Mkutano Mkuu Miaka yote
Sasa katika mwaka wake wa 190, mkutano mkuu ni desturi ya kudumu kila Aprili na Oktoba, lakini kumekuwa na mabadiliko ya kupendeza katika miaka iliyopita:
-
1830
Miezi miwili baada ya Kanisa kuanzishwa, Joseph Smith alisimamia mkutano mkuu wa kwanza kule Fayette, New York. Takribani waumini 30 na wengine kadhaa walihudhuria.
-
1850
Deseret News ilichapisha ripoti ya kwanza kamili ya mkutano kwa sababu mwanahabari kijana, George D. Watt, alikuwa ameweza kuandika muhtasari wa hotuba kwa kifupi.
-
1867
Mkutano mkuu ulidumu kwa muda wa siku nne badala ya siku tatu kama kawaida kwa sababu mkusanyiko ulipiga kura kuendelea kuwepo kwa siku moja zaidi.
-
1924
Mikrofoni zilitumika kwa mara ya kwanza kwenye mimbari ndani ya Tabenako. Awali, wanenaji walitegemea nguvu ya sauti zao ili waweze kusikika.
-
1949
Kwa kutumia kamera ndani ya Tabenako, mkutano kwa mara ya kwanza ulioneshwa kwenye televisheni.
-
1962
Hotuba zilifasiriwa katika lugha tofauti—Kijerumani, Kiholanzi, na Kihispania—kwa mara ya kwanza ndani ya Tabenako. Sasa hotuba zinafasiriwa katika zaidi ya lugha 90!
-
1967
Mkutano mkuu ulioneshwa kwenye TV kwa rangi. Wanaume wa Kwaya ya Tabenako walivalia makoti ya rangi ya samawati, na wanawake wakavalia blauzi za rangi ya salmoni.
-
1977
Ukibadilika kutoka siku tatu na vikao sita vikuu, mkutano ulichukua muda wa siku mbili na kujumuisha vikao vitano vikuu.
-
2000
Kituo kipya cha Mikutano Jijini Salt Lake, chenye uwezo wa kuchukua idadi ya watu 21,000 walioketi, kilikuwa mwenyeji wa mkutano mkuu kwa mara ya kwanza.