Kidijitali Pekee: Vijana Wakubwa
Je, Unafikiri Huna Lengo kama Kijana Mkubwa? Fikiria Tena
Kufikiria kuhusu kuongoza katika Kanisa siku moja kunaweza kuogopesha, lakini kuna njia unazoweza kuanza kuongoza sasa.
Siku kabla ya Ujio wa Pili wa Yesu Kristo, kutakuwa na “vita, na uvumi wa vita.
“… Taifa litainuka dhidi ya taifa, na ufalme dhidi ya ufalme; hapo patakuwa na njaa, na maradhi, na matetemeko ya ardhi, mahali mbali mbali.
“Na tena, kwa sababu uovu utaongezeka, upendo wa watu utapoa” (Joseph Smith—Mathayo 1:28–30).
Katikati ya machafuko kama haya, ni nani atasaidia kuwaongoza kaka na dada zetu, wote ndani na nje ya kundi, kurudi kwa Baba yetu wa Mbinguni?
Hapo ndipo tunapoingilia.
Jinsi Tunavyopaswa Kuongoza
Tumeitwa moja ya vizazi vikubwa vya vijana wakubwa. Rais Russell M. Nelson alituelezea sisi kama wale “ambao Mungu aliwaamini vya kutosha kuwatuma duniani wakati wa kipindi kizuri zaidi katika historia ya ulimwengu huu” (“Stand as True Millennials,” Liahona, Okt. 2016, 46).
Kwa hivyo, tunawezaje kuishi kulingana na uwezo wetu wa kuwa viongozi shupavu katika Kanisa la Bwana? Basi, ikiwa utatazama huku na huko, unaweza kugundua kwamba wewe tayari ni kiongozi kwa njia moja au nyingine.
Unaweza kuongoza katika wito wa Kanisa. Kama mmisionari, unaweza kuongoza majadiliano, kuwa msimamizi wa shughuli ya ufundishaji injili, au kupewa majukumu kuongoza kama kiongozi wa kanda au wa akina dada. Unaweza kuwa kiongozi katika familia yako au miongoni mwa rafiki zako. Unaweza kuwaongoza mababu zako kwenye ukombozi kupitia kazi ya historia ya familia. Unaweza kuwa hata kiongozi wa kisiasa, na unaweza daima kuongoza katika kazi yoyote unayochagua.
Lakini swali ni, ni kwa namna gani yatupasa kuongoza? Mwokozi aliongoza kupitia mfano Wake. Aliongoza kwa “Njoo, unifuate” badala ya “Njia yangu ni bora zaidi.” Alihudumu, alifundisha, aliwapenda, na kuwajali wale waliomzunguka. Yesu Kristo ni mfano bora wa kiongozi. Na ili kuwa kizazi shupavu cha viongozi, tunaweza kuanza kwa kujitahidi kuwa kama Mwokozi na kwa kufanya mambo haya madogo:
-
Omba kwa ajili ya wanaotaabika, wanaohitaji msaada, au juu ya wale unaowajibika kwao, na tafuta kujua jinsi ya kuwasaidia. Omba juu yao kwa jina kama watu binafsi, kama vile Mwokozi alivyohudumia, “mmoja mmoja” (3 Nefi 11:15).
-
Chukua muda kupekua maandiko hasa kwa ajili ya mifano mizuri ya uongozi, hususani kutoka kwa Mwokozi Mwenyewe.
-
Omba kwa ajili ya kata yako, kigingi, na viongozi wakuu wa Kanisa. Pia omba kwa ajili ya viongozi wa serikali, ili waweze kuvuviwa na kufanya kazi kwa roho ya amani na umoja.
-
Pata kuwajua wale wanaokuzunguka. Tafuta kujua juu ya matamanio yao, familia zao, masomo yao, na nia zao na hisia katika maisha (ona Waefeso 2:19).
-
Soma baraka zako za baba mkuu na tafakari jinsi unavyoweza kuwa bora mwenyewe.
Tunapofanya bidii ya kuongoza kwa haki, tunakuwa wanafunzi wa kweli na wafuasi wa Yesu Kristo na kustahili ushirika wa Roho Mtakatifu. Tunapofanya na kuheshimu maagano matakatifu, tunayo haki ya kupokea maandalizi muhimu na silaha za kiroho ili kwenda vitani dhidi ya adui.
Unaweza Kuanza Sasa
Je, wewe utakuwa kiongozi wa aina gani? Au, kumnukuu Mwokozi, “unapaswa kuwa [kiongozi] wa aina gani? Amin nawaambia, hata vile nilivyo” (3 Nefi 27:27).
Tukiwa tunakaribia Ujio wa Pili, Bwana atahitaji viongozi waadilifu zaidi ambao watamfuata nabii Wake na kujiandikisha kwenye vita hii. Anatuhitaji sisi. Tupo katika saa ya 11, na tuna mambo mengi ya kufanya. Tunaweza kuanza kujiandaa kuwa kizazi shupavu cha viongozi sasa. Hatujachelewa sana kuanza! Kama kuna vitu ambavyo unataka kuongea na askofu kuvihusu, anaweza kukusaidia kwenye njia ya toba. Ikiwa unahitaji mwongozo wa jinsi ya kujiboresha, anza kwa kuboresha uhusiano wako na Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo; Wanaweza kukuonesha mahali pa kwenda kutoka hapo. Wewe na mimi tumeitwa sasa kufanya kazi ya Bwana na kumsaidia nabii wetu kuiongoza nyumba ya Israeli kwenye usalama, na kama tunajaribu kufanya kwa uwezo wetu wote, tutafanikiwa.