2022
Kusaidia na Roho Mtakatifu
Machi/Aprili 2022


Kusaidia na Roho Mtakatifu

Unaweza kuhisi Roho Mtakatifu hata kabla haujabatizwa.

a boy helping his dad at a fruit stand

Mateo na baba yake kwa pamoja walielekea kwenye kibanda chao cha matunda cha familia. Mbwa wa Mateo, Zeus, aliwafuata.

“Ulimwuliza askofu kuhusu ubatizo wangu?” Mateo aliuliza. Tayari alikuwa na umri wa miaka minane, lakini alikuwa hajabatizwa kwa sababu ya janga la ulimwengu.

“Alisema hautaweza kubatizwa mwezi huu,” Baba alisema. “Huenda mwezi ujao.”

“SAWA.” Mateo alikunja uso. Hakika alitaka kubatizwa na kupokea kipawa cha Roho Mtakatifu. Lakini ilionekana kama isingewezekana!

Baba alifungua kibanda. Mateo alisaidia kubeba maboksi ya machungwa, malimao, maembe na ndizi. Kisha alisaidia kuyaweka kwenye rafu.

Mateo aliendelea kufikiria kuhusu Roho Mtakatifu wakati wakiendelea kushughulika. “Je, Roho Mtakatifu anakuwaje?” Mateo aliuliza.

“Roho Mtakatifu hunifariji ninapokuwa na huzuni,” Baba alisema. “Na hunifanya nihisi vizuri pale ninapomsaidia mtu.”

“Siwezi kungojea kubatizwa ili nimsikie Roho Mtakatifu pia!”

“Hata kabla hujabatizwa na kuthibitishwa, unaweza kumhisi Roho Mtakatifu” Baba alisema. “Unaweza kuhisi faraja Yake sasa. Kama wakati unaposali au kumfanyia mtu kitu chema. Kisha baada ya kuthibitishwa, daima unaweza kuwa na Roho Mtakatifu pamoja nawe.”

Mateo alifikiria kuhusu hilo. Je, amewahi kumsikia Roho Mtakatifu hapo kabla?

Haikuchukua muda mrefu wakawa wametoa maboksi yote. “Uko tayari kuwasaidia akina Sosa?” Baba aliuliza.

Mateo alikubali kwa kichwa. Bw. na Bi. Sosa kwa pamoja walikuwa na wakati mgumu kutembea. Hivyo Mateo alienda sokoni kwa ajili yao. Wakati mwingine aliwasaidia kazi za nyumbani pia.

boy helping take out trash

Mateo na Zeus walikwenda kwenye nyumba ya akina Sosa. Bi. Sosa aliwapungia kutokea kibaraza cha mbele ya nyumba. “Habari ya asubuhi!”

“Unahitaji vyakula leo?” Mateo aliuliza.

“Ndiyo. Nahitaji mkate, viazi na nyama ya ng’ombe.” Bi. Sosa alihesabu baadhi ya sarafu. “Hiyo itatosha.”

Mateo alichukua pesa zile. Aliona mfuko wa taka karibu na mlango. “Naweza kukusaidia kutoa huo?” aliuliza.

“Ndiyo. Asante!” Bi. Sosa alisema.

Baada ya kutoa taka, Mateo alinunua chakula. Alifikiria kuhusu vitu vyote alivyovifanya asubuhi hiyo. Alimsaidia Baba kwenye kibanda cha matunda. Aliwasaidia akina Sosa kununua chakula. Na alipata hisia nzuri ndani ya moyo. Alikuwa anahisi Roho Mtakatifu, kama vile Baba alivyosema!

Mateo alitumaini hangesubiri kwa muda mrefu ili kubatizwa. Alitaka kuwa na Roho Mtakatifu pamoja naye muda wote!

Kielelezo na Carolina Farías