2021
Mpango wa Kiungu wa Kuwa Zaidi
Julai 2021


“Mpango wa Kiungu wa Kuwa Zaidi,” Kwa Ajili ya Nguvu kwa Vijana, Julai 2021, 2–5.

Mpango wa Kiungu wa Kuwa Zaidi

Tunapoyatazama maisha ya kidunia katika uhalisia, tunaona kwamba katika maisha haya, swali siyo juu ya “kuwa au kutokuwa?” bali “ kuwa zaidi au kutokuwa zaidi?”

Picha
mvulana

Nimebarikiwa kuwa pamoja na mke wangu wakati wa kuzaliwa kwa kila mmoja wa watoto wetu na kuwepo pia wakati wa kufariki kwa kila mmoja wa wazazi wangu. Nilishangazwa na hisia nilizozihisi wakati wa kuzaliwa huko na wakati wa kifo. Nilihisi kwamba kitu kitakatifu kilikuwa kikitokea. Muda wetu hapa duniani ni sehemu ya kipekee ya milele ya uwepo wetu. Mbingu ndiyo mwanzo na mwisho wa kila maisha ya hapa duniani.

Kile tunachohitajika kujua wakati tuko hapa duniani kinaweza kueleweka tu kupitia kujua kile kilichotokea kabla ya kuzaliwa na kile kitachotokea baada ya kufariki. Kama maisha yetu hapa duniani yangekuwa ya kukidhi, basi sote “tungekula, kunywa, na kufurahi” (2 Nefi 28:7) bila kuwafikiria zaidi wengine. Lakini tunapoyatazama maisha ya duniani katika muktadha huu, tunaona kwamba swali siyo juu ya “kuwa au kutokuwa?” badala yake ni “kuwa zaidi au kutokuwa zaidi?”1

Picha
msichana

Kuelewa mpango wa wokovu—maisha yetu kabla ya kuzaliwa, malengo yetu ya kuishi duniani, maisha yetu baada ya kifo—na nafasi muhimu ambayo Mwokozi wetu, Yesu Kristo, aliyonayo katika mpango huo inatuonyesha kwamba Yeye atatusaidia katika maisha haya. Tunapofanya maagano pamoja Naye, sisi tunajiweka wenyewe kwenye njia ya agano—na hivyo kuwa zaidi kama Yeye na kama Baba yetu wa Mbinguni walivyo, hatua kwa hatua.

Maisha Yetu kabla ya Duniani

Ufunuo unatufundisha kwamba sisi ni watoto wa kiroho wa Mungu na kwamba tuliishi pamoja Naye kwa muda mrefu kabla ya kuja duniani. Baba yetu wa Mbinguni alitayarisha njia ili sisi tuwe kama Yeye. Wale waliochagua mpango wa wokovu wa Baba au mpango wa furaha katika maisha yale kabla ya kuzaliwa duniani—ambao ni sisi sote—tulichagua “kuwa zaidi.”

Picha
Mzee Christofferson pamoja na familia yake

Mzee Christofferson pamoja na mke wake na watoto.

Wakati Wetu Duniani

Tulikuja kwenye dunia iliyoumbwa na Mungu na Mwanawe, Yesu Kristo. Tukapokea mwili wa nyama na mifupa. Kuwa na mwili ni muhimu katika kupokea utukufu ambao Mungu anaufurahia. Kama tutaonyesha kwamba tutashika amri za Mungu, “utukufu utaongezwa juu ya vichwa [vyetu] milele na milele” (Ibrahimu 3:26). Hii inamanisha kwamba tutakuwa kama wazazi wetu wa mbinguni na kuishi pamoja nao milele. Tulishangilia kwa furaha kwa ajili ya uwezekano huu wa kitukufu.

Wewe na mimi tulisubiri kwa muda mrefu, lakini sasa tuko hapa duniani. Tunatazamia wakati ule tutakapofufuliwa na kuwa na miili mikamilifu, isiyokufa tena na kuingia katika ufalme wa selestia ili kufurahia uzima wa milele—kitu kilicho kizuri sana ambacho hatuwezi hata kukifikiria. Kwa wakati huu, sisi tunajifunza na kujitahidi “kufanya mambo yote yale Bwana Mungu [wetu] atakayotuamuru [sisi]” (Ibrahamu 3:25). Kwa sababu sisi tunaujua mpango wa Mungu, tunajua kwamba amri hizi hazijatolewa ili kubana uhuru wetu au furaha yetu—bali ni kinyume chake. Amri ni mwongozo wetu kwenye hatima ya uhuru na shangwe.

Yeye Alimleta Mwokozi

Bado, maisha ni magumu. Sote tunajikwaa tunapojifunza kuishi kwa imani. Lakini Mungu alituahidi kabla ya uumbaji wa dunia kwamba Yeye angemleta Mwokozi ili kutuokoa sisi kutokana na dhambi na mauti. Kwa mateso na kifo Chake mwenyewe—Upatanisho Wake—Yesu Kristo alilipia dhambi zetu na kutupa zawadi ya toba. Kwa sababu hiyo, tunapotubu, Yeye hutusamehe dhambi zetu na kututakasa kutokana na athari zake. Na kwa Ufufuko Wake, Mwokozi anatupatia sisi zawadi ya ufufuko wetu sisi wenyewe na maisha ya milele.

Picha
watu wakisujudia mbele ya Kristo

Kila Goti Litapigwa, na J. Kirk Richards

Kutembea Njia ya Agano

Kama vile tu tunavyozaliwa kimwili katika ulimwengu huu, ni lazima tuzaliwe tena kiroho katika ufalme wa mbinguni. Tunafanya hivyo kwa kuonyesha imani yetu katika Kristo, kwa kutubu, kubatizwa, na kumpokea Roho Mtakatifu. Huu ni mwanzo wa mabadiliko ya kiroho ambayo hudumu hadi mwisho wa maisha yetu ya hapa duniani. Wakati mwingine hii tunaita “kuvumilia hadi mwisho,” ambako kunamaanisha kwamba tunajitahidi kushika agano letu la ubatizo la utiifu kwa maisha yetu yote, tukitubu pale inapohitajika na kusonga mbele tena. “Ndiyo, na kila mara watu wangu wanapotubu,” Yesu anasema, “nitawasamehe makosa yao dhidi yangu” (Mosia 26:30).

Picha
ubatizo

Unaweza Kutegemea Msaada wa Mungu

Katika maisha yako kabla ya kuzaliwa, wewe ulimchagua Mungu, ulimchagua Kristo, ulichagua “kuwa zaidi” kwa msaada Wao. Na unaweza kutegemea msaada Wao. Washirika wa Uungu sio watazamaji wasiovutiwa katika maisha yako. Wanatupenda pasipo ukomo na wanatumia uwezo wao ili kutusaidia, kadiri sisi tutakavyowaruhusu. Wao daima wanaheshimu haki yetu ya kujiamulia, lakini wana hamu ya kutubariki. Yesu anatuhakikishia sisi, “sitawasahau ninyi, Ee nyumba ya Israeli. Tazama, nimekuchora viganjani mwa mikono yangu” (1 Nefi 21:15–16).

Kuwa Bora Zaidi Hatua kwa Hatua

Baadhi huhisi kwamba ufalme wa selestia ni tumaini halisi kwa wengine lakini si kwa ajili ya wao. Ukweli ni, hakuna yeyote anayestahili pasipo neema ya Yesu Kristo. Kwa shukrani, wewe unaweza kuifikia neema Yake. Yesu ametuambia kwamba Yeye ameushinda ulimwengu. Kwa ubatizo wako na maagano mengine, unajifunga wewe mwenyewe Kwake ili kwamba pamoja Naye, wewe pia uushinde ulimwengu.

Wewe huhitaji kupata ukamilifu hapa duniani. Nabii Joseph Smith alilinganisha hili na kupanda ngazi: unaanzia chini kabisa na kupanda ngazi moja baada ya nyingine katika kujifunza na kuishi kanuni za injili. Na kujifunza huko, alifundisha, kunaendelea hata baada ya maisha haya—“siyo yote tutayajua katika ulimwengu huu.”2

Picha
mvulana akiwa hekaluni

Udhaifu wowote, ugumu, au mateso tunayokabiliana nayo duniani, Mungu anawaahidi watoto Wake waaminifu kwamba hakuna baraka itakayozuiliwa kama tutabakia kwenye njia ya agano (au kwa haraka tukirudi kwenye njia hiyo). Ndipo yote yanakuwa sawa. Huo ndio mpango wa kiungu wa kuwa zaidi!

Muhtasari

  1. Truman G. Madsen, Eternal Man (1966), 31–32.

  2. Teachings of Presidents of the Church: Joseph Smith (2007), 268.

Chapisha