2022
Kumtafuta Yesu Kristo katika Agano la Kale
Januari 2022


“Kumtafuta Yesu Kristo katika Agano la Kale,” Kwa Ajili ya Nguvu Kwa Vijana, Jan. 2022.

Njoo, Unifuate

Kumtafuta Yesu Kristo katika Agano la Kale

Hapa kuna njia tatu unazoweza kumtafuta Mwokozi unapojifunza Agano la Kale mwaka huu.

Yesu Kristo

Chemsha bongo ya haraka: Ni vitabu gani vya maandiko vinamhusu Yesu Kristo? Hmm. Hebu tuone.

Kitabu cha Mormoni ni ushuhuda mwingine juu Yake.

Mafundisho na Maagano ni mkusanyiko wa jumbe kutoka Kwake kwenda kwa Joseph Smith na manabii wengine.

Agano Jipya linaelezea matukio ya maisha Yake.

Lakini vipi kuhusu Agano la Kale? Je linatufundisha kuhusu Yesu Kristo, pia?

Ndiyo! Ukweli ni kwamba, Mwokozi aliweka jitihada ya ziada katika kuwasaidia wafuasi Wake kuelewa nafasi Yake katika Agano la Kale: “Akaanza kutoka Musa na manabii wote, akawaeleza katika maandiko yote mambo yaliyomhusu Yeye mwenyewe” (Luka 24:27).

Hapa kuna njia tatu unazoweza kumtafuta Yesu Kristo unapochunguza Agano la Kale mwaka huu.

1. Maandiko ambayo humzungumzia Yesu Kristo yakitumia jina tofauti.

Katika Agano la Kale, Yesu Kristo mara nyingi ameitwa “Bwana” au “Mungu.” Matoleo ya Biblia zinazochapishwa na Kanisa hili hujumuisha tanbihi ambazo zinaweza kukusaidia kuelewa wakati aya inamrejelea Yesu Kristo. Kwa mfano, Musa alipoongea na Mungu katika kichaka kilichokuwa kikiwaka moto (ona Kutoka 3:6), tanbihi inafafanua kwamba alikuwa akiongea na Mwokozi.1 Rais Russell M. Nelson ametuhimiza kujifunza majina na vyeo tofauti vya Yesu Kristo vilivyotumika katika maandiko.2

2. Vitu na matukio ambayo yanatukumbusha juu ya Yesu Kristo.

Maandiko mengi ya Agano la Kale yanajumuisha alama ambazo zinaweza kutufundisha kuhusu Yesu Kristo na kutukumbusha juu ya msaada ambao Yeye anatupatia. Kwa mfano:

  • Maandiko mengi yanaelezea wakati ambapo watu waaminifu waliamriwa kutoa dhabihu za wanyama kama sehemu ya kuabudu kwao. Kwa mfano, kama wana wa Israeli walivyoweka alama kwenye milango yao kwa damu ya kondoo, waliokolewa kutokana na janga la kutisha. Dhabihu hizi zinatukumbusha kwamba Yesu Kristo aliruhusu Yeye mwenyewe auawe kama sehemu ya Upatanisho Wake ili kushinda kifo cha kimwili na kiroho. (Ona Kutoka 12:13.)

  • Wakati mmoja nabii aliyeitwa Eliya alilazimika kujificha jangwani. Alijihisi mwenye huzuni na akasema kwamba alitamani angekuwa amekufa. Wakati akiwa amelala, mkate na maji kimuujiza vikatokea, vikimuimarisha kimwili na kihisia kiasi cha kumtosha kusonga mbele. Hii inaweza kutukumbusha kuwa Yesu Kristo ni Maji ya Uhai na Mkate wa Uzima, chanzo halisi cha tumaini na uzima. (Ona 1 Wafalme 19:1–8.)

  • “Neno lako ni taa ya miguu yangu,” mtunga zaburi mmoja aliandika (Zaburi 119:105). Naye Mika alishuhudia, “Nikaapo gizani, Bwana atakuwa nuru kwangu” (Mika 7:8). Maneno yao yanatukumbusha kwamba Yesu Kristo ndiye Nuru ya Ulimwengu, akituongoza kurudi kwenye nyumba yetu ya mbinguni.

Unaposoma, unaweza hata kugundua mambo mengine ambayo yanakukumbusha wewe juu ya Yesu Kristo na uweza Wake wa kutuokoa sisi. Kwa mfano, familia ya Nuhu ilipookolewa kutokana na gharika ndani ya safina au Yona alipopewa muda wa kutubu wakati akiwa ndani ya nyangumi. Matukio haya yanaweza kutukumbusha sisi kwamba Mwokozi anaweza kutubeba ili kuvuka dhoruba za maisha na kutupatia fursa ya kurudi kwenye njia sahihi. (Ona Mwanzo 7:1; Yona 1:17.)

3. Aya ambazo zinatoa unabii juu ya kuzaliwa kwa Yesu Kristo.

Leo tunatazamia na kujiandaa kwa ajili ya Ujio wa Pili wa Yesu Kristo. Katika njia iliyo sawa na hiyo, manabii wa Agano la Kale walitazamia na kuandika kuhusu ujio Wake wa kwanza, Yeye alipozaliwa duniani. Kwa mfano:

  • Nabii aliyeitwa Balaamu alielezea jinsi “itakavyotokea Nyota katika Yakobo” (Hesabu 24:17). Hii inamaanisha kwamba Mwokozi angezaliwa katika ukoo wa Yakobo (au Israeli).

  • Nabii aliyeitwa Nathani alimwambia Mfalme Daudi kwamba Yesu Kristo angekuwa mmoja wa wazao wa Daudi—kwamba ukoo wake ungeimarisha “kiti cha enzi cha ufalme wake milele” (2 Samweli 7:13).

  • Nabii Isaya aliandika baadhi ya maelezo yajulikanayo vizuri sana juu ya Mwokozi katika Agano la Kale. Baadhi ya maneno yake yalitumika kama mashairi katika wimbo wa Handel wa Messiah, ambao mara kwa mara huimbwa wakati wa Krismasi. (Ona Isaya 7; 9; 40; 53.)

msichana akisoma maandiko kwa kutumia tochi

Kwa mazoezi kidogo, utaweza kumpata Yesu Kristo kote kwenye Agano la kale mwaka huu. Anakupenda wewe hasa, kama vile alivyowapenda Adamu na Hawa, Haruni na Miriamu3—na wengineo wengi ambao Yeye binafsi aliwahudumia katika hadithi hizi za kale, zenye kuvutia. Kwa imani katika Yesu Kristo, na kwa kusaidiana sisi kwa sisi, mwaka huu utakuwa mwaka wa kuvutia katika kusoma maandiko!