Faneva Mmisionari
Faneva aliangalia dirishani kwenye mtaa wenye watu wengi nje ya nyumba yake. Aliweza kuwaona watu wakisukuma mikokoteni ya mboga, mchele, nguo, na bidhaa nyingine za kuuza. Aliweza kusikia honi za gari na mbwa wakibweka. Kisha akasikia sauti nyingine.
“Mama, kuna mtu anabisha hodi!” Faneva aliita kwa sauti. Mama alifungua mlango. Vijana wawili waliovalia suti na tai walikuwa kwenye ngazi za mlangoni. Faneva hakuwahi kabla kumwona mtu amevaa hivyo mtaani kwake huko Madagaska.
“Sisi ni wamisionari kutoka Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho,” mmoja wao alisema. Tunawafundisha watu kuhusu Yesu. Tunaweza kushiriki ujumbe pamoja na ninyi?”
Faneva alifurahi wakati Mama alipowaalika kuingia ndani. Familia yote ilikusanyika ili kusikia kuhusu Yesu na jinsi Kanisa Lake lilivyokuwa tena duniani.
Kuanzia siku ile, wamisionari waliitembelea familia ya Faneva mara nyingi. Walileta kitabu kilichoitwa Hadithi za Kitabu cha Mormoni. Faneva alipenda kukisoma pamoja na familia yake!
Siku moja nitakuwa mmisionari na kushiriki Kitabu cha Mormoni na wengine, Faneva alijisemea mwenyewe.
Wakati mwingine wamisionari walipokuja, waliifundisha familia jinsi ya kuomba. Faneva alijifunza kwamba angeweza kuongea na Baba wa Mbinguni muda wowote, mahali popote.
Siku moja nitakuwa mmisionari na kuwafundisha watu kuhusu kuomba, Faneva alifikiria.
Siku moja wamisionari walikuwa na swali muhimu.
“Je, utafuata mfano wa Yesu Kristo na kubatizwa?” mmoja wao aliuliza.
Faneva alihisi furaha katika moyo wake. “Ndio!,” alisema.
“Ndio!” kaka yake na Mama walisema.
Baba alisema kwamba bado hakuwa tayari kubatizwa. Lakini alikuwa Sawa kama wanafamilia wengine watabatizwa. Na hivyo walibatizwa! Faneva alibatizwa na mmoja wa wamisionari ambao walimfundisha kuhusu Yesu.
Siku moja nitakuwa mmisionari na kuwasaidia watu kubatizwa, Faneva alifikiria.
Moja ya sehemu bora za kuwa muumini wa Kanisa ilikuwa kwenda kwenye darasa la Msingi. Faneva alipenda shughuli na kukutana na marafiki wapya. Lakini kitu kizuri kati ya yote ilikuwa kuimba nyimbo za Msingi. Jumapili moja katika Msingi, walikuwa wanaimba nyimbo za kushiriki injili.
“Ninataka kuwa mmisionari sasa,” Faneva aliimba. “Sitaki kusubiri hadi niwe mkubwa.”
Ninaweza kuanza kufanya kazi ya umisionari sasa, Faneva aligundua. Sihitaji kusubiri hadi siku nyingine!
Kuanzia hapo, Faneva alitafuta njia anazoweza kushiriki injili. Alijaribu kuwa mfano mzuri. Aliwaalika watu kuja kanisani. Aliwasaidia majirani zake. Baada ya miaka michache, alikuwa mkubwa vya kutosha kuweza kuwasaidia wamisionari kufundisha watu katika mji wake. Katika miaka michache baadaye, alihudumu misheni yeye mwenyewe—akikutana na watu wapya na kushiriki injili, kama vile wamisionari walivyo shiriki naye. ●