2023
Baada ya Kupitia Hofu: Kujenga Uthabiti na Kukumbatia Uponyaji
Septemba 2023


“Baada ya Kupitia Hofu: Kujenga Uthabiti na Kukumbatia Uponyaji,” Liahona, Sept, 2023.

Baada ya Kupitia Hofu: Kujenga Uthabiti na Kukumbatia Uponyaji

Uponyaji huja tunapotafuta msaada wa Mwokozi na kujenga kujitegemea kihisia.

picha ya mti isiyo na rangi iliyotiwa ndani ya duara la kijani

Watu wengi watapata uzoefu wa angalau tukio moja la kuleta hofu maishani mwao. Tumeona hili katika maisha yetu binafsi na kazini. Ni nini kinachosababisha hofu? Uzoefu mgumu kama vile ajali ya gari, kupoteza ajira, vita, unyanyasaji kimwili, unyanyasaji kingono, uonevu mkali, kumpoteza mpendwa, na mengine mengi.

Hofu ni uchungu, na wakati mwingine unaweza kuhisi kama huwezi kupata nafuu. Lakini bado ni muhimu kujua kwamba uchungu utatulia, na utapata amani tena unapomtegemea Baba yako wa Mbinguni na Mwokozi wako, Yesu Kristo.

Baba wa Mbinguni huruhusu sisi tupatwe na magumu. Hata kama Yeye hataamua mapema, kuumba, au kukubali uzoefu huu, Yeye anaweza kusaidia “mambo yote yafanyike pamoja kwa faida [yetu]” ikiwa tutamtumainia Yeye (Mafundisho na Maagano 90:24; ona pia 2 Nefi 32:9).

Tumekuta kwamba kumgeukia Baba wa Mbinguni na Mwokozi kama msaada ni muhimu sana katika mchakato wa uponyaji. Amani Yao huponya kihisia na kiroho. Tunajua kwamba katika upendo na huruma Yao, unaweza kupata nguvu za kupona. Pia tumepata baadhi ya mbinu ambazo zitakuruhusu kujenga juu ya nguvu zako binafsi na kusonga mbele katika uponaji.

Kila mmoja hupatwa na matukio ya kutia hofu kwa njia tofauti. Hakika, baadhi wanaweza kupatwa na tukio la kutia hofu, hali wengine wanaweza kuwa walihisi tu wasiwasi kidogo. Kwa sababu hii, kumbuka kutolinganisha uzoefu wako na wa wengine au kutumia uzoefu wako kama uzoefu wa kipimo.

Kujibu Matukio kwa Njia Tofauti

Sam na Lucy walikuwa wanasafiri pamoja, na dereva wa gari walililokuwa wamepanda alisinzia na kuacha njia. Hii ilisababisha gari lao kupinduka mara kadhaa. Sam hakuumia sana na mwanzoni alionekana kuchukulia tukio hilo kama jambo dogo. Alikuwa pale kumfariji Lucy, kwa vile ilibidi mkono wake uliovunjika uwekwe bandeji.

Wiki kadhaa baadaye, wakati nafasi ilipojitokeza kwa Sam kusafiri tena, alihisi hali ya wasiwasi tu akifikiria kuhusu masaa mengi barabarani.

Sam alikuwa akipatwa na cheche za kihisia kutokana na uzoefu wa hofu. Alisita kuzungumza na mtu yeyote kuhusu jambo hilo. Lakini alipokuwa akizungumza na Lucy, aligundua kwamba Lucy alikuwa katika ajali hapo awali na anajua vile yeye alivyohisi. Walijadili kile Lucy alichojifunza kutokana na uzoefu wake wa mapema alipokuwa akifanyia kazi imani katika Yesu Kristo, akiomba kwa ajili ya mwongozo, na kufaidika kwa ushauri wakati alipotaabika.

picha ya mti isiyo na rangi iliyotiwa ndani ya duara la kijani

Tumaini na Uponyaji kupitia Yesu Kristo

Bila kujali hofu zetu, uponyaji unaweza kuja kupitia Mwokozi Yesu Kristo. Kwa sababu ya Upatanisho wa Mwokozi usio na mwisho na huruma na rehema Yake, Yeye anaweza kuponya vidonda vyote vilivyopatikana katika maisha haya ya duniani, iwe uponyaji huo huja katika maisha haya au yajayo. Wakati mwingine huchukua muda mrefu kuliko tunavyotarajia au tunavyotaka—hata kwa msaada wa kiungu wa Mwokozi. Lakini Yeye anaweza kutuponya sisi (ona 3 Nefi 17:7).

Mzee Dieter F. Uchtdorf wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili alifunza: “Nuru ya Mungu ni halisi. Inapatikana kwa wote! Huvipa uzima vitu vyote. Ina nguvu za kulainisha maumivu ya vidonda sugu.”1

Hakuna anayejua kuteseka kwetu kwa mapana kama Baba wa Mbinguni na Mwokozi wanavyojua. Bwana “Alishuka chini ya vitu vyote, kiasi kwamba alielewa vitu vyote, ili aweze kuwa katika vyote na ndani ya vitu vyote” (Mafundisho na Maagano 88:6). Dada Amy A. Wright, Mshauri wa Kwanza katika Urais Mkuu wa Msingi, alifundisha:

“Sote tuna kitu maishani mwetu ambacho kimevunjika ambacho kinahitaji kurekebishwa, kutatuliwa, au kuponywa. Tunapomgeukia Mwokozi, tunapofunganisha mioyo yetu na akili zetu pamoja Naye, tunapotubu, Yeye huja kwetu ‘na uponyaji katika mbawa zake’ [2 Nefi 25:13], huweka mikono Yake kutuzunguka kwa upendo, na kusema, ‘Ni SAWA. … Tunaweza kurekebisha hili pamoja!’

“Ninashuhudia kwamba hakuna kitu chochote maishani mwako ambacho kimevunjika ambacho ni zaidi ya nguvu za uponyaji, ukombozi na za kuwezesha za Yesu Kristo.”2

Mifano ya uponyaji na njia za kupona zinapatikana katika maandiko—na katika maisha ya familia zetu, marafiki, na mababu zetu. Ni katika njia zipi watangulizi wetu walikuwa thabiti?3

Utambulisho Wetu wa Milele

Wakati Julio alipokuwa na umri wa miaka 13, alinyanyaswa kingono na mjomba wake. Baada ya muda, alianza kujiondoa kutoka kwa familia yake na kujitenga. Nyakati zingine, alikuwa kama vile hakuna chochote kilichokuwa kimetokea, lakini mara kwa mara alifurikwa na hisia. Daima ameweza kumudu maisha—hata hisia kali za furaha, kama vile kuzaliwa kwa mwanaye. Pia alihisi kuvunjika. Mwanaye sasa anakaribia umri sawa na wakati Julio aliponyanyaswa, na Julio anapofikiria uzoefu yamkini wa mwanaye, anapigana mieleka na mawazo na hisia kuhusu thamani yake mwenyewe na utambulisho wa milele.

Wakati hofu ni sehemu ya maisha yetu ya duniani, si utambulisho wetu wa milele. Utambulisho wetu ni ule wa mtoto wa Mungu. Rais Russell M. Nelson alifundisha:

Wewe ni nani?

“Kwanza kabisa, wewe ni mtoto wa Mungu.

“Pili, kama muumini wa Kanisa, wewe ni mtoto wa agano. Na tatu, wewe ni mfuasi wa Yesu Kristo.”4

Kwa nyongeza, hofu kamwe si taswira ya thamani yetu au ustahili wetu. Dada Joy D. Jones, Rais Mkuu wa Msingi wa awali, alifafanua dhana mbili wakati alipofunza:

Thamani ya kiroho ina maana kujithamini sisi binafsi jinsi Baba wa Mbinguni anavyotuthamini. …

“… Ustahili unapatikana kupitia utiifu. Tunapotenda dhambi, tunakuwa si wastahiki kamili, lakini kamwe hatukosi thamani.”5

Unyanyasaji Julio aliopitia katika mikono ya mjomba wake haukubadilisha thamani na ustahili wa Julio. Kamwe hakutenda dhambi lakini alitendewa dhambi. Wakati mwingine inaweza kuwa vigumu kukumbuka thamani na ustahili wako unapokuwa umenyanyaswa. Kumbuka, wewe haukutenda dhambi, thamani yako kamwe haijapungua, na una thamani kuendelea katika njia ya agano.

Julio alipoendelea kumtumainia Bwana, Yeye alimsaidia Julio kutambua kwamba uzoefu wa duniani haubadilishi upendo ambao Baba aliye Mbinguni anao kwa ajili yetu. Yeye kwa sasa anajifunza kukubali kwamba ingawa mambo mabaya yalitendeka, hayakubadilisha thamani yake ya msingi, utambulisho wa milele, au ustahili.

Kujitegemea Kihisia

Kukuza kujitegemea kihisia kutakusaidia utumie nyenzo binafsi za kiafya ili kukabiliana na changamoto na ugumu wa hisia. Unaweza kukuza uthabiti, uwezo wa kubadilika na kumudu majaribu—ikijumuisha hofu.

Uthabiti hujumuisha kutafuta msaada na mwongozo kutoka kwa Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo, kuwatumikia wengine, na kutumikiwa na wengine kama inavyohitajika na inavyofaa.

Matendo yafuatayo, yaliyopendekezwa na washauri wenye weledi, yatakusaidia ukuze uthabiti:

  1. Kujenga miunganiko na wengine

  2. Kuboresha afya njema kimwili

  3. Kupata dhumuni katika maisha

  4. Kukuza mawazo mazuri

  5. Kutafuta msaada pale unapouhitaji5

picha ya wanawake wawili isiyo na rangi iliyotiwa ndani ya mstatili wa kijani

1. Unganika na Wengine

Mahusiano mazuri kila mara hukuza uponyaji. Kuunganika na wale ambao wanakuimarisha na kukuhimiza kumgeukia Mwokozi na Baba yetu wa Mbinguni kunaweza kuleta tofauti unayohitaji ili kupona kikamilifu zaidi.

Sam alimfikia Lucy, akashiriki hofu yake na usumbufu. Uhusiano huu ulimsaidia kuwa na ufahamu zaidi na uthabiti. Alimsaidia kuona jinsi ambavyo angeweza kupona kihisia na kiroho.

Fikiria kuweka malengo na kukuza miunganiko imara na wengine unaowaamini. Kuhudumu ni njia moja tunayounganika na wengine Kanisani.

2. Jali Afya ya Kimwili

Hofu haihisiwi kihisia tu bali pia kimwili. Tunaweza kupitia ongezeko la uchovu, moyo kudunda kwa kasi, kichwa kugonga au maswala ya tumbo letu kuwa kwenye maumivu au kuhisi msokoto wa tumbo. Dalili hizi za kimwili zipo ili kutueleza kwamba kitu fulani si sawa na kwamba tunahitaji kushughulikia afya yetu. Kama tu vile tunavyoweza kufanya vitu ili kutunza vyema afya yetu ya kihisia, tunaweza pia kufikiria njia za kujitunza wenyewe kimwili baada ya kupitia hofu.

Kwanza, tambua dalili za kimwili unazopata. Kisha jaribu kutuliza mwili wako kwa kufokasi kwenye kupumua kwako na kushusha kupumua kwako. Jaribu kutambua jinsi unavyohisi wakati kupumua kwako ni haraka na kusiko na mpangilio ikilinganishwa na wakati kupumua kwako ni taratibu na kuna mpangilio.

Wakati mwingine hofu inaweza kusababisha jeraha ambalo linatuwekea ukomo, kwa hivyo fanya kile kilicho sahihi kwa mwili wako. Lakini mwendo, hasa mazoezi ya mwili, yanasaidia. Baadhi wanafurahia kutembea, au kukimbia, hali wengine wanaweza kupata msaada kwa kufanya kazi ngumu.

Kumbuka Neno la Hekima (ona Mafundisho na Maagano 89). Kujaribu kuficha uchungu kwa tabia zisizofaa au madawa ni kama tu “kuweka bandeji kwenye donda sugu.”7 Usaidie mwili wako ushughulikie msongo na maumivu badala ya kuuzuia.

3. Tafuta Dhumuni na Maana

Dhumuni letu kuu katika maisha ni kujiandaa kurudi kuishi na Baba yetu wa Mbinguni (ona Alma 12:24). Hofu inaweza kufifisha dhumuni hili na kutuzuia sisi kuona sisi ni akina nani. Kupata dhumuni mahususi katika vitendo vyetu vya kila siku hutusaidia kusonga mbele na hata kukumbuka dhumuni letu kuu katika maisha. Julio alianza kusonga mbele na kupata dhumuni katika matendo yake ya kila siku wakati alipotambua kwamba alikuwa anataka kumsaidia mwanaye.

Kupata maana katika hofu kunaweza kutusaidia tuone njia mbele, kutambua kwamba uzoefu wetu hutoa fursa kwetu za kukua na kuwa zaidi kama Kristo. Kwa mfano, ni rahisi kuwa na huruma kwa dhiki ya mwingine ikiwa tumeshapitia uzoefu mgumu sisi wenyewe.

Utafiti umegundua kwamba baada ya hofu, watu kila mara wanapata kile kinachoitwa “ukuaji baada ya hofu.” Ukuaji baada ya hofu unaoneshwa kwa mtu kupata ongezeko la nguvu baada ya uzoefu wa hofu, kama vile kuboreka kwa uhusiano, kuthamini zaidi maisha au sifa fulani za maisha, au ongezeko la ufahamu wa uwezekano katika maisha. Baada ya kupatwa na uzoefu wa tukio la hofu, tambua jinsi ulivyokua au unavyoweza kukua kwa sababu ya uzoefu badala ya kufokasi kwenye tukio lenyewe la hofu.

4. Kuza Mawazo Mazuri

Tukio la hofu linaweza kuathiri vile tunavyofikiria kutuhusu sisi wenyewe na ulimwengu unaotuzunguka. Baada ya kupata uzoefu wa hofu, tunaweza kuwa na mawazo hasi. Mawazo kama vile, “Mimi ni mdhaifu,” “Baba wa Mbinguni hanipendi,” na “Mimi sistahili” yanapunguza uwezo wetu wa kuwa thabiti. Mawazo haya kila mara yatashawishi jinsi tunavyohisi (ona Mithali 23:7; Mafundisho na Maagano 6:36).

Baada ya kuwa umetambua mawazo yako hasi, fikiria baadhi ya mawazo mazuri, mawazo halisi mbadala na uyaandike. Jikumbushe mawazo haya mazuri pale unapotambua mawazo hasi katika akili yako.

Ili kujifunza zaidi kuhusu jinsi ya kufanya hivi, pitia tena sura ya 2 ya Finding Strength in the Lord: Emotional Resilience (2021).

Unaweza pia kugeukia sala, kuandika kwenye shajara, kuyatafakari maandiko au hotuba za mkutano mkuu (ona Yoshua 1:8), au mazoezi mengine ya kutafakari.

5. Tafuta Msaada

Nyakati zingine, inafaa kufikiria msaada nje ya nyenzo zako mwenyewe. Lucy alitafuta msaada, ambao ulimwezesha yeye kumsaidia Sam. Wafikirie watu wengine—kama vile wanafamilia, marafiki, viongozi wa kata—ambao wanaweza kuwa msaada. Uponyaji wa hofu ni mojawapo ya nyakati ambapo unahitaji kutumia nyenzo zote yamkini katika maisha yako.

Kitabu cha Maelezo ya Jumla hutoa mwongozo juu ya ni wakati upi unaweza kufaa kutafuta msaada kutoka kwa washauri wenye weledi.8

Ni vigumu kutofokasi kwenye tukio la hofu, lakini tunapofuata ushauri wa nabii wa kuelekeza fokasi yetu juu ya Mwokozi na injili Yake, “mashaka na hofu yetu vitaondoka.”9 Kumbuka, wewe ni mwana au binti wa Baba wa Mbinguni mwenye upendo. Unapofokasi kwenye kusogea karibu Naye na kutumia nyenzo zenye msaada ambazo zinapatikana kwako, Bwana anaweza kusaidia uzoefu wowote wa hofu uwe wa manufaa kwako.

Muhtasari

  1. Dieter F. Uchtdorf, “Tumaini la Nuru ya Mungu,” Liahona, Mei 2013, 75.

  2. Amy A. Wright, “Kristo Huponya Kile Kilichovunjika,” Liahona, Mei 2022, 82, 84.

  3. Ona Chakell Wardleigh Herbert, “Recognizing and Healing from Generational Trauma” (digital-only article), Liahona, Jan. 2023, ChurchofJesusChrist.org.

  4. Russell M. Nelson, “Choices for Eternity” (worldwide devotional for young adults, May 15, 2022), broadcasts.ChurchofJesusChrist.org.

  5. Joy D. Jones, “Thamani Ipitayo Kipimo,” Liahona, Nov. 2017, 14–15

  6. Ona “Building Your Resilience,” American Psychological Association, Feb. 1, 2020, apa.org.

  7. “Building Your Resilience,” apa.org.

  8. Ona Kitabu cha Maelezo ya Jumla: Kutumikia katika Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho, 31.3.6, ChurchofJesusChrist.org; ona pia Justin K. McPheters and Rebecca M. Taylor, “Is Therapy Right for Me?” (digital-only article), Ensign, Feb. 2020, ChurchofJesusChrist.org; Kevin Theriot, “Finding a Mental Health Professional Who’s Right for You” (digital-only article), Liahona, Jan. 2019, ChurchofJesusChrist.org.

  9. Russell M. Nelson, “Kuvuta Nguvu ya Yesu Kristo kwenye Maisha Yetu,” Liahona, Mei 2017, 41.