Makala
Nimekuwa Nikikitarajia Kitabu Hiki Kitukufu
Watakatifu wa Siku za Mwisho kutoka Marekani walifanya mikutano midogo midogo katika nyumba zao huko Kameruni mapema mnamo 1974; hata hivyo, hakuna Mkameruni aliyehudhuria mikutano hiyo. Katika muda huo huo, Wakameruni walianza kujifunza kuhusu Kanisa na kuandika barua kwa Misheni ya Kimataifa ya Kanisa. Mwishoni mwa 1979, Agbortabot Ako Moses wa Mamfe alitambulishwa kwa mara ya kwanza Kanisani na rafiki. Akivutiwa na alichokisikia, Ako aliandika kwa Misheni ya Kimataifa kuomba maelezo zaidi na kuomba kuanzishwa kwa Kanisa nchini Kameruni.
“Barua ilipokelewa,” Ako baadaye aliandika, “na jibu la kufaa lilitumwa kwangu.” Vilivyojumuishwa kwenye barua ilikuwa ni pamoja na anwani za marais wa misheni wa huko Ghana na Nigeria na ahadi kwamba punde angepokea nakala ya Kitabu cha Mormoni. Kitabu hakikuja, hivyo Ako aliandika tenda, akiomba nakala nyingine itumwe. “Nadhani kilipotea wakati wa usafirishaji,” Ako aliandika. “Nimekuwa nikikitarajia kitabu hiki kitukufu kwa shauku kubwa.” Muda mfupi baadaye, kitabu kiliwasili. “Ninakisoma kwa umakini na kwa maombi,” aliandika. “Ninapenda sana kusoma.”
Kwa miaka 12 iliyofuatia, Ako aliandika barua mara kwa mara kwa idadi kubwa ya mawasiliano ya Kanisa iliyokuwa ikiongezeka nje ya Kameruni. Mara chache, alifanya safari ndefu kukutana na viongozi wa Kanisa mpakani mwa Nigeria na Kameruni.
Wakati huo huo, Wakameruni wengi waishio nje ya nchi walikuwa wakitambulishwa kwenye injili na kukubali ubatizo. Mara chache, waongofu hawa waliobatizwa walirejea Kameruni, ambako waliendelea na imani yao mpya majumbani mwao kwa msaada wa waumini wa nje ya nchi. Mnamo 1984, kikundi kilianzishwa huko Yaoundé, na watakatifu wa huko wakaanza kufanya mikutano ya mara kwa mara.
Hatimaye, mnamo Septemba 1991, Paul D. na Arlene Payne, wamisionari wazee wa Misheni ya Nigeria Lagos, waliwasili Yaoundé. Mnamo Septemba 28, Ako alipokea simu kutoka kwa akina Paynes akialikwa kuhudhuria mkutano, karibu kilometa 800 (maili 500) kutoka alipokuwa. “Hapo, tulikuwa na ibada ya kwanza na tulipangiwa majukumu ndani ya Kanisa,” anakumbuka. Ingawa alikuwa hajabatizwa bado, Ako kwa furaha alikubali jukumu na, ili kuwasaidia wamisionari kujijenga wenyewe ndani ya kameruni, mara kwa mara alisafiri safari ya takribani masaa 12 kati ya Mamfe na Yaoundé, akibadilisha magari mara 16 kwenda tu na vivyo hivyo kurejea. Mnamo Mei 8, 1992, Ako alikuwa miongoni mwa waongofu wa kwanza waliobatizwa wa Kameruni.
Mnamo Januari 1993, tawi lilianzishwa huko Yaoundé. Hata hivyo, mwaka uliofuatia, wamisionari walilazimika kuondoka kutokana na kukosa viza. Miaka kadhaa iliyofuatia, waumini waliendelea kushiriki injili na jirani zao, licha ya changamoto kubwa walizozipitia. Mnamo 2004, tawi la pili lilianzishwa huko Douala. Misheni iliundwa huko Yaoundé mnamo 2020. Leo kuna waumini 2,845 katika matawi 15 na Wilaya 2.