Zamu za Kuhudhuria Kanisani
“Ukirudi nyumbani, niambie ni nyimbo gani uliimba katika Shule ya Msingi,” Jenny alisema.
“Nitafanya hivyo!” dada yake Miriam alisema huku akivaa viatu vyake.
Si kila mtu katika familia ya Jenny angeweza kwenda kanisani kila Jumapili. Kulikuwa na watu sita katika familia ya Jenny. Lakini Mama alikuwa na pesa za kutosha kununua tiketi mbili za basi kila wiki. Kwa hiyo walilazimika kupanda basi kwenda kanisani kwa zamu.
Jenny alitamani aende kila juma. Alipenda kujifunza kuhusu Yesu Kristo. Alipenda kuimba katika Msingi. Alitaka kuwaona marafiki zake. Zaidi ya yote, alitaka kuhisi hali ya uchangamfu na furaha aliyokuwa akipata kila mara kanisani. Lakini leo ilibidi abaki nyumbani.
“Ni muda wa kuondoka.” Mama alimkumbatia Jenny na kaka yake na dada zake ili kuwaaga.
Jenny alijaribu kutabasamu huku Miriam na Mama wakiondoka. Lakini alihisi donge kooni alipokuwa akiwatazama wakiondoka. Natamani ingekuwa nafasi yangu kwenda, Jenny aliwaza. Ilikuwa vigumu kila wakati kukaa nyumbani.
“Unataka kupaka rangi?” Ndugu mdogo wa Jenny, Marco, aliinua kalamu za rangi na karatasi.
Jenny aliitikia kwa kichwa.
Kwa saa chache zilizofuata, Jenny alisoma hadithi na kupaka rangi pamoja na Marco na dada zao wakubwa. Ilikuwa ni furaha, lakini Jenny aliendelea kufikiria kuhusu kanisa. Je, walikuwa wakijifunza nyimbo mpya katika Msingi sasa hivi? Somo lilikuwa kuhusu nini leo?
Hatimaye Jenny alisikia mlango wa mbele ukifunguliwa. Mama na Miriam walikuwa nyumbani!
“Mama! Miriam! Jenny alikimbilia mlangoni na kuwakumbatia.
Mama aliweka mkoba wake chini. “Acha tuzungumze juu ya kile tulichojifunza kanisani.”
Kila mtu akaketi pamoja. Mama akachomoa kijitabu kidogo cha nyimbo alichokiweka kwenye mkoba wake. Familia ya Jenny iliimba “Families Can Be Together Forever.” Alijua maneno yote.
Kisha Jenny akamuuliza Miriam kuhusu Msingi. Miriam alifungua Kitabu chake cha Mormoni na kutoa kipande cha karatasi kilichokunjwa. Aliinua juu ili kila mtu aweze kuona. Ilikuwa ni picha aliyoipaka rangi ya Yesu akiwa na baadhi ya watoto.
“Tulipaka picha rangi na kuimba ‘I’m Trying to Be like Jesus.’ Kisha tukazungumza kuhusu jinsi Yesu anavyoweza kumsaidia kila mtu.”
“Tulizungumza kuhusu hilo katika Muungano wa Usaidizi wa Akina Mama pia,” Mama alisema. “Yesu Kristo anaweza kutusaidia tunapokuwa na hofu au upweke.” Mama akachomoa kipande cha karatasi kwenye mkoba wake. “Mwalimu alimpa kila mtu nukuu hii kutoka kwa nabii. ‘Unapochagua kuishi upande wa Bwana, hauko peke yako kamwe.’”*
“Hata hapa nyumbani!” Jenny alisema.
Mama alitabasamu. “Hata nyumbani. Daima tunaweza kumhisi Mwokozi karibu nasi.”
Jenny alitabasamu sana. Hakuweza kwenda kanisani kila wiki. Lakini angeweza kuhisi kuwa karibu na Yesu nyumbani. Na alikuwa na furaha kwa zamu yake ya kwenda kanisani tena hivi karibuni.