Mzaha wa Baiskeli
Rafiki zake walisema itakuwa ya kufurahisha. Lakini haikuonekana kuwa sawa.
Sam alinyonga baiskeli yake kwa kasi alivyoweza kuelekea kilimani. Aliegemea mbele alipokuwa akinyonga. Upepo ulipeperusha nywele zake. Rafiki yake Liam alimfuata nyuma.
“Umechoka?” Liam aliuliza.
“Hapana!” Sam alijibu.
Rafiki yao Eric alikuwa tayari amefika kileleni mwa kilima.
“Komm schon! Njooni!” Eric alipaza sauti.
Sam na Liam walifika kileleni mwa kilima. Wavulana hao waliegesha baiskeli zao na kukaa chini ya mti.
Liam alichukua jiwe na kulirusha. “Mimi nimechoka.” Hakukuwa na sehemu nyingi za kwenda kwenye kijiji chao kidogo huko Uswisi.
“Mimi pia,” Eric alisema. Alikwaruza vumbi kwa kijiti.
“Tungeweza kuendelea kunyonga baiskeli,” Sam alisema.
Liam alipangusa uso wake. “Hiki ndicho siku zote tumekuwa tukikifanya.”
“Tufanye kitu cha kufurahisha!” Eric alisema. Eric alinyanyuka na kuelekea kwenye maegesho ya baiskeli. Sam na Liam walimfuata.
Sam alihisi kama tumbo lake linakaba. Wakati mwingine kile ambacho Eric na Liam walidhani ni cha kufurahisha hakikuwa hivyo kwake. Eric na Liam walipenda kuwafanyia mzaha watoto wengine na kusema vibaya darasani. Lakini huenda wakati huu mambo yangekuwa tofauti.
Hata hivyo, hapakuwa na wavulana wengi darasani mwa Sam. Kama asingekuwa rafiki wa Eric na Liam, ni nani angekuwa rafiki yake?
“Tufungue vifuniko vyote vya vali kutoka kwenye matairi yote,” Eric aliwanong’oneza. “Tunaweza kuvificha vifuniko hivyo karibu na mti.” Erick alipiga magoti karibu na baiskeli nyekundu iliyong’aa na kufungua kifuniko cha tairi mojawapo.
Liam alicheka. “Ndiyo! Hilo litakuwa la kupendeza.”
Sam alishusha pumzi. Hapana Safari hii haikuwa tofauti. “Sijui,” alisema. “Labda tuondoke tu.”
Eric alitikisa mkono wa Sam. “Tufanye,” alisema. “Hata hivyo hakuna hata anayeangalia.”
“Hizi ni sehemu ndogo tu,” Liam alisema. “Hakuna hata mmoja atakayegundua kwamba vifuniko havipo.”
Sam alijaribu kupuuza hisia za ugonjwa ndani ya tumbo lake. Kuchukua vifuniko vya vali hakungeharibu baiskeli. Alitikisa mabega na kukubali kwa kichwa.
Wavulana watatu kwa haraka waliondoa vifuniko vya vali kutoka kenye matairi ya baiskeli na kurejea kwenye mti walipokuwepo awali. Walificha vifuniko vyote chini ya jiwe na walibaki kuangalia baiskeli. Liam na Eric walikuwa wanacheka cheka.
Punde mwanaume mmoja alitokea, akafungua baiskeli yake, na kuondoka.
“Unaona? Hata hajagundua,” Liam alisema.
Lakini mimi nimegundua Sam aliwaza.
Kwa siku iliyokuwa imebakia, Sam hakuacha kufikiria kuhusu vile vifuniko vya vali. Alitamani angeweza kuwarudishia wahusika, lakini hakuwa na njia ya kuwapata wamiliki wa zile baiskeli. Alipiga magoti na kumwelezea Baba wa Mbinguni.
“Ninajisikia vibaya,” Sam alisema. “Natamani nisingekuwa nimefanya kabisa. Tafadhali Baba wa Mbinguni, nisamehe.”
Siku iliyofuatia, Sam na rafiki zake waliendesha baiskeli zao hadi kwenye maegesho yale tena.
Kwa mara nyingine tena, Eric alisema, “Tufungue vifuniko vya vali!”
Kwa mara nyingine tena, Liam alikubali.
Sam alikumbuka ile sala yake. Na muda huu, alijihisi jasiri kidogo.
“Sidhani kama tunapaswa kufanya hilo,” alisema.
“Kwa nini?” Liam aliuliza, akiwa amekunja uso. “Hakuna hata mtu mmoja aliyegundua jana.”
“Mimi nisingependa mtu kuchezea baiskeli yangu,” Sam alisema. Kabla ya Eric na Liam kujibu, Sam alipanda kwenye baiskeli yake. “Tufukuzane kuelekea duka la mikate!” alipaza sauti. Kisha alianza kunyonga baiskeli kwa kasi kadiri alivyoweza.
Eric na Liam walinyakua baiskeli zao pia.
“Hii sio vizuri! Wewe umeanza kabla yetu,” Liam alisema.
Sam alichekelea pale rafikize walipokuwa wakimkimbiza. Alinong’ona asante kwa Baba wa Mbinguni. Alijihisi vizuri zaidi.