Kutoka Urais wa Kwanza
Kuzishinda Changamoto Zako
Changamoto yangu kubwa nilipokuwa mtoto ilikuwa ni wakati baba yangu alipofariki. Nilikuwa na umri wa miaka saba.
Nilikuwa na mama mwema na babu na bibi wakarimu. Nililia kwa machozi mengi. Shuleni wanafunzi wenzangu walinifanyia mzaha kwa sababu sikuwa naweza kutaja herufi au kufanya hesabu vizuri. Baadhi ya watoto wakubwa walinionea tulipokuwa ndani ya basi la shule. Natamani ningekuwa na vipaji kama wengine ambao walikuwa wakimbiaji wazuri au waimbaji wazuri.
Baada ya muda, nilianza kuhisi vizuri. Familia yangu ilinipenda na kunisaidia. Niliendelea kufanya kazi kwa bidii na pole pole nilianza kufanya vizuri shuleni. Pia niligundua vitu nilivyoweza kufanya vizuri. Nilifanya jitihada ili kuwa vizuri katika kufanya vitu hivyo. Baba wa Mbinguni alinisaidia.
Kadiri tunavyokua wakubwa, sote tunakumbana na changamoto. Baadhi yetu wana ugonjwa au ulemavu. Baadhi ni maskini na hawawezi kupata uangalizi mzuri wa kimatibabu au elimu. Baadhi hunyanyaswa kwa sababu ya rangi zao za ngozi au wanakotokea.
Unawezaje kuzishida changamoto zako?
-
Mtumaini Baba wa Mbinguni. Wakati mwingine tunaweza kuhisi kukata tamaa, lakini ni lazima tumtumaini Yeye Yeye anawapenda watoto Wake na ameahidi kutubariki.
-
Endelea kujaribu. Bwana ametufundisha kwamba sisi sote tuna vipaji tofauti. Tunaweza kugundua vipaji vyetu wenyewe. Kisha tunaweza kuvitumia vipaji hivyo ili kuboresha maisha yetu na kuwatumikia wengine.
Bila kujali kuna kiza kiasi gani baada ya jua kuzama, daima kutakuwa na mwangaza mwingi pale jua litakapochomoza. Hili ni kweli kuhusu maisha yetu. Kama njia moja imefungwa, tunaweza kutafuta nyingine. Kama kitu fulani kinaonekana kuwa kigumu sana kufanya, tunaweza kusonga mbele na kujifunza hadi tukiweze.
Ninakuahidi kwamba Baba wa Mbinguni atakusaidia kushinda changamoto zako. Anakupenda na atakusaidia kuwa kile ambacho Yeye anakutaka uwe.