Ndege Mdogo Alinikumbusha
Laura Linton
Utah, Marekani
Nilikuwa na miaka 26 wakati mimi na mume wangu tulipompoteza mtoto wetu wa kwanza. Kennedy aligunduliwa kuwa na uvimbe wa ubongo wakati alipokuwa na umri wa miezi 13 tu. Baada ya upasuaji mara tatu, mifululizo mitano ya tibakemikali, na madawa mengi na matibabu, aliaga dunia mikononi mwetu akiwa na umri wa miezi 20.
Nilivunjika moyo kumpoteza msichana wangu mdogo, mrembo, mwenye ari ya kujua, na mwenye nguvu. Ni kwa jinsi gani hili lilitokea? Ningewezaje kusonga mbele? Nilikuwa na maswali kadhaa, lakini sikuwa na majibu yoyote. Siku chache baada ya mazishi, mimi na mume wangu tulitembelea eneo la kaburi, lilikuwa bado limefunikwa na maua na utepe wa rangi ya waridi kutoka kwenye mazishi.
Nilipokuwa nikifikiria juu ya binti yangu, nilimwona ndege mdogo sana, mchanga asiyeweza kupaa, akirukaruka juu ya nyasi. Ndege huyu alinikumbusha kuhusu Kennedy kwa sababu alipenda wanyama. Ndege huyo alirukaruka juu ya kaburi na kucheza kwenye utepe na maua. Nilitabasamu, nikifahamu hivi ndivyo Kennedy angetaka. Ndege huyo kisha alirukaruka na kunikaribia. Sikuthubutu kusonga. Ndege huyo mdogo alirukaruka karibu nami, akaulalia mguu wangu, akafumba macho, na kulala.
Ni vigumu kwangu kueleza hisia nilizokuwa nazo kwa wakati huo. Nilihisi kana kwamba nilikuwa nikikumbatiwa na Kennedy. Nisingeweza kumkumbatia binti yangu, lakini ndege huyu mdogo—kiumbe cha Baba wa Mbinguni—kingeweza kupumzisha kichwa chake juu yangu, kunikumbusha kwamba Baba wa Mbinguni alielewa uchungu wangu na siku zote angekuwepo kuja kunifariji na kunisaidia katika majaribu haya.
Mzee David A. Bednar wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili alisema, “Wakati ambapo maneno hayawezi kutupa faraja tunayohitaji … , wakati mantiki na akili haviwezi kuleta uelewa wa kutosha kuhusu udhalimu na kutokuwa sawa katika maisha, … na wakati inaonekana kwamba labda tuko peke yetu kabisa, kwa kweli tunabarikiwa na neema nyororo ya Bwana” (“Neema Nyororo za Bwana,” Liahona, Mei 2005, 100).
Bado sikupata majibu ya maswali yangu yote, lakini neema hii nyororo ilinihakikishia kwamba mimi na Kennedy wote tunapendwa na Baba wa Mbinguni na kwamba kupitia dhabihu ya upatanisho ya Mwana Wake, Yesu Kristo, nina tumaini kwamba Kennedy, mume wangu, na mimi siku moja tutakuwa pamoja tena kama familia.