Nyumba za mikutano—Mahali pa Unyenyekevu na Kuabudu
Roho wa Bwana yuko katika nyumba zetu za mikutano na atatupa mwongozo wa kiungu wakati tunapojiweka katika unyenyekevu mbele Zake.
Mshirika mwaminifu wakati mmoja alishiriki nami uzoefu aliokuwa nao wakati akitimiza majukumu ya kuondoa viti na kuweka vitu sawa kwenye kituo cha kigingi baada ya mkutano wa kigingi. Baada ya dakika 30 ya kutekeleza majukumu haya, aligundua kuwa yeye ndiye mtu wa mwisho aliyebaki kwenye jengo hilo. Badala ya kuhisi yuko peke yake na kuharakisha kuondoka, hata hivyo, aligundua kuwa aina ileile ya amani aliyokuwa nayo wakati wa mkutano ilibaki na yeye na ilikuwa ikiongezeka.
Alipomaliza majukumu hayo na kutoka kwenye nyumba ya mkutano, alikutana na mshiriki mwingine ambaye alionekana akimwangalia kwa umakini. Kugundua kile rafiki yangu alichokuwa akifanya, muumini huyu akamshika mkono na kumwambia, “Ndugu, Bwana huona mambo haya madogo unayomfanyia, na Anatazama chini na kutabasamu.”
Miaka kadhaa baadaye alipokuwa akihudumu kama Askofu, rafiki huyo huyo alijikuta peke yake tena katika jengo la mkutano la kata yake. Baada ya kuzima taa kanisani, yeye alibaki kwa muda wakati mbalamwezi ulipoangaza kupitia madirishani hadi juu ya mimbari.
Hisia ile aliyoizoea ya amani ilimfunika tena, naye akaketi karibu na mbele ya kanisa na akatafakari nyakati takatifu ambazo alikuwa amepata katika mpangilio huo—mara nyingi aliwaona makuhani wakimega mkate kwenye meza ya sakramenti, nyakati zile wakati alipokuwa akimsikia Roho Mtakatifu akiandamana naye wakati alipokuwa akihutubia mkutano wa kata, huduma za Ubatizo alizoendesha, nyimbo nzuri za kwaya alizozisikia, na shuhuda nyingi kutoka kwa washiriki wa kata ambazo zilimgusa sana. Akiwa ameketi peke yake katika kanisa hilo lenye giza, alijihisi kuzidiwa na mkusanyiko wa athari hizi za matukio ya maisha yake na juu ya maisha ya washiriki wa kata yake, na akainamisha kichwa chake kwa shukrani kubwa.
Rafiki yangu alikuwa amefundishwa kwa busara na kwa usahihi kwamba mahali patakatifu zaidi duniani ni hekaluni na nyumbani, lakini kupitia matukio haya mawili yaliyotajwa hapo juu, pia alikuja kuelewa asili takatifu ya nyumba zetu za mikutano. Kwa sababu zimewekwa wakfu kwa mamlaka ya ukuhani, majengo haya yanakuwa maeneo ambapo Bwana humimina mafunuo juu ya watu wake na ambamo “nguvu za uchamungu hujidhihirisha” kupitia ibada ambazo hufanyika humo (ona Mafundisho na Maagano 84:20).
Nyumba ya mikutano inaungana pamoja na nyumbani ili kuleta shangwe iliyoahidiwa ambayo Watakatifu waaminifu wanaweza kuipata siku ya Sabato. Inakuwa mahali ambapo ibada ya pamoja ya washiriki husababisha mioyo yao kuwa “imeungana pamoja katika umoja na katika kupendana wao kwa wao” (Mosia 18:21) na kuelekea kwa Mwokozi. Kwa sisi kutoa shukrani sahihi na heshima kwa ajili ya kumwagika kwa baraka za kiroho ambazo zinakuja kwetu kupitia nyumba zetu za mikutano, tunapaswa kuingia katika maeneo haya ya kuabudu pamoja na fikra za kina na unyenyekevu wa dhati.
Maana ya Unyenyekevu
Katika utamaduni wetu wa Kanisa la siku za leo, neno unyenyekevu limekuwa sawa na neno kimya. Wakati sauti laini zinafaa makanisani mwetu, maoni ya mtazamo huu mdogo wa unyenyekevu hushindwa kuchukua maana kamili ya neno. Unyenyekevu linaweza kufuatiliwa kwenye kitenzi cha Kilatini revereri, ambacho kinamaanisha “simama kwa heshima ”1 Je, tunaweza kupata neno ambalo linaelezea kwa uwazi zaidi hisia za nafsi yetu wakati tunapotafakari kwa hakika yale ambayo Mwokozi amefanya kwa kila mmoja wetu?
Nimekumbushwa maneno ya wimbo mzuri tunaouimba makanisani mwetu: “I stand all amazed at the love Jesus offers me.”2 Maana hiyo kubwa ya kushukuru, kusifu, na kushangaa ndio kiini cha unyenyekevu, na inatuhimiza kujiepusha na aina yoyote ya lugha au tabia inayoweza kupunguza hisia hizo ndani yetu au ndani ya wengine.
Nyumba za Mikutano na Siku ya Sabato
Kutokana na ufunuo wa siku za leo, tunajua kwamba sehemu kuu ya kuabudu kwetu siku ya Sabato ni “kwenda kwenye nyumba ya sala na kutoa sakramenti [zetu] katika siku takatifu ya [Bwana]” (Mafundisho na Maagano 59:9). “Nyumba ya sala” ambamo ndani yake tunakusanyika siku ya Sabato ni nyumba zetu takatifu za mikutano.
Rais Russell M. Nelson ametusaidia kuelewa vizuri uhusiano wa karibu kati ya unyenyekevu wetu kwa Mwokozi na hisia zetu kuelekea siku ya Sabato. Katika kushiriki uzoefu wake wa kuitukuza Sabato, Rais Nelson alisimulia, “Nilijifunza kutoka katika maandiko kwamba mwenendo wangu na fikra zangu juu ya Sabato zinafanya ishara kati yangu na Baba yangu”3
Kama vile mwenendo wetu na tabia yetu juu ya Sabato ni ishara ya kujitoa kwetu kwa Bwana, mwenendo wetu, fikra zetu, na hata mtindo wetu wa mavazi tukiwa katika nyumba Yake ya sala vivyo hivyo huonyesha kiwango cha unyenyekevu tunaouhisi kwa Mwokozi.
Nyumba za Mikutano na Ibada
Mzee Jeffrey R. Holland wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili ameelezea uelewa wetu wa wazo hili, akitangaza:
“Kwa kuongezea kwenye kutenga muda kwa ajili ya kufundisha injili kunakolenga-nyumbani, huduma yetu ya Jumapili iliyorekebishwa … inayotilia mkazo sakramenti ya Chakula cha Bwana kama alama takatifu, inayotambuliwa kama tukio muhimu katika kuabudu kwetu kila wiki. Tunapaswa kukumbuka kwa njia binafsi kadiri iwezekanavyo kwamba Kristo alikufa kutokana na moyo uliopondeka kwa kubeba peke yake dhambi na huzuni ya familia nzima ya wanadamu.
“Kadiri ambavyo tumechangia kwenye mzigo huo wa mauti, tukio kama hilo linahitaji heshima yetu.”4
Ni muhimu kukumbuka kwamba mahali palipochaguliwa kwa ajili ya wakati huu wa juu wa heshima kwa Mwokozi ni kanisa katika nyumba ya mikutano. Katika kuongezea kwenye unyenyekevu tunaohisi wakati wa ibada ya sakramenti kila wiki, hisia zetu za unyenyekevu na heshima zinaimarishwa tunapozingatia ibada nyingine za ukuhani na baraka zinazofanywa katika nyumba ya mkutano, ikijumuisha kuwapa majina na kuwabariki watoto, ubatizo na uthibitisho, kutawazwa katika ukuhani, na kusimikwa kwa ajili ya miito. Kila moja ya ibada na baraka hizi zinaweza kuleta kumiminwa kwa Roho Mtakatifu ikiwa wale wanaoshiriki na wale wanaohudhuria wanakuja katika fikra za unyenyekevu.
Nyumba za Mikutano na Kuabudu
Siku ya Sabato inatupa fursa ya kumwabudu Bwana wakati wa masomo yetu ya nyumbani na kama kusanyiko wakati wa sakramenti na mikutano mingine. Tangu siku za mwanzo za Kanisa, Watakatifu wamefurahia kukusanyika pamoja kuongea na kujenga umoja wa ukaka na udada. Majumba yetu ya mikutano yamesanifiwa yakiwa na nafasi za kufanyia shughuli kama hizo wakati wa wiki. Hatupaswi kamwe kupoteza lengo la msingi la majengo haya, hata hivyo, ambayo yanatoa mahali pa kuabudu.
Kuabudu na unyenyekevu vina uhusiano wa karibu. “Wakati tunapomuabudu Mungu, tunamkaribia kwa upendo wa heshima, unyenyekevu, na kwa ibada ya kuabudu . Tunamtambua na kumkubali kama mfalme wetu mkuu, Muumba wa ulimwengu, Baba yetu mpendwa na anayetupenda milele.”5
Kusudi hili kuu la kuabudu kwa hiyo linapaswa kushawishi mwenendo wetu katika nyumba za mikutano hata wakati tunaposhiriki kwenye shughuli au burudani za kijamii. Uangalifu mkubwa unapaswa kuzingatiwa ili kupunguza machafuko, uchafu, au uharibifu wa sehemu yoyote ya jengo unaotokana na shughuli za Kanisa, na hatua inapaswa kuchukuliwa ili kulisafisha haraka au kulirekebisha ikitokea tukio kama hilo.
Watoto na vijana wanaweza kufundishwa kwamba unyenyekevu na utunzaji wa nyumba ya mikutano huendelea zaidi ya mikutano ya Jumapili. Ushiriki wa waumini katika usafishaji wa nyumba ya mkutano—hasa ushiriki wa pamoja wa wazazi na watoto—ni njia nzuri ya kukuza hali ya unyenyekevu kwa ajili ya majengo yetu. Kama inavyothibitishwa kutokana na uzoefu wa rafiki yangu katika kukiweka vizuri kituo cha kigingi baada ya mkutano, kitendo hicho cha kutunza nyumba ya mkutano ni njia ya kuabudu na inamwalika Roho wa Bwana.
Nyumba za Mikutano na Mwokozi
Chini ya maelekezo ya kinabii ya Rais Nelson, juhudi kubwa zinafanywa kuhakikisha kuwa jina la Yesu Kristo halitengwi kamwe tunapolitaja Kanisa Lake. Vivyo hivyo, hatupaswi kuruhusu Mwokozi aondolewe kutoka kitovu cha kuabudu kwetu—ikijumuisha maeneo yetu ya ibada.
Tumezoea kurejelea hekalu kama nyumba ya Bwana, ambayo ni jina sahihi na muhimu. Tunaweza kukabiliwa zaidi na kusahau, hata hivyo, kwamba kila moja ya nyumba zetu za mikutano zimewekwa wakfu kwa mamlaka ya ukuhani kama mahali ambapo Roho wa Bwana anaweza kukaa na mahali ambapo watoto wa Mungu—wote wa ndani na nje ya Kanisa—wanaweza kuja “kwenye ufahamu wa Mkombozi wao” (Mosia 18:30).
Mpango uliotangazwa hivi karibuni wa kupamba nyumba zetu za mikutano na mchoro wa usanii ambao kwa heshima unamwonyesha Mwokozi na matukio ya kimungu ya maisha Yake katika mwili wenye kufa na maisha ya baadaye imesanifiwa ili kuvuta macho yetu, akili, na mioyo yetu karibu naye. Unapoingia kwenye nyumba hizi za sala kwa ajili ya mikutano na shughuli, tunakukaribisha kwa upendo kutulia, kuangalia, na kutafakari michoro hii mitakatifu, uangalie pamoja na watoto wako, na uwaruhusu waongeze hisia zako za kuabudu na unyenyekevu kwa Mungu.
Nabii wa Agano la Kale Habakuki alitamka, “Bwana yuko ndani ya hekalu lake takatifu; dunia yote na inyamaze mbele yake” (Habakuki 2:20). Tukumbuke vivyo hivyo kuwa Roho wa Bwana yuko katika nyumba zetu za mikutano na atapenya na kuenea kwa kila moja ya mioyo yetu kwa kiwango ambacho tunaenenda wenyewe katika unyenyekevu mbele Zake.