Jinsi Nilivyopata Uponyaji kutokana na Unyanyasaji wa Kijinsia
Nilikuwa nimeishi ndoto mbaya. Lakini baadaye nilijifunza kuwa wakati wa nyakati zangu za giza zaidi, naweza kumtegemea Mwokozi wangu.
Ndoto yangu mbaya ilianza nilipokuwa na miaka saba tu na mama yangu aliolewa tena. Tulimpenda sana baba yangu wa kambo. Alikuwa mkarimu na alikubalika vyema na familia yetu. Kweli nilihisi salama kukaa karibu naye. Kila kitu kilikuwa vizuri hadi siku moja, wakati kila mtu alipokuwa na shughuli, aliponinyanyasa kingono.
Sikuelewa kile alichonifanyia. Nilihisi hofu, kukanganyikiwa, na aibu sana. Lakini niliogopa sana kumwambia mtu yeyote. Nilidhani ingeharibu furaha mpya ya familia yangu na kwamba hakuna mtu angeniamini. Kwa hiyo niliamua kukaa kimya.
Alikuwa ameniumiza mara hiyo moja tu, lakini kumbukumbu ya unyanyasaji huo ilinilemea akilini mwangu. Mwishowe nikaja kuwa na wazimu usiotibika wa kujiona naonewa kila wakati na kwamba mtu angeona kupitia maumivu yangu na kufunua siri yangu ambayo nilijaribu kuficha ukweli kwa kuwa marafiki wazuri na baba yangu wa kambo. Alikuwa mkarimu mahususi kwangu na hakika nilianza kumpenda tena.
Lakini baadaye mambo yakawa mabaya zaidi. Wakati mama alipoanza kufanya kazi usiku, baba yangu wa kambo alianza kuninyanyasa mara kwa mara. Nilihisi kukosa msaada. Nilitaka kuongea, lakini baba yangu wa kambo alipendwa sana, na nilidhani kila mtu angekuwa upande wake. Kwa hivyo wakati wa usiku nilipokuwa peke yangu, nilimwomba Mungu anisaidie kutunza siri yangu.
KUZUNGUMZA
Siku moja unyanyasaji hatimaye ulikoma. Sikujua kwa nini. Ingawa hakuwa akiniumiza tena, daima nilijiona ni mchafu na mwenye aibu. Nilijichukia mwenyewe. Wakati mwingine nilijadili iwapo kifo kingekuwa rahisi zaidi kuliko ukweli wangu. Bado nilitaka kuongea, lakini niliogopa kile ambacho ukweli ungefanya.
Kisha Jumapili moja kanisani nilipokuwa na miaka 14, nilisikiliza somo kuhusu kufanya maamuzi makubwa. Mwalimu wangu alitutia moyo kufunga na kusali na aliahidi kwamba Mungu angetuimarisha ili kufanya jambo sahihi. Baada ya kanisa, niliendelea kufikiria juu ya kile alichosema. Nilijiuliza kama nikiomba, Je, kweli Mungu angenisaidia kuongea?
Siku iliyofuata nilifunga kwa ajili ya kupata ujasiri ili kumwambia mama juu ya ule unyanyasaji. Sikuweza kufokasi wakati wa shule kwa sababu nilichoweza tu kufikiria ni jinsi ambavyo angelipokea. Wakati nilipofika nyumbani, nilijisikia naumwa sana. Nikaomba tena kwa ajili ya kupata nguvu, lakini nilijiona sijajiandaa kumwambia mama.
Jioni ile, nilimwendea Mama wakati akiwa anapika chakula cha jioni. Sikujua kitu cha kusema, lakini nilipomwangalia machoni mwake, nilipata ujasiri wa kuanza tu kuongea. Mara nilipoanza, kila kitu nilichokuwa nimekificha kwa miaka mingi nilikiongea.
Mama na mimi tulikaa kwenye kochi na kulia kwa pamoja. Baadaye, tuliwasiliana na rais wetu wa tawi na kuwaita polisi. Baba yangu wa kambo alipatikana na hatia kwa kile alichonifanyia, na nilipewa ulinzi niliohitaji—sikutaka kuonana naye tena.
Njia Kuelekea Uponyaji.
Wakati wa kipindi hicho, ilikuwa vigumu kuelezea tena tukio langu kwa mamlaka na marafiki kuniuliza baba yangu wa kambo alikuwa wapi, lakini kwa msaada wa familia yangu, sikuwa peke yangu tena. Kwa pamoja, tuliungana kwenye mada mpya ya familia: “Nayaweza mambo yote katika Kristo anitiaye nguvu” (Wafilipi 4:13). Familia yetu kubwa pia walionyesha upendo na msaada wao, na baada ya muda, tulianza kupona pamoja.
Mama na mimi sote tulihudhuria ushauri wa kitaalam, ambao ulikuwa msaada mkubwa! Mshauri wangu alikuwa ndiye hakika niliyemhitaji. Alinisaidia kuelewa hisia zote nilizopata na akanisaidia kukabiliana na kumbukumbu zangu mbaya. Sijawahi kugundua ni kiasi gani nilikuwa naumia hadi nilipoanza kujisikia mzima tena.
Sikufikiria maumivu yatatoweka kwa sababu tu niliongea, lakini pia sikugundua ni muda gani (na uvumilivu) itachukua ili kupona. Kwa muda mrefu, nilikuwa nimehisi sina maana. Ilinibidi nijifunze upya kujipenda.
Nilipata amani zaidi wakati nilipomgeukia Mwokozi wangu na Baba yangu wa Mbinguni. Kutambua kuwa Wao walijua hasa jinsi nilivyojisikia ilinipa nguvu na matumaini. Niliwategemea Wao wakati wa nyakati za giza nene. kadiri muda ulivyoenda kumbukumbu zilianza kufutika, na kweli nilijisikia amani kupitia upendo wa Mwokozi.
Mojawapo ya sehemu zenye thawabu zaidi za mchakato wa uponyaji ni kutambua kuwa nilikuwa na mambo mazuri mbeleni. Nilipokuwa ninanyanyaswa, sikuweza hata kufikiria kuwa na maisha ya kawaida. Nilihisi nimevunjika milele. Lakini kupitia msaada na uponyaji, nilipata vitu vya kuvitazamia mbeleni. Nilianza kuwaambia hadithi yangu wasichana wengine ambao walikuwa wakiumizwa, na hata niliamua kuhudumu misheni. Kutoa ushuhuda wangu kwa wengine kuliniimarisha mimi.
Sielezewi kwa kile ambacho baba yangu wa kambo alinifanyia. Alibadilisha maisha yangu milele, lakini ninachagua kutumia uzoefu wangu ili kuwasaidia wengine. Baadhi ya siku bado ni ngumu, lakini kupitia kila kitu, Bwana ameniimarisha, na najua ataendelea kunisaidia. Nimebadilishwa kutoka kuwa mwathiriwa kuwa mwenye kuokoka.