2023
Wakati Unapohisi Umepoteza Vyote, Mgeukie Bwana
Machi 2023


Ujumbe wa Kiongozi wa Eneo

Wakati Unapohisi Umepoteza Vyote, Mgeukie Bwana

Nguvu ya mjane inamsaidia Mzee Balilemwa kujifunza kwamba yote hayajapotea ikiwa utaweka imani yako kwa Baba yetu wa Mbinguni.

Ninakumbuka uzoefu niliopata takriban miaka 20 iliyopita kama rais mpya wa mkusanyiko niliyeitwa punde tu. Wakati huo, mjane na mwanaye, wote wakiwa si waumini wa Kanisa, walikuwa wamehama kutoka magharibi ya jiji na kuja ndani ya mipaka ya mkusanyiko wetu.

Mapema asubuhi moja, mimi na mke wangu tulishangazwa kusikia hodi mlangoni kwetu. Niliharakisha kushuka ngazi ili nifungue mlango, ndipo nilimkuta mwanamke ambaye siku za karibuni tu alikuwa amehamia kwenye eneo lile akiwa amesimama mbele yangu.

Niliwa nimetatizwa kwa muda wa matembezi yake, nilimkaribisha ndani. Mara tu tulipoketi, alianza kuelezea jinsi ilivyokuwa vigumu kwake kuipata nyumba yetu, hakika, alikuwa amewasiliana na angalau waumini wengine watatu wa Kanisa siku moja kabla ili kujua mahali tulipoishi.

Machozi yakimtiririka, alishiriki nasi kile alichokuwa anapitia wakati huo. Kwa miaka mitatu iliyopita, alikuwa amefungwa katika vita ya kisheria yenye maumivu na ya kuchosha juu ya kile alichokiita “mashemeji zake wenye uwezo na umaarufu” juu ya nani alikuwa mrithi halali wa mali za marehemu mume wake.

Alielezea uzoefu wa uchungu ambapo maamuzi ya awali ya Mahakama Kuu, ambayo yalikuwa upande wake, yalipopinduliwa kwenye Mahakama ya Rufaa. Mgogoro huu endelevu wa kisheria pia ulimgharimu pesa zake zote na hakuwa tena na uwezo wa kuendelea nao.

Alipokuwa tayari kuhudhuria mahakamani asubuhi ile kusikia maamuzi ya mwisho kwenye kesi yake, alihisi kwamba tumaini lake pekee lilikuwa kupita nyumbani kwetu ili kuniomba nisali kwa ajili yake.

Wakati wa mazungumzo yangu na mwanamke yule, mawazoni mwangu nilikuwa nikimsihi Baba wa Mbinguni kwa ajili ya mwongozo juu ya jinsi ya kumpa faraja na kumhakikishia kwamba Bwana ni mwenye rehema, kwamba atashughulikia swala lile kikamilifu na kwamba yote aliyohitajika kufanya ni kuamini na kumtumaini Bwana kwa moyo wote.

Nilifikiria andiko hili kutoka kitabu cha Mithali: “Mtumaini Bwana kwa moyo wako wote; wala usizitegemee akili zako mwenyewe.

“Katika njia zako zote mkiri Yeye, naye atayanyosha mapito yako” (Mithali 3:5–6).

Baba wa Mbinguni anajua kile kilicho bora zaidi kwa kila mmoja wetu, kama vile Nabii Isaya alivyofundisha: “Maana mawazo yangu si mawazo yenu, wala njia zenu si njia zangu; asema Bwana.

“Kwa maana kama vile mbingu zilivyo juu sana kuliko nchi, kadhalika njia zangu zi juu sana kuliko njia zenu, na mawazo yangu kuliko mawazo yenu” (Isaya 55:8–9).

Nilifahamu alikuwa akitazamia mbingu kuingilia kati, muujiza na nilijua, kama vile Nefi alivyofundisha: “Na kwamba anajidhihirisha kwa wale wote wanaomwamini, kwa nguvu za Roho Mtakatifu; ndio, kwa kila taifa, kabila, lugha, na watu, akifanya maajabu makuu, ishara, na miujiza, miongoni mwa watoto wa watu kulingana na imani yao” (2 Nefi 26:13).

“Tafadhali sali kwa ajili yangu,” mwanamke alisisitiza, lakini nilihisi msukumo wa Roho wa Bwana kukataa kwa tahadhari. Badala yake, nilimhimiza amgeukie Baba yetu wa Mbinguni, nilimhakikishia kwamba yeye alikuwa binti Yake mpendwa, kwamba alimjua na alitaka kilicho bora kwa ajili yake na kwamba alipaswa kuamini na kutumaini katika Bwana Yesu Kristo.

Nilimwambia jinsi nilivyoheshimishwa, kama kijana mdogo, kuweza kutumainiwa na kisha nilimwalika yeye na mke wangu waungane nami katika kumsihi Baba yetu wa Mbinguni kupitia Mwana Wake, Yesu Kristo. Alikubali na wote watatu tulipiga magoti kumsihi Baba yetu wa Mbinguni katika sala ya dhati.

Baada ya hapo, niligundua mwonekano wa nje wa mwanamke ulikuwa umebadilika. Alionekana asiye na hofu na tayari kukabiliana na chochote mbele yake kwa ujasiri kamili, akitumaini kwamba Bwana atapigana vita kwa niaba yake, kama vile Nabii Isaya alivyofundisha: “Naam, Bwana asema hivi, Hata jeshi la wafungwa wake aliye hodari watapokonywa mikononi mwake, na mateka yake aliye jabari wataokoka: kwa maana nitateta na yeye atetaye nawe, nami nitawaletea wana wako wokovu” (Isaya 49:25).

Akiwa na hilo, aliondoka nyumbani kwetu na kuelekea mahakamani.

Nilistaajabu kwa kile kilichokuwa kimetokea siku hiyo. Nilijua kwamba kila sala ya dhati inasikiwa na kujibiwa na Baba yetu wa Mbinguni, lakini kwa kuwa majibu tunayopokea si mara zote kile tulichotarajia kiwe kwa wakati huo, nilijawa na wasiwasi kwa ajili ya mwanamke yule. Hata hivyo, baada ya muda, nilifarijiwa kwa mafundisho ya Mtume Paulo kwa Timotheo kwamba tunapaswa kuishi kwa imani na si kwa woga: “Maana Mungu hakutupa roho ya woga, bali ya nguvu na ya upendo na ya moyo wa kiasi” (2 Timotheo 1:7).

Nikitazama nyuma siku ile inajaza moyo wangu kwa shukrani ya kina kwa kufanyia kazi imani yangu katika Bwana Yesu Kristo. Mtume Paulo alifundisha: “Lakini pasipo imani haiwezekani kumpendeza: kwa maana mtu amwendeaye Mungu lazima aamini kwamba yeye yuko, na kwamba huwapa thawabu wale wamtafutao” (Waebrania God must believe that he is, and that he is a rewarder of them that diligently seek Him” (Hebrews 11:6).

Kwenye mkutano mkuu wa Aprili 2021 Rais Russell M. Nelson alifundisha: “Imani katika Yesu Kristo ni msingi wa kuamini kote na mfereji wa nguvu ya kiungu.

“Kila kitu chema kwenye maisha—kila baraka inayowezekana yenye umuhimu wa milele—huanza na imani. Kumruhusu Mungu ashinde katika maisha yetu huanza na imani kwamba Yeye yu tayari kutuongoza. Toba ya kweli huanza na imani kwamba Yesu Kristo anao huo uwezo wa kutusafisha, kutuponya na kutuimarisha.”1

Ninajua Bwana atatenda miujiza katika maisha yetu kulingana na imani yetu. Hata wakati ziku zijazo zinapoonekana za kutokuwa na uhakika kwetu, ni kwa kuwa na imani kwa Bwana, Yesu Kristo pekee, kwamba tunaweza kuhakikishiwa amani.

Kwenye mkutano mkuu wa Aprili 2022 Rais Nelson alifundisha: “Tafuta na tarajia miujiza.

“Bwana atakubariki kwa miujiza ikiwa unamwamini Yeye, bila shaka kwa jambo lolote. Fanya kazi ya kiroho ili kutafuta miujiza. kwa sala mwombe Mungu akusaidie ufanyie kazi aina hiyo ya imani. Ninaahidi kwamba unaweza kupata uzoefu kwa ajili yako mwenyewe kwamba Yesu Kristo ‘anatoa nguvu kwa waliochoka na kwa wao wasio na nguvu huwaongezea nguvu.’”2

Siku ambayo mimi na mke wangu tulitembelewa na mjane, alinipigia simu kuniambia kuhusu maamuzi ya mwisho kwenye kesi yake. Alisema kwa shangwe: “Tumeshinda, tumeshinda! Imefika mwisho; Mungu wetu ni mwema!” Moyo wangu ulilainika kwa hisia za shukrani na unyenyekevu. Daima nitakuwa mwenye shukrani kuwa na uzoefu wa namna ile katika miaka ya mwanzo ya huduma yangu.

Baada ya miaka yote hii katika huduma Yake, ninatangaza hata kwa uhakika zaidi kwamba Mwokozi daima yu tayari kutusaidia pale tunapokumbuka kusihi Kwake: “Nitegemeeni katika kila wazo; msitie shaka, msiogope” (Mafundisho na Maagano 6:36).

Wakati mjane alipotambua kwamba rasilimali zake zote zilikuwa zimepotea na kwamba maadui wenye uwezo na umaarufu walisimama kwenye njia yake, alijua wapi hasa pa kugeukia na nani wa kumpa imani na tumaini lake: Baba yetu wa Mbinguni.

Tunakuwa salama juu ya mwamba ambao ni Yesu Kristo wakati tunapokuwa tumeweka imani yetu Kwake, kama vile mjane alivyofanya.

Muhtasari

  1. Russell M. Nelson, “Kristo Amefufuka; Imani Kwake Itahamisha Milima”, Mkutano mkuu wa Aprili 2021.

  2. Russell M. Nelson, “Nguvu ya Msukumo wa Kiroho”, Mkutano mkuu wa Aprili 2022.

Chapisha