2022
Baba wa Mbinguni Ananijua Mimi
Januari 2022


“Baba wa Mbinguni Ananijua Mimi,” Kwa Ajili ya Nguvu Kwa Vijana, Jan. 2022.

Dhima na Mimi

Vijana wakielezea jinsi wanavyoishi maneno ya Dhima ya Wasichana na ya Akidi ya Ukuhani wa Haruni

Baba wa Mbinguni Ananijua Mimi

“Mimi ni mwana mpendwa wa Mungu.”

anga la usiku milimani

Nilipokuwa nimepiga kambi pamoja na baba yangu, tulishiriki muda ambao kamwe sitausahau. Tulitembea upande mmoja wa mlima usiku tukiwa tumechelewa na tukatafuta mahali tukakaa pamoja. Tulipokuwa tukiangalia angani usiku ule, tulikuwa tumezungukwa na nyota angavu zaidi ambazo sijapata kuziona. Tulikaa pamoja kwa muda mrefu sana, tukitaja majina ya sayari na vilimia moja baada ya nyingine.

Nikiutazama ulimwengu ulio mbele yangu, nilijiona kuwa mdogo sana na nisiye muhimu. Sikuweza hata kufikiria ni sayari ngapi zingine ziko huko—“dunia zisizo na idadi,” au sio? Mimi ni nini ukilinganisha na yote hayo?

Nilimwuliza baba yangu kama kuna maisha mengine huko nje ya ulimwengu, nikiwa tayari nimeshalemewa kwa wazo hilo. Lazima atakuwa alisoma mawazo yangu, kwa sababu yeye alisema tu: “Hiki ndicho ninachojua. Baba wa Mbinguni ana uumbaji mwingi sana, kama unavyoona. Lakini kati ya uumbaji Wake wote, anakupenda wewe binafsi.

“Yeye anaona kila kitu wewe unachopitia na anataka kuliko chochote kuwa sehemu ya maisha yako. Anataka akuletee shangwe na akusaidie kurejea kuishi na Yeye milele.

Bado nilijiona mdogo chini ya anga kubwa la usiku ule, lakini niliamini ushuhuda wa baba yangu. Mimi ni wa muhimu kwa Baba wa Mbinguni. Na Yeye alitaka kuwa katika maisha yangu.

Nilikumbuka kile Rais Dieter F. Uchtdorf, wakati huo akiwa Mshauri wa Pili katika Urais wa Kwanza, alichofundisha: “Hii ni kweli iliyo kama uongo juu ya mwanadamu: akilinganishwa na Mungu, mwanadamu si chochote; lakini sisi ni kila kitu kwa Mungu.”1

Kama vile anga lile lililojaa nyota, uumbaji wa Mungu hauna mwisho—na ndivyo ulivyo upendo Wake kwa kila mmoja wa watoto Wake. Kwa kila mmoja wetu. Wakati mwingine ninafikiria nyuma katika ule wakati nilipokuwa nimekaa juu ya mlima katika mshangao wa ajabu. Yawezekana nikawa si chochote nikilinganishwa na Mungu, lakini Yeye hafikiri hivyo. Mini ni mwana Wake, na ananijua.

Mwandishi anaishi California, Marekani

Muhtasari

  1. Dieter F. Uchtdorf, “Wewe ni Muhimu Kwake,” mkutano mkuu wa Okt. 2011 (Ensign au Liahona, Nov. 2011, 20).