Mitume Hushiriki Jumbe za Matumaini
Viongozi wa Kanisa hutoa umaizi kuhusu kukaa karibu na Mungu, kuhudumia kwa upendo, na kwa uvumilivu kusonga mbele wakati wa janga kubwa.
Katika kukabiliana na kusambaa kwa virusi duniani kote, mamlaka huzuia mikusanyiko ya hadhara na kutekeleza zuio la kukaa ndani. Shule hufungwa, viongozi wa kiroho hufuta mikutano ya kanisa, na wale ambao hutembea nje hutakiwa kuvaa barakoa kwa ajili ya kujikinga.
Mwaka ni 1919, na janga la homa ya mafua ambalo lilianza mwaka mwaka mmoja kabla litachukua makumi milioni ya maisha.1 Nabii mpya wa Kanisa, Rais Hebert J.Grant(1856-1945), alitengwa Novemba 1918 ila hakuweza kuidhinishwa mpaka June1919 kwa sababu mkutano mkuu wa Aprili uliahirishwa.
Wakati wa huduma yake kufuatia hayo na siku nyingine za changamoto, Rais Grant alitoa ushauri unaoendana na siku zetu aliposema, “Tulikuja katika dunia hii kupata maarifa, hekima na uzoefu, kujifunza masomo, kupata maumivu, kuvumilia majaribu, na kupata ushindi wa maisha ya kimwili.” Kutoka kwenye maarifa aliyoyapata kupitia majaribio makali ya uzoefu binafsi, aliongeza, “Mimi … najua kwamba katika saa ya dhiki Watakatifu wa siku za Mwisho wanafarijiwa na kubarikiwa na kupozwa kuliko ilivyo kwa watu wengine!”2
Katika “saa yetu ya dhiki” ya sasa” pamoja na riwaya ya virusi vya korona, tunapata faraja na tulizo kutoka kwenye injili ya urejesho ya Yesu Kristo. Ufahamu wetu kwamba Baba yetu wa Mbinguni anawapenda watoto Wake na kwamba ameita manabii na mitume katika nyakati zetu kutuongoza kupita katika mawimbi ya maisha ya kimwili ni baraka kubwa.
Kutoka kwenye ushauri uliotolewa wakati wa mahojiano ya hivi karibuni, washiriki kadhaa wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili wanatukumbusha kuwa tunaweza kuhisi shangwe na kutazamia siku zijazo kwa tumaini bila kujali kinachotokea kwetu.3
Kazi Inasonga Mbele
Mzee Bruce R. MacConkie (1915-85) aliwahi kulilinganisha Kanisa na “msafara mkubwa” unaosonga mbele bila kujali upinzani.4 Mzee David A.Bednar anachukulia nguvu thabiti za msafara unaosonga mbele na maandalizi ya kiuvuvio ya Kanisa pamoja na historia yake kwenye dhiki.
“‘Mikono isiyo safi haiwezi kuzuia kazi hii kutoendelea,’5 na wala hakuna janga la ulimwengu litazuia hii kazi kutoendelea,” alisema. “Katikati ya changamoto zote tunazokabiliana nazo sasa tukipambana na hivi virusi, kazi inasonga mbele. … Hatujui itachukua muda gani, lakini tutashinda. Na tunaweza tusirudie mfumo wetu wa awali wa maisha kama tulivyoufahamu, lakini mengi ya marekebisho hayo na mabadiliko yatakuwa ni chanya mno.”
Mzee Quentin L. Cook alisema maandalizi ya uvuvio ya Kanisa yanajumuisha mifano katika wakati muafaka kama mkazo katika maadhimisho ya siku ya Sabato, kuimarisha akidi za Ukuhani wa Melkizedeki na Muungano wa Usaidizi wa AKina Mama, kuhamia katika kuhudumu, na kuanzishwa kwa Njoo,Unifuate, video za Kitabu cha Mormoni, na programu za watoto na vijana.
“Tutaangalia nyuma katika hili kama nyakati za msingi za maandalizi na siyo kama kitu tulichopaswa kuvumilia,” alisema.
Mzee M. Russell Ballard, Kaimu Rais wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili, anakubaliana nalo. Licha ya kufungwa kwa mahekalu na nyumba za ibada kwa muda, waumini wa Kanisa wana zana za kiroho wanazozihitaji ili kuendelea kusonga mbele.
Rais Ballard anakumbuka alivyohisi alipokuwa akirudi nyumbani kutoka Kanisani mnamo Desemba 7,1941, na kukuta kwamba Pearl Harbor imevamiwa na kwamba Marekani ilikuwa karibu kuingia katika Vita Kuu ya Pili ya Dunia. Kama watu wengi leo, alihofu kuhusu nyakati zijazo na kuona shaka kama kesho yake ingepotea.
“Ila hicho sio kilichojitokeza,” alisema. Kama watu huru wa dunia walivyoshinda hiyo vita, ndivyo dunia itakavyoshinda vita dhidi ya virusi vya korona. “Kila kitu kitakuwa sawa kadiri tunavyogeuza mioyo yetu kwa Baba yetu wa Mbinguni na kumtegemea Yeye na Mwokozi kama Mkombozi wa wanadamu wote,” alisema.
Njia nyingine ambayo Kanisa husonga mbele ni kupitia juhudi zake za umisionari, ambazo huendana na mabadiliko ya hali za dunia. Mzee Dieter F. Uchtdorf alisema kwamba viongozi wa Kanisa wamekuwa wakijifunza njia mpya za kushiriki injili hata kabla ya COVID-19 kuanza kuharibu kazi ya umisionari. Uharibifu huo umejumuisha kusafirisha maelfu ya wamisionari kurudi nchini mwao, kuwapumzisha wengine mapema, na kuwapangia wengine upya.
COVID-19 iliongeza uwezo wetu wa kufikiri kuhusu hili kwa kiasi kikubwa na kufumbua macho yetu,” alisema. Matokeo yake, teknolojia na mitandao ya kijamii sasa vinafungua milango ambayo hapo awali ilikuwa imefungwa na jamii zilizojifungia na nyumba zisizofikika na majengo ya ghorofa.
“Kazi ya Umisionari itaendelea kusonga mbele bila kujali janga la ugonjwa,” Mzee Uchtdorf aliongeza. “Tunaendelea kujifunza namna ya kuboresha kazi ya umisionari kwa sasa na kwa siku zijazo. Bwana ameahidi kuharakisha kazi Yake kwa ajili ya baraka za watoto wote wa Mungu (ona Mafundisho na Maagano 88:73). Nahisi kwamba tuko sahihi katikati ya mchakato huu wakati tunaishi katika wakati huu wa changamoto. Wamisionari wetu wa thamani ni watangulizi wa siku zetu, wakitoa mwanga wa kushiriki jumbe za injili katika njia mpya zinazoendana na hali yetu ili kwamba Kanisa la Yesu Kristo liendelee kusonga mbele, mpaka lijaze dunia yote’” (Mafundisho na Maagano 65:2).
Nafasi mpya za kushiriki injili sio tu vitu vipya vinavyofunguka. Mioyo inafunguka pia kwa sababu nyakati ngumu mara nyingi huwanyenyekeza watu na kuwageuza kumwelekea Mungu, alisema Mzee D. Todd Christofferson.
“Taratibu mawazo yao hufunguka, ‘Huenda nahitaji kitu zaidi ya akaunti yangu ya benki. Huenda kuna zaidi kwenye maisha kuliko kile ambacho nimekuwa nikiishi,’” alisema.
Mzee Christofferson anawahimiza waumini wa Kanisa kutafuta fursa za kimisionari, kama kushiriki jumbe zinazohusiana na injili na dhana kupitia mitandao ya kijamii, kuwasiliana na wamisionari wa kudumu kuhusu kuwa rafiki wa watu wanaowafundisha kwa mtandao, na kuwa karibu na wale ambao hawawezi kuwaona mara kwa mara.
Kujitenga Kijamii na Kujitenga Kiroho
Njia nyingine ambayo kanisa linasonga mbele ni kupitia mwitikio wa kiroho wa Watakatifu Wa Siku za Mwisho kwa changamoto za muda kama COVID-19. Kwa ajili ya ulinzi wa miili yetu, tunaongeza umbali wetu kutoka kwa wengine, ila kwa ulinzi wa roho zetu, tunasogea karibu na Baba yetu wa Mbinguni na Mwanae. Janga la COVID-19 limewapa waumini wengi wa Kanisa fursa nyingi za kuongeza ulinzi wao wa kiroho kwa kufuata ushauri wa Rais Russell M.Nelson wa kumsikiliza Bwana.
“Baba Yetu anajua kwamba pale tunapokuwa tumezingirwa na mashaka na woga, kitakachotusaidia hasa ni kumsikiliza Mwana Wake,” Rais Nelson alisema wakati wa mkutano mkuu wa Aprili 2020. Aliongeza, “Tunapotafuta kuwa wafuasi wa Yesu Kristo, jitihada zetu za kumsikiliza Yeye zinatakiwa ziwe za dhati zaidi. Inahitaji juhudi za kujitambua na thabiti ili kujaza maisha yetu ya kila siku kwa maneno Yake, mafundisho Yake, kweli Zake.”6
Wakati hatukaribishi kusimamishwa kwa mikutano ya Kanisa, kufungwa kwa mahekalu, au kupoteza ajira, kutumia muda mwingi nyumbani hutupatia “nafasi ya kufikiri kuhusu kuamka katika Mungu” (ona Alma 5:7), alisema Mzee Cook. “Labda matukio ya hivi karibuni yanaweza kuwa kengele ya kiroho ikitufanya tujikite sana katika mambo yale ya msingi. Ikiwa hivyo, itakuwa ni baraka kubwa katika kipindi hiki kujikita katika vitu ambavyo tunaweza kufanya sahihi katika maisha yetu na jinsi tunavyoweza kubariki maisha ya wengine tunapoinuka katika Mungu na kuenenda katika njia ya agano.”
Mzee Jeffrey R. Holland aliongeza, “Nyakati kama hizi zinatualika kutazama ndani ya mioyo yetu kuona kama tunapenda kile tunachokiona pale. Hapo ndipo [tuna] fikiri kuhusu [sisi] haswa ni nani na kipi haswa cha msingi.”
Nyakati kama hizi pia hutualika kuongeza imani yetu, huduma na shukrani, zikitushawishi “kuzingatia utegemezi wetu kwa Mungu na baraka kutoka Kwake ambazo mara nyingi tunazichukulia kirahisi,” alisema Mzee Holland. “Tunadaiwa na Baba yetu wa Mbinguni kuwa kidogo zaidi wenye kushukuru, kidogo zaidi wenye shukrani, na kidogo zaidi wenye kukumbuka matatizo mangapi yametatuliwa kwa sababu ya Mungu, malaika, ahadi za maagano, na sala.”
Katika kitovu cha shukrani yetu ni baraka ya kukumbuka “jinsi gani Bwana amekuwa na huruma kwa watoto wa watu, kutokea kuumbwa kwa Adamu hadi mpaka wakati [huu]” (Moroni 10:3). Washiriki wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili walisema kwamba tunapotakiwa “kujihifadhi mahala,” tunaweza kufuata mfano wa Nefi na Alma, tukikumbuka kwamba Yeye “ambaye katika yeye tumeamini,” Mwokozi Yesu Kristo, “bado atatukomboa [sisi]” (2 Nefi 4:19; Alma 36:27). Na tunaweza kukumbuka, kama Mtume Paulo alivyofundisha, kwamba hakuna kinachoweza “kututenganisha sisi na upendo wa Kristo” (ona Warumi 8:35).
Bwana Yesu Kristo“ndiye kinga yetu ya mwisho” (ona Zaburi 61:1–4), alisema Mzee Holland. “Chochote kile kitakachotokea, hatutatenganishwa kutoka upendo wa Mwokozi na ushirika Wake, hata kama hatutambui hilo kwa wakati husika. Roho haijazuiliwa na kirusi au mipaka ya kitaifa au utabiri wa kitabibu.”
“Fanya mambo Mema”
Hivi karibuni, wakati nasoma taarifa iliyoandaliwa na kamati ya Kanisa, Mzee Christofferson aliguswa na madhara ambayo “kujitenga” kunaweza kuleta kwa waumini wa Kanisa wakaao peke yao—mkubwa kwa mdogo.
“Kujitenga kunaweza kusababisha upweke, na upweke unaweza kuwa na matokeo mabaya ya kiafya na kiakili ,” alisema. “Kukabiliana na hilo, wanaharakati wa afya ya jamii wanashauri kwamba wale wanaokabiliwa na upweke watafute namna ya ‘kufanya mambo mema’ kwa ajili ya mwingine.”
Watakatifu wa Siku za Mwisho wanaweza kutafuta njia za kutumikia, kusaidia na kuwachangia wengine, hasa kwa wale walio wapweke, alisema Mzee Christofferson, na waumini wapweke wanaotoa huduma kwa wengine wanaweza kupunguza hisia zao za kujitenga.
“Fokasi katika kuhudumia,” alisema. “Kuna mengi tunaweza kufanya kwa ajili ya kila mmoja wetu kuhisi amejumuishwa na ukaka na udada. Huu ndio wakati ambao akidi ya wazee na Muungano wa Usaidizi wa Akina Mama wanaweza kutumia vipaji vyao na kutoa kile ambacho kwa upekee wanaweza kufanya.”
Na kuliko kumtumia mtu ujumbe kila mara, alishauri,“nafikiri ni jambo jema kumpigia mtu simu kwa kutumia ile teknolojia ya zamani iitwayo simu. Piga tu kuongea na kujumuika. Acha waisikie sauti.”
Juhudi kidogo za kuwafikia wengine zinaweza kuleta tofauti kubwa, kuifanya siku ya mtu iwe angavu katika njia tusizoweza kuzitambua. “Kuhudumia kwetu kunahitajika sana hasa watu wakiwa wamejitenga,” alisema Mzee Cook.
Mzee Holland alipendekeza, “Tunapaswa kutoa sehemu ya siku yetu kuwasiliana na watu wanaohitaji msukumo. Ni kweli, tunapata msukumo kwa kufanya hivyo, hivyo kila mmoja ‘anainuliwa’ (3 Nefi 27:14, 15), kama Mwokozi alivyosema Alitumwa duniani kufanya.”
Njia nyingine tunayoweza kujiinua na kuwainua wengine ni kujiandaa kwa ajili ya siku mahekalu yatakapofunguliwa tena. Kufungwa kwa Mahekalu—iwe ni kwa magonjwa ya ulimwengwu, matengenezo, au usafi— “hutoa fursa isiyo na kifani ya kujifunza kuhusu utafiti wa historia ya familia kufanya faharisi, na namna ya kuandaa majina mengi kwa ajili ya siku milango ya hekalu itakapofunguliwa tena,” alisema Mzee Bednar.
Bila kujali kama mahekalu yamefunguliwa au yamefungwa, Mzee Bednar aliongeza, wanachama wa Kanisa wanaweza kutia bidii ya kuwa wenye kustahili na kuwa na kibali cha kuingia hekaluni.
Mafunzo ambayo Bwana Angetaka Sisi Tujifunze
Kama Mzee Bednar alivyobainisha, wakati hakuna ambaye angechagua uzoefu wa janga la COVID–19, janga hili la siku za mwisho hata hivyo limetukumba.
“Tukiwa na mtazamo wa milele uletwao na injili ya urejesho na rehema zitokanazo na Upatanisho wa Mwokozi, tunaweza kujifunza masomo kutokana na majaribu ya maisha haya ambayo hutuandaa kwa ajili ya baraka za milele,” alisema. Tunahitaji kuomba. Tunahitaji kutafuta. Tunahitaji kuuliza. Tunahitaji kuwa na macho ya kuona na masikio ya kusikia. Lakini tunaweza kubarikiwa katika njia za kipekee ili kujifunza masomo ambayo yatatubariki sasa na milele.”
Pamoja na madhara yake makubwa katika familia duniani kote, COVID-19 imewafundisha watu kuonyesha kuwajali zaidi wengine, alisema Rais Ballard.
“Tunapata kugundua jinsi gani familia zetu ni za thamani, jinsi gani majirani zetu ni wa thamani, na jinsi gani waumini wenzetu wa Kanisa ni wa thamani,” alisema. “Kuna masomo tunajifunza sasa yatakayotufanya kuwa watu bora.”
Na wakati kimbunga cha sasa kitakapopita, tutarajie nini tena? Mengi kama ilivyo sasa, alisema Mzee Uchtdorf. Watoto wa Mungu ndani na nje ya Kanisa wataendelea kukabiliana na changamoto.
“Tunaishi katika nyakati tunazohitaji kujifunza,” alisema. Na somo muhimu zaidi tunaloweza kujifunza ni kwamba jibu la changamoto zijazo pia ni jibu la changamoto ya sasa: injili ya Yesu Kristo.
Kwa sababu Watakatifu wa Siku za Mwisho wanayo injili ya urejesho ya Yesu Kristo, Mzee Holland alisema, wanaweza kujifunza kuwa wenye mtazamo chanya na wa tumaini, kufanya kwa kadiri wawezavyo na kulichukua neno la Bwana aliposema,“Hebu na tufurahi na kufanya mambo yote yaliyo katika uwezo wetu; na tusimame imara, na uhakika mkubwa sana, kuuona wokovu wa Mungu, na mkono wake kuonekana” (Mafundisho na Maagano 123:17)
“Kuna mengi ya kufurahia tunapoifanya upya imani yetu, Kumuamini zaidi Bwana, na kuona muujiza wa ukombozi Wake” alisema Mzee Holland.