2021
Rangi 7 kwa Maisha ya Furaha Zaidi
Julai 2021


“Rangi 7 kwa Maisha ya Furaha Zaidi,” Kwa Ajili ya Nguvu kwa Vijana, Julai 2021, 8–11.

Rangi 7 kwa Maisha ya Furaha Zaidi

Hatua hizi rahisi ufanyazo kila siku huongeza furaha kwenye maisha yako.

Picha
kijana akichora

Kielelezo na Katy Dockrill

“Tazama! Nimetengeneza hii kwa ajili yako!” kijana wangu wa kiume alisema huku ameshikilia picha yake karibu kabisa na uso wangu. Karatasi iligusa pua yangu na kilichokuwepo ni matone mengi ya rangi mbalimbali. Ilikuwa haiwezekani kuona chochote kwa uwazi.

Niliposukuma ule mchoro nyuma, ndipo matone yale yalipoonekana vizuri.

“Unafikiri hii ni nini?” aliuliza.

Mwanangu amefanya kazi masaa mengi kuchora kile alichodhania ni uhalisia wa picha za sisi wawili—isipokuwa nywele zangu mimi siyo za njano.

“Sikuwa na kahawia ya kutosha” aliongezea. “Na manjano ni rangi ya furaha hata hivyo.”

Nilipoiangalia kwa makini kazi yake hiyo, niliweza kuona jinsi gani kwa upendo mwanangu alikuwa amechora picha hii. Sikuweza kuhesabu idadi ya rangi. Zilikuwa nyingi sana. Na alikuwa sahihi, mimi nilionekana mwenye furaha tele—ukijumuisha na nywele za manjano.

Fikiria juu ya mchoro uliouona. Utaona kwamba hakuna rangi hata moja inayoifanya iwe nzuri. Ukweli ni, unapotazama rangi moja peke yake, haivutii hata kidogo. Bali, unapoziunganisha zote kwa pamoja, unaona kazi nzuri ya sanaa yenye kuvutia.1

Kutafuta furaha katika maisha ni sawa sawa na kuchora. Kuna rangi ndogondogo za dhati, au shughuli za kila siku, tunazoweza kufanya ili kutengeneza maisha yaliyojaa furaha. Zikifanywa zenyewe au zikifanywa mara moja tu, shughuli hizi hazitaonekana bora zaidi. Lakini tunapoziunganisha pamoja tena na tena katika jitihada za kila siku na kila wiki, zinaweza kutengeneza wingi wa maisha ya furaha.

Hapa kuna rangi au shughuli saba unazoweza kuzikuza ili kutengeneza furaha zaidi katika maisha yako.

Rangi ya 1: Changamana na watu watakaokuinua kiroho.

Picha
kijana akitazama juu

Furaha inategemea sana watu unaochangamana nao. Hii haimaanishi kwamba huwezi kuwa rafiki na watu ambao hawana furaha nyakati zingine. Ukweli ni kwamba sote tunapitia kutokuwa na furaha wakati fulani.

Lakini hakikisha unautumia muda wako kwa kukaa na watu wanaokuinua na kukutia moyo. Marafiki wazuri wanaokusaidia wewe kuishi viwango vya Mungu wanaweza kuleta tofauti kubwa kwenye furaha yako. Na jaribu kuwa rafiki mwenye kuinua kiroho kwa wengine. Wewe unaweza kufanya tofauti kubwa katika maisha ya wengine pia.

Rangi ya 2: Tumia muziki ili kuongeza furaha yako.

Picha
noti za muziki

Muziki una nguvu kubwa katika akili yako. Unaweza kiuhalisia kubadili kemia katika ubongo wako. Muziki mzuri unaweza kukusaidia kujisikia chanya, mwenye furaha, na mwenye kuvutiwa. Jitengenezee orodha ya nyimbo za furaha, za kutia moyo, na za kukuza imani za kusikiliza mara kwa mara.

Rangi ya 3: Toka nje.

Picha
miti

Kufurahia uumbaji wa Mungu kunaponya sana roho na miili yetu. Ni muhimu sana kwa furaha yako kuwa na kawaida ya kutenga muda wa kuwa mbali na skirini za runinga, kompyuta, na simu ili kwenda nje na kufurahia mwanga wa jua, mimea na wanyama wanaokuzunguka. Nenda matembezini pamoja na famili yako na marafiki zako, chezeni michezo ya nje, someni na kujifunza nje ya nyumba. Utashangazwa ni vizuri kiasi gani unahisi unapofanya hayo.

Rangi ya 4: Lala usingizi wa kutosha.

Picha
kitanda

Bwana amesema kwamba usingizi ni muhimu kwa afya ya akili na mwili wako (ona Mafundisho na Maagano 88:124). Kama betri ya simu inahitaji kuchajiwa upya, akili yako inahitaji usingizi ili ifanye kazi vizuri. Kama vile tu unavyojipangia muda wa kuamka asubuhi, hakikisha pia unajipangia muda wa kulala (na usiende kulala ukiwa na simu yako!).

Rangi ya 5: Kuwa na maongezi ya kina na nafsi yako.

Picha
vijana wakizungumza

Kutumia ujumbe mfupi wa simu na mitandao ya kijamii ili kuongea na marafiki zako na familia inaweza kuwa ya kupendeza. Lakina kuwa na maongezi ya ana kwa ana inafanya kitu fulani akilini mwako na rohoni mwako kitu ambacho mawasiliano ya kielekroniki hayawezi. Hakikisha unachangamana na familia yako na marafiki zako. Tenga muda wa kusikiliza na kuzungumza na wale wanaokuzunguka.

Rangi ya 6: Fanya mazoezi ya mara kwa mara na jaribu kula chakula bora.

Picha
chakula

Ubongo wako unaweza kufanya kazi tu kwa kichocheo unachoupatia. Vyakula ambavyo vimechakatwa kwa hali ya juu na vyenye sukari nyingi (nyakati zingine vinajulikana kama vyakula taka) vinaweza kuwa na ladha nzuri lakini mara nyingi huifanya akili na mwili wako kuwa goigoi. Habari njema ni kwamba unapokula zaidi matunda, mboga za majani, na nafaka, tamaa yako ya kula vyakula taka inapungua. Bwana ametupatia mwili mmoja tu, hivyo ni vyema zaidi tukautunza vizuri!

Rangi ya 7: Omba na Utafakari.

Picha
mvulana akitafakari

Bwana na manabii na mitume Wake mara kwa mara wametushauri tutenge muda wa kuomba na kutulia. Kuomba na kutafakari vinaathari chanya katika maeneo ya ubongo ambayo yanahusika na furaha. Kama utatenga muda kwa mara kwa mara kutafakari na kuomba, furaha yako itaongezeka kidogo kila wakati. Baada ya kipindi cha muda mrefu, utagundua tofauti kubwa katika jinsi unavyojisikia amani na unavyojiamini.

Je, unatafuta Mawazo Zaidi?

Hizi rangi chache tu ni kati ya hatua za kila siku tunazoweza kuchukua ili kujaza miili na roho zetu kwa furaha. Kwa mawazo zaidi, tazama kupitia kijitabu cha Kwa Ajili ya Nguvu kwa Vijana ili kutambua kanuni ambazo zimekufanya wewe au wengine kuwa na furaha huko nyuma. Je, wewe unashawishika kufanya nini ili kujumuisha vitu hivyo kwa uendelevu zaidi katika maisha yako ya kila siku?

Daima kumbuka kwamba chanzo kikuu cha furaha yetu ni Mwokozi wetu, Yesu Kristo. Bila kujali hali yako, Yeye amesimama tayari kukubariki na kukusaidia kwenye magumu yako yote. Yeye atakusaidia kupata furaha unayoitumainia.

Muhtasari

  1. Mzee David A. Bednar wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili alifundisha, “Kama vile … rangi zinavyokamilishana na kuzalisha kazi ya sanaa yenye kuvutia, vivyo hivyo mwendelezo wetu katika kufanya vitu vinavyoonekana kuwa vidogo kunaweza kutuongoza kwenye matokeo ya kipekee kiroho” (mkutano mkuu wa Okt. 2009 [Ensign au Liahona, Nov. 2009, 19–20]).

Chapisha