Kitabu cha Mormoni: Je, Maisha Yako Yangekuwaje Bila Kitabu Hiki?
Katika njia ya muujiza mkubwa na ya pekee, Kitabu cha Mormoni kinatufundisha juu ya Yesu Kristo na injili Yake.
Mwaka wa 1986, nilialikwa kutoa mhadhara maalumu katika chuo kikuu huko Accra, Ghana. Kule nilikutana na waheshimiwa kadhaa, akiwemo mfalme wa kikabila wa Kiafrika. Tukiwa tunasalimiana kabla ya mhadhara, mfalme aliongea nami kupitia mkalimani wake, ambaye baadaye alinitafsiria. Nilimjibu mkalimani, na kisha mkalimani alitafsiri majibu yangu kwa mfalme.
Baada ya mhadhara wangu, mfalme alinilenga mimi moja kwa moja, lakini safari hii bila ya mkalimani wake. Kwa mshangao wangu, aliongea Kiingereza fasaha—Kiingereza cha Malkia, naweza kuongezea!
Mfalme alionekana kushangaa. “Kwani wewe ni nani?” aliuliza.
Nikajibu, “Mimi ni Mtume wa Yesu Kristo aliyetawazwa.”
Mfalme akauliza, “Ni nini unaweza kunifundisha mimi kumhusu Yesu Kristo?”
Nikajibu kwa swali: “Naomba nikuulize ni kipi ambacho tayari unakijua kumhusu Yesu Kristo?”
Jibu la Mfalme lilionyesha wazi kuwa alikuwa mwanafunzi mzuri wa Biblia na mtu aliyempenda Bwana.
Kisha nikamwuliza kama alijua utumishi wa Kristo kwa watu wa Amerika ya kale.
Kama nilivyotarajia, hakujua.
Nilimwelezea kwamba baada ya Kusulubiwa na Kufufuka, alikuja kwa watu wa Amerika ya kale, ambako alifundisha injili Yake. Alianzisha Kanisa Lake na aliwataka wanafunzi Wake kutunza kumbukumbu ya utumishi Wake miongoni mwao.
“Kumbu kumbu hiyo,” niliendelea, “ni kile tunachokijua kama Kitabu cha Mormoni. Ni ushuhuda mwingine wa Yesu Kristo. Ni andiko mwenza na Biblia Takatifu.”
Hadi kufikia hapo, mfalme akawa na shauku sana. Nikamgeukia rais wa misheni aliyeambatana nami na kumwuliza kama alikuwa na nakala ya ziada ya Kitabu cha Mormoni. Akatoa kimoja toka kwenye mkoba wake.
Nikafungua 3 Nefi aya ya 11 na pamoja mfalme na mimi tukasoma mahubiri ya Mwokozi kwa Wanefi. Kisha nikampa nakala ya Kitabu cha Mormoni. Mjibizo wake ulinigusa akili na moyo wangu daima: “Ungeweza kunipa almasi au rubi, lakini hakuna kilicho cha thamani zaidi ya elimu ya ziada kuhusu Bwana Yesu Kristo.”
Baada ya kupata uzoefu wa nguvu za maneno ya Mwokozi katika 3 Nefi, mfalme alitangaza, “Kama nikiongoka na kujiunga na Kanisa, nitalileta kabila langu lote pamoja nami.”
“Ee, Mfalme,” nikajibu, “haiendi hivyo. Uongofu ni wa mtu binafsi. Mwokozi aliwahudumia Wanefi mmoja mmoja. Kila mtu anapata ushahidi na ushuhuda wa injili ya Yesu Kristo.”1
Kaka na dada zangu, Kitabu cha Mormoni ni cha thamani kiasi gani kwenu? Kama utapewa almasi au rubi au Kitabu cha Mormoni, utachagua nini? Kiukweli, ni kipi cha thamani kubwa kwako?
Kumbuka katika kikao cha Jumapili asubuhi cha Aprilii 2017 cha mkutano mkuu, Rais Thomas S. Monson alimwomba “kila mmoja wetu ajifunze kwa maombi na kutafakari Kitabu cha Mormoni kila siku.”2 Wengi wameitikia wito wa nabii.
Acha nisema kwamba siyo mimi wala Riley mwenye miaka nane ambaye alijua kuna mtu alikuwa anatupiga picha. Tazama kwamba Riley anasoma Kitabu cha Mormoni chake kwa msaada wa alamisho ya “I Am a Child of God”.
Kitu chenye msukumo kinatokea wakati mtoto wa Mungu anapotaka kujua zaidi kumhusu Yeye na Mwana Wake Mpendwa. Hakuna sehemu yoyote kweli hizo zinafundishwa kiufasaha na kwa nguvu kuliko katika Kitabu cha Mormoni.
Tangu changamoto ya Rais Monson miezi sita iliyopita, nimejaribu kufuata ushauri wake. Miongoni mwa vitu vingine, nimeweka orodha ya Kitabu cha Mormoni ni nini, kinathibisha, nini kinakanusha, nini kinatimiza, nini kinafafanua, na nini kinafunua.3 Kuangalia Kitabu cha Mormoni kupitia lensi hizi imekuwa ni zoezi la umaizi na msukumo! Ninapendekeza kwa kila mmoja wenu.
Katika kipindi hiki cha miezi sita, niliyaalika makundi kadhaa—wakiwemo Ndugu zangu katika Akidi ya Kumi na Wawili, wamisionari huko Chile, na marais wa misheni na wake zao waliokusanyika Argentina—kufikiria maswali matatu yanayohusiana ambayo ninawaomba ninyi myafikirie leo:
Kwanza, maisha yako yangekuwaje bila ya Kitabu cha Mormoni? Pili, ni nini ambacho hungekijua? Na tatu, ni nini ambacho usingekuwa nacho?
Majibu yenye shauku kutoka vikundi hivi yalitoka moja kwa moja mioyoni mwao. Haya ni machache kati ya maoni yao:
“Bila ya Kitabu cha Mormoni, ningechanganyikiwa kuhusu mafundisho ya kuchanganya na maoni kuhusu vitu vingi sana. Ningekuwa kama nilivyokuwa kabla sijalipata Kanisa, nilipokuwa natafuta elimu, imani, na tumaini.”
Mwingine alisema: “Nisingejua kuhusu jukumu la Roho Mtakatifu katika maisha yangu.”
Mwingine: “Nisingeweza kuelewa vizuri kusudi langu hapa duniani!”
Msemaji mwingine alisema: “Nisingejua kwamba kuna mwendelezo wa kuishi baada ya maisha haya. Kwa sababu ya Kitabu cha Mormoni, ninajua kwamba hakika kuna maisha baada ya kifo. Hili ndilo lengo la mwisho ambalo kwalo tunafanyia kazi.”
Mchango huu wa mwisho umenifanya mimi niyaangalie maisha yangu miongo iliyopita nikiwa daktari mwanafunzi. Moja ya majukumu yanayotishaaliyonayo daktari wa upasuaji, mara kadhaa, ni kuijulisha familia wakati mpendwa amefariki. Katika hospitali moja niliyofanyakazi, chumba maalum kilijengwa kwa ukuta ororo ambapo familia ingeweza kupokea taarifa kama hizo. Pale, baadhi ya watu wanaonyesha huzuni yao kwa kugonga vichwa vyao kwenye zile kuta ororo.Jinsi nilivyotamani kuwafundisha wale watu kwamba kifo, ingawa ni vigumu kwa wapendwa wa marehemu, ni sehemu muhimu ya maisha yetu ya milele. Kifo kinaturuhusu sisi kuendelea katika ulimwengu ujao.3
Mwingine alijibu swali langu alisema: “Sikuwa na maisha hadi niliposoma Kitabu cha Mormoni. Japokuwa niliomba na kwenda kanisani maishani mwangu, Kitabu cha Mormoni kilinisaidia kufanya mawasiliano na Baba wa Mbinguni kwa mara ya kwanza.”
Mwingine alisema: “Bila ya Kitabu cha Mormoni, nisingejua kwamba Mwokozi hakuteseka tu kwa ajili ya dhambi zangu, bali Anaweza kuponya maumivu na huzuni zangu.”4
Na mwingine: “Nisingeweza kujua kwamba tuna manabii wa kutuongoza.”
Kujizamisha sisi wenyewe mara kwa mara katika ukweli wa Kitabu cha Mormoni kunaweza kuwa uzoefu wa kubadilisha-maisha. Mmoja wa mjukuu wetu mmisionari, Dada Olivia Nelson, alimuahidi mchunguzi kwamba kama angesoma Kitabu cha Mormoni kila siku, matokeo ya majaribio ya mitihani yake ya chuo yangepanda.Alifanya hivyo, na matokeo yakapanda.
Wapendwa kaka na dada, ninashuhudia kwamba Kitabu cha Mormoni hakika ni neno la Mungu. Kina majibu ya maswali mengi ya maisha yanayovutia. Kinafundisha mafundisho ya Kristo.5 Kinapanua na kufafanua kweli nyingi za “halisi na thamani”6 ambazo zilikuwa zimepotea kwa ajili ya muda wa karne nyingi na tafsiri nyingi mno za Biblia.
Kitabu cha Mormoni kinaleta uelewa kamili na wenye mamlaka wa Upatanisho wa Yesu Kristo kupatikana sehemu yoyote. Kinafundisha nini maana halisi ya kuzaliwa tena. Kutoka katika Kitabu cha Mormoni tunajifunza kuhusu kukusanyika kwa Israeli iliyotawanyika. Tunajua kwa nini tupo hapa duniani. Kweli hizi na nyingine zina nguvu sana na zimefundishwa kwa ushawishi katika Kitabu cha Mormoni kuliko kwenye kitabu kingine chochote.Uwezo mkubwa wa injili ya Yesu Kristo upo kwenye Kitabu cha Mormoni. Nukta.
Kitabu cha Mormoni kinaangazia mafundisho ya Bwana na kuanika mbinu za adui.7 Kitabu cha Mormoni kinafundisha mafundisho ya kweli ili kuondoa mila za uongo za kidini—kama vile desturi yenye dosari ya kufanya ubatizo wa watoto wachanga.8 Kitabu cha Mormoni kinaonesha madhumuni ya maisha kwa kututaka sisi tutafakari umuhimu wa uzima wa milele na “furaha isiyo na-mwisho.”9 Kitabu cha Mormoni kinavunjavunja imani za uongo kwamba furaha inaweza kupatikana katika uovu10 na kwamba matendo mazuri binafsi ndiyo tu yanayotakiwa kurudi katika uwepo wa Mungu.11 Kinafuta milele dhana ya uongo kwamba ufunuo ulimalizika na Biblia na kwamba mbingu zimefunikwa leo.
Ninapofikiria juu ya Kitabu cha Mormoni. Ninafikiria neno nguvu. Kweli za Kitabu cha Mormoni zina nguvu za kuponya, kufariji, kurejesha, kusaidia, kuimarisha, kuliwaza, na kuchangamsha nafsi zetu.
Wapendwa ndugu na dada, ninaahidi kwamba unaposoma kwa maombi Kitabu cha Mormoni kila siku, utafanya maamuzi mazuri—kila siku. Ninaahidi kwamba mnapotafakari kile mnachojifunza, madirisha ya mbinguni yatafunguka, na mtapokea majibu ya maswali yenu na mwongozo wa maisha yenu mwenyewe. Ninaahidi kwamba mnapozama kila siku kwenye Kitabu cha Mormoni, mnaweza kuepushwa dhidi ya maovu ya siku, hata baa lenye kunasa la ponografia na madawa mengine ya kulevya.
Wakati ninapomsikia yoyote, ikijumuisha mimi mwenyewe, akisema,“Ninajua Kitabu cha Mormoni ni cha kweli,” ninataka kupaza sauti, “Hiyo safi, lakini haitoshi!” Tunahitaji kuhisi, kwa kina “katika sehemu ya ndani” ya mioyo yetu,12 kwamba Kitabu cha Mormoni bila shaka ni neno la Mungu. Lazima tuhisi kiundani zaidi kwamba hatutataka kuishi siku moja bila hicho. Ninaweza kufupisha maneno ya Rais Brigham Young kwa kusema, “Natamani ningekuwa na sauti ya radi saba ili kuwaamsha watu”13 kwenye ukweli na nguvu za Kitabu cha Mormoni.
Tunatakiwa kuwa kama mmisionari huyu kijana anayehudumu Ulaya aliyehisi kwa ndani kuhusu ukweli wa Kitabu cha Mormoni kwamba alimkimbilia na nakala ya kumbukumbu hizi takatifu mtu ambaye yeye na mwenzi wake walimkuta bustanini.
Ninashuhudia kwamba Joseph Smith alikuwa na ni nabii wa kipindi hiki cha mwisho. Alikuwa ni yeye ambaye, kupitia kipawa na nguvu za Mungu, alitafsiri hiki kitabu kitakatifu. Hiki ndicho kitabu ambacho kitasaidia kuuandaa ulimwengu kwa Ujio wa Pili wa Bwana.
Ninashuhudia kwamba Yesu Kristo ndiye Mwana pekee wa Mungu aliye hai. Yeye ni Mwokozi wetu, Mkombozi wetu, Mfano wetu mzuri, na Mwombezi wetu kwa Baba. Alikuwa Masiya aliyeahidiwa, Masiya wa duniani, na atakuwa Masiya wa milenia. Ninashuhudia kwa nafsi yangu yote kwamba kwa muujiza mkubwa na wa pekee, Kitabu cha Mormoni kinatufundisha juu ya Yesu Kristo na injili Yake.
Ninajua kwamba Rais Thomas S. Monson ni nabii wa Mungu hapa duniani leo. Ninampenda na kumkubali kwa moyo wangu wote. Nashuhudia hivi, katika jina takatifu la Yesu Kristo, amina.
Orodha za Kitabu cha Mormoni za Rais Nelson
Kitabu cha Mormoni ni:
-
Ushuhuda Mwingine wa Yesu Kristo. Waandishi wake wakuu—Nefi, Jacob, Mormon, Moroni—na mtafsiri wake, Joseph Smith, wote walikuwa mashahidi wa Bwana.
-
Kumbukumbu ya utumishi Wake kwa watu walioishi Amerika ya kale.
-
Kweli, kama ilivyoshuhudiwa na Bwana Mwenyewe.
Kitabu cha Mormoni kinashuhudia:
-
Utambulisho binafsi wa Baba wa Mbinguni na Mwanawe Mpendwa, Yesu Kristo.
-
Umuhimu wa kuanguka kwa Adamu na hekima ya hawa, kwamba watu wanaweza kuwa na furaha.
Kitabu cha Mormoni kinakanusha dhana kwamba:
-
Ufunuo uliisha na Biblia.
-
Watoto wachanga wanahitaji kubatizwa.
-
Furaha inaweza kupatikana katika uovu.
-
Uzuri wa mtu binafsi unatosha kwa ajili ya kutukuka (ibada na maagano yanahitajika).
-
Kuanguka kwa Adamu kuliwatia watu dosari kwa “dhambi ya asili.”
Kitabu cha Mormoni kinatimiza unabii wa biblia kwamba:
-
“Kondoo wengine” wataisikia sauti Yake.
-
Mungu atatenda“kazi kuu na maajabu,”akiongea “nje mavumbini.”
-
“Kijiti cha Yuda” na “kijiti cha Yusufu” kitakuwa kimoja.
-
Israeli iliotawanyika itakusanyika “katika siku za mwisho” na jinsi hayo yatafanyika.
-
Nchi ya urithi kwa ajili ya ukoo wa Joseph ni Nusu Tufe ya Magharibi.
Kitabu cha Mormoni kinafafanua kuelewa kuhusu:
-
Maisha yetu kabla ya kuzaliwa.
-
Kifo. Ni sehemu muhimu ya mpango mkuu wa furaha wa Mungu.
-
Maisha baada ya kifo yanaanzia katika paradiso.
-
Jinsi kufufuka kwa mwili, kuunganika tena na roho, inakuwa nafsi isiyokufa.
-
Jinsi hukumu yetu ya Bwana itakuwa dhidi ya matendo yetu na matamanio ya moyo wetu.
-
Jinsi ibada ufanyika kiusahihi: kwa mfano, ubatizo, sakramenti, kutawaza kwa Roho Mtakatifu.
-
Upatanisho wa Yesu Kristo.
-
Ufufuko.
-
Jukumu kubwa la malaika.
-
Asili ya milele ya ukuhani.
-
Jinsi tabia ya mwanadamu inavyoshawishika na uwezo wa neno kuliko upanga.
Kitabu cha Mormoni kinafafanua taarifa ambazo kale hazikujulikana:
-
Ubatizo ulifanyika kabla Yesu Kristo hajazaliwa.
-
Mahekalu yalijengwa na kutumika na watu katika Amerika ya kale.
-
Joseph, mwana wa 11 wa Israeli, aliona kazi ya unabii ya Joseph Smith.
-
Nefi (600–592 K.K.) aliona uvumbuzi na kuanzishwa koloni Amerika.
-
Sehemu halisi na za thamani za Biblia zilikuwa zimepotea.
-
Nuru ya Kristo hutolewa kwa kila mtu.
-
Umuhimu wa uhuru binafsi na haja ya upinzani katika vitu vyote.
-
Tahadhari kuhusu “makundi ya dini.”