“Ningetaka Mkumbuke,” Liahona, 2023.
“Ningetaka Mkumbuke”
Mosia 5:12
Kila mmoja wetu amepatiwa vikumbusho binafsi vya Kristo. Vitegemee na mkumbuke Yeye.
Kama sehemu ya maisha yetu ya duniani, sote hatuko tu chini ya pazia la usahaulifu bali pia hali ya usahaulifu. Pazia la usahaulifu hutufanya sisi tusahau mandhari na kweli tulizozijua katika hali yetu kabla ya kuzaliwa. Hali yetu ya usahaulifu hutuongoza kusahau na kuchepuka kutoka kwenye kweli tulizojifunza au kujifunza tena katika maisha haya. Isipokuwa tushinde hali yetu ya kuanguka ya usahaulifu, kiuhalisia tutakuwa “wepesi kwa kutenda maovu lakini wanyonge kumkumbuka Bwana Mungu [wetu]” (1 Nefi 17:45).
Vikumbusho vya Kristo
Kwa kila amri Yeye anayoitoa, Mungu anaahidi “kututayarishia [sisi] njia ya [sisi] kutimiza kitu ambacho ametuamuru” (1 Nefi 3:7). Ili kwamba tuweze kutii amri Yake ya kukumbuka, Bwana alitayarisha vikumbusho.
Hakika, vitu vyote vimeumbwa na vimefanywa ili kutushuhudia na kutukumbusha kuhusu Kristo (ona Musa 6:63; ona pia Alma 30:44). Imedhamiriwa, kwa mfano, kwamba tumkumbuke Yeye wakati “twatembea kwenye miti na uwanda wa mwitu, na kusikia ndege wakiimba kwa uzuri katika miti.”1 Mawe yanaweza hata kupaza sauti kama ushuhuda na ukumbusho wa Yesu (ona Luka 19:40). Kwa kweli, ulimwengu wote, kwa sauti na kuona, hutoa ushahidi wa ajabu na hutoa vimbusho vya kustaajabisha juu ya Muumba wake.
Vikumbusho vinavyoonekana vya hovyo katika uumbaji wote ndivyo vinavyopewa ukubwa na vikumbusho rasmi tunavyovipata katika ibada takatifu. Abinadi alifundisha kwamba Israeli ya kale walipewa ibada kali za kufanya ili “kuwakumbusha kuhusu Mungu na jukumu lao Kwake” (Mosia 13:30). Manabii wa siku za leo wamefundisha jambo hilo hilo. Rais Spencer W. Kimball (1895–1985) alitangaza, “Nadhani kamwe hakungekuwa na ukengeufu, kamwe hakungekuwepo uhalifu, kama watu wangekumbuka, wangekumbuka hasa, mambo waliyoyawekea agano katika kingo za maji au katika meza ya sakramenti na hekaluni.”2
Upatanisho wa Kristo ni kwa wote na kwa mtu binafsi. Vivyo hivyo vikumbusho Vyake. Kwa hivyo, kama nyongeza kwenye ibada zinazofanana zinazotolewa kwa wote, Yeye hutupatia vikumbusho Vyake vilivyo tofauti na binafsi. Kwa mfano, udongo au tope la kawaida yawezekana lisisababishe watu wengi kumkumbuka Yesu au kufurikwa na hisia na shukrani kwa ajili Yake. Lakini bado mtu ambaye uoni wake ulirudishwa wakati Yesu alipopaka macho yake udongo pengine alimkumbuka Yesu kwa furaha kila wakati alipotazama udongo au tope! (ona Yohana 9:6–7). Pia yawezekana kwamba Naamani asingeweza kuuona mto, hasa Yordani, pasi na kufikiria juu ya Bwana ambaye alimponya yeye pale (ona 2 Wafalme 5:1–15). Kila mmoja wetu amepatiwa kikumbusho kimoja binafsi au zaidi vya Kristo. Vitegemee na mkumbuke Yeye.
Kumshuhudia Kristo
Kumbukumbu na historia ni mambo ya ziada ambayo Bwana alisababisha yaandaliwe ili yatusaidie tutii amri Yake ya kukumbuka. Maandiko—kumbukumbu za shughuli za Mungu kwa watoto Wake—huzumgumza mara nyingi kuhusu kutoa ushahidi, au “kushuhudia,” juu Yake (ona 2 Wakorintho 8:3; 1 Yohana 5:7; 1 Nefi 10:10; 12:7; Mafundisho na Maagano 109:31; 112:4).
Kumbukumbu takatifu, ikijumuisha shajara binafsi, hutusaidia kushuhudia. Nyakati za kina na Roho ni zawadi ambayo, kwa sasa, tunaamini kamwe hatutazisahau. Lakini hali yetu ya usahaulifu husababisha msisimko wa hata uzoefu wa kina sana kufifia pale muda unapopita. Ingizo la shajara, picha, au kumbukumbu inaweza kutusaidia siyo tu kukumbuka nyakati za kina lakini pia hurudisha hisia na Roho tuliyemhisi. Haishangazi, basi, kwamba amri ya kwanza baada ya Kanisa kuanzishwa katika kipindi hiki ilikuwa, “Pawepo na kumbukumbu itakayotunzwa miongoni mwenu” (Mafundisho na Maagano 21:1). Kumbukumbu iliyotunzwa vizuri hukuza kumbukumbu yetu na inaweza kutushawishi juu ya makosa yetu na kutuleta kwa Mungu (ona Alma 37:8).
Hatimaye, bila shaka, tunaweza kushuhudia juu ya ukweli kwa sababu tumepokea ushahidi wa ukweli kutoka kwa Roho Mtakatifu, ambaye ndiye “kumbukumbu ya mbinguni” (Musa 6:61). Katika wajibu huu, Roho Mtakatifu huandika ukweli katika “vibao ambavyo ni mioyo [yetu] ya nyama” (2 Wakorintho 3:3). Yeye hutusaidia kumkumbuka Kristo na kila kitu ambacho Yeye ametufundisha (ona Yohana 14:26).
Muunganiko kati ya Yesu, kumbukumbu, Roho Mtakatifu, na kukumbuka unaonyeshwa katika Moroni 10:3–5. Tumeahidiwa kwamba kama tutasoma Kitabu cha Mormoni, kumbukumbu takatifu, katika roho ya kukumbuka na kumwomba Mungu katika jina la Kristo kwa moyo wa dhati, kwa kusudi halisi na imani katika Kristo, Roho Mtakatifu atadhihirisha kwetu ukweli wa kumbukumbu hii. Na kama kumbukumbu hiyo ni ya kweli, basi Yesu ndiye Kristo.
Kumbuka Kukombolewa
Kumkumbuka Yesu huongoza kwenye ukombozi na wokovu. Fikiria wajibu ambao kukumbuka kulileta katika ukombozi wa Alma mdogo. Wakati malaika alipomtokea Alma, alileta amri kwa ajili ya Alma “usijaribu kuangamiza kanisa tena.” Lakini hata kabla ya kutoa hiyo amri, malaika alitangaza, “Ukumbuke utumwa wa babu zako … na kumbuka vile vitu vikuu ambavyo [Kristo] amewatendea; kwani walikuwa utumwani, na Yeye … amewakomboa” (Mosia 27:16; msisitizo umeongezewa).
Mamlaka ya malaika ya kukumbuka hayakuwa tu elekezo la hekima lenye matumizi mapana. Kwa ajili ya Alma, lilikuwa dokezo mahususi, dokezo la upendo, kwa ajili ya jinsi ambavyo angenusurika uzoefu wa kifo aliokuwa karibu kuupata.
Miaka ishirini au zaidi baadaye, Alma alishiriki na Helamani mwanawe, katika utondoti wa aina ya kuvutia, kile ambacho yeye alipitia alipokuwa amelala hajiwezi na bila kusema kwa siku tatu, “kukaribia kifo kwa kutubu” (Mosia 27:28). Baada ya malaika kuondoka, Alma alikumbuka, sawa; lakini yote aliyoweza kukumbuka ilikuwa ni dhambi zake.
“Nilisumbuliwa na adhabu ya milele,” Alma alikumbuka. “… Ndiyo, nilikumbuka dhambi zangu zote na uovu, kwa ajili hiyo niliadhibiwa na uchungu wa jahanamu” (Alma 36:12–13). Wazo la kusimama mbele za Mungu lilimjaza Alma kwa “hofu kuu isiyoelezeka” kwamba alifikiria kutoroka, siyo tu kwa kufa bali kwa “kutokuwepo kwa nafsi wala mwili” (Alma 36:14–15).
Hapa tunapaswa kutua na kuelewa: Alma si tu alikuwa analipia adhabu kali ya siku tatu ambayo ilikuwa imeamuliwa mapema kuwa matokeo sahihi kwa ajili ya dhambi zake. La, yeye alikuwa mwanzoni mwa hitimisho—siku tatu za kwanza—za “kuzungukwa na minyororo ya kifo kisicho na mwisho” (Alma 36:18).
Hakika, angebakia katika hali hiyo mbaya kwa zaidi ya siku tatu—bila kikomo—isingekuwa ukweli kwamba, kwa rehema, yeye kwa njia fulani, mahali fulani, alikumbuka kwamba baba yake alikuwa ametoa unabii “unaohusu ujio wa Yesu Kristo, Mwana wa Mungu, kuleta upatanisho kwa ajili ya dhambi za ulimwengu.” Kisha alisema:
“Sasa, nilipofikiria wazo hili, nililia ndani ya moyo wangu: Ee Yesu, wewe Mwana wa Mungu, nihurumie, mimi ambaye nina uchungu, na nimezungukwa na minyororo ya kifo kisicho na mwisho.
“Na sasa, tazama, nilipofikiri hivi, sikukumbuka uchungu wangu tena; ndio, sikuteseka na ufahamu wa dhambi zangu tena” (Alma 36:17–19).
Alma alikuwa amefuata amri ya malaika ya kukumbuka. Alimkumbuka Yesu. Na kama vile tu Yesu alivyokuwa amewakomboa mababu wa Alma kutoka utumwani, Yeye alimkomboa Alma kutokana na utumwa wake.
Ni rehema nyororo na ukombozi mkuu kiasi gani! Ni badiliko la moyo na akili la kushangaza jinsi gani! Alma, ambaye muda mchache mapema alifikiria kutoroka kutoka uwepo wa Mungu kwa kutokuwepo kwa nafsi wala mwili, sasa alimwona Mungu na malaika Zake watakatifu na “alitamani kuwa hapo” (Alma 36:22).
Mabadiliko ya kimiujiza yalianzishwa na ukumbusho tu. Uzoefu wa Alma unatoa maana halisi ya maneno ya mwisho ya mahubiri ya Mfalme Benyamini: “Na sasa, Ee mwanadamu, kumbuka, na usiangamie” (Mosia 4:30).
Yeye Anatukumbuka Sisi
Tunapojitahidi daima kumkumbuka Yesu, ni muhimu kuelewa kwamba Yeye daima anatukumbuka sisi. Yeye ametuchora katika viganja vya mikono Yake (ona Isaya 49:16). Fikiria hilo, Yesu mwenye fadhili hatatusahau, hawezi, kutusahau, na bado Yeye kwa urahisi sana na kwa hiari husahau dhambi zetu ambazo zilimchubua.
Hilo ni la thamani kukumbuka.