2023
Kuwa Wakweli kwetu sisi wenyewe, Mungu na wengine
Machi 2023


Ujumbe wa Urais wa Eneo

Kuwa Wakweli kwetu sisi wenyewe, Mungu na wengine

Moja ya mafanikio makubwa ya maisha yetu ni kukuza uaminifu, uadilifu wa kweli ndani yetu sisi wenyewe.

Mwokozi wetu anatualika sote tumfuate Yeye. Njia Zake zimenyooka na ni safi, ziko wima na ni za uaminifu. Hii ndiyo njia pekee ya sisi kupata shangwe, amani na furaha katika maisha yetu.

Siku moja wakati wa huduma ya Mwokozi wetu hapa duniani, mwanasheria alichagua kumpa changamoto kwenye mada ya injili. Akikusudia kumtega Yesu, aliuliza, “Mwalimu, nifanye nini ili niurithi uzima wa milele?”

Yesu alijibu kwa swali lake mwenyewe: “Imeandikwa nini katika torati? Wasomaje?”

Mwanasheria alijibu, “Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote, na kwa akili zako zote; na jirani yako kama nafsi yako”.

Naye Yesu akamwambia, “Umejibu vema; fanya hivi nawe utaishi” (ona Luka 10:25–28).

Mwaliko huu wa Mwokozi wa kuishi kulingana na kweli za injili umetolewa kwa wote, kwa sababu Yeye anatupenda na upendo Wake unaweza kutusaidia kuushinda ulimwengu ambao unajaribu kutukanganya, kutupofusha, kutudhoofisha na kutuzuia kufikia uwezekano wetu wa kiungu. “Sauti na mashinikizo ya ulimwengu yanavutia na ni mengi. Lakini sauti nyingi ni za udanganyifu, za kulaghai na zinaweza kututoa kwenye njia ya agano.”1

Watu wa Anti-Nefi-Lehi walionesha nguvu ya badiliko ambayo huja kwa watu wanaoikubali injili na kufanya maagano ya kumfuata Yesu Kristo. Walitoa mfano wa uongofu kamili ambao huja kutokana na juhudi ya dhati ya kufuata mfano wa Mwokozi katika kila kipengele cha maisha yetu. Kitabu cha Mormoni kinafundisha: “Na walikuwa miongoni mwa watu wa Nefi, na pia wakahesabiwa miongoni mwa watu ambao walikuwa kwenye kanisa la Mungu. Na pia walitambulika kwa juhudi yao kwa Mungu, na pia kwa watu; kwani walikuwa wakamilifu na wa kuaminiwa na wa kusimama wima kwa vitu vyote; na walikuwa imara kwa imani yao ya Kristo, hadi mwisho” (Alma 27:27).

Kama wafuasi wa Yesu Kristo, hatupaswi kushauriana kanuni na kweli ambazo zimetuweka huru. Tunapaswa kuchagua kama vile watu wa Anti-Nefi-Lehi walivyofanya kwa kuwa waaminifu kikamilifu na wima katika mambo yote, bila kujali matokeo yangeweza kuwa nini.

Mnamo Agosti mwaka huu, tulijifunza kuhusu Ayubu kwenye Njoo, Unifuate. Alilindwa na kushinda majaribu kwa sababu ya imani yake na hususan kwa sababu ya uaminifu wake na uadilifu wake mwenyewe.

“Kama aishivyo Mungu, aliyeniondolea haki yangu; Huyo Mwenyezi aliyeitesa nafsi yangu;

“Kwa kuwa uhai wangu ukali mzima ndani yangu, Na roho ya Mungu i katika pua yangu;

“Hakika midomo yangu haitanena yasiyo haki, Wala ulimi wangu hautatamka udanganyifu.

“Haki yangu naishika sana, wala sitaiacha: Moyo wangu hautanisuta wakati nikiwapo hai” (Ayubu 27:2–4, 6).

Ni jinsi gani maisha ya Ayubu yalivyo ya kuvutia. Mungu alipendezwa na Ayubu na alisema haya kumuhusu: “Kwa kuwa hapana mmoja aliye kama yeye duniani, mtu mkamilifu na mwelekevu, mwenye kumcha Mungu na kuepukana na uovu, naye hata sasa anashikamana na utimilifu wake” (Ayubu 2:3).

Sifa hizi kuu za uaminifu na uadilifu zipo tele kwa ajili yetu. Ikiwa tutazitumia kikamilifu, zitatatua matatizo yote katika maisha yetu, ndoa zetu, familia zetu, jamii zetu, Kanisani na katika nchi zetu. Zitafuta majanga ya migogoro, kukosa uaminifu na huzuni (ona 2 Nefi 2:27).

Moja ya mafanikio makubwa ya maisha yetu kama wafuasi waongofu wa Yesu Kristo ni kukuza uaminifu, uadilifu wa kweli ndani yetu sisi wenyewe. Hii ina maana kwamba tunakuwa hai kiroho, wakweli kiakili, waaminifu kimaadili na daima wenye kuwajibika kwa Mungu.

Uaminifu na uadilifu ni funguo ambazo zitafungua milango ya mafanikio yoyote katika maisha yetu.

Tunapaswa daima kukumbuka kwamba kamwe hatuko peke yetu. Hakuna tendo ambalo halitatazamwa, hakuna neno linalozungumzwa ambalo halitasikilizwa, hakuna wazo linalofikiriwa ambalo halijulikani kwa Mungu. Hakuna giza ambalo linaweza kuficha mambo tunayofanya. Tumepewa uwezo wa kufikiri, kutafakari na kuchagua.

Kuwa mwaminifu kwako mwenyewe, kwa wengine na kwa Mungu. Usiseme uongo, usiibe, usilaghai au kudanganya katika njia yoyote.

“Unapokuwa mwaminifu, unajenga nguvu kwenye tabia ambayo itakuruhusu kuwa mwenye huduma kubwa kwa Mungu na kwa wengine. Utabarikiwa kwa amani ya akili na heshima binafsi. Utaaminiwa na Mungu na utastahili kuingia ndani ya mahekalu Yake matakatifu.”2

Kitabu cha Mormoni kinafundisha: “Wanadamu wapo ili wapate shangwe” (ona 2 Nefi 2:25). Shangwe hii huja kutokana na kuwa mwaminifu na kuishi kanuni za uadilifu mbele za wanadamu na mbele za Mungu.

Nilisoma hadithi hii ya kuvutia kuhusu uzoefu aliopata Rais Howard W. Hunter (1907–1995) ndani ya duka dogo huko California. Alimpa muuzaji senti 10 kwa ajili ya vipande 10 vya vitafunwa. Wakati akihesabu vipande baadaye, aligundua kwamba alikuwa na vipande 11 badala ya 10 alivyolipia. Wakati angeweza tu kupuuzia kosa—hata hivyo, ilikuwa senti tu na nani angejua tofauti—hakufikiri mara mbili na alirejea dukani. Alielezea tatizo kwa muuzaji, akaomba radhi na kulipia kipande cha ziada cha kitafunwa, akimwacha muuzaji akiwa na mshangao mkubwa3.

Wapendwa kaka zangu na dada zangu, wapendwa wavulana na wasichana, wapendwa watoto, ikiwa sisi si waaminifu katika mambo madogo, itakuwa ngumu sana kwa sisi kuwa waaminifu katika mambo makubwa.

Ikiwa tunaishi kulingana na kweli, ni waaminifu na tuko wima katika mambo yote na hatusikilizi shinikizo, vivuruga mawazo, tamaduni au mila za ulimwengu ulioanguka, Mwokozi anaahidi kwenu:

“Heri ninyi watakapowashutumu na kuwaudhi na kuwanenea kila neno baya kwa uongo, kwa ajili yangu.

“Furahini, na kushangilia; kwa kuwa thawabu yenu ni kubwa mbinguni” (ona Mathayo 5:11–12).

Ninajua kwamba maisha yetu yatakuwa ya shangwe na furaha tele ikiwa tutafanya mambo haya.

Muhtasari

  1. Russell M. Nelson, “Tenga muda kwa ajili ya Bwana”, Liahona, Nov. 2021, 120.

  2. Kwa Ajili ya Nguvu kwa Vijana [kijitabu, 2011], 19.

  3. Ona Teachings of Presidents of the Church: Howard W. Hunter [2015], 233.