Maandiko Matakatifu
Musa 8


Mlango wa 8

(Februari 1831)

Methusela anatoa unabii—Nuhu na wanawe wahubiri injili—Uovu mkubwa waenea—Wito wa toba hausikilizwi—Mungu atangaza maangamizi ya wenye mwili wote kwa Gharika.

1 Na siku zote za Henoko zilikuwa miaka mia nne na thelathini.

2 Na ikawa kwamba Methusela, mwana wa Henoko, hakuchukuliwa, ili agano la Bwana lipate kutimizwa, alilolifanya kwa Henoko; kwa maana yeye hakika aliagana na Henoko kwamba Nuhu atakuwa tunda la viuno vyake.

3 Na ikawa kwamba Methusela akatoa unabii kwamba kutoka viuno vyake zitachipuka falme zote za dunia (kupitia Nuhu), naye akajitwalia utukufu.

4 Na hapo ikatokea njaa kubwa katika nchi, na Bwana akailaani dunia kwa laana kali, na wakazi wake wengi wakafa.

5 Na ikawa kwamba Methusela akaishi miaka mia moja na themanini na saba, na akamzaa Lameki;

6 Na Methusela akaishi, baada ya kumzaa Lameki, miaka mia saba na themanini na miwili, naye akazaa wana na mabinti;

7 Na siku zote za Methusela zilikuwa miaka mia tisa na sitini na tisa, naye akafa.

8 Na Lameki aliishi miaka mia moja na themanini na miwili, na akamzaa mwana,

9 Naye akamwita jina lake Nuhu, akisema: Mwana huyu atatufariji juu ya kazi zetu na sulubu za mikono yetu, kwa sababu ya ardhi ambayo Bwana ameilaani.

10 Na Lameki aliishi, baada ya kumzaa Nuhu, miaka mia tano na tisini na mitano, na akawazaa wana na mabinti zake;

11 Na siku zote za Lameki zilikuwa miaka mia saba na sabini na saba, naye akafa.

12 Na Nuhu alikuwa na umri wa miaka mia nne na hamsini, naye akamzaa Yafethi; na miaka arobaini na miwili baadaye akamzaa Shemu kwake yeye aliyekuwa mama wa Yafethi, na alipokuwa na umri wa miaka mia tano akamzaa Hamu.

13 Naye Nuhu na wanawe walimsikiliza Bwana, nao wakamsikia, nao wakaitwa wana wa Mungu.

14 Na wakati watu hawa walipoanza kuongekeza juu ya uso wa dunia, na mabinti wakazaliwa kwao, na wana wa watu wakawaona mabinti wale kuwa ni wazuri, nao wakawachukua kuwa wake zao, hata kadiri walivyowachagua.

15 Na Bwana akamwambia Nuhu: Mabinti za wana wako wamejiuza wenyewe; kwa maana tazama hasira yangu inawaka dhidi ya wana wa watu, kwa kuwa hawataisikiliza sauti yangu.

16 Na ikawa kwamba Nuhu akatoa unabii, na kufundisha mambo ya Mungu, hata kama ilivyokuwa hapo mwanzoni.

17 Naye Bwana akasema kwa Nuhu: Roho yangu haitashindana na mwanadamu daima, kwa kuwa yeye atajua kwamba wenye nyama wote watakufa; hata hivyo siku zake zitakuwa miaka mia moja na ishirini; na kama wanadamu hawatatubu, nitaleta gharika juu yao.

18 Na katika siku zile palikuwepo na mapandikizi ya watu duniani, nao walitafuta kuyaondoa maisha ya Nuhu; lakini Bwana alikuwa pamoja na Nuhu, na uwezo wa Bwana ulikuwa juu yake.

19 Na Bwana akamtawaza Nuhu kwa mfano wake yeye mwenyewe, na akamwamuru kwamba aende akaitangaze Injili yake kwa wanadamu, hata kama vile ilivyotolewa kwa Henoko.

20 Na ikawa kwamba Nuhu akawasihi wanadamu kwamba yawapasa kutubu; lakini hawakuyasikiliza maneno yake;

21 Na pia, baada ya kuwa wamemsikiliza, wakamjia mbele yake, wakisema: Tazama, sisi tu wana wa Mungu; je, hatujajichukulia sisi wenyewe mabinti wa watu? Na hatuli na kunywa na kuoa, na kuozesha? Na wake zetu hutuzalia watoto, nao ni watu wenye nguvu, ambao ni kama watu wa kale, watu mashuhuri. Nao hawakusikiliza maneno ya Nuhu.

22 Na Mungu akaona kwamba uovu wa wanadamu umekuwa mkubwa duniani; na kila mtu aliinuliwa na dhana ya mawazo ya moyo wake, ambayo yalikuwa uovu tu siku zote.

23 Na ikawa kwamba Nuhu aliendeleza mahubiri yake kwa watu, akisema: Sikilizeni, na yatiini maneno yangu;

24 Amini na kutubu dhambi zenu na mbatizwe katika jina la Yesu Kristo, Mwana wa Mungu, hata kama baba zetu, nanyi mtampokea Roho Mtakatifu, ili mpate kufunuliwa mambo yote; na kama hamkufanya hili, gharika itakuja juu yenu; hata hivyo wao hawakusikiliza.

25 Na hii ilimhuzunisha Nuhu, na moyo wake ulipata uchungu kwamba Bwana amemuumba mtu juu ya dunia, nalo lilimhuzunisha moyoni mwake.

26 Na Bwana akasema: Nitamwangamiza mwanadamu niliyemuumba, kutoka uso wa dunia, wote mwanadamu na mnyama, na kitambaacho, na ndege wa angani; kwani ilimhuzunisha Nuhu kwamba nimewaumba, na kwamba nimevifanya hivyo; naye amenilingana; kwa kuwa wametafuta kuutoa uhai wake.

27 Na hivyo Nuhu akapata neema machoni pa Bwana; kwa maana Nuhu alikuwa mtu mwenye haki, na mkamilifu katika kizazi chake; naye alitembea pamoja na Mungu, na pia vile vile wanawe watatu, Shemu, Hamu, na Yafethi.

28 Dunia ikawa imeharibika mbele za Mungu, nayo ikawa imejaa dhuluma.

29 Na Mungu akaangalia juu ya dunia, na, tazama, ikawa imeharibika, maana kila mwenye mwili amejiharibia njia yake duniani.

30 Na Mungu akamwambia Nuhu: Mwisho wa kila mwenye mwili umekuja mbele zangu, kwa maana nchi imejazwa dhuluma, na tazama nitawaharibu wenye mwili wote kutoka duniani.