, mimi na mke wangu tulisafiri na wana wetu wawili wadogo kwenda Ufaransa kutembelea maeneo ambayo nilikuwa nimetumikia kama mmisionari. Tulitembelea matawi ya Kanisa ambapo nilikuwa nimetumikia na kufurahia na waumini ambao niliwafundisha. Pia tulitembelea maeneo ya kihistoria.

Eneo moja lilikuwa mahame ya Château de Châlucet. Kasri hili la kale lilishambuliwa na kuharibiwa pakubwa karne nyingi zilizopita. Mimea ilikuwa imemea kuzunguka mahame hayo, na njia ya kufika pale ilikuwa imesonga na yenye mwinuko mkali. Tulikuwa na wakati mgumu kukwea, lakini ilitosheleza juhudi zetu mara tulipowasili.

Wavulana walifurahia kushuka katika kile kilichokuwa kwa wakati mmoja gereza la chini ya ardhi na juu kabisa kwenye kile kilichokuwa kimesalia kwenye kuta za kasri. Kasri hilo lilichangamsha fikra zao jinsi tu lilivyokuwa limefanya kwangu miaka 24 kabla.

Wakati tulipokuwa huko, dhoruba ya majira ya jua ilitokea kwa mbali. Ilikaribia kwa kasi. Mawingu meusi na radi vilitanda angani, na kufuatiwa na milio mikubwa ya ngurumo.

Tulikimbia kulielekea gari huku dhoruba ikisonga kwa kasi upande wetu. Punde, mbubujiko, mkali wa mvua ulitulowesha na njia ikageuka kuwa tope. Tulikuwa na wasiwasi kwamba tungepoteza mwelekeo na kuanguka chini ya mteremko mkali, wa mawe.

Tuliona kimbilio fulani kwenye miti pembeni mwa njia. Tulijibana pamoja chini ya kimbilio na kuwaza ingechukua muda kiasi gani kusubiri kushuka chini.

“Acha tusali,” mwana wetu mdogo alisema.

Alijitolea kusali na akasali kwamba mvua ingetulia ili tuweze kushuka chini ya mlima kwa usalama. Alitutazama na kusema, “Sasa kile tunachohitaji sana ni imani ya kutosha.”

Nilieleza kwamba sala huwa hazifanyi kazi siku zote kwa namna hiyo.

“La,” alisema, “itatulia kwa takriban ndani ya dakika 10!”

Baada ya takriban dakika 10, mvua ilitulia.

“SAWA, twendeni!” alisema.

“Kama tutaondoka sasa hivi, mvua itaanza tena na tutazuiliwa,” mwana wetu mkubwa alisema.

“Hapana!” mdogo alijibu. “Twendeni!”

Tulipita katika sehemu za njia zilizokuwa zimekauka, tukishikilia vichaka na matawi tulipokuwa tukisonga. Karibu na gari, tulisali kutoa shukrani. Punde, mvua ilianza tena.

“Unaona kile imani ndogo inachoweza kufanya?” mwana wetu alisema kwa unyenyekevu.

Alitufundisha somo kuu siku hiyo.