2021
Andika
Julai 2021


“Andika,” Kwa ajili ya Nguvu kwa Vijana, Julai 2021, 18-19.

Andika

Kuandika mawazo yako unapokuwa unajifunza maandiko kunaweza sana kukusaidia kujifunza.

“Kila wakati ninapoanza kusoma maandiko, ninasinzia!” mmisionari mmoja alimwambia rais wake wa misheni. “Kana kwamba maandiko ni kidonge cha usingizi!”

Rais wake akamjibu, “Je umewahi kuandika muhtasari wakati unaposoma?”

“Hapana,” alisema yule mmisionari.

“Ni rahisi sana kusinzia au mawazo yako kwenda pembeni kama unasoma tu,” rais akasema, “lakini haiwezekani kusinzia unapoongeza kuandika!”

Ushauri wa rais wa misheni huyu aliompa mmisionari wake aliyekuwa akitaabika ulileta tofauti kubwa. Hivyo basi kama unatafuta njia mpya ya kuimarisha usomaji wako wa maandiko, ijaribu hiyo. Unapoandika kuhusu kile unachosoma, kuna uwezekano wa kujikuta mwenyewe ukijihusisha zaidi na kusoma vizuri zaidi pia.

Hizi ni baadhi ya njia tulizoona kuwa za msaada zaidi.

Kaka Steven Lund:

Picha
Steven Lund

Ninaiweka karatasi karibu ninaposoma. Pale Roho anaponipa msukumo wakati ninaposoma, ninaandika misukumo hiyo.

Nilipata wazo hilo kutoka kwa Mzee Richard G. Scott (1928–2015) wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili, ambaye alisema: “Andika mahali salama mambo muhimu anayojifunza kutoka kwa Roho. Utagundua kwamba unapoandika hisia zenye thamani kubwa, mara nyingi zitazidi kuja. Pia, maarifa unayopata yatakuwa nawe maisha yako yote” (“To Acquire Knowledge and the Strength to Use It Wisely,” Ensign, June 2002, 32).

Ninajua maneno hayo ni ya kweli. Ninapotayarisha mahubiri au somo, siendi tu kwenye maandiko pekee yake bali pia kwenye kile nilichoandika wakati nilipokuwa ninasoma.

Kaka Ahmad Corbitt:

Picha
Ahmad Corbitt

Mimi naipenda kujifunza kulingana na mada. Ninasoma maandiko kutokea mwanzo hadi mwisho, lakini pia napenda kuruka ruka na kujifunza mada. Kwa mfano, nitatumia Mwongozo wa Maandiko ili kupata maandiko juu ya imani au kukusanyika kwa Israeli. Kisha siyo tu naandika mihtasari, bali ninaandika chini kile ninachojifunza ili kuhakikisha ninakielewa kabisa. Daima ninashangazwa ni kiasi gani ninaelewa mambo vizuri zaidi ninapofanya hivi. Pia nachagua maandiko ya kukariri.

Kaka Bradley Wilcox:

Picha
Bradley Wilcox

Ninatunza shajara ya kujifunzia ambamo ninaandika maandiko katika maneno yangu mwenyewe. Kwa mfano, “Kwani mwanadamu wa asili ni adui kwa Mungu” (Mosia 3:19) inakuwa “Kwani mtu mwenye kiburi na asiyetubu anachagua kuwa adui kwa Mungu, lakini Mungu siyo adui yake. Mungu ni rafiki yake mkubwa.”

Pia ninaandika maswali. Yanaweza kuwa maswali ambayo ninafikiria kabla ya kusoma, au yanaweza kuwa maswali yanayochochewa na kile ninachosoma. Kwa vyovyote vile, hunifanya niwe mwenye fokasi.

Nguvu ya Kuandika Mawazo Yako

Kila mmoja wetu katika anajifunza maandiko kwa njia tofauti, lakini sote tunaandika tunapofanya hivyo!

Kusoma kunatusaidia kuyafanya mawazo na hisia kuwa vya kwetu. Hilo ni muhimu. Na tunapoongea au kuandika, tunagundua na kuelezea mawazo na hisia zetu kutoka ndani kuja nje. Tunaona hiyo inatusaidia kuufanya ukweli wa injili kuwa wetu vizuri zaidi.

Mvulana moja aligundua ukweli huu yeye mwenyewe wakati alipoombwa kutoa mahubiri katika mkutano wa sakramenti. Alikuwa amewasikia watu wengine wengi wakitoa mahubiri lakini hakuweza kukumbuka kila kitu. Safari hii ilikuwa tofauti. Alipoandika muhtasari wa mahubiri yake mwenyewe, siyo tu ilimsaidia kutoa mahubiri yaliyopangiliwa, bali aliyakumbuka kwa muda mrefu.

Kitu hicho hicho kinaweza kutokea katika kujifunza kwako maandiko. Kama unasinzia unapofungua maandiko yako, ni wakati wa kuamka. Jaribu kutoa penseli, kalamu, simu, au komputa, na anza kuandika. Utashangazwa na utofauti utakaokuja!

Chapisha