2021
Je, Nilikuwa Mwenye Kustahili?
Julai 2021


“Je, Nilikuwa Mwenye Kustahili?” Kwa Ajili ya Nguvu kwa Vijana, Julai 2021, 22–23.

Je, Nilikuwa Mwenye Kustahili?

Nilikuwa mwathiriwa wa unyanyasaji kwa muda mrefu kwa kadiri ninavyoweza kukumbuka. Je, hiyo iliathiri jinsi Bwana alivyoniona mimi?

msichana anayeonekana mnyonge

Kielelezo na Trent Gudmundsen

Mwanzoni, utoto wangu ulikuwa wa kawaida sana.

Tulienda kanisani na kuhudhuria mikutano na shughuli zote za Kanisa. Nilienda shuleni na nilicheza na marafiki zangu. Kama kijana, nilifanya mambo yote ambayo kijana wa kawaida hufanya. Nilikaa na marafiki zangu na nilikuwa katika kwaya na klabu ya maigizo. Nilihudhuria dansi. Lakini kulikuwa na siri nyeusi sana chini ya furaha ile, kwa nje ni wa kawaida.

Kutokea wakati nikiwa takribani umri wa miaka miwili nimekuwa mwathirika wa unyanyasaji wa kingono kutoka kwa kaka zangu wawili wakubwa. Pia waliwanyanyasa dada zangu. Tulikuwa wadogo sana kuelewa kilichokuwa kikitendeka, lakini nilivyokuwa mkubwa, nilianza kuelewa kidogo. Nilihisi giza na mchafu popote nilipokuwa katika uwepo wa kaka zangu hao.

Kuchanganyikiwa Kwangu Kulikua

Baada ya kuhudhuria darasa la Wasichana ambapo walifundisha kuhusu maadili, nilielewa maana ya maadili na usafi wa kimwili. Niliwasikiliza viongozi wangu wakinisihi mimi na wengine katika darasa langu kubaki wasafi kimaadili.

Nilijiuliza, “Je, ninawezaje kuwa msafi kimaadili?” Kadiri ninavyoweza kurudisha nyuma kumbukumbu yangu, nimekuwa mwathiriwa wa unyanyasaji wa kingono. Sikuweza kufanya lolote bali kujiuliza Bwana anawaza nini juu yangu. Je, mimi ni msichana mwenye maadili? Je, mimi ni mwenye kustahili kwenda kwenye miadi na mvulana mwadilifu katika kata na shule yangu? Je, unyanyasaji nilioteseka unanifanya nisiwe mwenye kustahili ndoa ya hekaluni?

Niliwaza sana kuhusu hilo. Haikuingia akilini kwangu kwamba ningedhaniwa nisiye na maadili wakati kile kilichotendeka kwangu hakikuwa chaguo langu. Je, kwa nini sikuweza kuhisi kuwa mwenye maadili? Je, sikuwa mwenye kustahili upendo wa Bwana? Je, nilihitaji toba?

Nilijaribu Tu Kusahau

Kwa hakika sikujua. Nilihisi kuwa mimi sio wa kulaumiwa, lakini wakati huo huo, nilijihisi mchafu na nisiye na hadhi na aliyedhalilishwa. Sikuweza kupata ujasiri wa kuwaambia wazazi wangu wala mtu mwingine yeyote. Nilijaribu mara kadhaa, lakini nilihisi kama najiaibisha na sikujua jinsi ya kusema hayo maneno. Nilijaribu tu kusahau kama ilikuwa inatokea.

Nilipokuwa na umri wa miaka 15, dada zangu wadogo walipata ujasiri ambao mimi niliukosa. Waliongea na mshauri shuleni. Muda mfupi baadae, mmoja wa kaka zangu alikamatwa na kuhukumiwa kwenda jela miaka mitatu. Lakini bado, kwa miaka kadhaa baadae, niliteseka kwa hofu hiyo hiyo kwamba sikuwa mwenye maadili au asiyestahili.

Nilipata Ujasiri wa Kupata Msaada

Hatimaye, siku moja nilipata ujasiri wa kwenda kumwona askofu wangu. Yeye alinieleza kwamba Bwana hataniwajibisha mimi kwa matendo yote ya kingono ambayo nililazimishwa kama mtoto na kama msichana. Alinihakikishia kwamba halikuwa kosa langu kabisa. Mbele za Bwana nilikuwa sina waa. Bado nilikuwa mwenye maadili!

Kwa ushauri nasihi kutoka kwa wataalamu na msaada kutoka kwa askofu wangu, nimeweza kuachana na unyanyasaji—na maumivu na mateso ulionisababishia—nyuma yangu. Sasa hakika ninayo furaha na maisha ya kawaida. Nilifunga ndoa hekaluni na mwanaume mwadilifu, na tunalea familia yetu kwa furaha.

Nyakati zingine yaliyopita yanaweza kuingilia mawazo yangu, tena, ninaweza nikakumbuka maumivu ambayo nilijisikia ninapofikiria ustahili wangu.

Ninajiuliza ni vijana wengine wangapi walio katika hali kama ile mimi nilikuwa nayo, kujisikia aibu na kudhalilika, wakijiuliza kuhusu maadili yao na wapi wanafaa katika mpango wa Mungu.

Kwa vijana hawa ninataka kusema, Bwana anawapenda.

Moyo wake unauma kwa ajili yenu.

Yeye anajua kwamba ninyi sio wa kulaumiwa.

Yeye anajua kwamba hakika ninyi ni wenye maadili.

Yeye atakusaidieni kupata ujasiri na nguvu ya kuishi maisha yenu kwa furaha.