Miito ya Misheni
Sura ya 3: Somo la 3—Injili ya Yesu Kristo


“Sura ya 3: Somo la 3—Injili ya Yesu Kristo,” Hubiri Injili Yangu: Mwongozo wa Kushiriki Injili ya Yesu Kristo (2023)

“Sura ya 3: Somo la 3,” Hubiri Injili Yangu

Sura ya 3: Somo la 3

Injili ya Yesu Kristo

Picha
Ujio wa Pili, na Harry Anderson

Watu Wanaweza Kujiuliza

  • Yesu Kristo ni nani? Ni kwa jinsi gani Yeye anaweza kunisaidia mimi na familia yangu?

  • Inamaanisha nini kuwa na imani katika Yesu Kristo? Ni kwa jinsi gani imani katika Yeye hubariki maisha yangu?

  • Inamaanisha nini kutubu?

  • Ni kwa jinsi gani ninaweza kuhisi amani ya Mungu na kusamehewa baada ya kufanya chaguzi mbaya?

  • Dhumuni la ubatizo ni nini?

  • Kipawa cha Roho Mtakatifu ni nini?

  • Inamaanisha nini kuvumilia hadi mwisho?

Injili ya Yesu Kristo ndivyo jinsi tunavyokuja kwa Kristo. Injili ni rahisi vya kutosha kwamba hata mtoto anaweza kuelewa. Somo hili linafokasi kwenye injili na mafundisho ya Kristo, ikijumuisha imani katika Yesu Kristo, toba, ubatizo, kipawa cha Roho Mtakatifu, na kuvumilia hadi mwisho. Pia linafokasi juu ya jinsi ambavyo injili ya Yesu Kristo huwabariki watoto wote wa Mungu.

Neno injili kiuhalisia humaanisha “habari njema.” Injili ya Yesu Kristo ni habari njema kwa sababu inatoa mafundisho—ukweli wa milele—tunaouhitaji ili tuje Kwake na kuokolewa (ona 1 Nefi 15:14). Injili hutufundisha jinsi ya kuishi vyema, kuwa na maisha yenye maana. Habari njema ya injili hutoa njia kwa ajili yetu kusamehewa dhambi, kutakaswa, na kurudi katika uwepo wa Mungu.

Mapendekezo ya Kufundisha

Sehemu hii hutoa sampuli ya muhtasari wa kukusaidia ujiandae kufundisha. Pia inajumuisha mifano ya maswali na mialiko ambayo ungeweza kutumia.

Unapojiandaa kufundisha, kwa maombi fikiria hali na mahitaji ya kiroho ya kila mtu. Amua kile ambacho kitakuwa na msaada sana cha kufundisha. Jiandae kufafanua maneno ambayo watu wanaweza kuwa hawayaelewi. Panga kulingana na muda ulionao, ukikumbuka kufanya masomo kuwa mafupi.

Chagua maandiko ya kutumia wakati unapofundisha. “Msingi wa Mafundisho” sehemu ya somo hujumuisha maandiko mengi yenye msaada.

Fikiria ni maswali yapi ya kuuliza wakati unapofundisha. Panga mialiko ya kutoa ambayo itamtia moyo kila mtu kutenda.

Sisitiza baraka zilizoahidiwa za Mungu, na shiriki ushuhuda wako wa kile unachofundisha.

Picha
wamisionari wakiifundisha familia

Unachoweza Kuwafundisha Watu kwa Dakika 15–25

Chagua moja au zaidi ya kanuni zifuatazo za kufundisha. Msingi wa mafundisho kwa kila kanuni umetolewa baada ya muhtasari huu.

Misheni Takatifu ya Yesu Kristo

  • Mungu alimtuma Mwanaye Mpendwa, Yesu Kristo, kuja duniani kutukomboa kutokana na dhambi na kifo.

  • Kwa sababu ya upatanisho wa Yesu, tunaweza kusafishwa dhambi zetu na kutakaswa pale tunapotubu.

  • Baada ya Yesu kusulubiwa, Yeye alifufuka. Kwa sababu ya Ufufuko Wake, sisi sote tutafufuka baada ya kufa. Hii inamaanisha kwamba roho na mwili wa kila mtu vitaunganika tena, na kila mmoja wetu ataishi milele katika mwili mkamilifu, uliofufuka.

Imani katika Yesu Kristo

  • Imani ni kanuni ya kwanza ya injili ya Yesu Kristo.

  • Imani katika Yesu Kristo inajumuisha kuwa na imani kwamba Yeye ndiye Mwana wa Mungu na kumtumainia Yeye kama Mwokozi na Mkombozi wetu.

  • Imani katika Yesu Kristo ni kanuni ya matendo na yenye nguvu.

  • Tunaimarisha imani yetu kwa kusali, kujifunza maandiko, na kutii amri.

Toba

  • Imani katika Yesu Kristo hutuongoza kutubu. Toba ni mchakato wa kumgeukia Mungu na kugeuka kutoka dhambini. Tunapotubu, matendo yetu, matamanio, na fikra zetu hubadilika kuwiana zaidi na mapenzi ya Mungu.

  • Tunapotubu kwa dhati, Mungu hutusamehe. Msamaha unawezekana kwa sababu Yesu Kristo alifanya upatanisho kwa ajili ya dhambi zetu.

  • Tunapotubu, tunahisi amani kadiri hatia na huzuni yetu inapoponywa.

  • Toba ni mchakato wa maisha yote. Mungu hutukaribisha turudi tena kila wakati tunapotubu. Yeye kamwe hatakata tamaa juu yetu.

Ubatizo: Agano Letu La Kwanza na Mungu

  • Ubatizo ndiyo jinsi tunavyoingia kwa mara ya kwanza katika uhusiano wa agano na Mungu.

  • Ubatizo una sehemu mbili: ubatizo kwa maji na ubatizo kwa Roho. Wakati tunapobatizwa na kuthibitishwa, tunatakaswa dhambi zetu, ikitupatia mwanzo mpya katika maisha.

  • Tunabatizwa kwa kuzamishwa, kufuata mfano wa Yesu.

  • Watoto hawabatizwi hadi wakiwa na umri ya miaka minane. Watoto ambao wanafariki kabla ya umri huo wanakombolewa kupitia Upatanisho wa Yesu Kristo.

  • Tunashiriki sakramenti kila wiki katika ukumbusho wa dhabihu ya Yesu na kufanya upya maagano yetu na Mungu.

Kipawa cha Roho Mtakatifu

  • Roho Mtakatifu ni mshiriki wa tatu wa Uungu.

  • Baada ya kubatizwa, tunapokea kipawa cha Roho Mtakatifu kupitia ibada ya uthibitisho.

  • Wakati tunapopokea kipawa cha Roho Mtakatifu, tunaweza kuwa na wenza Wake katika maisha yetu yote kama tutakuwa waaminifu.

  • Roho Mtakatifu atatutakasa, atatuongoza, atatufariji, na atatusaidia tuujue ukweli.

Vumilia hadi Mwisho

  • Kuvumilia kunajumuisha kuendelea kutumia imani katika Kristo kila siku. Tunaendelea kushika maagano yetu na Mungu, kutubu, kutafuta wenza wa Roho Mtakatifu na kushiriki sakramenti.

  • Kwa uaminifu tunatafuta kumfuata Yesu Kristo, Mungu anaahidi kwamba tutapata uzima wa milele.

Injili ya Yesu Kristo Huwabariki Watoto Wote wa Mungu

  • Kuishi injili huongeza shangwe yetu, hushawishi matendo yetu, na hurutubisha uhusiano wetu.

  • Tuna uwezekano mkubwa wa kuwa na furaha—sote kama watu binafsi na kama familia—wakati tunapoishi mafundisho ya Yesu Kristo.

  • Kupitia injili ya Yesu Kristo, familia zinabarikiwa katika maisha haya na wanaweza kuunganishwa milele na kuishi katika uwepo wa Mungu.

Maswali Ambayo Ungeweza Kuwauliza Watu

Maswali yafuatayo ni mifano ya kile ambacho ungeweza kuwauliza watu. Maswali haya yanaweza kukusaidia uwe na mazungumzo ya maana na uelewe mahitaji ya mtu na mtazamo wake.

  • Je, najua nini kuhusu Yesu Kristo?

  • Je, inamaanisha nini kwako kuwa na imani katika Yesu Kristo?

  • Ni mabadiliko yapi unataka kuyafanya katika maisha yako?

  • Ni upi uelewa wako juu ya toba?

  • Ni upi uelewa wako juu ya ubatizo? Ni kipi unaweza kufanya sasa kujiandaa kwa ajili ya ubatizo?

  • Ni jinsi gani Roho Mtakatifu angeweza kukusaidia katika safari yako ya kurudi kwenye uwepo wa Mungu?

  • Ni changamoto ipi ambayo wewe au familia yako inakabiliana nayo? Tunaweza kushiriki baadhi ya njia ambazo kwazo injili ya Yesu Kristo inaweza kukusaidia?

Mialiko Unayoweza Kuitoa

  • Je, utamwomba Mungu katika sala akusaidie ujue kwamba kile tulichofundisha ni cha kweli? (Ona “Umaizi wa Kufundisha: Sala” katika sehemu ya mwisho ya somo la 1.)

  • Je, utahudhuria kanisani Jumapili hii kujifunza zaidi kuhusu kile tulichokufundisha?

  • Je, utasoma Kitabu cha Mormoni na kusali ili kujua ikiwa ni neno la Mungu? (Unaweza kupendekeza sura au mistari mahususi.)

  • Je, utafuata mfano wa Yesu na kubatizwa? (Ona “Mwaliko wa Kubatizwa na Kuthibitishwa,” ambao unafuatia punde tu baada ya somo la 1.)

  • Je, tunaweza kupanga muda kwa ajili ya matembezi yetu yajayo?

Mafundisho ya Msingi

Sehemu hii inatoa mafundisho na maandiko kwa ajili ya kujifunza ili kuimarisha ufahamu na ushuhuda wako wa injili na kukusaidia ufundishe.

Picha
Hao Thenashara Yesu Aliwatuma, na Walter Rane

Misheni Takatifu ya Yesu Kristo

Baba wa Mbinguni alimtuma Mwana Wake Mpendwa, Yesu Kristo, kuja duniani ili kufanya iwezekane kwa ajili ya sisi wote kupata shangwe katika ulimwengu huu na uzima wa milele katika ulimwengu ujao. “Na hii ndiyo injili, habari njema, … kwamba [Yesu Kristo] alikuja duniani … kuchukua dhambi za ulimwengu, na kuutakasa ulimwengu, na kuusafisha kutokana na udhalimu wote; ili kupitia kwake wote waweze kuokolewa” (Mafundisho na Maagano 76:40–42).

Kama wenye miili ya kufa, sote tunatenda dhambi, na sote tutakufa. Dhambi na kifo vingetuzuia kuwa na uzima wa milele pamoja na Mungu isipokuwa tumpate Mkombozi (ona 2 Nefi 9). Kabla ya ulimwengu kuumbwa, Baba wa Mbinguni alimchagua Yesu Kristo atukomboe. Katika dhihirisho kuu la upendo, Yesu alikuja duniani na kutimiza misheni hii ya kiungu. Yeye alifanya iwezekane kwa ajili yetu kukombolewa kutoka dhambi zetu, na Yeye alihakikisha kwamba sisi sote tutafufuka baada ya kufa.

Yesu Kristo aliishi maisha yasiyo na dhambi. Mwishoni mwa huduma Yake duniani, Yeye alijichukulia juu Yake dhambi zetu kwa kuteseka Kwake katika Gethsemane na wakati aliposulubiwa (ona 1 Nefi 11:33). Mateso ya Yesu yalikuwa makubwa sana kiasi kwamba yalimsababisha “kutetemeka kwa sababu ya maumivu, na kutoka damu kwenye kila kinyweleo” (Mafundisho na Maagano 19:18). Baada ya Kusulubiwa Kwake, Yesu alifufuka, akapata ushindi juu ya kifo. Kwa pamoja, matukio haya ni Upatanisho wa Yesu Kristo.

Dhambi zetu hutufanya sisi kuwa wachafu kiroho, na “hakuna kitu kichafu chaweza kuishi na Mungu” (1 Nefi 10:21). Kwa nyongeza, sheria ya haki huhitaji matokeo kwa ajili ya dhambi zetu.

Dhabihu ya upatanisho wa Yesu hutoa njia kwa ajili yetu kusafishwa dhambi zetu na kutakaswa pale tunapotubu. Pia hutoa njia ya kukidhi madai ya haki (ona Alma 42:15, 23–24). Mwokozi alisema, “Mimi … nimeteseka mambo haya kwa ajili ya watu wote, ili kwamba wasiteseke kama watatubu; lakini kama hawatatubu lazima wateseke kama Mimi” (Mafundisho na Maagano 19:16–17). Isingekuwa Yesu Kristo, dhambi zingemaliza matumaini yote ya kuwepo katika siku zijazo pamoja na Baba wa Mbinguni.

Katika kujitoa Kwake kama dhabihu kwa ajili yetu, Yesu hakuondoa jukumu letu binafsi. Tunahitaji kuwa na imani katika Yeye, kutubu, na kujitahidi kutii amri. Tunapotubu, Yesu atadai kwa niaba yetu haki Zake za rehema ya Baba Yake (ona Moroni 7:27–28). Kwa sababu ya maombezi ya Mwokozi, Baba wa Mbinguni hutusamehe, kutuondelea mzigo na hatia ya dhambi zetu (ona Mosia 15:7–9). Tunasafishwa kiroho na tunaweza hatimaye kukaribishwa katika uwepo wa Mungu.

Misheni ya kiungu ya Yesu ilikuwa pia kutuokoa kutokana na kifo. Kwa sababu Yeye alifufuka, sisi sote tutafufuka baada ya kufa. Hii inamaanisha kwamba roho na mwili wa kila mtu vitaunganika tena, na kila mmoja wetu ataishi milele katika mwili mkamilifu, uliofufuka. Kama isingekuwa Yesu Kristo, kifo kingemaliza matumaini yote kwa ajili ya kuwepo katika siku zijazo pamoja na Baba wa Mbinguni.

Kujifunza Maandiko

Mungu Alimtuma Mwanaye

Wokovu kupitia Yesu Kristo

Jifunze Zaidi kuhusu Kanuni Hii

Imani katika Yesu Kristo

Kanuni ya kwanza ya injili ni imani katika Bwana Yesu Kristo. Imani ndiyo msingi wa kanuni zingine zote za injili.

Imani katika Yesu Kristo hujumuisha kuamini kwamba Yeye ndiye Mwana Pekee wa Mungu. Hujumuisha kumtumainia Yeye kama Mwokozi na Mkombozi wetu—kwamba Yeye ndiye njia yetu pekee ya kurudi kwenye uwepo wa Mungu (ona Matendo ya Mitume 4:10–12; Mosia 3:17; 4:6–8). Tunaalikwa kutumia “imani isiyotingishika kwake, tukitegemea kabisa ustahili wa yule aliye mkuu katika kuokoa” (2 Nefi 31:19).

Imani katika Yesu Kristo inajumuisha kuamini kwamba Yeye aliteseka kwa ajili ya dhambi zetu katika dhabihu Yake ya upatanisho. Kwa sababu ya dhabihu Yake, tunaweza kusafishwa na kutakaswa pale tunapotubu. Kusafishwa huku hutusaidia tupate amani na tumaini katika maisha haya. Pia hututuruhsu tupokee utimilifu wa shangwe baada ya sisi kufa.

Imani katika Yesu Kristo hujumuisha kutumaini kwamba kupitia Yeye, sisi sote tutafufuka baada ya kufa. Imani hii inaweza kutusaidia na kutufariji katika nyakati za upotevu? Huzuni ya kifo inaweza kuondoshwa kwa ahadi ya Ufufuo.

imani katika Yesu Kristo inajumuisha kuamini na kutumainia kwamba Yeye alijichulia juu Yake maumivu yetu, magonjwa, na udhaifu wetu (ona Isaya 53:3–5). Yeye anajua kwa uzoefu Wake jinsi ya kutusaidia kwa huruma kupitia changamoto za maisha (ona Alma 7:11–12; Mafundisho na Maagano 122:18). Tunapotumia imani, Yeye anatusaidia tusonge mbele kupita dhiki.

Kupitia imani yetu katika Yeye, Yesu anaweza kutuponya kimwili na kiroho. Yeye daima yu tayari kutusaidia kadiri tunavyokumbuka mwaliko Wake wa “nitegemeeni katika kila wazo; msitie shaka, msiogope” (Mafundisho na Maagano 6:36).

Kanuni ya Matendo na Nguvu

Imani katika Yesu Kristo Huongoza kwenye matendo. Tunaonesha imani yetu kwa kutii amri na kufanya mema kila siku. Tunatubu dhambi zetu. Tunakuwa waaminifu Kwake. Tunajitahidi kuwa zaidi kama Yeye.

Tunapotumia imani, tunaweza kupata uzoefu wa nguvu za Yesu katika maisha yetu ya kila siku. Yeye atakuza jitihada zetu bora zaidi. Yeye atatusaidia tukue na tushinde majaribu.

Kuimarisha Imani Yetu

Nabii Alma alifundisha kwamba kujenga imani kunaweza kuanza na “kutamani kuamini” (Alma 32:27). Kisha, ili imani yetu katika Yesu Kristo ikue, tunahitaji kuilea kwa kujifunza maneno Yake, kutumia mafundisho Yake, na kutii amri Zake. Alma alifundisha kwamba kadiri kwa subira, tunavyojitahidi kulisha neno la Mungu katika mioyo yetu, “litamea mizizi [na litakuwa kama] mti utakaokua na kuzaa matunda yasiyo na mwisho”—hivyo kuimarisha imani yetu (Alma 32:41; ona mstari wa 26–43).

Kujifunza Maandiko

Imani, Nguvu, na Wokovu

Mafundisho ya Imani

Mifano ya Imani

Matendo na Utii

Imani iongozayo kwenye Toba

Jifunze Zaidi kuhusu Kanuni Hii

  • Mwongozo wa Maandiko: “Yesu Kristo,” “Patanisha, Upatanisho,” “Imani

  • Kamusi ya Biblia: “Imani

  • Mada za Injili: “Yesu Kristo,” “Upatanisho wa Yesu Kristo,” “Imani katika Yesu Kristo

Toba

Toba ni Nini?

Toba ni kanuni ya pili ya injili. Imani katika Yesu Kristo na upendo wetu kwa ajili Yake hutuongoza kutubu (ona Helamani 14:13). Toba ni mchakato wa kumgeukia Mungu na kugeuka kutoka dhambini. Tunapotubu, matendo yetu, matamanio, na fikra zetu hubadilika kuwiana zaidi na mapenzi ya Mungu. Msamaha wa dhambi unawezekana kupitia Yesu Kristo na dhabihu Yake ya upatanisho.

Toba ni zaidi ya kuonesha utashi wa kubadili tabia au kushinda udhaifu. Toba ni kumgeukia Kristo kwa dhati, ambaye hutupatia nguvu ya kupata uzoefu wa “badiliko kuu” katika mioyo yetu (Alma 5:12–14). Tunapopata uzoefu wa badiliko hili la moyo, tunazaliwa tena kiroho (ona Mosiah 27:24–26).

Kupitia toba, tunakuza mtazamo mpya juu ya Mungu, sisi wenyewe, na ulimwengu. Tunahisi upya upendo wa Mungu kwa ajili yetu sisi kama watoto Wake—na upendo wa Mwokozi kwetu. Fursa ya kutubu ni moja ya baraka kuu ambazo Mungu ametupatia sisi kupitia Mwanaye.

Mchakato wa Toba

Tunapotubu, tunatambua dhambi zetu na kuhisi majuto ya kweli. Tunakiri dhambi zetu kwa Mungu na kuomba msamaha Wake. Pia tunaungama dhambi kubwa kwa viongozi wa Kanisa walioidhinishwa, ambao wanatusaidia tutubu. Tunafanya kile tunachoweza kufanya urejeshaji, ambayo humaanisha kujaribu kurekebisha tatizo ambalo matendo yetu yanaweza kuwa yamelisababisha. Toba ya kweli inadhihirishwa vyema kwa matendo ya haki kwa kipindi fulani cha muda.

Toba ni mchakato wa kila siku katika maisha yetu yote. “Wote tumetenda dhambi, na kupungukiwa na utukufu wa Mungu” (Warumi 3:23). Tunapaswa kuendela kutubu, tukikumbuka kwamba sisi “twayaweza mambo yote katika Kristo atutiaye nguvu” (Wafilipi 4:13). Bwana ametuhakikishia kwamba “kila mara watu wangu wanapotubu nitawasamehe makosa yao” (Mosia 26:30).

Baraka za Toba

Toba ni kanuni chanya ambayo huleta shangwe na amani. Inatuleta kwenye “uwezo wa Mkombozi, uongozao kwenye wokovu wa [roho zetu]” (Helamani 5:11).

Tunapotubu, hatia na huzuni yetu huponywa katika mchakato wa muda. Tunahisi ushawishi wa Roho kwa wingi sana. Hamu yetu ya kumfuata Mungu inakuwa imawa.

Picha
Rais Russell M. Nelson

Watu wengi hufikiria toba kama adhabu—jambo la kuepukwa. … Lakini hisia hii ya kuwa unaadhibiwa inazalishwa na Shetani. Anajaribu kutuzuia kutazama kwa Yesu Kristo, ambaye anasimama kwa mikono iliyonyooshwa, akitumaini na kuwa tayari kutuponya, kutusamehe, kutusafisha, kutuimarisha na kututakasa” (Russell M. Nelson, “Tunaweza Kufanya Vizuri Zaidi na Kuwa Bora Zaidi,” Liahona, Mei 2019, 67).

Kujifunza Maandiko

Toba

Ukombozi na Msamaha

Rehema kwa Wale Ambao Wanatubu

Jifunze Zaidi kuhusu Kanuni Hii

Picha
msichana akibatizwa

Ubatizo: Agano Letu La Kwanza na Mungu

Imani katika Yesu Kristo na toba hutuandaa sisi kwa ibada za ubatizo na uthibitisho. Ubatizo ni ibada ya kwanza ya kuokoa ya injili ya Yesu Kristo. Tunapopokea ibada hii ya shangwe ya tumaini, tunafanya agano letu la kwanza na Mungu.

Ibada ni tendo takatifu au utaratibu unaofanywa kwa mamlaka ya ukuhani. Baadhi ya ibada, kama ubatizo, ni muhimu kwa wokovu wetu.

Kupitia ibada, tunafanya maagano na Mungu. Maagano haya ni ahadi takatifu kati yetu na Mungu. Yeye anaahidi kutubariki pale tunapotimiza ahadi zetu Kwake. Tunapaswa kuwa na msimamo imara wa kutimiza ahadi zetu na Mungu.

Mungu ametoa ahadi na maagano ya kutusaidia sisi kuja Kwake na kupata uzima wa milele. Tunapopokea ibada za ukuhani na kutimiza ahadi husika, tunaweza kupata uzoefu wa “nguvu za kiungu” katika maisha yetu (Mafundisho na Maagano 84:20).

Agano la Ubatizo

Mwokozi alifundisha kwamba ubatizo ni muhimu kwetu ili kuingia katika ufalme wa mbinguni (ona Yohana 3:5). Pia ni muhimu kwetu ili kuwa waumini wa Kanisa la Yesu Kristo. Mwokozi wetu aliweka mfano kwa kubatizwa (ona Mathayo 3:13–17).

Tunapobatizwa na kushika agano letu, Mungu anaahidi kutusamehe dhambi zetu (ona Matendo ya Mitume 22:16; 3 Nefi 12:1–2). Hii baraka kuu inawezeshwa kupitia upatanisho wa Yesu Kristo, ambaye “alitupenda na alituosha dhambi zetu katika damu yake” (Ufunuo 1:5). Mungu pia anaahidi kutubariki na wenza wa Roho Mtakatifu ili tuweze kutakaswa, kuongozwa, na kufarijiwa.

Katika sehemu yetu ya agano la ubatizo, sisi tunashuhudia kwamba tuko radhi kujichukulia juu yetu jina la Yesu Kristo. Pia tunaahidi ya kwamba tutamkumbuka Yeye daima na kushika amri Zake. Tunaahidi kuwapenda na kuwatumikia wengine, “kuomboleza na wale wanaoomboleza; … kuwafariji wale ambao wanahitaji kufarijiwa, na kusimama kama mashahidi wa Mungu nyakati zote na katika vitu vyote, na katika mahali popote” (Mosia 18:9; ona mstari wa 8–10, 13). Tunaonesha msimamo wa kumtumikia Yesu Kristo hadi mwisho wa maisha yetu (ona Mafundisho na Maagano 20:37; Mosia 2:17).

Uaminifu wetu wa agano unaohusiana na ubatizo ni jukumu kubwa. Pia unavutia na kuleta shangwe. Unatengeneza uhusiano maalumu kati yetu na Baba wa Mbinguni ambapo kupitia huo Yeye daima anatoa upendo Wake.

Ubatizo kwa Kuzamishwa Majini

Yesu alifundisha kwamba tunahitaji kubatizwa kwa kuzamishwa majini kwa ajili ya ondoleo la dhambi zetu (ona Mafundisho na Maagano 20:72, 74). Ubatizo kwa kuzamishwa majini unaashiria kifo, kuzikwa, na Ufufuko wa Yesu Kristo (ona Warumi 6:3–6).

Ubatizo kwa kuzamishwa majini pia una ishara ya nguvu sana kwa ajili yetu binafsi. Unawakilisha kifo cha maisha yetu ya zamani, mazishi ya maisha hayo, na kuibuka katika kuzaliwa tena kiroho. Tunapobatizwa, tunaanza mchakato wa kuzaliwa tena na kuwa wana na mabinti wa kiroho wa Kristo (ona Mosia 5:7–8; Warumi 8:14–17).

Watoto

Watoto hawabatizwi hadi wanapofika umri wa uwajibikaji, ambao ni umri wa miaka minane (ona Mafundisho na Maagano 68:27). Watoto ambao wanafariki kabla ya umri huo wanakombolewa kupitia Upatanisho wa Yesu Kristo (ona Moroni 8:4–24; Mafundisho na Maagano 137:10). Kabla watoto hawajabatizwa, wanapaswa kufundishwa injili ili wajiandae kwa hatua hii muhimu katika maisha yao ya kufanya agano na Mungu.

Sakramenti

Baba yetu wa Mbinguni anatutaka tuwe waaminifu kwa maagano tunayofanya na Yeye. Ili kutusaidia tufanye hivyo, Yeye anatuamuru sisi tukutane kila mara ili kupokea sakramenti. Sakramenti ni ibada ya ukuhani ambayo Yesu Kristo aliianzisha kwa Mitume Wake kabla ya Upatanisho Wake.

Kushiriki sakramenti ni kusudi muhimu sana la mkutano wa sakramenti kila wiki. Mkate na maji hubarikiwa na kupitishwa kwa mkusanyiko. Mkate huwakilisha dhabihu ya Mwokozi ya mwili Wake kwa ajili yetu. Maji huwakilisha damu Yake, ambayo Yeye aliimwaga kwa ajili yetu.

Tunashiriki ishara hizi katika ukumbusho wa dhabihu ya Mwokozi na kufanya upya maagano yetu na Mungu. Tunapokea tena upya ahadi kwamba Roho atakuwa pamoja nasi.

Kujifunza Maandiko

Mfano wa Kristo

Agano la Ubatizo

Sifa za Ubatizo

Baraka za Ubatizo Zilizoahidiwa

Haja ya Mamlaka

Yesu Anaanzisha Sakramenti

Maombi ya Sakramenti

Kupokea Sakramenti

Jifunze Zaidi kuhusu Kanuni Hii

Picha
Kristo akimwekea mikono mwanamke

Kipawa cha Roho Mtakatifu

Kupokea Kipawa cha Roho Mtakatifu

Ubatizo una sehemu mbili. Yesu alifundisha kwamba tunahitaji “kuzaliwa kwa maji na kwa Roho ili kuingia ufalme wa Mungu (Yohana 3:5; msisitizo umeongeweza). Joseph Smith alifundisha, “Ubatizo kwa maji ni nusu tu ya ubatizo, na hauna faida yoyote bila nusu ile nyingine—ambayo ni, ubatizo kwa Roho Mtakatifu.”(Teachings of Presidents of the Church: Joseph Smith [2007], 95).

Ubatizo kwa maji sharti ufuatiwe na ubatizo wa Roho ili uweze kuwa kamili. Tunapopokea ubatizo kamili, tunasafishwa dhambi zetu na kuzaliwa tena kiroho. Kisha tunaanza maisha mapya ya kiroho kama wafuasi wa Kristo.

Tunapokea ubatizo wa Roho kupitia ibada inayoitwa uthibitisho. Ibada hii inatekelezwa na mtu mmoja au zaidi wenye ukuhani ambao huweka mikono yao juu ya kichwa chetu. Kwanza wanatuthibisha kama muumini wa Kanisa, kisha wanatunukia kipawa cha Roho Mtakatifu juu yetu. Hii ni ibada sawa na ile ambayo ilirejelewa katika Agano Jipya na Kitabu cha Mormoni (ona Matendo ya Mitume 8:14–17; 3 Nefi 18:36–37).

Roho Mtakatifu ni mshiriki wa tatu wa Uungu. Yeye hufanya kazi kwa umoja na Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo. Wakati tunapopokea kipawa cha Roho Mtakatifu, tunaweza kupokea wenza Wake katika maisha yetu kadiri tunavyokuwa waaminifu.

Jinsi Roho Mtakatifu anavyotubariki

Kipawa cha Roho Mtakatifu ni mojawapo ya vipawa vikuu vya Baba wa Mbinguni. Roho Mtakatifu hutusafisha na kututakasa, kutufanya tuwe watakatifu, wakamilifu zaidi, zaidi kama Mungu (ona 3 Nefi 27:20). Yeye hutusaidia tubadilike na tukue kiroho pale tunapotafuta kufuata maagizo ya Mungu.

Roho Mtakatifu hutusaidia tujifunze na tutambue ukweli (ona Moroni 10: 5). Yeye pia huthibitisha ukweli kwenye mioyo na akili zetu. Kwa nyongeza, Roho Mtakatifu hutusaidia tufundishe ukweli (ona Mafundisho na Maagano 42:14). Tunapojifunza na kufundisha ukweli kwa nguvu ya Roho Mtakatifu, Yeye huubeba na kuupeleka kwenye mioyo yetu (ona 2 Nefi 33:1).

Tunapotafuta maelekezo kutoka kwa Roho Mtakatifu kwa unyenyekevu, Yeye atatuongoza (ona 2 Nefi 32:5). Hii inajumuisha kutushawishi katika jinsi tunavyoweza kuwatumikia wengine.

Roho Mtakatifu hutupa nguvu za kiroho ili kutusaidia tushinde udhaifu. Yeye hutusaidia tukinze majaribu. Yeye hutuonya juu ya hatari za kiroho na kimwili.

Roho Mtakatifu atatusaidia tupite changamoto za maisha. Yeye hutufariji wakati wa majaribu au huzuni, akitujaza tumaini (ona Moroni 8:26). Kupitia Roho Mtakatifu, tunaweza kuhisi upendo wa Mungu kwa ajili yetu.

Kujifunza Maandiko

Asili ya Roho Mtakatifu

Baraka na Ushawishi kutoka kwa Roho Mtakatifu

Umuhimu wa Kipawa cha Roho Mtakatifu

Jifunze Zaidi kuhusu Kanuni Hii

Picha
Yesu akiwa amewabeba watoto

Vumilia hadi Mwisho

Wakati tunapobatizwa na kuthibitisha, tunaingia katika agano na Mungu. Miongoni mwa vitu vingine, tunaahidi kushika amri Zake na kumtumikia Yeye kwa siku zetu zote zilizosalia (ona Mosia 18:8–10, 13; Mafundisho na Maagano 20:37).

Baada ya kuingia katika njia ya injili kupitia ubatizo na uthibitisho, tunafanya kila juhudi kubakia kwenye njia. Tunapoondoka kutoka kwenye njia hata kidogo tu, tunatumia imani katika Kristo ili kutubu. Baraka za toba huturuhusu turudi katika njia ya injili na kubakia na baraka za maagano yetu na Mungu. Tunapotubu kwa dhati, Mungu daima yu radhi kutusamehe na kutukaribisha tena.

Kuvumilia hadi mwisho humaanisha kubaki waaminifu kwa Mungu hadi mwisho. wa maisha yetu—kupitia nyakati nzuri na nyakati ngumu, kupitia mafanikio na dhiki. Kwa unyenyekevu tunamruhusu Kristo atufinyange na atufanye tuwe zaidi kama Yeye. Tunamtegemea Kristo kwa imani, na tumaini, bila kujali kile kinachokuja katika maisha yetu.

Kuvumilia hadi mwisho hakumaanishi tu kusubiri hadi tufe. Badala yake, humaanisha kufokasi maisha yetu, fikra zetu, na matendo yetu kwa Yesu Kristo. Hujumuisha kuendelea kuonesha imani katika Kristo kila siku. Pia tunaendelea kutubu, kushika maagano yetu na Mungu, na kutafuta wenza wa Roho Mtakatifu.

Kuvumilia hadi mwisho hujumuisha, “kusonga mbele kwa imani imara katika Kristo, kwa mngʼaro mkamilifu wa tumaini, na upendo kwa Mungu na wanadamu wote.” Baba yetu wa Mbinguni anaahidi kwamba tunapovumilia hadi mwisho, “tutapokea uzima wa milele” (2 Nefi 31:20).

Kujifunza Maandiko

Vumilia hadi Mwisho

Baraka za Wale Ambao Wanavumilia

Jifunze Zaidi kuhusu Kanuni Hii

  • Mada za Injili: “Dhiki

  • Mwongozo wa Maandiko, “Vumilia,” “Dhiki

Picha
familia ikitabasamu

Injili ya Yesu Kristo Huwabariki Watoto Wote wa Mungu

Injili ya Yesu Kristo ni kwa ajili ya watoto wote wa Mungu. Maandiko hufundisha kwamba “wote ni sawa kwa Mungu” bila kujali asili au hali yetu. Yeye huwaalika wote “kuja Kwake, na kupokea wema Wake, na hamkatazi yeyote kuja Kwake” (2 Nefi 26:33).

Injili hutubariki sisi katika maisha yetu yote ya duniani na milele yote. Tuna uwezekano mkubwa wa kuwa na furaha—sote kama watu binafsi na kama familia—wakati tunapoishi kwa mafundisho ya Yesu Kristo (ona Mosia 2:41; “Familia: Tangazo kwa Ulimwengu,” ChurchofJesusChrist.org). Kuishi injili huongeza shangwe yetu, hushawishi matendo yetu, na hurutubisha uhusiano wetu.

Kuishi Injili ya Yesu Kristo kunaweza pia kutulinda kutokana na kufanya chaguzi ambazo zingetuathiri kimwili au kiroho. Inatusaidia tupate nguvu na faraja katika nyakati za majaribu na huzuni. Inatoa njia kuelekea kwenye maisha ya shangwe milele.

Mojawapo ya jumbe kuu za injili ya urejesho ni kwamba sisi sote ni sehemu ya familia ya Mungu. Sisi ni wana na mabinti Zake wapendwa. Bila kujali hali ya familia yetu hapa duniani, kila mmoja wetu ni mshiriki wa familia ya Mungu.

Sehemu nyingine kubwa ya ujumbe wetu ni kwamba familia zinaweza kuunganishwa milele. Familia imeamriwa na Mungu. Mpango wa furaha wa Baba wa Mbinguni huwezesha uhusiano wa familia kuendelea zaidi ya kaburi. Ibada na maagano matakatifu ya hekaluni yanawezesha familia kuwa pamoja milele.

Kupitia nuru ya injili, familia zinaweza kusuluisha kutoelewana, ubishi, na changamoto. Familia zilizosambaratishwa na mfarakano zinaweza kuponywa kupitia toba, msamaha, imani katika nguvu za Upatanisho wa Yesu Kristo.

Injili ya Yesu Kristo hutusaidia tukuze mahusiano ya familia yenye nguvu. Nyumbani ndiyo mahali bora pa kufunza na kujifunza kanuni za injili. Nyumba iliyoanzishwa kwa kanuni za injili itakuwa mahali pa kimbilio na usalama. Itakuwa mahali ambapo Roho wa Bwana anaweza kuishi.

Kujifunza Maandiko

Jifunze Zaidi kuhusu Kanuni Hii

Muhtasari Mfupi hadi wa Wastani wa Somo

Muhtasari ufuatao ni sampuli ya kile ambacho ungemfundisha mtu fulani kama una muda mfupi tu. Unapotumia muhtasari huu, chagua kanuni moja au zaidi za kufundisha. Msingi wa mafundisho kwa kila kanuni ulitolewa mapema katika somo hili.

Unapofundisha, uliza maswali na usikilize. Toa mwaliko ambao utawasaidia watu wajifunze jinsi ya kusonga karibu na Mungu. Mwaliko mmoja muhimu ni kwa mtu kukutana nawe tena. Urefu wa somo utategemea maswali unayouliza na kusikiliza unakofanya.

Picha
wamisionari wakiwafundisha wanawake

Unachoweza Kuwafundisha Watu kwa Dakika 3–10

  • Mungu alimtuma Mwanaye Mpendwa, Yesu Kristo, kuja duniani kutukomboa kutokana na dhambi na kifo.

  • Imani katika Yesu Kristo ni kanuni ya matendo na yenye nguvu. Imani hutusaidia tupate uzoefu wa nguvu za Mungu zenye kuimarisha katika maisha yetu.

  • Imani katika Yesu Kristo hutuongoza kutubu. Toba ni mchakato wa kumgeukia Mungu na kugeuka kutoka kwenye dhambi. Tunapotubu, matendo yetu, matamanio, na fikra zetu hubadilika kuwiana zaidi na mapenzi ya Mungu.

  • Tunapotubu, Mungu anatusamehe. Msamaha unawezekana kwa sababu Yesu Kristo alipatanisha kwa ajili ya dhambi zetu.

  • Ubatizo una sehemu mbili: ubatizo kwa maji na ubatizo kwa Roho. Wakati tunapobatizwa na kuthibitishwa, tunatakaswa dhambi zetu, ikitupatia mwanzo mpya katika maisha.

  • Baada ya kubatizwa kwa maji, tunapokea kipawa cha Roho Mtakatifu kupitia ibada ya uthibitisho.

  • Tunapofuata njia ya injili kwa uaminifu hadi mwisho wa maisha yetu, Mungu anaahidi kwamba tutakuwa na uzima wa milele.

Chapisha