2022
Mtumaini Bwana
Januari 2022


“Mtumaini Bwana,” Kwa Ajili ya Nguvu kwa Vijana, Jan. 2022.

Mtumaini Bwana

(Mithali 3:5–6)

Mungu anakualika wewe kumtumaini Yeye katika mambo yote.

Wakati mwingine mambo magumu yanapotokea, sisi tunajiuliza kama tunaweza kumtumaini mtu yeyote, ikijumuisha Mungu. Tunaogopa kwamba anaweza kutuangusha pia. Habari njema ni kwamba Mungu anatupenda sisi kiukamilifu kabisa. Yeye ni mkarimu na mwema na ni mwaminifu. Yeye habadiliki na ni wa kutegemewa.

Na kwa sababu hiyo, tunaweza kumtumaini yeye bila kujali lolote. Dhima ya Vijana kwa mwaka huu ni “Mtumaini Bwana” (Mithali 3:5–6).

Hapa kuna mifano ya jinsi kila mmoja wetu katika Urais Mkuu wa Wasichana na Wavulana tulivyokuja kumtumaini Bwana.

Picha
Urais Mkuu wa Wasichana

Michelle D. Craig

Bonnie H. Cordon

Rebecca Craven

Tumaini Malengo ya Mungu

Siku kadhaa tu kabla ya kufikisha miaka 16, familia yangu ilihamia upande mwingine wa nchi. Nilidhani lilikuwa jambo la kutisha! Nikiangalia nyuma, ninaweza kuona wazi kabisa kwamba baadhi ya baraka kubwa zaidi kwa familia yetu na kwa ajili yangu zilikuja kwa sababu ya kuhama huko nilipokuwa kijana. Yawezekana tusielewe ratiba ya Bwana kwa wakati huo, lakini tunamtumaini Yeye kwa sababu tunaweza kutumaini moyo Wake na sababu Zake.

Michelle D. Craig

Tumaini Wakati wa Bwana

Kwa sababu ya wito wa baba yangu kama rais wa misheni, nilipokea wito wangu wa kuhudumu misheni yangu mwenyewe mapema zaidi kuliko umri wa kawaida wa akina dada wamisionari. Hii ilimaanisha ningeingia kituo cha mafunzo ya umisionari kabla ya mahafali ya kumaliza sekondari. Kwangu mimi ratiba hiyo haikuleta maana, lakini nilipokea uthibitisho imara kabisa wa kiroho wa kumtumaini Bwana. Nilifanya, na mambo yalienda vizuri kabisa.

Kumtumaini Bwana inamaanisha kusonga mbele hata wakati ambapo njia haiko wazi.

Bonnie H. Cordon

Mtumaini Mungu katika Nyakati Ngumu

Wakati nikikua, baba yangu alifanya kazi kama afisa wa Jeshi. Upande pekee usiofurahisha kwenye kazi yake ni kwamba alipaswa kwenda vitani. Nilikuwa na umri wa miaka 13 wakati baba yangu alipoondoka kwenda Vietnamu kwa mara ya pili. Hofu ya kutokurudi kwake daima ilikuwa mawazoni mwangu, kadhalika na tumaini langu kwa Bwana lilikuwa mawazoni mwangu daima. Kabla ya kuondoka, baba yangu alinipa baraka za baba akinihakikishia kwamba Bwana angekuwa na mimi na kunisaidia wakati baba yangu hayupo. Nilihisi amani. Ingawa sikuwa na uhakika kwamba baba angerejea nyumbani salama, nilitumaini kwamba kila kitu kingekuwa sawa, bila kujali litakalotokea.

Rebecca Craven

Picha
Urais Mkuu wa Wavulana

Ahmad S. Corbitt

Steven J. Lund

Bradley R. Wilcox

Jitumainishe Mwenyewe kwa Mungu

Nilipojiunga na Kanisa kama kijana mdogo, niliamua kutoa maisha yangu, muda, na moyo wangu kwa Bwana. Ingawa azimio hilo la kudumu lilikuwa la kuogopesha kidogo, nilijua lilikuwa sahihi. Nilihisi kwamba Baba yangu wa Mbinguni alilitaka hili kutoka kwangu, na nilikuwa na amani kufanya hivyo. Ninafurahi kwa kuchagua kumtumaini Mungu na kuacha Yeye ashinde katika maisha yangu. Ninao uhakika kwamba kama ningetegemea akili zangu mwenyewe, maisha yangu yasingekuwa yanakaribia kuwa na utajiri wa shangwe, furaha, na amani.

Ahmad S. Corbitt

Tumaini katika Mwongozo wa Kiungu wa Bwana

Baada ya kuhudumu misheni yangu, nilihisi kusukumwa kujiunga na jeshi badala ya kurudi chuoni. Hili lilikuwa jambo la mwisho nililotaka kulifanya! Nilihisi kukanganyikiwa, lakini nilikuwa nimejifunza kutumaini katika Mungu, na nilipata imani ya kutosha kumsikiliza Yeye na kutii. Nilikuwa askari kwa miaka mitatu.

Mambo mengi mazuri katika maisha yangu yamemiminika kutokana na uamuzi huo, ikijumuisha kukutana na mke wangu wa siku za baadae.

Steven J. Lund

Tumaini katika Misukumo ya Mungu ya Kutenda Sasa

Baada ya kufundisha darasa la sita kwa miaka mitatu, nilijifunza kwamba kama nitafundisha kwa miaka minne zaidi, wilaya ya shule ingenilipia ada ya masomo yangu ya shahada ya uzamili. Ilionekana kana kwamba ni mpango mzuri—hadi Roho aliponisukuma niache kazi yangu na nirejee na kupata shahada yangu kwa wakati huo. Mke wangu alikuwa na msukumo wa namna hiyo hiyo, hivyo tulisonga mbele. Ilimaanisha tungepaswa kulipia ada sisi wenyewe. Lakini kwa sababu tulifanya hivyo, mimi niliajiriwa kufundisha huko BYU—Provo. Dirisha hilo la fursa lisingeweza kuwa wazi kama tungelisubiri miaka minne zaidi. Hatukujua jinsi ambavyo mambo yangekuwa, lakini Bwana alielekeza njia zetu kama vile tu Yeye alivyoahidi.

Bradley R. Wilcox

Chapisha