Waasisi Katika Kila Nchi
Piano ya Ludovic
Ludovic alikuwa mwenye furaha kwa kumtumikia Baba wa Mbinguni.
Ludovic alichukua baadhi ya viti vya kujikunja na kwenda navyo mtaa wa jirani. Ilikuwa ni Jumapili, na ibada ingeanza punde tu. Nyumba ambamo ibada hufanyikia huko Togo haikuwa na viti vya kutosha. Hivyo Ludovic siku zote alileta viti kutoka kwenye nyumba ya babu yake.
“Kwa nini umeacha kanisa zuri na kwenda kwenye kijumba kidogo?” mtu moja alimuuliza. “Kanisa lako halina hata mabenchi!” mtu mwingine alisema, huku akicheka.
Ludovic alijifanya kutowasikia. Ninapaswa kuendelea kufanya tu kile kilicho sahihi, Ludovic aliwaza.
Ludovic alijifunza kuhusu Kanisa kwa mara ya kwanza alipokuwa na miaka 10 Sasa alikuwa na miaka 12. Yeye na familia yake walikuwa wamebatizwa karibuni. Alikuwa na ukuhani na alisaidia kupitisha sakramenti. Wakati mwingine aliweka akiba pesa yake ya chakula cha mchana ili kununua mkate wa sakramenti kila wiki. Ludovic alikuwa mwenye furaha kwa kumtumikia Baba wa Mbinguni.
Ilipofika muda wa ibada kuanza, chumba kile kidogo kilifurika. Baadhi ya watu walikaa kwenye viti vilivyoletwa na Ludovick Watu wengine walisimama.
Ibada ilianza kwa wimbo. “Israel, Israel, God is calling,” Ludovic aliimba. Anapenda kuimba awapo kanisani.
Baada ya ibada kuisha, Ludovic huimba huku midomo ikiwa imefumbwa na akiwa anakusanya viti. Huendelea kuimba hivyo akiwa anaelekea nyumbani. Kisha alipata wazo! Alichukua piano yake ya kuchezea. Labda anaweza kujua jinsi ya kupiga wimbo wa “Israel, Israel, God Is Calling”!
Ludovic aliimba noti za wimbo huo midomo ikiwa imefumba na kubonyeza kwenye kinanda mpaka akaweza. Haikuchukua muda sana akawa amejifundisha jinsi ya kupiga wimbo wote.
Kisha alikumbuka kwamba familia yake ilikuwa na baadhi ya rekodi za nyimbo za Kanisa. Alizisikiliza na kujifunza jinsi ya kupiga nyimbo zingine pia. Ludovic alifanya mazoezi tena na tena.
“Kwa nini usipige kanisani wakati tukiwa tunaimba?” Siku moja Baba wa Ludovic aliuliza.
Tumbo la Ludovic likapata mtafaruku. “Mimi ni mwenye haya sana,” alisema. “Itakuwaje kama nikikosea?”
“Basi, utaendelea kupiga,” Baba alisema. “Wewe ni mpiga piano mzuri kuliko unavyojifikiria.”
Jumapili iliyofuata, Ludovic hakubeba tu viti. Alibeba pia kinanda chake cha kuchezea hadi kanisani. Ulipofika muda wa wimbo wa kufungua, kwa hofu aliweka vidole vyake kwenye kinanda. Kisha alianza kupiga. Kila mtu aliimba kwa kufuatisha kinanda. Na ilionekana kuwa jambo zuri.
Ludovic alipiga kinanda kanisani kila Jumapili baada ya siku hiyo. Wakati mwingine alikosea. Lakini hakukata tamaa. Wakati wimbo ulipokuwa mgumu kuucheza, waliimba pasipo piano, na Ludovic aliongoza wimbo huo.
Ludovic alitabasamu. Hakujali kwamba walifanya ibada kwenye nyumba ya mtu mwingine. Hakujali hata watu walipomfanyia mzaha. Cha muhimu kwake ilikuwa kwamba Ludovic alikuwa anatumia vipaji vyake kumtumikia Mungu.