Rafiki kwa Rafiki
Toba ihusianayo na Lifti
Nilipokuwa na miaka 11, familia yangu iliishi kwenye jengo la ghorofa 12 huko Hong Kong. Kila siku baada ya shule, nilikimbia kwenye jengo hilo na kupanda lifti hadi kwenye fleti tuliyokuwa tunakaa.
Siku moja niliingia kwenye lifti na kubonyeza vitufe vyote, hivyo vyote vikawaka. Kwa hiyo lifti ingesimama kwenye kila ghorofa. Milango ya lifti ilianza kufunga, lakini ghafla mkono ukaingizwa na kufungua mlango. Alikuwa ni mmoja wa jirani yangu tunayekaa naye ghorofani. Hakusema chochote kuhusu vitufe vilivyobonyezwa, lakini nilikuwa na hofu. Ilionekana kama ilichukua milele kufika nyumbani!
Kwa hakika, lifti ilisimama ghorofa iliyofuatia, ikasubiria na kisha kuendelea juu. Mara tu milango ilipofunguka kwenye ghorofa yangu, nilitoka nje. Nilifika nyumbani nikiwa natokwa jasho kwa sababu nilikimbia kwa kasi sana!
Punde tu baada ya kufika nyumbani, simu iliita. Alikuwa ni yule jirani niliyekuwa naye kwenye lifti. Nilipatwa na hofu nikimsubiria mama yangu amalize kuongea na ile simu.
Baada ya kukata simu, mama yangu aliuliza “Je, ulibofya vitufe vyote kwenye lifti?”
Nisingeweza kumdanganya mama yangu. “Ndio,” nilisema.
Mama yangu alitabasamu. “SAWA, tupandishe juu tukaongee na jirani yetu.”
Tulipandisha juu kwa pamoja. Nilibonyeza kengele ya mlangoni, na jirani yangu akaja mlangoni. Niliinamisha kichwa changu nilipokuwa nikiomba samahani kwa kubonyeza vitufe vyote. Niliahidi nisingerudia tena.
Jirani yetu alikuwa mwema. Alisema, “Ilimradi hutafanya tena, nadhani hilo halina tatizo.”
Baada ya kuomba samahani kwa jirani, nilijisikia vizuri. Na sikubonyeza vitufe vyote kwenye lifti tena.
Uzoefu huu ulinisaidia kujifunza kuhusu toba. Nilitambua kwamba nilifanya kitu kibaya. Nilihisi uchungu na kuomba msamaha. Na sikurudia tena. Kisha nilijihisi mwenye furaha! Toba inaweza kukuletea furaha pia.