Maandiko Matakatifu
Mafundisho na Maagano 58


Sehemu ya 58

Ufunuo uliotolewa kupitia Joseph Smith Nabii, huko Sayuni, katika Wilaya ya Jackson, Missouri, 1 Agosti 1831. Mapema, siku ya Sabato ya kwanza baada ya kuwasili kwa Nabii na kundi lake Wilayani Jackson, Missouri, ibada ya kanisa ilikuwa imefanyika na waumini wawili walikuwa wamepokelewa kwa ubatizo. Katika wiki hiyo, baadhi ya Watakatifu wa Colesville kutoka Tawi la Thompson na wengine waliwasili (ona sehemu ya 54). Wengi walikuwa na shauku ya kutaka kujua matakwa ya Bwana juu yao katika sehemu mpya ya kukusanyika.

1–5, Wale watakaostahimili taabu watavikwa utukufu; 6–12, Watakatifu wajitayarishe kwa ajili ya harusi ya Mwanakondoo na karamu ya Bwana; 13–18, Maaskofu ndiyo waamuzi katika Israeli; 19–23, Watakatifu watatii sheria za nchi; 24–29, Wanadamu watumie haki yao ya kujiamulia kufanya mema; 30–33, Bwana huamuru na kutengua; 34–43, Ili kutubu, wanadamu lazima wakiri na kuacha dhambi zao; 44–58, Watakatifu wanunue urithi wao na wakusanyike Missouri; 59–65, Injili ni lazima ihubiriwe kwa kila kiumbe.

1 Sikilizeni, Enyi wazee wa kanisa langu, na yasikilizeni maneno yangu, na mjifunze kwangu ni nini matakwa yangu juu yenu, na pia juu ya nchi hii ambayo nimewaleta.

2 Kwani amini ninawaambia, heri yule ashikaye amri zangu, iwe katika maisha au kifo; na yule aliye mwaminifu katika taabu, thawabu yake ni kubwa katika ufalme wa mbinguni.

3 Hamuwezi kuona kwa macho yenu ya asili, kwa wakati huu, mipango ya Mungu wenu juu ya mambo yale ambayo yatakuja hapo baadaye, na utukufu utakaofuata baada ya taabu kubwa.

4 Kwani baada ya taabu kubwa huja baraka. Kwa hiyo siku yaja ambayo ninyi mtavikwa utukufu mkubwa; saa ingali, lakini i karibu.

5 Kumbukeni hili, ambalo ninawaambia kabla, kwamba muweze kuliweka moyoni, na kupokea lile ambalo litafuata.

6 Tazama, amini ninawaambia, kwa sababu hii nimewatuma ninyi—ili muweze kuwa watiifu, na kwamba mioyo yenu iweze kuandaliwa kutoa ushuhuda wa mambo ambayo yatakuja;

7 Na pia muweze kupewa heshima katika kuweka msingi, na katika kutoa ushuhuda wa nchi ambapo Sayuni ya Mungu itasimama;

8 Na pia kwamba karamu ya vitu vinono iweze kuandaliwa kwa maskini; ndiyo, karamu ya vitu vinono, karamu ya divai iliyokaa juu ya urojorojo wake uliochujwa sana, ili ulimwengu uweze kujua kwamba vinywa vya manabii havitashindwa;

9 Ndiyo, karamu ya nyumba ya Bwana, iliyoandaliwa vyema, ambayo kwayo mataifa yote yataalikwa.

10 Kwanza, matajiri na wasomi, wenye hekima na maarufu;

11 Na baada ya hapo yaja siku ya uwezo wangu, halafu maskini, kiwete, na kipofu, na kiziwi, watakuja katika harusi ya Mwanakondoo, na kula karamu ya Bwana, iliyoandaliwa kwa ajili ya siku ile kuu ijayo.

12 Tazama, Mimi, Bwana, nimenena hili.

13 Na ili ushuhuda upate kwenda kutoka Sayuni, ndiyo, kutoka kinywani mwa mji wa urithi wa Mungu—

14 Ndiyo, kwa dhumuni hili nimekutuma hapa, na nimemchagua mtumishi wangu Edward Partridge, na nimempangia huduma yake katika nchi hii.

15 Lakini kama hatatubu dhambi zake, ambazo ni kutokuamini na upofu wa moyo, na atii asije akaanguka.

16 Tazama huduma yake imetolewa kwake, na hautatolewa tena.

17 Na yeyote asimamaye katika huduma hii ameteuliwa kuwa mwamuzi katika Israeli, kama vile ilivyokuwa katika siku za kale, kugawa ardhi ya urithi wa Mungu kwa watoto wake;

18 Na kuwahukumu watu wake kwa ushuhuda wa haki, na kwa msaada wa wasaidizi wake, kulingana na sheria za ufalme ambazo hutolewa na manabii wa Mungu.

19 Kwani amini ninawaambia, sheria yangu itashikwa katika nchi hii.

20 Acheni mtu yeyote asijifikirie kuwa yeye ni mtawala; bali mwacheni Mungu amtawale yule anaye hukumu, kulingana na ushauri wa matakwa yake yeye mwenyewe, au, katika maneno mengine, yeye ambaye hushauri au aketiye juu ya kiti cha hukumu.

21 Na mtu yeyote asivunje sheria za nchi, kwani yule ambaye hushika sheria za Mungu hana haja ya kuvunja sheria za nchi.

22 Kwa hiyo, mzitii mamlaka zilizopo, hadi atawalapo mwenye haki ya kutawala, na kuwatiisha maadui wote chini ya miguu yake.

23 Tazama, sheria ambazo mmezipokea kutoka mkononi mwangu ni sheria za kanisa, na katika nuru hii mtazishikilia. Tazama, hapa ndipo penye hekima.

24 Na sasa, kama nilivyosema juu ya mtumishi wangu Edward Partridge, nchi hii ni nchi ya makazi yake, na wale aliowateua kuwa washauri wake; na pia nchi ya makazi ya yule ambaye nimemteua kutunza ghala yangu;

25 Kwa hiyo, waacheni wazilete familia zao katika nchi hii, kama vile watakavyoshauriwa kati yao na Mimi.

26 Kwani tazama, si vyema kwamba niamuru katika mambo yote; kwani yule alazimishwaye katika mambo yote, huyo ni mvivu na siyo mtumishi mwenye busara; kwa hiyo hapokei thawabu yoyote.

27 Amini ninawaambia, wanadamu yawapasa kujishughulisha kwa shauku katika kazi njema, na kufanya mambo mengi kwa hiari yao wenyewe, na kutekeleza haki nyingi;

28 Kwani uwezo upo ndani yao, ambamo wao ni mawakala juu yao wenyewe. Na kadiri wanadamu watakavyofanya mema hawatakosa thawabu zao.

29 Lakini yule asiyefanya lolote mpaka ameamriwa, na kupokea amri kwa moyo wenye mashaka, na kuzishika kwa uvivu, huyo amelaaniwa.

30 Mimi ni nani niliyemuumba mwanadamu, asema Bwana, ambaye sitamshika na hatia yule ambaye hatii amri zangu?

31 Mimi ni nani, asema Bwana, ambaye nimeahidi na nisitimize?

32 Ninaamuru na wanadamu hawatii; ninatengua nao hawapati baraka.

33 Ndipo husema mioyoni mwao: Hii siyo kazi ya Bwana, kwani ahadi zake hazijatimia. Lakini ole wao, kwani thawabu yao ujira wao unawavizia chini, na wala haitoki juu.

34 Na sasa natoa kwenu maelekezo zaidi kuhusu nchi hii.

35 Ni hekima iliyo ndani yangu kwamba mtumishi wangu Martin Harris yapasa awe mfano kwa kanisa, katika kuweka fedha zake mbele ya askofu wa kanisa.

36 Na pia, hii ni sheria kwa kila mtu ajaye katika nchi hii kupokea urithi; naye atafanya kulingana na maelekezo ya sheria.

37 Na ni hekima pia kwamba pawepo na ardhi iliyonunuliwa katika Independence, kwa ajili ya mahali pa ghala, na pia kwa ajili ya nyumba ya uchapishaji.

38 Na maelekezo mengine juu ya mtumishi wangu Martin Harris yatatolewa kwake kwa njia ya Roho, ili aweze kupokea urithi wake kama aonavyo yeye kuwa vyema;

39 Na atubu dhambi zake, kwa vile yeye hutafuta sifa za ulimwenguni.

40 Na pia mtumishi wangu William W. Phelps asimame katika ofisi niliyomteua, na kupokea urithi wake katika nchi;

41 Naye pia ana haja ya kutubu, kwani Mimi, Bwana, sijapendezwa naye, kwani anatafuta kujikweza, na siyo mnyenyekevu vya kutosha mbele zangu.

42 Tazama, yule ambaye ametubu dhambi zake, huyu anasamehewa, na Mimi, Bwana, sizikumbuki tena.

43 Kwa hili mnaweza kujua kama mtu ametubu dhambi zake—tazama, ataungama na kuziacha.

44 Na sasa, amini, ninasema juu ya mabaki ya wazee wa kanisa langu, wakati haujafika bado, na hautafika kwa miaka mingi, kwa wao kupokea urithi wao katika nchi hii, isipokuwa wametamani kwa njia ya sala ya imani, pekee kama itakavyoteuliwa kwao na Bwana.

45 Kwani, tazama, watawasukuma watu pamoja hata kutoka miisho ya dunia.

46 Kwa hiyo, jikusanyeni pamoja; na wale wasioteuliwa kukaa katika nchi hii, na wahubiri injili katika maeneo ya jirani; na baada ya haya na warejee majumbani kwao.

47 Na wahubiri njiani, na kutoa ushuhuda juu ya ukweli katika mahali pote, wakiwaita matajiri, wakubwa na wadogo, na maskini kutubu.

48 Na wajenge makanisa kadiri wakazi wa dunia watakavyotubu.

49 Na acha pawepo na wakala aliye chaguliwa kwa sauti ya kanisa, kwa kanisa la Ohio, kupokea fedha za kununulia ardhi katika Sayuni.

50 Na ninatoa amri kwa mtumishi wangu Sidney Rigdon, kwamba ataandika maelezo juu ya nchi ya Sayuni, na taarifa ya mapenzi ya Mungu, kama vile itakavyojulishwa kwake na Roho;

51 Na waraka na hati, itawakilishwa kwa makanisa yote ili kupata fedha, ili ziwekwe katika mikono ya askofu, au katika mikono yake mwenyewe au mikono ya wakala, kama itakavyoonekana kwake kuwa ni vyema au kama atakavyoelekeza, kwa kununulia ardhi kwa ajili ya urithi kwa watoto wa Mungu.

52 Kwani, tazama, amini ninawaambia, Bwana ataka kwamba wanafunzi na wanadamu wafungue mioyo yao, hata kwa kununua eneo la nchi hii yote mapema, kama vile muda utakavyoruhusu.

53 Tazama, hii ndiyo ilipo hekima. Na wafanye hili vinginevyo wasije wakakosa kabisa urithi, isipokuwa kwa umwagaji wa damu.

54 Na tena, kadiri itakavyopatikana ardhi, na wafanya kazi wa kila aina watumwe katika nchi hii, kufanya kazi kwa ajili ya watakatifu wa Mungu.

55 Na mambo haya yote na yafanyike katika utaratibu; na haki ya kuwa na ardhi ijulishwe kila wakati na askofu au wakala wa kanisa.

56 Na kazi ya kukusanyika na isifanywe kwa haraka, wala kwa kukimbia; bali na ifanyike kama itakavyoshauriwa na wazee wa kanisa kwenye mikutano, kulingana na taarifa watakazokuwa wakizipokea mara kwa mara.

57 Na mtumishi wangu Sidney Rigdon atakase na kuweka wakfu kwa Bwana ardhi hii, na eneo la ujenzi wa hekalu.

58 Na mkutano uitishwe; na baada ya hayo, watumishi wangu Sidney na Joseph Smith, Mdogo, warejee, na pia Oliver Cowdery pamoja nao, kumaliza mabaki ya kazi ambayo nimewateua katika nchi yao wenyewe, na zilizosalia kama itakavyoamriwa na mikutano.

59 Na pasiwepo na mtu yeyote atakayerejea kutoka nchi hii bila kutoa ushuhuda njiani, kwa kile akijuacho na kwa uhakika zaidi kile anachokiamini.

60 Na kile kilichowekwa juu ya Ziba Peterson kichukuliwe kutoka kwake; na asimame kama muumini katika kanisa, na afanye kazi kwa mikono yake mwenyewe, pamoja na ndugu zake hadi atakaporudiwa vya kutosha kwa dhambi zake zote; kwani yeye haziungami, na anafikiria kuzificha.

61 Na waliobaki kati ya wazee wa kanisa hili, ambao wanakuja katika nchi hii, ambao baadhi yao wamebarikiwa kupita kiasi, pia wafanye mkutano katika nchi hii.

62 Na mtumishi wangu Edward Partridge aongoze mkutano utakaofanywa na hao.

63 Na wao pia warejee, wakihubiri injili njiani, wakitoa ushuhuda wa mambo yaliyofunuliwa kwao.

64 Kwani, amini, sauti lazima iende mbele kutoka mahali hapa kwenda katika ulimwengu wote, na hata sehemu za mbali zaidi za ulimwengu—injili lazima ihubiriwe kwa kila kiumbe, na ishara zikiwafuata wenye kuamini.

65 Na tazama Mwana wa Mtu yu aja. Amina.