Krismasi huko Mali
Mwandishi anaishi Texas, Marekani.
Judith hakuweza kungojea kusherehekea kuzaliwa kwa Yesu pamoja na tawi lake.
“Angels we have heard on high sweetly singing o’er the plains” (Wimbo wa Kanisa, na. 203).
Ilikuwa Siku ya Krismasi. Judith aliimba na midomo amefunga alipokuwa akitembea kwenda kwenye jengo la kanisa. Yeye na ndugu zake walikuwa wakienda kwenye dhifa ya Krismasi ya tawi lao.
Dada yake, Esther, alitabasamu. “Je huo ni ‘Angels We Have Heard on High?’”
“Ndiyo! Ni wimbo wangu niupendao. Nategemea tutauimba leo.” Judith alitabasamu.
“Ninaupenda wimbo huo!” Désiré, kaka yake, aliongezea. Aliimba kwa sauti kubwa, “Gl-o-o-o-ria!”
Wote walicheka. Judith hakuweza kungoja kusherehekea pamoja na tawi lao. Sio watu wengi huko Mali wanasherehekea Krismasi. Katika sehemu hii ya Afrika, watu wengi hawakujua mengi kuhusu Yesu. Kwao, Krismasi ilikuwa siku ya kawaida tu.
Mitaa ilikuwa imejaa watu. Wachuuzi waliuza matikiti maji ya kijani isiyokoza. Watu vijana na wazee walibeba mitungi ya maji vichwani mwao. Mvulana mdogo aliongoza punda aliyekuwa anavuta mkokoteni. Judith aliangalia juu kwenye mnara mrefu, mwembamba wa msikiti. Lilikuwa jengo zuri ambamo wengi wa majirani zao Waislamu waliabudu.
Judith, Esther, na Désiré walizoea kwenda kwenye kanisa la Baba. Lakini majira ya joto yaliyopita, walijiunga na Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho. Sasa wao watatu walikuwa wanakwenda kanisani pamoja kila wiki. Judith alipenda kujifunza kuhusu Yesu katika Msingi.
Mwishowe walifika kwenye dhifa. Familia nyingi za tawi zilikuwa tayari pale. Projekta ilikuwa inaonesha video za Krismasi kwenye ukuta wa kanisa dogo. Judith alimwangalia Yosefu akimwongoza Mariamu kupitia Bethlehemu juu ya punda. Mitaa yenye shughuli nyingi, vumbi ilimkumbusha juu ya Mali!
Baada ya video kwisha, teksi ilisimama. Dada Valerie, rais wa Muungano wa Usaidizi wa Akina Mama, aliteremka.
“Nimeleta chakula!” alisema.
Kila mtu alisaidia kuleta sahani kwenye kibaraza cha juu. Ilikuwa ni karamu! Kachumbari ya viazi, karoti, maharage mabichi, wali unaong’aa wa njano, kuku wa kukaanga … vyote vilikuwa vitamu sana!
“Asanteni sana, Dada Valerie!” Judith alisema.
Kisha watoto wadogo kila mmoja alipata mpira, mwanasesere, au gari la kuchezea. Hapakuwa na zawadi za kutosha kwa ajili ya Judith kupata moja, lakini hakujali. Alipenda kuwaona watoto wadogo wakitabasamu.
Dhifa ilikwisha kwa kuimba. Judith alitabasamu wakati walipoimba “Angels We Have Heard on High.”
Tawi lote waliimba pamoja. Ilikuwa ya kupendeza sana! Yesu kwa kweli alizaliwa miaka yote hiyo iliyopita! Judith alikuwa na shukrani sana kwamba yeye, Désiré, na Esther walijua kuhusu Yesu Kristo. Na alikuwa na furaha sana kusherehekea kuzaliwa Kwake.