2022
Mpango wa Mungu wa Furaha na Hatima Yako ya Kiungu
Januari 2022


“Mpango wa Mungu wa Furaha na Hatima Yako ya Kiungu,” Kwa Ajili ya Nguvu kwa Vijana, Jan. 2022.

Mpango wa Mungu wa Furaha na Hatima Yako ya Kiungu

Kuelewa na kuishi kulingana na mpango wa furaha kunakuruhusu wewe kufikia hatima yako ya kiungu.

kukwea mlima

Vielelezo na Albert Espí

Ni nini kinakuja akilini unaposikia neno hatima? Je, unafikiri ni kitu kilichopangiliwa kabla na kisichoweza kuzuilika? Kitu cha kuogofya au kupendeza ambacho hakiwezi kubadilishwa bila kujali kile unachofanya? Au yawezekana unafikiria juu ya shujaa katika sinema au kitabu, ambaye alipangiwa kukamilisha wito, kuokoa ulimwengu, au kuwa mfalme au malkia?

Kamusi yawezekana ikakubali tafsiri hizo; hata hivyo, tunapoongelea juu ya hatima ya kiungu, tunamaanisha kitu tofauti. Tofauti na hatima unazozisoma katika vitabu au kuziona katika sinema, kufikia hatima yako ya kiungu inawezekana kwa sababu wewe ni mwana wa Mungu, lakini pia inakutaka wewe utumie haki yako ya kujiamulia.

Mungu anao uwezo wote mbinguni na duniani. Maagano tunayofanya na Baba yetu wa Mbinguni yanamruhusu Yeye kuwa mshirika wetu tunapotembea kupita dhoruba za maisha. Hatima yetu ya kiungu—uwezekano wetu tunapokuwa wabia na Mungu—inafanywa iwezekane kupitia mpango Wake wa furaha.

Kuelewa mpango wa Baba wa Mbinguni kwa ajili ya furaha yako kutakuruhusu wewe kutambua utambulisho na dhumuni lako la milele. Na kuchagua kufanya na kushika maagano yako na Mungu kutakuruhusu wewe kufikia dhumuni hilo.

Katika kitabu cha Musa tunasoma kwamba “Musa alikuwa amenyakuliwa juu katika mlima mrefu sana, naye akamwona Mungu uso kwa uso, na akaongea naye” (Musa 1:1–2). Kupitia maongezi haya binafsi, Mungu alimfundisha Musa kuhusu utambulisho wake wa milele. Ingawa Musa alikuwa na mwili wenye kufa na asiye mkamilifu, alijifunza kitu muhimu kuhusu yeye mwenyewe: yeye alikuwa hakika mwana wa Mungu (ona Musa 1:6).

Kumbuka Wewe U Nani

Shetani anakutaka wewe usahau kuwa u nani. Wakati Shetani akijaribu kumdanganya Musa kutokana na kazi ambayo Bwana aliiandaa kwa ajili yake, Musa kwa ujasiri zaidi alijibu, “Wewe ni nani? Kwani tazama, mimi ni mwana wa Mungu” (Musa 1:13; msisitizo umeongezwa). Musa kisha akatamka, “Nenda zako, Shetani; usinidanganye” (Musa 1:16; msisitizo umeongezwa).

Kwa maneno mengine, Musa alisema: “Huwezi kunidanganya mimi, kwa maana najua mimi ni nani. Huna nuru na utukufu wa Mungu. Kwa hivyo kwa nini nikuabudu wewe au niamini udanganyifu wako?”

Kamwe usisahau kwamba Mungu anakupenda na anatamani kukusaidia na kukubariki. Na Yeye anayo mapenzi ya kiungu kwako wewe binafsi kama mmoja wa watoto Wake. Tafadhali chukua muda ili kujifunza inamaanisha nini hasa kuwa mtoto wa Mungu. Kisha weka malengo na fanya chaguzi ambazo zitakusaidia wewe kuishi sawa sawa na maarifa hayo kila siku.

Ninayo Kazi kwa Ajili Yako

Unayo mambo mengi na shauku zinazokukabili. Unazo kazi za shule, marafiki, majukumu ya kifamilia, na pengine ajira. Ndiyo, changamoto yako ni kuwekea usawa majukumu haya yote muhimu ya maisha pasipo kusahau dhumuni kuu katika maisha. Mungu anayo kazi kwa ajili yako kuikamilisha (ona Musa 1:6). Hili ni jibu la swali “Je, kwa nini niko hapa duniani?”

Kama mtoto wa Mungu, wewe ulikuja duniani kupokea mwili wa nyama na mifupa. Kwa mwili wako, wewe unaweza kuchagua kwa uaminifu kumfuata Yesu Kristo. Unaweza kuchagua kutii amri za Mungu, kupokea ibada takatifu, na kufanya na kushika maagano ya injili. Kufanya mambo haya kutakuandaa wewe kutimiza hatima yako ya kiungu.

Kusudi hili likiwa wazi akilini mwako, unaweza kuona umuhimu wa kupokea sakramenti kila wiki, kujifunza maandiko, kusali kila siku, kuweka malengo muhimu, na kuwatumikia wengine. Mambo haya yanasaidia kukukumbusha wewe kwa nini uko hapa, na yatasaidia kukukumbusha kuwa mwenye kustahili kupokea ufunuo binafsi ambao unahitaji ili kuwa mwenye furaha na kubakia kwenye njia ya agano. Unapotubu na kumfuata Bwana kwa bidii, utapokea maelekezo binafsi katika kila kipengele cha maisha yako.

Kupanda milima kupitia msitu wenye maporomoko ya maji

Jitahidi kuwa Yule Uliyekusudiwa Kuwa

Shughuli na mashaka ya ulimwengu, au kukosa kwako usalama, vinaweza kukusababisha wewe usahau jukumu lako muhimu katika mpango mkuu wa wokovu. Kama hii ikitokea, ninakualika uje kwa Kristo (ona Moroni 10:32). Hakuna chochote katika mpango wa Mungu wa milele kinachowezekana pasipo Yeye, na kwa Yeye, kila kitu chema kinafikika.

Kujitahidi kumfuata Mwokozi ndiyo njia iliyo bora ya kutunza mtazamo wa injili. Imani na matumaini yakiwa katika Yeye, kwa kujiamini unaweza kuzikabili changanoto za maisha. Pia utakuwa na uhakika mkubwa zaidi unapofanya chaguzi zako, unapotatua matatizo yako, unapofanya kazi kuelekea malengo ya haki, na unapoyakabili majaribu.

Maamuzi yako yatakuwa na matokeo ya milele. Kupitia Yesu Kristo na neema Yake ya kulipia dhambi, wewe unaweza kuwa na furaha katika maisha haya na katika maisha yajayo. Unaweza ukafikia hatima yako ya kiungu ya kupokea yote Yeye aliyo nayo na kuishi aina ya maisha Anayoishi, ambayo ni “uzima wa milele, … kipawa ambacho ni kikuu katika vipawa vyote vya Mungu” (Mafundisho na Maagano 14:7).