Miito ya Misheni
Sura ya 3: Somo la 4— Kuwa Wafuasi wa Yesu Kristo kwa Maisha Yote


“Sura ya 3: Somo la 4— Kuwa Wafuasi wa Yesu Kristo kwa Maisha Yote,” Hubiri Injili Yangu: Mwongozo wa Kushiriki Injili ya Yesu Kristo (2023)

“Sura ya 3: Somo la 4,” Hubiri Injili Yangu

Sura ya 3: Somo la 4

Kuwa Wafuasi wa Yesu Kristo kwa Maisha Yote

Picha
Mwanakondoo Aliyepotea, na Del Parson.

Kufundisha Somo Hili

Ubatizo ni ibada yenye shangwe ya matumaini. Wakati tunapobatizwa, tulionesha hamu yetu ya kumfuata Mungu na kuingia katika njia inayoongoza kwenye uzima wa milele. Pia tunaonesha ahadi yetu ya kuwa wafuasi wa Yesu Kristo kwa maisha yote.

Somo hili limepangwa kulingana na maagano tunayofanya katika ubatizo. Linajumuisha sehemu muhimu zifuatazo, kila moja ina vifungu vidogo:

Wasaidie watu waelewe kwamba kanuni na amri unazowafundisha ni sehemu ya agano watakalofanya kwenye ubatizo. Waoneshe ni jinsi gani kila sehemu ya somo hili itawasaida wao “waje kwa Kristo … na wapokee wokovu wake” (Omni 1:26; ona pia 1 Nefi 15:14)

Utataka kufundisha somo hili katika matembezi kadhaa. Mara chache matembezi yanapaswa kuwa zaidi ya dakika 30. Kwa kawaida ni vyema kuwa na matembezi ya muda mfupi, ya kila mara ambayo yanafundisha sehemu ndogo ya nyenzo.

Panga kile utakachofundisha, wakati utakapokifundisha, na ni muda gani utatumia. Fikiria mahitaji ya watu unaowafundisha, na utafute mwongozo wa Roho Mtakatifu. Una uhuru wa kuchagua kufundisha kulingana na kile ambacho kitawasaidia vyema watu wajiandae kwa ajili ya ubatizo na uthibitisho wao.

Baadhi ya sehemu katika somo hili zinajumuisha mialiko mahususi. Tafuta mwongozo katika kuamua jinsi gani na wakati gani utatoa mialiko. Kuwa makini juu ya kiwango cha kila mtu cha uelewa. Msaidie aishi injili hatua moja kwa wakati.

Picha
mwanamke akipokea sakramenti

Agano Letu la Kuwa Radhi Kujichukulia juu Yetu Jina la Yesu Kristo

Tunapobatizwa, tunafanya agano la kumfuata Yesu Kristo “kwa kusudi kamili la moyo.” Pia tunashuhudia kwamba “tuko radhi kujichukulia juu [yetu] jina la Kristo” (2 Nefi 31:13; ona pia Mafundisho na Maagano 20:37).

Kujichukulia juu yetu jina la Yesu Kristo humaanisha kwamba tutamkumbuka Yeye, na kujitahidi kuishi kama wafuasi Wake maisha yetu yote. Tunaruhusu nuru Yake ing’are kupitia kwetu hadi kwa wengine. Tunajiona wenyewe kama watu Wake na kumweka Yeye kwanza katika maisha yetu.

Sehemu zifuatazo zinaelezea njia mbili ambazo kupitia hizo tunamkumbuka na kumfuata Yesu Kristo.

Sali Kila Mara

Sala inaweza kuwa mazungumzo mepesi na Baba wa Mbinguni ambayo hutoka moyoni. Katika sala, tunaweza kuzungumza na Yeye kwa uwazi na kwa uaminifu. Tunaelezea upendo wetu Kwake na shukrani kwa ajili ya baraka zetu. Pia tunaomba msaada, ulinzi, na maelekezo. Tunapofunga sala zetu, tunapaswa kuchukua muda wa kutulia na kusikiliza.

Yesu alifundisha, “Lazima msali siku zote kwa Baba katika jina langu” (3 Nefi 18:19, msisitizo umeongezwa; ona pia Musa 5:8). Tunaposali katika jina la Yesu Kristo, tunakumbuka wote Yeye na Baba wa Mbinguni.

Yesu aliweka mfano kwa ajili yetu kufuata wakati tunaposali. Tunaweza kujifunza mengi kuhusu sala kwa kujifunza sala za Mwokozi katika maandiko (ona Mathayo 6:9–13; Yohana 17).

Sala zetu zinaweza kujumuisha vipengele vifuatavyo:

  • Anza kwa kumwita Baba wa Mbinguni.

  • Kuonesha hisia za moyo wetu, kama vile shukrani kwa ajili ya baraka tulizopokea.

  • Kuuliza maswali, kutafuta mwongozo, na kuomba baraka.

  • Kumalizia kwa kusema, “Katika jina la Yesu Kristo, amina.”

Maandiko yanatuasa tusali asubuhi na jioni. Hata hivyo, tunaweza kusali wakati wowote na katika mazingira yoyote. Kwa ajili ya sala zetu binafsi na za familia, inaweza kuwa na maana zaidi kupiga magoti wakati tunaposali. Tunapaswa daima kuwa na sala katika mioyo yetu. (Ona Alma 34:27; 37:36–37; 3 Nefi 17:13; 19:16.)

Sala zetu zinapaswa kuwa zenye kuonesha kujali na za kutoka moyoni. Tunaposali, tunapaswa kuepuka kusema mambo yale yale katika njia ile ile.

Tunasali kwa imani, uaminifu, na nia halisi ili kutenda juu ya majibu tunayopokea. Tunapofanya hivyo, Mungu atatuongoza na kutusaidia tufanye maamuzi mazuri. Tutahisi kuwa karibu na Yeye. Yeye atatupatia uelewa na ukweli. Yeye atatubariki kwa faraja, amani na nguvu.

Kujifunza Maandiko

Jifunze Zaidi kuhusu Kanuni Hii

  • Mwongozo wa Maandiko: “Sala

  • Kamusi ya Biblia: “Sala

  • Mada za Injili: “Sala

Kujifunza Maandiko

Nefi alifundisha, “Sherehekea maneno ya Kristo; [kwani] yatawaelezea vitu vyote mnavyostahili kutenda” (2 Nefi 32:3; ona pia 31:20).

Kujifunza maandiko ni njia muhimu ya kumkumbuka na kumfuata Yesu Kristo. Katika maandiko tunajifunza juu ya maisha Yake, huduma, na mafundisho. Pia tunajifunza juu ya ahadi Zake. Tunaposoma maandiko, tutapata uzoefu wa upendo Wake. Nafsi zetu zinakua, imani yetu katika Yeye inaongezeka, na akili zetu zinaaangazwa. Shuhuda zetu juu ya misheni Yake ya kiungu zinakuwa imara.

Tunamkumbuka na kumfuata Yesu kadiri tunavyotumia maneno Yake katika maisha yetu. Tunapaswa kujifunza maandiko kila siku, hasa Kitabu cha Mormoni.

Maandiko ya Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa siku za Mwisho, ni Biblia Takatifu, Kitabu cha Mormoni, Mafundisho na Maagano, na Lulu ya Thamani Kuu. Hivi pia vinaitwa “vitabu nguzo.”

Kujifunza Maandiko

Jifunze Zaidi kuhusu Kanuni Hii

  • Mwongozo wa Maandiko: “Maandiko

  • Mada za Injili: “Maandiko

Picha
Yesu Kristo akifundisha umati wa watu

Agano Letu la Kushika Amri za Mungu

Tazama: Kuna njia nyingi za kufundisha amri zilizo katika sehemu hii. Kwa mfano, ungeweza kuzifundisha katika matembezi machache. Au ungeweza kufundisha baadhi yake kama sehemu ya masomo matatu ya kwanza. Wakati unapofundisha amri, hakikisha unaziunganisha na agano la ubatizo na mpango wa wokovu.

Tunapobatizwa, tunaagana na Mungu kwamba tutashika amri Zake (Mosia 18:10; Alma 7:15).

Mungu ametupa amri kwa sababu Yeye anatupenda. Yeye anataka yaliyo mema zaidi kwa ajili yetu, sasa na milele yote. Kama Baba yetu wa Mbinguni, Yeye anajua kile tunachohitaji kwa ajili ya ustawi wetu wa kiroho na kimwili. Yeye pia anajua kile kitakachotuletea sisi furaha tele. Kila amri ni kipawa cha kiungu, kilichotolewa ili kuongoza maamuzi yetu, kutulinda sisi, na kutusaidia tukue.

Sababu mojawapo ya sisi kuja duniani ni kujifunza na kukua kupitia kutumia haki yetu ya kujiamulia kwa busara (ona Ibrahimu 3:25). Kuchagua kutii amri za Mungu—na kutubu wakati tunapoanguka—hutusaidia tutembee safari hii ya duniani yenye changamoto.

Amri za Mungu ni chanzo cha nguvu na baraka (ona Mafundisho na Maagano 82:8–9). Kwa kushika amri, tunajifunza kwamba amri si sheria za usumbufu ambazo zinazuia uhuru wetu. Uhuru wa kweli huja kutokana na kutii amri. Utiifu ni chanzo cha nguvu ambazo huleta nuru na maarifa kupitia Roho Mtakatifu. Unatuletea furaha kuu na hutusaidia tufikie uwezekano wetu wa kiungu kama watoto wa Mungu.

Mungu anaahidi kutubariki tunaposhika amri Zake. Baadhi ya baraka ni mahususi kwa amri fulani. Baraka Zake za juu zaidi ni amani katika maisha haya na uzima wa milele katika ulimwengu ujao. (Ona Mosia 2:41; Alma 7:16; Mafundisho na Maagano 14:7; 59:23; 93:28; 130:20–21.)

Baraka za Mungu ni za kiroho na kimwili. Nyakati zingine, tunahitaji kuwa na uvumilivu katika kuzisubiria, tukitumainia kwamba zitakuja kulingana na mapenzi Yake na wakati Wake (ona Mosia 7:33; Mafundisho na Maagano 88:68). Ili kutambua baadhi ya baraka hizi, tunahitaji kuwa wasikivu na wepesi kutambua. Hii ni kweli hasa juu ya baraka ambazo huja katika njia rahisi na zinazoonekana za kawaida.

Baadhi ya baraka zinaweza kuwa wazi tu katika utambuzi. Zingine inawezekana zisije hadi mpaka baada ya maisha haya. Bila kujali wakati na asili ya baraka za Mungu, tunaweza kuhakikishiwa kwamba zitakuja alimradi tunajitahidi kuishi injili ya Yesu Kristo (ona Mafundisho na Maagano 82:10).

Mungu anawapenda watoto Wake wote kikamilifu. Yeye ni mvumilivu kwa udhaifu wetu, na Yeye anatusamehe tunapotubu.

Amri Kuu Mbili

Wakati Yesu alipoulizwa, “Ni amri gani iliyo kuu?” Yeye alijibu, “Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili zako zote.”

Yesu kisha alisema amri kuu ya pili yafanana na ya kwanza: “Mpende jirani yako kama nafsi yako” (Mathayo 22:36–39). “Hakuna amri nyingine iliyo kuu kuliko hizi” (Marko 12:31).

Kama watoto wa Mungu wa kiroho, tunao uwezo mkubwa wa upendo. Ni sehemu ya urithi wetu wa kiroho. Kuishi amri kuu mbili—kumpenda Mungu kwanza na kumpenda jirani—ni sifa fafanuzi ya wafuasi wa Yesu Kristo.

Upendo wa Mungu

Kuna njia nyingi tunazoweza kuonesha upendo wetu kwa Mungu. Tunaweza kushika amri Zake (ona Yohana 14:15, 21). Tunaweza kumweka Yeye kwanza katika maisha yetu, kuyaweka mapenzi yetu chini ya yale ya Kwake. Tunaweza kukita matamanio yetu, fikra, na mioyo yetu Kwake (ona Alma 37:36). Tunaweza kuishi kwa shukrani kwa ajili ya baraka ambazo Yeye ametupatia—na kuwa wakarimu katika kushiriki baraka hizo (ona Mosia 2:21–24: 4:16–21). Kupitia sala na huduma kwa wengine, tunaweza kuonesha na kuzidisha upendo wetu Kwake.

Kama vile amri zingine, amri ya kumpenda Mungu ni kwa ajili ya manufaa yetu. Kile tunachokipenda huamua kile tunachokitafuta. Kile tunachokitafuta huamua kile tunachokifikiria na kukifanya. Na kile tunachokifikiria na kukifanya huamua sisi ni akina nani—na sisi tutakuwa akina nani.

Upendo kwa Wengine

Kuwapenda wengine ni mwendelezo wa upendo wetu kwa Mungu. Mwokozi alitufundisha njia nyingi za kuwapenda wengine (ona, kwa mfano, Luka 10:25–37 na Yohana 25:31–46). Tunawafikia na kuwakaribisha ndani ya mioyo yetu na maishani mwetu. Tunapenda kwa kuhudumia—kwa kujitolea wenyewe hata katika njia ndogo ndogo. Tunawapenda wengine kwa kutumia vipaji ambavyo Mungu ametupatia sisi ili kuwabariki.

Kuwapenda wengine hujumuisha kuwa na subira, kuwa wakarimu, na kuwa waaminifu. Hujumuisha kusamehe bila kinyongo. Humaanisha kuwatendea watu wote kwa heshima.

Tunapompenda mtu fulani, sisi na mtu huyo sote tunabarikiwa. Mioyo yetu inakua, maisha yetu yanakuwa na maana zaidi, na shangwe yetu huongezeka.

Baraka

Amri kuu mbili—kumpenda Mungu na kumpenda jirani yetu—ni msingi wa amri zote za Mungu (ona Mathayo 22:40). Tunapompenda Mungu kwanza, na pia kuwapenda wengine, kila kitu katika maisha yetu kitasogea katika sehemu yake sahihi. Upendo huu utaathiri mtazamo wetu, matumizi ya muda wetu, maslahi tunayoyatafuta, na mpangilio wa vipaumbele vyetu.

Kujifunza Maandiko

Jifunze Zaidi kuhusu Kanuni Hii

  • Mwongozo wa Maandiko: “Hisani,” “Upendo

  • Mada za Injili: “Hisani,” “Upendo

Mfuate Nabii

Mungu huwaita manabii kuwa wawakilishi Wake duniani. Kupitia manabii Wake, Yeye hufunua ukweli na hutoa mwongozo na maonyo.

Mungu alimwita Joseph Smith kuwa nabii wa kwanza wa siku za mwisho (ona somo la 1). Warithi wa Joseph Smith vile vile waliitwa na Mungu ili kuliongoza Kanisa Lake, ikijumuisha nabii ambaye analiongoza leo. Tunapaswa kupata sadikisho la wito wa kiungu wa nabii aliye hai na kufuata mafundisho yake.

Mafundisho ya manabii na mitume walio hai yanatoa nanga ya ukweli wa milele katika ulimwengu wenye viwango vinavyobadilika. Tunapowafuata manabii wa Mungu, mkanganyiko na ugomvi wa ulimwengu hautatushinda. Tutapata furaha kuu katika maisha haya na kupokea mwongozo kwa ajili ya sehemu hii ya safari yetu ya milele.

Kujifunza Maandiko

Jifunze Zaidi kuhusu Kanuni Hii

Shika Amri Kumi

Mungu alifunua Amri Kumi kwa nabii wa kale aliyeitwa Musa ili kuwaongoza watu wake. Amri hizi zinatumika vivyo hivyo katika siku yetu. Zinatufundisha sisi kumwabudu na kuonesha staha kwa Mungu. Pia zinatufundisha jinsi ya kutendeana.

Kujifunza Maandiko

Jifunze Zaidi kuhusu Kanuni Hii

  • Mwongozo wa Maandiko: “Amri, Kumi

  • Mada za Injili: “Amri Kumi

Picha
mwanamume akimbeba mwanamke

Ishi Sheria ya Usafi wa Kimwili

Sheria ya usafi wa kimwili ni sehemu muhimu ya mpango wa Mungu kwa ajili ya wokovu na kuinuliwa kwetu. Kujamiiana kati ya mume na mke kumetawazwa na Mungu kwa ajili ya uumbaji wa watoto na kwa ajili ya dhihirisho la upendo ndani ya ndoa. Vitendo vya kujamiiana na nguvu ya kuumba uhai wa binadamu vinakusudiwa kuwa vizuri na vitakatifu.

Sheria ya usafi wa kimwili ni kujizuia uhusiano wowote wa kimapenzi nje ya ndoa halali kati ya mwanamume mmoja na mwanamke mmoja. Sheria hii pia humaanisha uaminifu kamili na uaminifu kwa mwenzi wa mtu baada ya ndoa.

Ili kutusaidia tutii sheria ya usafi wa kimwili, manabii wametuasa kuwa wasafi katika fikra zetu na maneno. Tunapaswa kuepuka ponografia ya aina yoyote. Katika kushika sheria ya usafi wa kimwili, tunapaswa kuwa na maadili katika tabia zetu na mwonekano wetu.

Wanaotarajia kubatizwa wanapaswa kuishi sheria ya usafi wa kimwili.

Toba na Msamaha

Mbele za Mungu, kuvunja sheria ya usafi wa kimwili ni dhambi kubwa (ona Kutoka 20:14; Waefeso 5:3). Ni kutumia vibaya nguvu takatifu ambazo Yeye amezitoa za kuumba uhai. Lakini Yeye huendelea kutupenda hata kama tumevunja sheria hii. Yeye anatualika tutubu na kuwa wasafi kupitia dhabihu ya Yesu Kristo ya kulipia dhambi. Kukata tamaa kwa sababu ya dhambi kunaweza kubadilishwa kwa amani ya kupendeza ya msamaha wa Mungu (ona Mafundisho na Maagano 58:42–43).

Baraka

Mungu ametoa sheria ya usafi wa kimwili ili kutubariki sisi na watoto wa kiroho Yeye anaowatuma duniani. Kutii sheria hii ni muhimu kwa amani binafsi na kuwa na upendo, tumaini, na umoja katika uhusiano wetu wa kifamilia.

Tunapoishi sheria ya usafi wa kimwili, tutalindwa dhidi ya madhara ya kiroho ambayo huja kutokana na kujamiiana nje ya ndoa. Sisi pia tutaepukana na shida za kihisia na kimwili ambazo huambatana na uhusiano kama huo. Tutakua katika kujiamini kwetu mbele ya Mungu (ona Mafundisho na Maagano 121:45). Tutakuwa wawazi zaidi kwa ushawishi wa Roho Mtakatifu. Tutakuwa tumejiandaa vyema kufanya maagano matakatifu hekaluni ambayo huziunganisha familia zetu milele.

Kujifunza Maandiko

Jifunze Zaidi kuhusu Kanuni Hii

  • Mwongozo wa Maandiko, “Usafi wa kimwili.”

  • Mada za Injili: “Usafi wa kimwili

Kushika Sheria ya Kulipa Zaka

Heshima kubwa ya uumini katika Kanisa ni fursa ya kulipa zaka. Tunapolipa zaka, tunasaidia kuendeleza kazi ya Mungu na kuwabariki watoto Wake.

Sheria ya Zaka ina chanzo chake katika nyakati za Agano la Kale. Kwa mfano, nabii Ibrahimu alilipa zaka ya vyote alivyovimiliki (ona Alma 13:15; Mwanzo 14:18–20).

Neno zaka kiuhalisia humaanisha sehemu moja ya kumi. Tunapolipa zaka, tunachangia sehemu moja ya kumi ya mapato yetu kwa Kanisa (ona Mafundisho na Maagano 119:3–4; faida hueleweka kumaanisha mapato). Yote tuliyonayo ni zawadi kutoka kwa Mungu. Tunapolipa zaka, tunaonesha shukrani Kwake kwa kurudisha sehemu ya kile ambacho Yeye ametupatia.

Kulipa zaka ni onyesho la imani yetu. Pia ni njia ya kumheshimu Mungu. Yesu alifundisha kwamba “utafuteni … kwanza ufalme wa Mungu” (Mathayo 6:33), na kulipa zaka ni njia ya kufanya hivyo.

Picha
Senti ya Mjane, na Sandra Rast

Matumizi ya Fedha za Zaka

Fedha za zaka ni takatifu. Tunatoa zaka yetu kwa mshiriki wa uaskofu, au katika maeneo mengine tunaweza kulipa mtandaoni. Uaskofu unapopokea zaka, wanaipeleka makao makuu ya Kanisa.

Baraza linalojumuisha Urais wa Kwanza, Akidi ya Mitume Kumi na Wawili, na Uaskofu Kiongozi huamua jinsi ya kutumia fedha za zaka katika kazi ya Mungu (ona Mafundisho na Maagano 120:1). Hii inajumuisha:

  • Kujenga na kutunza mahekalu na majumba ya mikutano.

  • Kutafsiri na kuchapisha maandiko.

  • Kusaidia shughuli na uendeshaji wa mikusanyiko ya Kanisa.

  • Kusaidia kazi ya umisionari kote duniani.

  • Kusaidia kazi ya historia ya familia.

  • Kufadhili shule na elimu.

Zaka haitumiki kuwalipa viongozi wa Kanisa. Wao wanatumikia kwa kujitolea bila malipo.

Baraka

Tunapolipa zaka, Mungu anaahidi baraka ambazo ni kuu zaidi kuliko chochote tunachotoa. Yeye “atafungua … madirisha ya mbinguni, na kuwamwagieni … baraka, hata isiwepo nafasi ya kutosha kuhifadhi” (Malaki 3:10; ona mstari wa 7–12). Baraka hizi zinaweza kuwa za kiroho na za kimwili.

Kujifunza Maandiko

Jifunze Zaidi kuhusu Kanuni Hii

Tii Neno la Hekima

Sheria ya Bwana ya Afya

Miili yetu ni zawadi takatifu kutoka kwa Mungu. Kila mmoja wetu anahitaji mwili ili kuwa zaidi kama Yeye. Miili yetu ni muhimu sana kiasi kwamba maandiko yanaifananisha na mahekalu (ona 1 Wakorintho 6:19–20).

Bwana anatutaka tuitendee miili yetu kwa heshima. Ili kutusaidia kufanya hivyo, Yeye alifunua sheria ya afya inayoitwa Neno la Hekima. Ufunuo huu unatufundisha kuhusu kula vyakula vyenye kuleta afya na kutotumia vitu ambavyo vinadhuru miili yetu—hasa pombe, tumbaku, na vinywaji vya moto (kumaanisha chai na kahawa).

Katika roho ya Neno la Hekima, manabii wa sasa wametuonya dhidi ya kutumia vitu ambavyo vina madhara, ni haramu, au ni vya kuleta uraibu. Manabii pia wameonya dhidi ya kutumia vibaya dawa zinazoshauriwa na daktari. (Rais wako wa misheni atajibu maswali kuhusu ikiwa vitu vingine katika eneo lako havifai kutumiwa.)

Baraka

Bwana alitoa Neno la Hekima kwa ajili ya ustawi wetu wa kimwili na kiroho. Yeye anaahidi baraka kuu wakati tunaposhika amri hii. Baraka hizi zinajumuisha afya, hekima, hazina ya maarifa, na ulinzi (ona Mafundisho na Maagano 89:18– 21).

Kutii Neno la Hekima kutatusaidia tuwe wapokeaji wazuri wa ushawishi wa Roho Mtakatifu. Ingawa sote tunapatwa na changamoto za kiafya, kutii sheria kutatusaidia tuwe na afya zaidi katika mwili, akili, na roho.

Wanaojiandaa kwa ajili ya ubatizo wanapaswa kutii Neno la Hekima.

Kwa ajili ya miongozo kuhusu kuwasaidia watu ambao wanahangaika na uraibu, ona sura ya 10.

Kujifunza Maandiko

Jifunze Zaidi kuhusu Kanuni Hii

  • Mwongozo wa Maandiko: “Neno la Hekima

  • Mada za Injili: “Afya,” “Neno la Hekima

  • Msaada wa Maisha: “Uraibu

Itakase Siku ya Sabato

Siku ya Mapumziko na Kuabudu

Sabato ni siku takatifu ambayo Mungu ameitenga kwa ajili yetu kila wiki kupumzika kutokana na kazi zetu za kila siku na kumwabudu Yeye. Mojawapo ya Amri Kumi alizopewa Musa ni “ikumbuke siku ya sabato uitakase” (Kutoka 20:8); ona pia mstari wa 9–11).

Katika ufunuo wa siku za leo, Bwana alithibitisha kwamba Sabato, “ni siku iliyoteuliwa kwako kupumzika kutokana na kazi zako, na utoe dhabihu zako za shukrani kwa Aliye Juu sana” (Mafundisho na Maagano 59:10). Yeye pia alisema Sabato inatakiwa kuwa siku ya kufurahia, ya maombi, na kutoa shukrani (ona mstari wa 14–15).

Kama sehemu ya kuabudu kwetu siku ya Sabato, tunahudhuria mkutano wa sakramenti kila wiki. Katika mkutano huu, tunamwabudu Mungu na kushiriki sakramenti ili kumkumbuka Yesu Kristo na Upatanisho Wake. Tunaposhiriki sakramenti, tunafanya upya maagano na Mungu na kuonesha kwamba tuko tayari kutubu dhambi zetu. Ibada ya sakramenti ni kiini cha kuitakasa kwetu siku ya Sabato.

Kanisani pia tunashiriki katika madarasa ambapo tunajifunza zaidi kuhusu injili ya Yesu Kristo. Imani yetu hukua pale tunapojifunza maandiko pamoja. Upendo wetu hukua tunapohudumiana na kuimarishana.

Kwa nyongeza kwenye kupumzika kutokana na kazi zetu siku ya Sabato, tunapaswa kujizuia kufanya manunuzi na shughuli zingine ambazo zitafanya ionekane kama ni siku ya kawaida. Tunaziweka kando shuguli za ulimwengu na kufokasi fikra na matendo yetu kwenye mambo ya kiroho.

Siku ya Kutenda Mema

Kutenda mema siku ya Sabato ni muhimu sawa na kile tunachojizuia kutokukifanya ili kuitakasa siku hiyo. Tunajifunza injili, kuimarisha imani, kujenga uhusiano, kutoa huduma, na kushiriki katika shughuli za kuinua pamoja na wanafamilia na marafiki.

Picha
wanandoa wakisoma maandiko

Baraka

Kuitakasa siku ya Sabato kunaonesha utii wetu kwa Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo. Tunapofanya shughuli zetu za Sabato ziwiane na nia ya Mungu kwa ajili ya siku hiyo, tutahisi shangwe na amani. Tutalishwa kiroho na kufanywa upya kimwili. Pia tutahisi kuwa karibu na Mungu na kuzidisha uhusiano wetu na Mwokozi wetu. Tutaweza kujilinda na “duniani pasipo mawaa” (Mafundisho na Maagano 59:9). Sabato itakuwa “ya furaha” (Mafundisho na Maagano 58:13; ona pia mstari wa 14).

Kujifunza Maandiko

Jifunze Zaidi kuhusu Kanuni Hii

  • Mada za Injili: “Siku ya Sabato

  • Mwongozo wa Maandiko: “Siku ya Sabato

Tii na Heshimu Sheria

Watakatifu wa Siku za Mwisho wanaamini katika kutii sheria na kuwa raia wema (ona Mafundisho na Maagano 134; Makala ya Imani 1:12). Waumini wa Kanisa wanahimizwa kutoa huduma ili kuboresha jamii na mataifa yao. Pia wanahimizwa kuwa ushawishi muhimu kwa kuwa na maadili bora katika jamii na serikali.

Waumini wa Kanisa wanaalikwa kushiriki katika serikali na shughuli za kisiasa kulingana na sheria. Waumini ambao wanashikilia wadhifa serikalini wanatenda katika nafasi kama hizo kama raia wa kawaida wenye kuwajibika, siyo kama wawakilishi wa Kanisa.

Kujifunza Maandiko

Jifunze Zaidi kuhusu Kanuni Hii

Picha
Mkuu katika Ufalme, na J. Kirk Richards

Agano Letu la Kumtumikia Mungu na watu Wengine

Huduma

Tunapobatizwa, tunafanya agano la kumtumikia Mungu na kuwatumikia wengine. Kuwatumikia wengine ni mojawapo ya njia za msingi za kumtumikia Mungu (ona Mosia 2:17). Nabii Alma aliwafundisha wale ambao walitamani kubatizwa kwamba walipaswa kuwa “radhi kubebeana mizigo, ili iwe miepesi” na “kuomboleza na wale wanaoomboleza … na kuwafariji wale wanaohitaji kufarijiwa” (Mosia 18:8–9).

Punde baada ya ubatizo, waumini wapya kwa kawaida wanapokea wito wa kutumikia katika Kanisa. Miito hii ni ya kujitolea na haina malipo. Tunapoikubali na kutumikia kwa bidii, tunakua katika imani, kukuza vipaji, na kuwabariki wengine.

Sehemu nyingine ya huduma yetu katika Kanisa ni kuwa “kaka mhudumu” au “dada mhudumu.” Katika jukumu hili, tunawahudumia watu na familia tulizopangiwa.

Kama wafuasi wa Yesu Kristo, tunatafuta fursa za kuhudumu kila siku. Kama Yeye, “tunazunguka huko na huko, tukitenda kazi njema” (Matendo ya Mitume 10:38). Tunawasaidia majirani zetu na wengine katika jumuia yetu. Tunaweza kushiriki katika fursa za kuhudumu kupitia JustServe pale inapopatikana. Tunaweza kusaidia juhudi za kibinadamu za Kanisa na kushiriki katika kutatua majanga.

Kujifunza Maandiko

Jifunze Zaidi kuhusu Kanuni Hii

  • Mwongozo wa Maandiko: “Huduma

  • Mada za Injili: “Huduma

Picha
watu wakizungumza

Kushiriki Injili

Kama sehemu ya agano letu la ubatizo, tunaahidi “kusimama kama mashahidi wa Mungu” (Mosia 18:9). Njia moja ya kusimama kama mashahidi ni kwa kushiriki injili ya Yesu Kristo. Kuwasaidia wengine waipokee injili ni mojawapo ya aina ya huduma ya furaha kubwa sana tunayoweza kuitoa (ona Mafundisho 18:15–16). Ni dhihirisho lenye nguvu la upendo wetu.

Tunapopata uzoefu wa baraka za kuishi injili, kwa asili tunataka kushiriki na wengine baraka hizo. Wanafamilia, marafiki, na wale tunaofahamiana nao kila mara wanavutiwa wakati tunapoonesha mfano wa uaminifu na wanaona jinsi injili inavyobariki maisha yetu. Tunaweza kushiriki injili katika njia za kawaida na za asili (ona Kitabu cha Maelezo ya Jumla, sura ya 23).

Waalike wengine washiriki pamoja nasi katika shughuli za huduma, jamii, burudani, na za Kanisa. Tunaweza kuwalika kwenye mkutano wa Kanisa au ibada ya ubatizo. Tunaweza kuwaalika watazame video mtandaoni ambazo zinaelezea injili ya Yesu Kristo, wasome Kitabu cha Mormoni, au wahudhurie ufunguzi wa hekalu. Kuna mamia ya mialiko tunayoweza kuitoa. Kila mara, mwaliko kwa urahisi humaanisha kujumuisha familia zetu, marafiki, na majirani katika kile ambacho tayari tunakifanya.

Kama tukiomba, Mungu atatusaidia tutambue nafasi za kushiriki injili na kuwaambia wengine kuhusu jinsi ambavyo injili huyabariki maisha yetu.

Kwa maelezo zaidi kuhusu kutumia kanuni za kupenda, kushiriki, na kualika, ona “Ungana na Waumini” katika sura ya 9.

Kujifunza Maandiko

Jifunze Zaidi kuhusu Kanuni Hii

Mfungo na Matoleo ya Mfungo

Mungu alianzisha sheria ya mfungo kama njia kwa ajili yetu kukuza nguvu za kiroho na kuwasaidia wale walio katika shida.

Kufunga kunamaanisha kushinda bila chakula na maji kwa muda fulani. Kanisa kwa kawaida linatenga Jumapili ya kwanza ya mwezi kama siku ya kufunga. Siku ya kufunga kwa kawaida humaanisha kushinda bila chakula na maji kwa kipindi cha saa 24 kama tuko vizuri kimwili. Vipengele vingine muhimu vya Jumapili ya mfungo vinajumuisha sala na kutoa ushuhuda. Pia tunahimizwa kufunga wakati mwingine tunapohisi haja ya kufanya hivyo.

Kujenga Nguvu ya Kiroho

Kufunga kunaweza kutusaidia tuwe wanyenyekevu, tusogee karibu na Mungu, na tuhisi kufanywa upya kiroho. Kabla ya kuanza huduma Yake, Yesu Kristo alifunga (ona Mathayo 4:1–2). Maandiko yameandika matukio mengi ya manabii na watu wengine wakifunga ili waweze kuongeza nguvu zao za kiroho na kutafuta baraka maalumu kwa ajili yao wenyewe au kwa ajili ya watu wengine.

Kufunga na sala huenda pamoja. Tunapofunga na kusali kwa imani, tunakuwa wasikivu katika kupokea ufunuo. Tunakuwa wasikivu zaidi katika kutambua ukweli na kuelewa mapenzi ya Mungu.

Kuwasaidia Wale Walio katika shida

Tunapofunga, tunatoa mchango Kanisani ili kusaidia kuwatunza watu walio katika shida. Haya yanaitwa matoleo ya mfungo. Tunaalikwa kutoa matoleo ya mfungo angalau sawa na thamani ya milo ambayo hatukuila. Tunahimizwa kuwa wakarimu na kutoa zaidi ya thamani ya milo miwili kama tunaweza. Kutoa matoleo ya mfungo ni njia mojawapo ambayo kupitia hiyo tunaweza kuwahudumia wengine.

Matoleo ya mfungo yanatumika kutoa chakula na mahitaji mengine kwa watu walio na mahitaji, katika sehemu husika na ulimwenguni kote. Kwa maelezo kuhusu jinsi ya kuchangia matoleo ya mfungo, ona “Kuchangia Zaka na Matoleo Mengine” katika somo hili.

Kujifunza Maandiko

Kufunga

Kuwajali Wale Wenye Mahitaji

Jifunze Zaidi kuhusu Kanuni Hii

  • Mwongozo wa Maandiko: “Mfungo, Kufunga

  • Kitabu cha Maelezo ya Jumla,: 22.2.2

  • Mada za Injili: “Kufunga na Matoleo ya Mfungo

Picha
familia nje ya hekalu

Agano Letu la Kuvumilia hadi Mwisho

Tunapobatizwa, tunafanya agano na Mungu la “kuvumilia hadi mwisho” katika kuishi injili ya Yesu Kristo (2 Nefi 31:20; ona pia Mosia 18:13). Tunajitahidi kuwa wafuasi wa Yesu Kristo kwa maisha yote.

Nabii wa Kitabu cha Mormoni Nefi alielezea ubatizo kama lango ambalo kwalo tunaingia katika njia ya agano (ona 2 Nefi 31:17). Baada ya ubatizo, tunaendelea “kusonga mbele kwa uthabiti katika Kristo” (2 Nefi 31:20).

Kadiri “tunavyosonga mbele” kwenye njia ya ufuasi, tunajiandaa kwenda hekaluni. Kule tunafanya maagano na Mungu wakati tunapopokea ibada za hekaluni. Ndani ya hekalu, tutapokea endaumenti ya nguvu na kuunganishwa kama familia milele. Kushika maagano tunayofanya hekaluni kutafungua mlango kwa kila nafasi ya kiroho na baraka ambazo Mungu anazo kwa ajili yetu.

Tunapoendelea kwa uaminifu kwenye njia ya injili, hatimaye tutapokea kipawa kikuu cha Mungu—kipawa cha uzima wa milele (ona 2 Nefi 31:20; Mafundisho na Maagano 14:7).

Sehemu zifuatazo zinaeleza baadhi ya vipengele vya kile ambacho Mungu amekitoa ili kutusaida tuvumilie hadi mwisho wa safari yetu ya duniani—na tupate shangwe ndani ya safari hiyo.

Ukuhani na Vikundi vya Kanisa

Ukuhani ni mamlaka na nguvu za Mungu. Kupitia ukuhani, Baba wa Mbinguni hutimiza kazi Yake “kuleta kutokufa na uzima wa milele” wa watoto Wake (Musa 1:39). Mungu anatoa mamlaka na nguvu kwa wana na mabinti Zake duniani ili wasaidie kutekeleza kazi hii.

Ukuhani hutubariki sisi sote. Ibada kama vile ubatizo na sakramenti zinapokelewa kupitia wale wanaoshikilia ofisi za ukuhani. Sisi pia tunapokea baraka za uponyaji, faraja na ushauri.

Ukuhani na Uongozi wa Kanisa na Miito

Kanisa linaongozwa na Yesu Kristo kupitia manabii na mitume. Viongozi hawa wanaitwa na Mungu, kutawazwa, na kupewa mamlaka ya ukuhani ili kutenda katika jina la Mwokozi.

Hapo kale, Kristo aliwapa Mitume Wake mamlaka ya ukuhani huu huu, ambao uliwawezesha waliongoze Kanisa Lake baada ya Yeye kupaa kwenda mbinguni. Hatimaye mamlaka hayo yalipotea wakati watu walipoikataa injili na kuwaua Mitume.

Wajumbe wa mbinguni walirejesha ukuhani mnamo mwaka 1829 kupitia Nabii Joseph Smith, na Bwana alianzisha Kanisa Lake pamoja na mitume na manabii. (Ona somo la 1.)

Katika ngazi ya wenyeji, maaskofu na marais wa vigingi wana mamlaka ya ukuhani ili kuongoza mikusanyiko ya Kanisa.

Wakati wanaume na wanawake wanapoitwa na kusimikwa kutumikia katika Kanisa, wanapewa mamlaka kutoka kwa Mungu ili kutenda kazi katika wito huo. Mamlaka haya yanatolewa kwa wamisionari, viongozi, walimu, na wengine hadi pale wanapopumzishwa kutoka katika miito yao. Yananaibishwa chini ya maelekezo ya wale ambao wanashikilia funguo za ukuhani.

Mamlaka ya ukuhani yanaweza kutumika tu kwa haki (ona Mafundisho na Maagano 121:34–46). Mamlaka haya ni uaminifu mtakatifu wa kumwakilisha Mwokozi na kutenda katika jina Lake. Daima inakusudiwa kuwabariki na kuwahudumia wengine.

Picha
wavulana wakiwa katika shule ya Jumapili

Ukuhani wa Haruni na Ukuhani wa Melkizedeki

Katika Kanisa, ukuhani hujumuisha Ukuhani wa Haruni na Ukuhani wa Melkizedeki. Chini ya maelekezo ya wale wanaoshikilia funguo za ukuhani, Ukuhani wa Haruni na Ukuhani wa Melkizedeki hutunukiwa juu ya waumini wanaume wa Kanisa wenye kustahili. Baada ya ukuhani sahihi kuwa umetunukiwa, mtu huyo anatawazwa kwenye ofisi katika ukuhani ule, kama vile shemasi au mzee. Ni lazima atawazwe na mtu ambaye ana mamlaka haya muhimu.

Wakati mwanamume au mvulana anapokea ukuhani, yeye hufanya agano na Mungu la kutimiza wajibu mtakatifu, kuwatumikia wengine, na kusaidia kulijenga Kanisa.

Wavulana wanaweza kupokea Ukuhani wa Haruni na kutawazwa kuwa mashemasi kuanzia Januari ya mwaka wanapofikisha miaka 12. Wanaweza kutawazwa kuwa walimu katika mwaka wanapofikisha miaka 14 na makuhani katika mwaka wanapofikisha miaka 16. Waongofu wanaume wenye umri unaoruhusu wanaweza kupokea Ukuhani wa Haruni punde baada ya ubatizo na uthibitisho. Wenye Ukuhani wa Haruni husimamia ibada kama vile sakramenti na ubatizo.

Baada ya kutumikia kwa muda kama kuhani katika Ukuhani wa Haruni, mwanamume mwenye kustahili ambaye ana angalau miaka 18 anaweza kupokea Ukuhani wa Melkizedeki na kutawazwa kama mzee. Wanaume wanaopokea Ukuhani wa Melkizedeki wanaweza kutekeleza ibada za ukuhani kama vile kutoa baraka za uponyaji na faraja kwa wanafamilia na wengine.

Ona Kitabu cha Maelezo ya Jumla, 38.2.9.1, kwa ajili ya maelezo kuhusu waumini wapya kupokea ukuhani.

Akidi na Vikundi vya Kanisa

Akidi za Ukuhani Akidi ni kundi lililoundwa la wenye ukuhani. Kila kata ina akidi ya wazee kwa ajili ya wanaume watu wazima. Akidi za mashemasi, walimu, na makuhani ni kwa ajili ya wavulana.

Muungano wa Usaidizi Muungano wa Usaidizi hujumuisha wanawake wenye umri wa miaka 18 na zaidi. Washiriki wa Muungano wa Usaidizi huimarisha familia, watu binafsi, na jamii.

Wasichana. Wasichana wanajiunga na kikundi cha Wasichana kuanzia Januari ya mwaka wanapofikisha miaka 12.

Picha
mwanamke akifundisha darasa

Msingi. Watoto wa miaka 3 hadi 11 ni sehemu ya kundi la Msingi.

Shule ya Jumapili. Watu wazima wote na vijana wanahudhuria Shule ya Jumapili, ambapo wanakutana kujifunza maandiko pamoja.

Kwa maelezo zaidi kuhusu ukuhani, ona Kitabu cha Maelezo ya Jumla, sura ya 3.

Kwa maelezo zaidi kuhusu akidi za ukuhani na vikundi vya Kanisa, ona Kitabu cha Maelezo ya Jumla, sura ya 8–13.

Kujifunza Maandiko

Jifunze Zaidi kuhusu Kanuni Hii

  • Kitabu cha Maelezo ya Jumla, sura ya 3: “Kanuni za Ukuhani

  • Mada za Injili: “Ukuhani wa Haruni,” “Ukuhani wa Melkizedeki,” “Ukuhani

Ndoa na Familia

Ndoa

Ndoa kati ya mwanamume na mwanamke imeamriwa na Mungu. Ni kiini cha Mpango wa Mungu kwa ajili ya maendeleo ya watoto Wake.

Muungano wa mume na mke katika ndoa unapaswa kuwa uhusiano wao wenye thamani zaidi duniani. Wana wajibu mtakatifu wa kuwa waaminifu wao kwa wao, na waaminifu kwa agano lao la ndoa.

Mume na mke wako sawa machoni pa Mungu. Mmoja hapaswi kumtawala mwingine. Maamuzi yao yanapaswa kufanywa kwa umoja na upendo, pamoja na ushiriki kamili wa wote.

Mume na mke wanapopendana na kufanya kazi pamoja, ndoa yao inaweza kuwa chanzo cha furaha yao kuu. Wanaweza kusaidiana pamoja na watoto wao kusonga mbele hadi uzima wa milele.

Familia

Kama vile ndoa, familia imeamriwa na Mungu na ni kiini cha mpango Wake kwa ajili ya furaha yetu ya milele. Familia zetu zina uwezekano mkubwa wa kuwa na furaha wakati tunapoishi kwa mafundisho ya Yesu Kristo. Wazazi wanawafundisha watoto wao injili ya Yesu Kristo na kuweka mfano wa kuiishi. Familia hutoa fursa kwa ajili yetu za kupendana na kutumikiana.

Wazazi wanapaswa kuzifanya familia zao kuwa kipaumbele cha juu. Ni fursa na ni wajibu mtakatifu kwa wazazi kuwatunza watoto wanaoweza kuwazaa au kuwaasili.

Familia zote huwa na changamoto. Na tunapotafuta msaada wa Mungu na kushika amri Zake, changamoto za familia zinaweza kukusaidia ujifunze na ukue. Wakati mwingine changamoto hizi hutusaidia tujifunze kutubu na kusamehe.

Picha
baba akiifundisha familia

Viongozi wa Kanisa wamewahimiza waumini kuwa na jioni ya nyumbani kila wiki. Wazazi wanatumia muda huu kuwafundisha watoto wao injili, na kuimarisha uhusiano wa familia, na kuwa na burudani ya pamoja. Viongozi wa Kanisa pia wametoa tamko ambalo hufundisha kweli muhimu kuhusu familia (ona “Familia: Tangazo kwa Ulimwengu,” ChurchofJesusChrist.org).

Njia zingine za kuimarisha familia zinajumuisha sala za familia, kujifunza maandiko, na kuabudu pamoja kanisani. Pia tunaweza kufanya utafiti wa historia ya familia, kukusanya hadithi za familia, na kuwatumikia wengine.

Watu wengi wana fursa chache za uhusiano wa ndoa au wa familia yenye upendo. Wengi wamepitia talaka na wengine wana hali ngumu za kifamilia. Hata hivyo, injili hutubariki sisi kama watu binafsi bila kujali hali ya familia yetu. Tunapokuwa waaminifu, Mungu atatoa njia kwa ajili yetu kuwa na baraka za familia zenye upendo, iwe ni katika maisha haya au katika maisha yajayo.

Kujifunza Maandiko

Ndoa

Familia

Jifunze Zaidi kuhusu Kanuni Hii

Kazi ya Hekalu na Historia ya Familia kwa ajili ya Mababu Waliofariki Dunia

Baba wa Mbinguni anawapenda watoto Wake wote na anatamani wokovu wao na kuinuliwa kwao. Bado mabilioni ya watu wamefariki bila kuisikia injili ya Yesu Kristo au kupokea ibada okozi za injili. Ibada hizi zinajumuisha ubatizo, uthibitisho, kutawazwa katika ukuhani kwa ajili ya wanaume, endaumenti ya hekaluni, na ndoa ya milele.

Kupitia neema na rehema Yake, Bwana ametoa njia nyingine kwa watu hawa ili wapokee injili na ibada zake. Katika ulimwengu wa Roho, injili inahubiriwa kwa wale waliofariki bila kuipokea (ona Mafundisho na Maagano 138). Katika mahekalu, tunaweza kufanya ibada kwa niaba ya mababu zetu na wengine waliofariki. Wafu hawa katika ulimwengu wa roho wanaweza kisha kuikubali au kuikataa injili na ibada zilizofanywa kwa niaba yao.

Picha
familia ikijifunza maandiko

Kabla ya kufanya ibada hizi, tunahitaji kuwatambua mababu zetu ambao hawakuzipokea. Kuwatambua washiriki wa familia yetu ili waweze kupokea ibada ni kusudi muhimu la kazi yetu ya historia ya familia. Tunapopata taarifa kuhusu wao, tunaziongeza katika data ya Kanisa kwenye FamilySearch.org. Kisha sisi (au wengine) wanaweza kuwafanyia ibada za uwakilishi kwa niaba yao hekaluni.

Tunapowatambua mababu zetu na kufanya ibada kwa niaba yao, familia zetu zinaweza kuwa zimeungana milele.

Kujifunza Maandiko

Jifunze Zaidi kuhusu Kanuni Hii

  • Kitabu cha Maelezo ya Jumla, sura ya 28: “Ibada za Hekaluni kwa ajili ya Wafu

  • Mada za Injili: “Ubatizo wa Wafu,” “Historia ya Familia

Mahekalu, Endaumenti, Ndoa ya Milele, na Familia za Milele

Mahekalu

Hekalu ni nyumba ya Bwana. Ni mahali patakatifu ambapo tunaweza kufanya maagano na Mungu wakati tunapopokea ibada takatifu. Tunapoyashika maagano haya, tutaweza kuwa na nguvu za uungu zikijidhihirisha katika maisha yetu (ona Mafundisho na Maagano 84:19–22; 109:22–23).

Endaumenti

Mojawapo ya ibada tunayopokea hekaluni inaitwa endaumenti. Neno endaumenti linamaanisha “kipawa.” Kipawa hiki cha elimu na nguvu hutoka kwa Mungu. Wakati wa endaumenti, tunafanya maagano na Mungu ambayo yanatufunga Kwake na Mwanaye, Yesu Kristo (ona sura ya 1).

Watu wazima wanastahili kupokea endaumenti zao wenyewe baada ya uumini wa Kanisa kwa angalau mwaka mmoja. Kwa maelezo zaidi kuhusu endaumenti, ona Kitabu cha Maelezo ya Jumla, 27.2.

Ndoa ya Milele na Familia ya Milele

Mpango wa Mungu wa furaha unawezesha uhusiano wa familia kuvumilia zaidi ya kaburi. Katika hekalu tunaweza kuoana kwa muda na milele. Hii inafanya iwezekane kwa familia kuwa pamoja milele.

Baada ya wenza wa ndoa kupokea endaumenti zao, wanaweza kuunganishwa au kuoana kwa milele yote. Watoto wao wanaweza kuunganishwa pamoja nao.

Mume na mke ambao wameunganishwa hekaluni lazima washike maagano waliyoyafanya ili kupokea baraka za ndoa ya milele.

Picha
wanandoa wakitembea mtaani

Kujifunza Maandiko

Jifunze Zaidi kuhusu Kanuni Hii

  • Kitabu cha Maelezo ya Jumla, sura ya 27: “Ibada za Hekaluni kwa ajili ya Walio Hai

  • Mada za Injili: “Mahekalu,” “Endaumenti,” “Ndoa

  • temples.ChurchofJesusChrist.org

Chapisha