“Huko San Diego, Marekani,” Kwa ajili ya Nguvu Kwa Vijana, Julai 2021, 20–21.
Jinsi Tunavyoabudu
Huko San Diego, Marekani
Habari! Jina langu ni Chace B. Nina umri wa miaka14, na ninaishi San Diego. San Diego iko upande wa kusini mwishoni mwa jimbo la California, Marekani. Sura ya hii sehemu ni tofauti sana. San Diego ni nyumbani kwa bandari, tambarare, mabonde, makorongo, na vilima. Kwa kawaida ni eneo la joto kali na jua mwaka mzima.
Kutana na familia yangu?
Familia yangu na mimi tunaishi katika milima ya San Diego. Ninaishi pamoja na mama yangu; dada yangu mwenye umri wa miaka 10, Payslie; na abuelito na abuelita (babu na bibi yangu). Tunaishi shambani na wanyama wengi. Tunajaribu kuishi maisha ya kawaida sana na ya mtindo wa zamani.
Kuifanya Sakramenti kuwa Maalumu
Wakati wa karantini ya COVID-19, Jumapili ingeweza kufanywa kitu cha kawaida sana nyumbani kwenye makochi yetu na ndani ya mavazi yetu ya kawaida. Nilitaka kufanya kitu ili kuhakikisha Jumapili ilikuwa siku maalumu. Niliamua kuitengenezea familia yetu trei letu wenyewe la sakramenti kama mojawapo ya lengo langu la kiroho kwa ajili ya Programu mpya ya Watoto na Vijana.
Kwanza, nilichukua kipande cha ubao na kutoboa matundu upande mmoja kwa ajili ya vikombe. Kisha nikachonga trei upande ule mwingine wa ubao kwa ajili ya mkate. Abuelita wangu akanisaidia kupiga msasa ubao huo hadi ukawa nyororo. Halafu tukabandika mshikio na kuunganisha ule ubao.
Jumapili ya kwanza tulienda kutayarisha sakramenti na hatukuweza kupata vikombe ambavyo vilitosha katika yale matundu ya trei. Sote tulitafuta vikombe kwa masaa mengi. Baada ya kitambo niliamua kwamba kuwepo ama kusiwepo kwa vikombe vinavyofaa bado tutakwenda kupokea sakramenti. Hatutakubali hili lituzuie kushika kitakatifu siku ya Sabato.
Jumapili ile tulipopokea sakramenti, palikuwa na ukimya, nia, na unyenyekevu zaidi. Nilijisikia kuridhika kwa lengo nililoliweka na kulitimiza. Ninajua na kuweza kuhisi kwamba Baba yangu wa Mbinguni alifurahi kwa lengo langu na uchaguzi uliohusika.