2023
Kuponywa Hekaluni
Septemba 2023


“Kuponywa Hekaluni,” Liahona, Sept. 2023.

Sauti za Watakatifu wa Siku za Mwisho

Kuponywa Hekaluni

Hekaluni, nilihisi hakikisho la kina kwamba Bwana ananipenda na anajali mapambano yangu.

wanandoa mbele ya hekalu

Picha kwa hisani ya mwandishi; usuli wa picha ya Hekalu la Durban Afrika Kusini na Matthew Reier

Mwana wetu wa kwanza alizaliwa mfu mnamo 2017. Miezi tisa kabla ya Hekalu la Durban Afrika Kusini kuwekwa wakfu mnamo 2020, mwana wetu wa pili alizaliwa mfu.

Wakati huo, nilihisi kama Hanna wa Agano la Kale. “Nilikuwa na uchungu rohoni mwangu, na nikamwomba Bwana nikilia sana” (1 Samweli 1:10).

Nilihisi mnyonge na kukasirika, na nilikuwa na uchungu mkali. Nilitaabika kihisia, kimwili na kiroho. Kushikilia fimbo ilikuwa kama kushikilia uzi ambao ulikuwa unateleza pole pole kutoka mikononi mwangu. Nilikuwa kwa kweli ninateketea katika “tanuru ya mateso” (Isaya 48:10).

Nina shukrani sana kwamba nilipokea msaada na uponyaji kutoka kwa familia yangu, maandiko, na sala. Pia nilipokea msaada kutoka kwa washauri. Kilele cha uponyaji wangu, hata hivyo, kilikuja ndani ya hekalu.

Nilipoanza kutumikia hekaluni, nilianza kujazwa na ongezeko la nuru. Nilijihisi nyumbani pale. Pia nilihisi hakikisho la kina kwamba Bwana ananipenda na anajali mapambano yangu.

Nilipoendelea kutumikia katika nyumba ya Bwana, nilianza kutazama majina ya mababu zangu katika njia tofauti. Hayakuwa tu majina. Nilitambua, kwa mfano, kwamba mmoja wa mabibi alikuwa binti, mama, bibi, shangazi, dada, mpwa. Kufa kwake lazima ilikuwa jambo gumu kwa jamaa zangu waliobakia. Lakini baraka zilizotolewa kwa bibi huyu katika hekalu kupitia ibada takatifu kwa niaba hufanyiza furaha kuu na tamu ambayo inapita uchungu wowote ambao jamaa walio hai wangeweza kuhisi juu ya kifo chake.

Ufahamu huu umenibariki ninapofikiria kuhusu wavulana wetu wa thamani, asili ya milele ya roho zetu, na mpango wa wokovu wa Baba wa Mbinguni. Kuwapoteza wavulana wetu kunanipa msukumo wa kufanya kadiri niwezavyo kuishi injili.

Baadhi ya siku bado ni ngumu sana kuliko zingine. Lakini kushikilia ahadi zangu za agano hufanya siku hizo kuwa rahisi.

Kuazima maneno ya Rais Russell M. Nelson, “Tunawakosa [wana] wetu sana. Hata hivyo, kwa sababu ya injili iliyorejeshwa ya Yesu Kristo, hatuna wasiwasi kuwahusu [wao]. Tunapoendelea kuheshimu maagano yetu na Mungu, tunaishi kwa matarajio ya kuwa [nao] tena.”1

Muhtasari

  1. Russell M. Nelson, “Njoo, Unifuate,” Liahona,, Mei 2019, 88.