“Watu wa Kufundishwa Gerezani,” Liahona, Sept. 2023.
Taswira za Imani
Watu wa Kufundishwa Gerezani
Ndani ya gereza, Dada Llanos kamwe hakupoteza mtazamo wa dhumuni lake kama mwakilishi wa Yesu Kristo, akiwafundisha wafungwa wenzake kuhusu utambulisho wao wa kiungu na jinsi ya kusali.
Dada Aketzaly Llanos alikuwa mmisionari wa mfano mwema akiwa na ushuhuda imara. Awali alipangiwa kwenda Misheni ya Costa Rica San José East, lakini alitumikia pamoja na mke wangu, Janeen, pamoja na mmi katika Misheni ya Mexico Aguascalientes kwa mwaka mmoja kabla ya kupata viza ya kwenda Costa Rica.
Mnamo Aprili 2022 tulimuaga Dada Llanos wakati akipanda ndege kwenda Mji wa Mexico, ambapo angepanda ndege nyingine kwenda Costa Rica. Chini ya masaa 24 baada ya kusema kwaheri, hata hivyo, polisi katika Mji wa Mexico walitupigia simu.
“Tumemkamata Aketzaly Llanos katika uwanja wa ndege akiwa na risasi ya kijeshi,” walisema. “Huu ni uhalifu wa uvunjaji wa sheria za nchi, na atashitakiwa.”
Mara moja, niliwasiliana na ofisi ya Kanisa ya eneo ya mambo ya kisheria, na wakaajiri mwanasheria kushughulikia kuachiliwa kwa Dada Llanos. Mwanasheria hakuwa muumini wa Kanisa. Aliweka sharti kutusaidia lakini alionyesha kukosa rajua. Alieleza kwamba kuwa na risasi ya kijeshi kama wewe si mwanajeshi ni kosa baya, bila kujali nia ya mtu.
Baadaye, Dada Llanos alituambia aliokota risasi hiyo mtaani katika eneo lake la mwisho. Alidhani ingekua kitu cha ukumbusho. Risasi, hata hivyo, ilifanana na mnyororo wa funguo zilizouzwa nje ya mgodi wa fedha katika mojawapo ya maeneo yake ya awali. Wachunguzi wa serikali, hata hivyo, walimchukulia kama gaidi. Ndani ya siku chache, Dada Llanos aliondolewa kutoka kwenye jela ya uwanja wa ndege hadi gereza la ulinzi mkali ambapo wahalifu wabaya wa kike hufungwa.
Sala za Imani
Sala kwa ajili ya Dada Llanos kuachiliwa zilianza mara moja. Mimi pamoja na Janeen tuliwaalika wamisionari 115 waliokuwa wakitumikia katika misheni yetu kuonesha imani kwamba tungeweza kuona muujiza, kama ilikuwa mapenzi ya Bwana. Niliwasiliana na marais wa misheni katika Mji wa Mexico, misheni ya Costa Rica San José East, na Kituo cha Mafunzo ya Umisionari cha Mexico, na wakawaalika wamisionari wao kujiunga katika sala.
Ndani ya gereza, Dada Llanos kamwe hakupoteza mtazamo wa dhumuni lake kama mwakilishi wa Yesu Kristo. Aliwafundisha wafungwa wenzake tisa kusali kwa kutoa sala asubuhi na jioni kama kundi kila siku. Aliwafundisha kuhusu utambulisho wao wa kiungu.
Mmoja wa wafungwa wenzake alitamka, “Mimi kwa kweli ni mtu mbaya kwa sababu ya kile nilichofanya kilichonileta hapa, na Mungu ananichukia.” Dada Llanos alimtazama machoni na kusema, “La. Wewe si mtu mbaya. Wewe ni mtu ambaye alifanya jambo baya. Lakini wewe ni mtoto wa Mungu, na Yeye anakupenda!”
Mfungwa mwenzake mwingine alisimulia ndoto aliyopata wiki chache kabla ya Dada Llanos kukamatwa. Mfungwa huyu aliota kwamba ndege aina ya quetzal ilitua ndani ya gereza ili kumsaidia. Kabla ya Dada Llanos kujiunga na Kanisa, alikuwa na mchoro wa picha ya ndege ya quetzal mgongoni. Wakati mfungwa mwenzake alipoona picha hiyo, alijua alipaswa kusikiliza ujumbe wa umisionari wa Dada Llanos.
Dada Llanos alimfundisha kuhusu Urejesho wa injili ya Yesu Kristo na kumpatia nakala ya Kitabu cha Mormoni alichokuwa amekuja nacho gerezani—nakala ile ile ambayo akina dada wamisionari walikuwa wamempa Dada Llanos miaka mitano kabla alipokuwa anachunguza Kanisa.
Mashitaka ya mwanzo yalipangwa haraka katika Mji wa Mexico. Mimi na Janeen tulienda kutoa ushahidi. Tulipokutana na timu ya wanasheria nje ya mahakama, mwanasheria alikuwa na wasi wasi, akitembea kwenda na kurudi kwenye njia ya waenda kwa miguu.
Nilimwita kando na kusema: “Leo utahisi utulivu mwingi na amani nyingi kuliko vile ambavyo umewahi kuhisi katika chumba cha mahakama. Acha nikwambie kwa nini. Zaidi ya wamisionari 500 na familia zao wanasali kwa ajili yako na ufanisi wako leo. Wanasali pia kwamba hakimu atalainisha moyo na kwamba atamwachilia Dada Llanos kutoka gerezani.
Mwanasheria alijawa na machozi, na akaonesha shukrani zake kwa ajili ya imani na sala za watu wengi kwa niaba yake.
Saa 4 asubuhi kesi ilianza, lakini nilihitajika kusubiri nje mpaka zamu yangu ya kutoa ushahidi itakapofika. Masaa mawili marefu yakapita. Kisha askari wa mahakama akaja nje na kusema hakimu amesema hahitaji kusikia ushahidi wangu—tayari yeye amekwishafanya maamuzi yake.
Kwa wasiwasi, niliingia kwenye chumba cha mahakama, na hakimu alianza kuzungumza. Alisema kuhusu sheria Dada Llanos aliyokuwa amevunja na kuhusu mashitaka makali ambayo yalikuwa yanamkabili.
“Bila kujali hayo yote,” aliendelea, “Mimi ninaamini ushahidi ambao umekishwa kutolewa kuhusu tabia nzuri ya Dada Llanos.” Kisha alinukuu sehemu fiche ya sheria ambayo ilimruhusu yeye kutoa msamaha, na mara moja alimuachilia huru.
“Mungu katika Upande Wangu”
Huu ulikuwa muujiza tulioutafuta! Badala ya kufungwa kifungo cha miaka minne au mitano gerezani, Dada Llanos alikuwa ameachiwa huru. Baada ya kesi, mwanasheria wake alisema kwamba siku hiyo ilikuwa mojawapo ya siku muhimu sana katika kazi yake.
“Kwa kweli nilihisi Mungu akiwa upande wangu,” alisema. “Ninataka kujifunza zaidi kuhusu imani yenu.”
Nilimwalika kwenye Kituo cha Wageni cha Hekalu la Mexico City Mexico. “Utawaona wamisionari wengine walio wazuri kama Dada Llanos,” Nilimwambia. “Utaona uchangamfu katika macho yao, na utajiuliza mwenyewe kwa nini.”
Masaa kumi na mawili baadaye, Dada Llanos aliachiwa, bado akiwa na mavazi ya gerezani. Alizimia mikononi mwa Janeen. Mara sote tulipokuwa tumelia sana kiasi cha kutosha kuzungumza, Dada Llanos alisema kwa mshangao, “Rais, nimepata baadhi ya watu wa kufundishwa gerezani!”
Uzoefu huu wote ulithibitisha kwamba “Mungu hajakoma kuwa Mungu wa miujiza” (Mormoni 9:15). Mimi sina shaka kwamba imani na sala za watu wengi zilimsaidia mwanasheria kukanusha kesi yake na kulainisha moyo wa hakimu.
Kwa sababu Dada Llanos alikamatwa, wanawake kadhaa waliofungwa walipokea tumaini kupitia injili ya Yesu Kristo, mwanasheria alichipusha mbegu ya imani, na sisi tuliimarishwa katika uthibitisho wetu kwamba Mungu anaweza kututumia sisi kuendeleza kazi Yake bila kujali pale tulipo.