Mlango wa 5
(Juni–Oktoba 1830)
Adamu na Hawa wazaa watoto—Adamu amtolea Mungu dhabihu na kumtumikia—Kaini na Habili wanazaliwa—Kaini anaasi, anampenda Shetani kuliko Mungu, na anakuwa Mwangamizaji—Uuaji na uovu unaenea—Injili yahubiriwa kutoka mwanzo.
1 Na ikawa kwamba baada ya Mimi, Bwana Mungu, kuwafukuzia nje, kwamba Adamu akaanza kuilima nchi, na kuwa mtawala juu ya wanyama wote wa mwituni, na kula mkate kwa jasho la uso wake, kama vile Mimi Bwana nilivyomwamuru. Naye Hawa, pia, mke wake, alifanya kazi pamoja naye.
2 Na Adamu akamjua mke wake, naye akamzalia wana na mabinti, nao wakaanza kuongezeka na kuijaza nchi.
3 Na tangu wakati ule na kuendelea, wana na mabinti wa Adamu wakaanza kugawana wawili wawili katika nchi, na kuilima nchi, na kuwachunga wanyama, nao pia wakazaa wana na mabinti.
4 Na Adamu na Hawa, mke wake, wakalilingana jina la Bwana, nao wakaisikia sauti ya Bwana kutoka njia iendayo kwenye Bustani ya Edeni, akiwaambia, nao hawakumwona; kwani walikuwa wametengwa kutoka mbele yake.
5 Naye akawapa amri, ya kwamba wamwabudu Bwana Mungu wao, na wamtolee wazao wa kwanza wa mifugo yao, kwa ajili ya sadaka kwa Bwana. Na Adamu akawa mtiifu kwa amri za Bwana.
6 Na baada ya siku nyingi malaika wa Bwana akamtokea Adamu, akisema: Kwa nini wamtolea Bwana dhabihu? Na Adamu akasema: Mimi sijui, ila Bwana ameniamuru.
7 Na ndipo yule malaika akanena, akisema: Jambo hili ni mfano wa dhabihu ya Mzaliwa Pekee wa Baba, ambaye amejaa neema na kweli.
8 Kwa hiyo, nawe utafanya yale yote uyafanyayo katika jina la Mwana, nawe utatubu na kumlingana Mungu katika jina la Mwana milele yote.
9 Na katika siku ile Roho Mtakatifu akashuka juu ya Adamu, ambaye humshuhudia juu ya Baba na Mwana, akisema: Mimi ndiye Mzaliwa wa Pekee wa Baba kutoka mwanzo, na sasa na milele, kwamba kwa vile wewe umeanguka nawe upate kukombolewa, na wanadamu wote, hata vile wengi watakavyotaka.
10 Na katika siku ile Adamu akambariki Mungu naye akajawa na Roho Mtakatifu, na akaanza kutoa unabii juu ya familia zote za dunia, akisema: Na libarikiwe jina la Mungu, kwani kwa sababu ya uvunjaji wangu wa sheria macho yangu yamefunguliwa, na katika maisha haya nitakuwa na shangwe, na tena katika mwili nitamwona Mungu.
11 Naye Hawa, mke wake, alisikia mambo haya yote na akafurahi, akisema: Kama isingelikuwa kwa uvunjaji wetu wa sheria kamwe tusingelikuwa na uzao, na kamwe tusingelijua mema na maovu, na shangwe ya ukombozi wetu, na uzima wa milele ambao Mungu huutoa kwa wote walio watiifu.
12 Na Adamu na Hawa wakalibariki jina la Mungu, na wakawajulisha wana na mabinti wao mambo yote.
13 Na Shetani akaja miongoni mwao, akisema: Mimi pia ni Mwana wa Mungu; naye akawaamuru, akisema: Msiamini; nao hawakuamini, nao wakampenda Shetani zaidi kuliko Mungu. Na watu wakaanza tangu wakati ule na kuendelea kuwa na tamaa za kimwili, kupenda anasa, na uovu.
14 Na Bwana Mungu akawaita watu kwa njia ya Roho Mtakatifu kila mahali na kuwaamuru kwamba watubu;
15 Na kadiri wengi watakavyoamini katika Mwana, na kutubu dhambi zao, wataokolewa; na kadiri wengi wasivyoamini na kutokutubu, watahukumiwa; na maneno yakaenea kutoka kinywani mwa Mungu kama tamko rasmi; kwa hiyo lazima yatatimizwa.
16 Na Adamu na Hawa, mkewe, hawakuchoka kumlingana Mungu. Na Adamu akamjua Hawa, mkewe, naye akapata mimba na kumzaa Kaini, na akasema: Nimempata mtu kutoka kwa Bwana; kwa sababu hiyo asije kukataa maneno yake. Lakini tazama, Kaini hakusikiliza, akisema: Bwana ni nani hata nipaswe kumjua yeye?
17 Na tena akashika mimba na kumzaa ndugu yake Habili. Na Habili alisikiliza sauti ya Bwana. Na Habili alikuwa mfugaji wa kondoo lakini Kaini alikuwa mkulima.
18 Na Kaini alimpenda Shetani zaidi kuliko Mungu. Na Shetani akamwagiza, akisema: Mtolee Bwana sadaka.
19 Na baada ya wakati kupita ikawa Kaini akaleta matunda ya nchi kama sadaka kwa Bwana.
20 Naye Habili, pia akaleta wazao wa kwanza wa wanyama wake, na sehemu zake zilizonona. Na Bwana akamtakabali Habili, na sadaka yake;
21 Bali kwa Kaini, na kwa sadaka yake, hakuitakabali. Sasa Shetani alijua hiyo, nayo ikamfurahisha. Na Kaini alikuwa na ghadhabu kali, na uso wake ukakunjamana.
22 Na Bwana akamwambia Kaini: Kwa nini una ghadhabu? Na kwa nini uso wako umekunjamana?
23 Kama ukitenda vyema, utakubaliwa. Na kama hukutenda vyema, dhambi inakuotea mlangoni, na Shetani anatamani kukupata wewe; na isipokuwa umesikiliza amri zangu, nitakutoa kwake, na itakuwa kwako kulingana na tamaa zake. Nawe utaweza kumtawala;
24 Kwa maana tangu sasa na kuendelea utakuwa baba wa uwongo wake; nawe utaitwa Mwangamizaji; kwa kuwa nawe pia ulikuwepo kabla ya ulimwengu.
25 Na itasemwa katika wakati ujao—Kwamba machukizo haya yalitoka kwa Kaini; kwa maana yeye alikataa ushauri mkuu ambao ulitoka kwa Mungu; na hii ni laana nitakayoiweka juu yako, isipokuwa ukitubu.
26 Na Kaini alikuwa na ghadhabu, na hakuisikiliza tena sauti ya Bwana, wala ya Habili, ndugu yake, aliyekuwa akienenda katika utakatifu mbele za Bwana.
27 Na Adamu na mke wake waliomboleza mbele za Bwana, kwa sababu ya Kaini na ndugu zake.
28 Na ikawa kwamba Kaini akamtwaa mmoja wa binti za ndugu zake kuwa mke, na wao wakampenda Shetani zaidi kuliko Mungu.
29 Na Shetani akamwambia Kaini: Niapie kwa koo lako, na kama ukisema hakika utakufa; na ndugu zako waniapie kwa vichwa vyao, na kwa Mungu aliye hai, kwamba hawatasema; kwa maana kama watasema, hakika watakufa; na hii ili baba yako asipate kujua; na leo hii nitamtoa ndugu yako Habili mikononi mwako.
30 Naye Shetani akamuapia Kaini kwamba yeye atafanya kulingana na maamrisho yake. Na mambo haya yote yalifanyika kwa siri.
31 Na Kaini akasema: Hakika mimi ndiye Mahani, bwana wa siri hii kuu, ili nipate kuua na kufaidika. Kwa sababu hiyo Kaini aliitwa Bwana Mahani, naye alifurahia katika uovu wake.
32 Na Kaini akaenda kondeni, na Kaini akazungumza na Habili, ndugu yake. Na ikawa kwamba wakati walipokuwa kondeni, Kaini akamwinukia Habili, ndugu yake, na kumwua.
33 Na Kaini alifurahia katika lile alilolifanya, akisema: Niko huru; hakika mifugo ya ndugu yangu inaangukia mikononi mwangu.
34 Na Bwana akamwambia Kaini: Yuko wapi Habili, ndugu yako? Naye akasema: Sijui. Kwani mimi ni mlinzi wa ndugu yangu?
35 Naye Bwana akasema: Umefanya nini? Sauti ya damu ya ndugu yako inanililia kutoka ardhini.
36 Na sasa umelaaniwa wewe kutoka dunia ambayo wewe umeifungua kinywa chake ipokee damu ya ndugu yako kwa mkono wako.
37 Utakapoilima ardhi haitakupa mazao yake. Utakuwa mtoro na asiye na kikao duniani.
38 Na Kaini akamwambia Bwana: Shetani alinijaribu kwa sababu ya mifugo ya ndugu yangu. Nami pia nikawa na ghadhabu; kwa kuwa sadaka yake uliipokea na ya kwangu hukuipokea; adhabu yangu ni kubwa zaidi kuliko niwezavyo kuichukua.
39 Tazama umenifukuza leo kutoka uso wa Bwana, nami nitafichika mbali na uso wako; nami nitakuwa mtoro na asiye na kikao duniani; hata itakuwa, kwamba kila anionaye ataniua, kwa sababu ya uovu wangu, kwa kuwa mambo haya hayajafichika kwa Bwana.
40 Na Mimi Bwana nikamwambia: Yeyote atakayekuua wewe, atalipizwa kisasi mara saba. Nami Bwana nikamtia alama Kaini, asije mtu yeyote akamwona akamwua.
41 Na Kaini akaondolewa kutoka uwepo wa Bwana, na mke wake na wengi wa ndugu zake walikaa katika nchi ya Nodi, mashariki mwa Edeni.
42 Na Kaini akamjua mke wake, naye akapata mimba na kumzaa Henoko, naye pia alizaa wana na mabinti wengine wengi. Na alijenga mji, naye akauita jina la mji ule kwa jina la mwanawe, Henoko.
43 Naye Henoko akamzaa Iradi, na wana na mabinti. Na Iradi akamzaa Mahujaeli, na wana na mabinti wengine. Na Mahujaeli akamzaa Methushaeli, na wana na mabinti wengine. Na Methushaeli akamzaa Lameki.
44 Na Lameki akajitwalia wake wawili; jina la wa kwanza ni Ada, na jina la yule mwingine ni Sila.
45 Na Ada akamzaa Yabali; yeye ndiye baba yao wakaao katika mahema, na walikuwa wafugaji wa wanyama; na jina la nduguye lilikuwa Yubali, huyu ndiye alikuwa baba yao wapigao kinubi na filimbi.
46 Na Sila, naye akamzaa Tubal-Kaini, mfuaji wa kila chombo cha kukatia shaba nyeupe na chuma. Na dada ya Tubal-Kaini aliitwa Naama.
47 Na Lameki akawaambia wake zake, Ada na Sila: Isikieni sauti yangu, enyi wake za Lameki, sikilizeni usemi wangu; maana nimemwua mtu kwa majeraha yangu, na kijana kwa maumivu yangu.
48 Kama Kaini akilipishwa kisasi mara saba, hakika Lameki atalipishwa mara sabini na saba;
49 Kwa maana Lameki alikwishaingia katika agano na Shetani, kwa mfano wa Kaini, ambapo alikuwa Bwana Mahani, bwana wa ile siri kubwa ambayo iliingizwa kwa Kaini na Shetani; na Iradi, mwana wa Henoko, akiwa anajua siri yao, alianza kuifichua kwa wana wa Adamu;
50 Kwa sababu hiyo Lameki, akiwa amekasirika, akamwua, siyo kama kwa Kaini, ndugu yake Habili, kwa ajili ya kupata faida, bali alimwua kwa ajili ya kiapo.
51 Kwa maana, kutoka siku za Kaini, palikuwepo na makundi maovu ya siri, na kazi zao zilikuwa gizani, nao walijuana kila mtu na ndugu yake.
52 Kwa sababu hiyo Bwana akamlaani Lameki, na nyumba yake, nao wote walioagana na Shetani; kwa maana hawakuzishika amri za Mungu, na hiyo haikumpendeza Mungu, naye hakuwahudumia wao, na kazi zao zilikuwa ni machukizo, nazo zikaanza kuenea miongoni mwa wana wa watu. Nazo zilikuwa miongoni mwa wana wa watu.
53 Na miongoni mwa mabinti za watu mambo haya hayakunenwa, kwa sababu Lameki aliinena siri hiyo kwa wake zake, nao wakamwasi, nao wakayasema nje, na wala hawakuwa na huruma;
54 Kwa hiyo Lameki akadharauliwa, na kufukuzwa, na hakuja miongoni mwa wana wa watu, asije akafa.
55 Na hivyo ndivyo kazi za gizani zilivyoanza kuenea miongoni mwa wana wote wa watu.
56 Na Mungu akailaani dunia kwa laana kali, naye alikasirishwa kwa uovu, na wana wote wa watu ambao aliwafanya;
57 Kwa maana hawakuisikiliza sauti yake, wala kumwamini Mwanaye wa Pekee, hata yeye ambaye alimtangaza kuwa atakuja katika wakati wa meridiani, ambaye aliandaliwa kabla ya msingi wa ulimwengu.
58 Na hivyo Injili ikaanza kuhubiriwa, kutoka mwanzo, ikitangazwa na malaika watakatifu waliotumwa kutoka katika uwepo wa Mungu, na kwa sauti yake yeye mwenyewe, na kwa kipawa cha Roho Mtakatifu.
59 Na hivyo vitu vyote vilithibitishwa kwa Adamu, kwa agizo takatifu, na kwa Injili iliyohubiriwa, na tangazo lililoletwa, kwamba hii lazima iwepo duniani, hadi mwisho wake; na hivyo ndivyo ilivyokuwa. Amina.