2023
Kanisa Linaboresha Hali ya Elimu katika Jumuia ya Waganda wa Nakivale
Machi 2023


Habari za Eneo

Kanisa Linaboresha Hali ya Elimu katika Jumuia ya Waganda wa Nakivale

Shule sita zilipata uboreshaji muhimu kwenye nyenzo zao.

Makabidhiano ya shangwe yalifanyika katika makazi ya wakimbizi wa Uganda ya Nakivale mnamo Juni yakiashiria kukamilika kwa mradi mkubwa wa kuboresha hali ya elimu kwenye makazi.

Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho, kwa ushirikiano na shirika lisilo la kiserikali la Windle International Uganda, walisaidia shule sita kuboresha nyenzo zao muhimu za elimu katika eneo.

Kama sehemu ya mradi, Kanisa lilifadhili ujenzi wa madarasa ya kudumu 18 katika shule sita. Takriban madawati na viti 380 pia vilitolewa kama samani kwa madarasa yaliyojengwa.

Kwa nyongeza, Kanisa lilitoa kompyuta za mezani 20 kwa ajili ya matumizi kwa watoto wa Shule ya Sekondari Nakivale. Sambamba na hilo, uunganishwaji wa intaneti na mtandao wa data kwa miezi 12 kwa ajili ya Maabara ya kompyuta ya Shule ya Sekondari Nakivale ulifanyika. Hii itawapa wanafunzi fursa isiyo na kifani ya kufanya utafiti na kujifunza mtandaoni.

Mradi ulisaidia pia kutoa nyenzo za kujifunzia kwa baadhi ya shule kubwa kwenye eneo. Vitabu vya Mtaala Mpya wa Shule za Sekondari kwa ajili ya walimu na wanafunzi wa Shule ya Sekondari Nakivale vilitolewa. Chuo cha Mafunzo ya Ufundi cha Nakivale pia kilipokea rundo la nyenzo za mafunzo ya ufundi.

Nakivale ni mji wa wakaazi takriban 120,000 na inasemekana ni kambi ya wakimbizi ya nane kwa ukubwa ulimwenguni.

Waliohudhuria wakati wa sherehe za makabidhiano walikuwa Sala Odokodit kiongozi wa Kanisa kutoka Masaka, Uganda, Mzee na dada Bird, wamisionari wa kanisa wa Huduma za Kibinadamu na viongozi na wawakilishi kadhaa kutoka kwenye jumuia.

Mzee Bird aliwaambia wanajumuia na wanafunzi kwamba Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho liko “hapa ili kuwasaidia kaka zetu na dada zetu wapokee wingi wa vitu ambavyo Bwana Amevihifadhi kwa ajili yenu.”