Familia ya Milele ya Alonso
“For the temple is a holy place where we are sealed together” (Kitabu cha Nyimbo za Watoto, 95).
“Naweza kuwa na Mamá na Papá tena?”
“Pasaka ni wakati mzuri wa kufikiria kuhusu Yesu na kukumbuka Ufufuo Wake,” Dada Rojas alisema. Alishikilia juu picha ya Yesu. “Kwa sababu Yake, watu waliofariki wataishi tena.”
Alonso aliinua kichwa chake wakati mwalimu wake wa Msingi aliposema hivyo. Je, hiyo inamaanisha kwamba naweza kuwaona wazazi wangu tena? Alonso aliwaza.
Mamá alifariki miaka mingi iliyopita. Alonso hakumkumbuka vizuri, lakini alipenda kuona picha zake. Kisha Papá akafariki pia.
Sasa Alonso aliishi na Abuela, bibi yake. Alikuwa anamfundisha kuhusu Kanisa lake, Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho. Angebatizwa na kuthibitishwa mwaka ujao, wakati ambapo angefikisha umri unaofaa.
Kisha Dada Rogers akashikilia juu picha ya jengo jeupe. “Zawadi nyingine ya kupendeza kutoka kwa Yesu Kristo ni mahekalu. Hili ni mojawapo ya mahekalu hapa Chile.”
Alonso alitazama sanamu ya dhahabu juu ya jengo. Ilikuwa ya kupendeza! Aliwaza ni nini kinafanyika ndani yake.
“Mahekalu ni mahali familia zinapounganishwa milele,” Dada Rojas alisema. “Hekalu hili kule Santiago ni mahali nilipounganishwa na wazazi wangu baada ya kujiunga na Kanisa. Kwa sababu tuliunganishwa, naweza kuwa nao hata baada ya maisha haya.”
Alonso alisisimka wakati aliposikia hilo. “Naweza kuunganishwa na wazazi wangu?” aliuliza. “Hata kama tayari wameaga dunia?”
Dada Rojas aliitikia kwa kichwa. “Ndiyo! Hiyo ndiyo mojawapo ya sababu ya mahekalu kuwa muhimu sana. Yanawabariki wanafamilia wetu wote, ikiwa ni pamoja na wale ambao wameaga dunia.”
Kwa muda uliosalia kwa siku hiyo, Alonso aliendelea kufikiria juu ya mahekalu. Alimuomba Abuela amfundishe zaidi. Alizungumza kuhusu mavazi meupe ambayo watu huvalia ndani na kazi ya sanaa ya kupendeza kwenye kuta.
“Kizuri zaidi ya yote, ni mahali ambapo unaweza kuunganishwa na wazazi wako,” Abuela alisema. “Tutawaomba watu wawili kutoka katika kata kuwawakilisha wakati wa kuunganisha.”
“Tunaweza kwenda kesho?” Alonso aliuliza. “Nataka kuwa na Mamá na Papá milele!”
Abuela alitabasamu. “Nina furaha unataka kwenda,” alisema. “Lakini hekalu lililo karibu nasi ni Concepción. Hatuna hela za kutosha kwa ajili ya tiketi za basi.”
“Nitasaidia kuweka akiba kwa ajili ya safari!” Alonso alisema.
Kuanzia hapo, wakati wowote Alonso alipopata senti mtaani au kupata nafasi ya kupata pesa, alilipa zaka na kisha kuongeza zilizobaki kwenye hazina yao ya hekaluni.
Baada ya miezi mingi ya kuweka akiba, Alonso na Abuela hatimaye walikuwa na hela za kutosha kusafiri kwenda hekaluni. Waliwaomba Kaka na Dada Silva kwenda nao. Siku ya safari, walisafiri kwa muda mrefu wakitumia basi kwenda katika jiji la Concepción. Ilikuwa inakaribia machweo wakati Alonso alipoona kitu chenye rangi ya dhahabu kwa mbali.
“Naweza kumuona malaika Moroni!” Alonso alisema, akionesha sanamu iliyokuwa juu ya paa la kuba lenye rangi ya samawati.
Walilala katika ghorofa iliyokuwa kando ya hekalu. Asubuhi, Alonso aliingia ndani ya hekalu kwa mara ya kwanza. Aliona picha kubwa ya Yesu ndani. Yeye na abuela walivalia mavazi meupe. Alihisi furaha na amani.
Ilipowadia wakati wa kuunganishwa, Alonso aliingia ndani ya chumba kizuri kilichopambwa kwa vioo kwenye kuta. Mhudumu wa hekaluni alimwonesha Alonso, Abuela, na kina Silva jinsi ya kupiga magoti wakizunguka meza maalum inayoitwa madhabahu. Ilikuwa imefunikwa kwa kitambaa laini.
Kaka na Dada Silva walikuwepo kwa niaba ya mama na baba wa Alonso. Abuela alikuwepo kwa niaba ya dada yake aliyeaga dunia kabla ya Alonso kuzaliwa.
Akiwa amefumba macho yake, Alonso alipata taswira ya familia yake ikiwa pamoja.
Siwezi kungoja kuwaona tena, Alonso aliwaza. Nina shukrani sana kwamba familiia zinaweza kuwa pamoja milele! ●