2023
Kupata na Kuonesha Huruma
Septemba 2023


“Kupata na Kuonesha Huruma,” Liahona, Sept. 2023.

Vijana Wakubwa

Kupata na Kuonesha Huruma

Mfano kamili wa Mwokozi hutufundisha nguvu za kuonesha huruma ili kuwabariki wengine.

mtoto akilia akiwa kwenye ndege

Je, unapata nini unapochanganya ndege ndogo na mama aliyezidiwa na majukumu na mvulana mdogo anayesababisha kero? Hali ya usumbufu sana. Kutoka kwenye safu chache nyuma, nilitazama mambo yakijitokeza. Ilikuwa kitu kama hivi:

Mvulana mdogo: nahisi njaa!

Mama: Basi, acha niangalie kwenye mkoba wangu nione nilichonacho.

Mvulana mdogo: Hapanaaa!

Mama: Lakini si unahisi njaa?

Mvulana mdogo: Nipe hicho!

Mama: Nikupe nini?

Mvulana mdogo: Hichooo!

Mama: Kipenzi, siwezi kukupa mkufu wangu.

Mvulana mdogo: Nautaka!

Unaelewa vyema. Kwa zaidi ya dakika 20 zilizofuata, mama yule alitumia mbinu tofauti tofauti kujaribu kumtuliza: hongo, mchepuo, ucheshi, hata vitisho kadhaa. Haikufua dafu. “Ni safari fupi tu,” nilijikumbusha. “Atakuwa SAWA.”

Lakini hakuwa SAWA. Usumbufu ulizidi, na akaanza kufuta machozi kutoka kwenye macho yake. Ingawa sikumjua, nilihisi kuvutwa kumsaidia. Bila kujua, nilianza kuwaombea wote wawili.

Sikuwa abiria pekee aliyeathiriwa na jambo hili. Pale tu hisia zilipofika kilele, abiria mwingine alikuja kumsaidia. Alikuwa mwanamke mzee kidogo, aliyekuwa ameketi upande mwingine wa njia. Kwa ukarimu mwangavu, alimgeukia yule mama kijana, kwa utulivu alizungumza maneno machache ya hakikisho na aliushika mkono wake. Hivyo tu. Na hiyo ilitosha.

Wanawake hawa wawili waliendelea kushikana mikono katika safari yote iliyobakia. Ingawa yule mvulana mdogo aliendelea kupiga kelele kwa wingi sana, mama yake alionekana kuwa shwari. Ilikuwa ni muujiza.

Huruma na Rehema: Sifa Mbili za Ufuasi

Katika msamiati wetu wa kisasa, muujiza huu una jina: huruma. Huruma, kwa ufafanuzi, ni kitendo nyeti cha kupata uzoefu kwa niaba ya mtu mwingine, kwa mawazo, hisia, au matukio. Huruma ni neno la kisasa; hutalipata mahala popote katika maandiko. Lakini wataalamu wa lugha wameona kwamba huruma inahusiana kwa karibu sana na rehema. Na kama neno la kimaandiko, rehema lipo kwa wingi.

Huruma ni uwezo wa kujihusisha na uchungu wa mtu mwingine, na rehema ni tendo la hisani ambalo linatokana na uwezo huo. Yesu Kristo alionesha vyote huruma na rehema alipokuwa anahudumia, kubariki, kuponya, na kufanya upatanisho. Kama wafuasi wa Kristo, sharti tujifunze kupata uzoefu wa huruma na kuonesha huruma. Hii ni miongoni mwa sifa za ufuasi.

Wakati huruma inapofanya maajabu yake makubwa, hutusaidia kufahamu na kisha kuitikia uchungu wa mtu mwingine, uhitaji, hofu, au huzuni. Katika hali ya huyu mama kijana, mwanamke mzee ambaye tukidhania alikuwa na uzoefu wa miongo mingi wa kuwatunza watoto na wajukuu angeweza kutoa faraja kwa sababu alikuwa amepitia magumu kama hayo yeye mwenyewe. Kwa sababu ya uzoefu wake, yeye alikuwa na sifa za kutenda kama mfariji.

Ni nini kinachompa sifa Yesu Kristo kutufariji sisi? Mzee Neal A. Maxwell (1926–2004) wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili alifundisha: “Yesu anajua jinsi ya kutusaidia sisi katikati ya majonzi yetu na magonjwa yetu kwa usahihi kwa sababu Yesu tayari amejichukulia majonzi yetu na magonjwa yetu [ona Alma 7:12–13]. Yeye anayajua moja kwa moja; kwa hiyo huruma Yake imelipia.”1

Yesu akiwatembelea Wanefi

Kristo katika Nchi ya Neema, na Simon Dewey

Kupata Huruma na Kuwasaidia Wengine

Ni magumu yapi umevumilia ambapo kupitia hayo “umepata” uwezo wa kuwahurumia wengine na kuonesha rehema kwao? Je, wewe umeteseka athari za umaskini, unyanyasaji, ujinga, maradhi, kutelekezwa, dhambi, au usumbufu wa aina yoyote. Kama ulipitia hayo, pengine uliibuka kutoka kwenye mateso yako ukiwa mwenye hekima zaidi, imara zaidi na mwanadamu mwenye kuelewa zaidi.

Kwa kifupi, umelipia huruma. Uko tayari kuleta tofauti katika maisha ya wale wanaoteseka. Wapi pa kuanzia? Nina mapendekezo mawili:

Kwanza: jitahidi kuwa msikivu zaidi kwa mateso ya wengine. Cha kuhuzunisha, kuna uwezekano kuwa na mtu aliye na uchungu na ilhali kubakia kutojali mateso yao. Ni kwa jinsi gani tunaweza kuwa wasikivu zaidi? Mfano wa Yesu Kristo unaweza kutufundisha.

Baada ya Ufufuko Wake, wakati Yesu Kristo alipowatembelea Wanefi, Alifafanua mafundisho Yake na kuwafundisha injili. Wakati aliponyamaza, Aliwatazama watu na kusema, “Ninahisi kwamba nyinyi ni wadhaifu, kwamba hamwezi kufahamu maneno yangu yote” (3 Nefi 17:2). Yesu kisha aliwaambia waende nyumbani, wakapumzike, wakatafakari mafundisho Yake, na warudi kesho yake wakiwa wamejitayarisha na tayari kwa mengine zaidi (ona 3 Nefi 17:3).

Mwisho wa hadithi, sivyo? Bado. Usikivu wa Yesu kisha unaongezeka pale Yeye anapoagalia nyuso za wafuasi Wake:

“Na ikawa kwamba baada ya Yesu kusema hivyo, alielekeza macho yake tena kwa umati, na akaona kuwa wanalia, na walikuwa wanamwangalia kwa uthabiti kama wanaotaka kumwomba akae nao kwa muda mrefu zaidi.

Na akawaambia: Tazama, matumbo yangu yamejawa na huruma juu yenu” (3 Nefi 17:5–6). Na Yeye alipowaangalia kwa kusudi halisi, aliwaona kwa ukamilifu zaidi. Na hii ilichochea jibu Lake la huruma.

Katika ulimwengu ulioanguka uliojaa watu walioanguka, hatuhitaji kutazama sana kuona machozi katika macho ya watoto wa Baba yetu wa Mbinguni. Lakini tunapaswa kutazama. Kama Mwokozi, tunaweza kuchagua kuwaona watu kupitia lenzi ya mahitaji yao. Na mara tunapoweza kuona, tunaweza kutumikia.

Mzee Ulisses Soares wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili alisema kwamba “tunapojitahidi kwa kukusudia kuhusisha mtazamo wa huruma katika njia ya maisha yetu, kama ilivyoonyeshwa kwenye mfano na Mwokozi, tutakuwa makini sana kwenye mahitaji ya watu. Kwa ongezeko hilo la umakini, hisia za dhati za kujali na upendo zitapenya katika kila tendo letu.”2

Pili, toa aina ya msaada ambao wewe pekee ndiye mwenye sifa ya kuutoa. Baada ya Yesu kujua mahitaji ya Wanefi huko nchi ya Neema, aliwaita karibu. Kisha aliwaponya wagonjwa wao na kuwabariki watoto wao. Yeye alifanya vitu ambavyo Mwokozi wa ulimwengu pekee angevifanya.

Wewe pamoja na mimi vilevile tunaweza kuoanisha uzoefu wetu na uwezo wetu kukidhi mahitaji ya wengine. Hatuwezi kusuluhisha shida za kila mtu, lakini tunaweza kuinua mzigo wa wale wanaoteseka ambao mateso yao tunaweza kuwa tumeyapitia. Labda tusiweze kumponya mkoma, lakini tunaweza kuwafariji wagonjwa. Labda tusiweze kumwinua mtu kutoka kwenye umasikini, lakini tunaweza kushiriki kanuni za kuishi ndani ya kipato, kushiriki mlo, na kuchangia matoleo ya mfungo kwa ukarimu zaidi. Labda tusiweze kusamehe dhambi, lakini tunaweza kuwasamehe wale waliotukosea.

Kuweka Huruma katika Vitendo

Je, unapata nini unapochanganya ndege ndogo na mama aliyezidiwa na majukumu na mvulana mdogo anayesababisha kero? Nafasi ya kuonyesha huruma na rehema.

Ndege yetu ilitua na mama kijana akashuka, begi mkono mmoja, mvulana mkono mwingine. Ilitokea kwamba alikuwa na ndege nyingine ya kupanda na alikuwa karibu kuikosa. Nilitazama wasiwasi wake kwenye lami wakati mizigo yake ikitolewa. Nilihesabu mizigo yake: gari la kutembelea mtoto, kiti cha kwenye gari, sanduku, begi la mkononi, begi la nepi. Alihitaji msaada. Huruma yangu ilihitaji kukua kuwa rehema.

Bila kujitambulisha, nilichukua mizigo yake mingi na kusema, “Nitabeba hii. Mbebe huyu. Kimbia langoni. Nitakufuata.” Alikubali kwa heshima, na tukakimbia uwanjani. Tulipokuwa tunafika langoni, nilimwona mwanamke akimsihi mfanyakazi wa ndege kuzuia ndege isiondoke kwa dakika chache tu. Tulifika pumzi zikiwa zimetuishia lakini tukiwa washindi. Mwanamke kijana na mwanake huyu walikumbatiana kwa machozi ya shangwe na faraja kabla ya kuingia ndani ya ndege.

Kitendo hiki kidogo cha huduma hakikubadilisha ulimwengu, lakini kilibariki maisha ya mtoto wa Mungu mwenye uhitaji. Kama vile tu kilivyomsaidia rafiki yangu mpya kuelekea mwisho wa safari yake, kilinisaidia kuendelea kwenye safari yangu ya kiroho. Kuchagua huruma na rehema kulinisaidia kuwa zaidi kama Yesu Kristo. Na hii inifurahisha.

Haijalishi pale tulipo—kazini au shuleni, kanisani au kwenye ndege—tunaweza kuwa wawakilishi wa Mwokozi wenye huruma. Ni nani Mwokozi angetoa huruma kwake leo?

Muhtasari

  1. Neal A. Maxwell, “From Whom All Blessings Flow,” Ensign, May 1997, 12.

  2. Ulisses Soares, “Huruma ya Kudumu ya Mwokozi,” Liahona, Nov. 2021, 14.