2023
Akina Kaka na Akina Dada katika Bwana
Septemba 2023


“Akina Kaka na Akina Dada katika Bwana,” Liahona, Sept. 2023.

Akina Kaka na Akina Dada katika Bwana

“Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee”—na Yeye alitupa sisi mmoja na mwingine.

Kristo akimfufua mwana wa mjane wa Naini

Kristo anamfufua mwana wa mjane wa Naini.

Akisafiri kutoka Kapernaumu, Mwokozi wetu alienda katika mji uitwao Naini. Karibu na lango la mji, Yeye aliona msafara wa mazishi. Kifo kisichotarajiwa cha mwana wa pekee kilimuacha mjane masikini peke yake.

“Bwana alipomwona alimwonea huruma akamwambia, Usilie.

“Akakaribia, akaligusa jeneza; wale waliokuwa wakilichukua wakasimama. Akasema, Kijana, nakuambia, Inuka.

Yule kijana alipoketi na akaanza kusema, Yesu “akampa mama yake” (ona Luka 7:11–15; msisitizo umeongezwa).

Kote katika huduma Yake, iwe ni 1 au ni 99,1 Mwokozi wetu kwa ukamilifu anaonesha mfano wa huruma, imani, tumaini, hisani, upendo, msamaha, rehema, na huduma.2 Yeye anamwalika kila mmoja wetu “Njoo, Unifuate” (Luka 18:22) na kuwa “kama vile nilivyo” (3 Nefi 27:27).3

“Hata vile nilivyo”

Ili kufuata mfano kamili wa Mwokozi wetu na kuwa kama Yeye alivyo, tunakubali mwaliko wa kutembea pamoja Naye kwenye njia Yake ya agano (ona Musa 6:34). Sisi wakati mwingine tunatambua njia ya agano kupitia ibada za wokovu na kuinuliwa ambazo zimebainishwa—ubatizo na uthibitisho ili kupokea kipawa cha Roho Mtakatifu na kuwa muumini wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho; kutawazwa katika Ukuhani wa Melkidezeki (wanaume); endaumenti katika nyumba ya Bwana (kwa kila mmoja wetu kama mtu binafsi); na kuunganishwa hekaluni.

Ibada ambayo ni muhimu kwa ajili ya wokovu na kuinuliwa ni tendo takatifu linalofanywa kwa mamlaka yaliyoidhinishwa ya ukuhani ambayo hutufundisha agano ambalo kwalo ibada inahusika. Kwa njia fulani, tunaweza kufikiria ibada ya wokovu na kuinuliwa kama tendo la nje ambalo huleta uhusiano wa kuunganishwa na Mungu na Mwanawe Mtakatifu katika maisha yetu kwa agano.

Kila mmoja wetu, kama mwana au binti mpendwa wa Mungu, hufanya maagano yetu matakatifu na Mungu. Tunafanya hivyo kama watu binafsi, katika jina letu wenyewe, mmoja mmoja. Huu muunganiko na Mungu wa maagano humpa kila mmoja wetu nguvu, tumaini, na ahadi. Maagano haya yanaweza kubadilisha asili yetu hasa, kutakasa matamanio yetu, na vitendo vyetu, na kutusaidia kumweka mwanamume wa asili au mwanamke wa asili kando pale tunapokubali ushawishi wa Roho Mtakatifu. Kwa agano, kupitia Upatanisho wa Kristo Bwana, kila mmoja wetu anaweza kuwa kama mtoto wa Mungu—“mtiifu, mpole, mnyenyekevu, mwenye subira, mwenye upendo tele” (Mosia 3:19).

Kutumikia Pamoja kwa Agano

“Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee”(Yohana 3:16)—na Yeye alitupa sisi mmoja na mwingine. Agano la kuwa wa—kuunganika na Mungu na mmoja na mwingine kwa agano—hutualika sisi kutimiza utambulisho mtakatifu na dhumuni kwa kuwasiliana na mbingu na kuunganika na kuunda jamii ya Watakatifu tunapowapenda na kuwatumikia wale walio karibu nasi. Katika kutoa fursa kwa ajili ya msimamo wa agano na kuwa wa agano, Mungu hana upendeleo. Yeye humwalika kila mmoja wetu, wanawake na wanaume, waliooana au waseja, bila kujali sisi ni akina nani na hali zetu, kuja Kwake na kwa kila mmoja kwa agano.

Tunapokuwa wa agano na Bwana, sisi pia tunakuwa wa agano na kila mmoja. Mambo ya kupendeza hutendeka tunapompenda Bwana na kushirikiana, kushauriana, na kutumikiana. Huduma ya agano huimarisha uhusiano na Bwana na mmoja na mwingine. Hii hujumuisha uhusiano wetu binafsi na Baba yetu wa Mbinguni, familia, mkusanyiko wa Kanisa, jamii, na vizazi vya familia. Tunapoishi maagano yetu, tunapoteza uchoyo wetu na kupata kiini chetu katika Kristo.

Mpango Mtakatifu wa Furaha wa Mungu

Katika mpango mtakatifu wa furaha wa Mungu, Rais Russell M. Nelson alisema “mbingu ziko wazi kwa wanawake ambao wamepokea endaumenti ya nguvu ya Mungu ikitiririka kutoka kwenye maagano yao ya ukuhani kama ilivyo kwa wanaume ambao wana ukuhani.”4

Alisema Rais Camille N. Johnson, Rais Mkuu wa Muungano wa Usadizi, “Sisi tuna haki ya kupata nguvu za ukuhani kwa sababu ya ustahili binafsi.”5 Akimnukuu Rais Nelson, alisema, “Tunahitaji wanawake ambao wanajua jinsi ya kufikia nguvu ambazo Mungu huzitoa kwa washika maagano.”6 Washika maagano ambao hutafuta na kuishi kwa imani, unyenyekevu, na bidii, Rais Johnson alifunza, wanaweza kupokea mwongozo, uvuvio, vipawa vya Roho, ufunuo, na “msaada na nguvu za kuwa zaidi kama Yesu Kristo na Baba wa Mbinguni.”7 Tunapotoa vipawa vyetu vya kipekee katika ushirikiano na Bwana na kila mmoja, tunatengeneza “mwili mmoja” (1 Wakorintho 12:13).

Katika mpango wa Mungu, akina mama na akina baba ni wenza na wasaidizi. Tunasaidiana mmoja na mwingine kama wenza sawa katika upendo na wema ili kuleana na kutunzana mmoja na mwingine na familia zetu. Usafi wa mawazo na tabia ni kitu kinachohitajika kwa ajili ya ufunuo na mwongozo kwa wanawake na wanaume. Katika nyumba zao, akina baba na waume wanapaswa kusimamia kwa ukarimu, unyenyekevu, na upendo usiyo na unafiki—sifa njema ambazo wanaume na wanawake wanahitaji katika mahusiano yetu yote.8

Mbingu hulia wakati, katika uhusiano wowote, kuna unyanyasaji, ukandamizaji, au ulazimishaji wa aina yoyote kwa wanaume au wanawake. Ushawishi, uvumilivu, ukarimu, na maarifa safi ni sifa kama za Kristo ambazo kila mmoja wetu anazitafuta—iwe tumeoana, ni waseja, wajane, au watalikiwa (ona Mafundisho na Maagano 121:41–42). Hii ni kwa sababu msimamo wetu mbele za Bwana na katika Kanisa Lake unaamuliwa na tabia zetu na wema wetu binafsi katika kushika maagano.

wanaume na wanawake wakiwa wamekusanyika katika mkutano wa baraza

Kushauriana katika Baraza

Katika roho hii hii, katika Kanisa la Bwana tunashauriana katika baraza tunapotumikia pamoja. Katika mabaraza yetu, viongozi hutafuta umaizi na mawazo kutoka kwa wote. Ninamshukuru kila mmoja wa hawa wanawake na wanaume wa kipekee ambao nimepata nafasi ya kutumikia nao, bega kwa bega, katika mabaraza simamizi ya Kanisa. Akina dada na akina kaka waungwana husaidia kukusanya Israeli kupitia huduma ya umisionari, hutuandaa kukutana na Mungu kupitia ukuhani na huduma ya familia, huunganisha familia kwa umilele kupitia huduma ya hekalu na historia ya familia, na huwahudumia wale walio na mahitaji kupitia huduma ya kujitegemea.

Katika kila hali, tunafikia maamuzi bora na ufanisi mkubwa katika huduma ya Bwana tunapothamini michango ya kila mmoja na kufanya kazi pamoja, akina kaka na akina dada katika kazi Yake.

Vivyo hivyo, nina shukrani kwamba, katika vigingi vyetu na kata zetu, akina kaka na akina dada viongozi na waumini wanaungana katika kazi ya wokovu na kuinuliwa. Kote Kanisani, chini ya maelekezo ya viongozi wa misheni waliojitolea, mabaraza ya uongozi wa misheni hujumuisha mzee na dada kiongozi mfunzaji ambaye huwaongoza wamisionari wetu, kila mmoja ambaye kazi na majukumu yake yanathaminiwa na ni muhimu. Katika jeshi la Marekani, makasisi Watakatifu wa Siku za Mwisho, maofisa wanaume na wanawake waliothibitishwa na Kanisa, hubariki wale wanaotumikia katika matawi mbalimbali ya huduma.9 Katika uhudumiaji, wavulana na wasichana wetu wana fursa na hitaji la kutumikia. Katika huduma yetu, sisi sote tunasimama pamoja.

Njia moja ya kusimama kama mashahidi wa Mungu ni kutumikia kama mashahidi wa ibada za injili ya urejesho. Akina dada na akina kaka husimama kama mashahidi wa ubatizo, kwa ajili ya wote walio hai na wafu. Akina kaka na akina dada husimama kama mashahidi kwa ajili ya ibada za ziada katika nyumba ya Bwana. Hapa, chini ya funguo za rais wa hekalu, akina dada hufanya ibada takatifu kwa niaba ya akina dada na akina kaka.

Katika mpango mtakatifu wa Mungu, Rais Dallin H. Oaks, Mshauri wa Kwanza katika Urais wa Kwanza alisema, “nguvu za ukuhani hutubariki sisi sote. Funguo za ukuhani huelekeza wanawake vile vile wanaume, na ibada za ukuhani na mamlaka ya ukuhani ni kwa wanawake na vile vile kwa wanaume. … Yeyote anayefanya kazi katika ofisi au wito aliopokea kutoka kwa yule anayeshikilia funguo za ukuhani mtu huyo hutumia mamlaka ya ukuhani katika kutimiza majukumu yake.”10

Inuka juu ya Ulimwengu

Tunapojitahidi “kuwa na umoja,” hata kama vile Yesu Kristo alivyo na umoja na Baba (Yohana 17:21), sharti “tumvae … Bwana Yesu Kristo”.(Warumi 13:14).

Tunaweza kutakaswa wakati, neema kwa neema, tunapojifunza na kufanya sifa za Yesu Kristo ziwe zetu—ili tupende kwa ukamilifu zaidi, tusamehe kwa urahisi zaidi, tuhukumu kidogo tu, tutumikie na kufanya dhahibu zaidi, tuwe mfano wa huruma zaidi na zaidi kila mara.

Acha tutumainie fundisho na mfano wa Kristo, tukifurahia katika ukweli na kuwa wafuasi Wake wanyenyekevu (ona 2 Nefi 28:14)—kila mmoja wetu binafsi na kama akina kaka na akina dada katika Bwana.11